Ndugu wawili hawa wakaendelea kutembea huku wamebana macho kidogo, kama tu mababu zao walivyofanya kwa miaka mia nne iliyopita. Toka kipindi wageni walipofika mafundisho mapya na utawala mpya, na bunduki za kulinda vitu hivyo. Na katika miaka hiyo mia nne ulinzi pekee wa watu wa jamii ya Kino umekuwa ni kufumba kidogo macho na kukaza midomo na kuacha mambo yalivyo. Huo ndiyo ulikuwa ulinzi wao thabiti.
Umati uliozidi kukusanyika ulikuwa tulivu na makini, walikuwa wamehisi umuhimu wa wa siku hii. Mtoto yoyote aliyeleta vuruga, aliyelia kwa kele au kutaka kuchukua kofia na kuvuruga nywele za watu alinyamazishwa mara moja. Siku hii ilikuwa muhimu sana kiasi kwamba mzee mmoja alifika kushuhudia akiwa kabebwa mabegani mwa mpwa wake. Sasa umati ukawa umetoka kwenye nyumba zao za miti na majani na kuingia mjini kwenye nyumba za mawe, zilizopakwa chokaa. Barabara za mji zilikuwa ni pana kiasi. Na kwa mara nyingine tena, walipopita mbele ya kanisa na ombaomba wakajiunga nao; wauza maduka waliwaangalia wakipita; watu waliokunywa pombe wakaacha kunywa na kuungana na msafara, wauzaji nao baada ya kupoteza wateja, wakafunga na kuungana na umati. Na jua nalo likazidi ukali.
Taarifa za ujio wa umati zilitangulia kufika mbele kuliko umati wenyewe. Katika ofisi zao, wanunuzi wa lulu wakazidi kujiweka tayari. Walitoa makabrasha na kuweka mezani ili Kino atakapofika waonekane kuwa walikuwa wametingwa na kazi. Na waliweka lulu zao kwenye kabati, walionelea haitakuwa sawa kwa lulu mbovu kuonekana mbele ya lulu nzuri inayokuja. Habari za uzuri wa lulu ya Kino zilikuwa zimewafikia.
Ofisi za wanunua lulu zilikuwa zimerundikana pamoja kwenye mtaa mmoja mwembamba, madirishani kulikuwa kumewekwa nondo.
Mtu mmoja mkakamavu alikuwa amekaa katika ofisi moja. Uso wake ulikuwa wa baba mtu mzima na mpole, macho yake yaling’aa kirafiki. Alikuwa ni mtu wa matani mengi, mwenye kusalimu watu wote, mtu mwenye shangwe. Lakini bado alionekana kama ana huzuni ndani yake. Angeweza kukumbuka kifo cha shangazi yako katikati ya kicheko na machozi yake yakalengalenga kwa huzuni. Asubuhi hii alikuwa ameweka ua kwenye chupa mezani pake. Alikuwa kanyoa ndevu vizuri kabisa, mikono yake ilikuwa safi na kucha zake zilisuguliwa vyema. Mlango wa ofisi yake ulikuwa wazi na alikuwa akiimba kwa sauti ya chini isiyosikika vizuri. Mkononi alikuwa akichezea sarafu vidoleni mwake kama mwanamazingaombwe stadi. Kisa ghafla akasikia sauti ya vishindo vya umati ukija. Vidole vyake vikazidi kuongeza kasi ya kuchezea sarafu, na mara Kino alipotokea akahamishia mkono ule chini ya meza.
“Habari za asubuhi rafiki yangu,” alisalimia mtu yule. “Nikusaidie nini?”
Kino alishangaa-shangaa ndani mule mwenye mwanga hafifu, maana alikuwa ametoka nje kwenye mwanga mkali. Lakini macho ya mnunuzi yule yalikuwa yameshazoea, yalionekana makali na ya ukatili kama ya mwewe, lakini hapohapo sura yake ilionyesha tabasamu. Na chini ya meza, bado aliendelea kuchezea ile sarafu kwa vidole vyake.
“Nina lulu,” alisema Kino. Juan Tomas aliyekuwa amesimama pembeni yake, akaguna kwa maana aliona kama Kino hajaitendea haki lulu yake kwa kusema vile. Majirani wengine walikuwa wakichungulia kupitia mlangoni, watoto wadogo walijivuta dirishani kuchungulia, wengine walichuchumaa na kupiga magoti ili wachungulie kwa chini.
“Una lulu, moja tu? Wakati mwingine watu huleta dazani nzima. Hebu tuione lulu yako, tutaikadiria thamani yake na kukupa bei nzuri.” Vidole vyake vilizungusha sarafu kwa kasi hata zaidi.
Hapo Kino alitoa pochi ya ngozi, akafungua polepole na kutoa kipande kichafu cha ngozi ya swala, na kisha kutoa lulu ile na kuiweka kwenye sinia jeusi lililokuwa mezani na kisha kukaza macho yake kumuangalia mnunuzi usoni. Mnunuzi hakuonyesha ishara zozote, uso wake haukubadilika lakini mkono uliokuwa chini ya meza ukizungusha sarafu haukuweza kufanya kazi yake barabara. Sarafu ilimteleza na kumuangukia pajani. Aliishika lulu ile na kuizungusha ndani ya sahani; aliinua kwa vidole viwili na kuisogeza karibu na macho yake huku akiigeuzageuza.
Pumzi ikambana Kino kwa shauku, majirani zake nao vilevile. Minong’ono ilisikika kati yao, “Yupo kuikagua-bado hajataja bei-bado hawajakubaliana bei.”
Mlanguzi yule akairudisha lulu kwenye sinia, na akaigusagusa kwa kidole kama vile kuinyanyapaa, kisha akaonyesha tabasamu la huzuni na dharau.
“Samahani rafiki,” akasema huku akibinua mabega.
“Ni lulu ya thamani sana,” alisema Kino.
Dalali yule akaizungushazungusha tena lulu ile, kisha akasema. “Umewahi kusikia juu ya dhahabu ya mpumbavu? Lulu hii ni kama dhahabu ya mpumbavu. Ni kubwa mno. Nani atainunua? Hakuna soko kwa lulu kama hii. Ni ya kustaajabia tu. Samahani sana. Ulifikiri ni kitu cha thamani, lakini ni kitu cha kustaajabia tu.”
Sasa jasho likamtoka Kino usoni kwa wasiwasi. “Hakuna lulu kama hii duniani,” alisema kwa sauti. “Hakuna aliyewahi kuona lulu kama hii.”
“Sivyo hata kidogo,” alisema dalali. “Lulu hii ni kubwa na si bora. Kwaajili ya kustaajabia au maonyesho inafaa; pengine baadhi ya majumba ya makumbusho wanaweza kuichukua na kuitunza sehemu ya makombe ya baharini. Labda naweza kukupa peso elfu moja tu.”
Uso wa Kino ukawa mwekundu kwa hasira. “Ina thamani ya peso elfu hamsini, najua bei yake, unataka kunitapeli.”
Dalali akasikia sauti ya umati ukiguna waliposikia bei aliyotaja. Na akaingiwa na uoga kidogo.
“Usinilaumu mimi,” alisema haraka. Mimi ni dalali ni mkadiria bei tu. Waulize wengine. Nenda kawaonyeshe lulu yako ofisini mwao-au tuwaite waje hapa ili ujionee mwenyewe kwamba hakuna njama yoyote. Kijana,” alimwita kijakazi wake. “Nenda kamwite fulani na fulani. Waambie wafike hapa, lakini usiwaambie kwanini. Waambie tu ninataka kuwaona.” Hapo alitoa sarafu nyingine kutoka kabatini na kuanza kuizungusha vidoleni mwake.
Majirani wa Kino walinong’ona kati yao. Walikuwa na wasiwasi kuwa kitu kama hiki kitatokea. Lulu ilikuwa ni kubwa lakini ilikuwa na rangi ya tofauti na zingine. Walikuwa na mashaka nayo toka walipoiona kwa mara ya kwanza. Hata hivyo walionelea kuwa peso elfu moja si haba. Kwa mtu maskini zilikuwa ni pesa nyingi. Jana yake tu Kino alikuwa hana chochote, peso elfu moja ni nyingi.
Lakini Kino akibaki imara. Aliona hatima yake; hatima mbaya ikimnyemelea, mbwa mwitu wakimzunguka, ndege wala mizoga wakimzengea. Alihisi uovu ukimzunguka na kumtanda, na hakua na jinsi ya kujisaidia. Alisikia muziki wa uovu masikioni mwake.
Umati pale mlangoni ulisogea pembeni na kuwaruhusu wanunuzi watatu wa lulu kuingia. Na kisha kukawa kimya kabisa, watu waliogopa wasije wakashindwa kusikia yaliyoongelewa au kuona ishara. Kino alikuwa kimya na makini kabisa. Alihisi kuguswa mgongoni, alipogeuka akakutana na macho ya Juana. Akipogeuka kutazama mbele nguvu mpya ilikuwa imemuingia.
Walanguzi wale walisimama wima, hawakuangaliana wala kuiangalia lulu ile. Yule aliyewaita akaanza kwa kusema, “Nimethaminisha thamani ya lulu hii, lakini mmiliki wake anaona kama nataka kumpunja. Naomba nanyi muichunguze na kutoa bei yenu.” Hapo akamgeukia Kino na kumwambia, “Umeona mwenyewe, sijataja kiasi cha bei nilichoithaminisha.”
Mnunuzi wa kwanza akajidai kuwa ndiyo anaiona lulu kwa mara ya kwanza. Aliichukua na kuizungusha-zungusha vidoleni mwake, na kisha kwa dharau akairudisha kwenye sinia.
“Mimi nitoe kwenye hili suala,” alisema kikauzu. “Siwezi kununua. Siihitaji. Hii siyo lulu-ni dubwasha tu.” Alimaliza kusema na kukunja midomo.
Mlanguzi wa pili, mtu mmoja mfupi mwenye aibu-aibu; akaichukua lulu na kuichunguza kwa makini. Alitoa lensi mfukoni mwake na kuichunguza lulu ile kwa kutumia lensi. Hapo akacheka kicheko cha dharau na kusema.
“Kuna lulu zilizotengenezwa kwa saruji na ni bora kuliko hii. Nafahmu lulu za namna hii. Si lulu bora, itapoteza rangi yake na kumegukameguka baada ya miezi michache tu. Angalia mwenyewe-.” Alisema huku akimpatia Kino lensi na kumuelekeza jinsi ya kutumia. Kino; ambaye hajawahi kuiona lulu kupitia lensi ya kukuza, alishangaa kuona sura ya ajabu ya lulu.
Mlanguzi wa tatu aliichukua lulu kutoka kwa Kino. “Nina mteja ambaye anapendelea vitu kama hivi,” alisema. “Nitakupatia peso mia tano, pengine labda nitaweza kumuuzia mteja wangu kwa peso kama mia sita hivi.”
Kino akainyakua lulu yake haraka kutoka mikononi mwa mlanguzi yule. Alifunga kwenye kipande kile cha ngozi ya swala na kukiweka mfukoni.
Yule mlanguzi mwenye ofisi akasema, “Nafahamu kuwa nitaonekana mpumbavu, lakini bei yangu bado ipo mezani. Peso elfu moja-unafanya nini?” alimuuliza Kino alipoona anaweka lulu yake mfukoni.
“Mnataka kunitapeli,” alisema Kino kwa kufoka. “Sitauza lulu yangu hapa. Ikibidi kwenda makao makuu nitakwenda.”
Hapo walanguzi wale waliangaliana kwa wasiawasi. Walijua kuwa hila zao zimepita kiasi; walijua kuwa wataadhibiwa iwapo watashindwa kuipata lulu ile, yule mlanguzi mwenye ofisi akasema haraka, “Naweza kukuongezea mpaka kufikia peso elfu moja na mia tano.”
Lakini Kino hata hakusikia, akaanza kupenya katika ya umati kuondoka, hasira imemjaa, hata mwendo wake ulikuwa wa hasira. Juana alimfuata nyuma, akilazimika kukimbia polepole kuendana naye.
Jioni ilipofika, majirani wa Kino walikuwa wamekaa ndani ya nyumba zao wakila mikate ya mahindi na maharage huku wakijadiliana yaliyotokea asubuhi. Hawakujua wasimamie lipi. Waliona kuwa ilikuwa ni lulu nzuri, lakini hata wao hawajawahi kuona lulu kama ile, na bila shaka walanguzi wale wanajua vema maswala ya lulu na thamani yake kuliko wao. “Na kumbuka kwamba wale walanguzi hawakuzungumza hili suala kati yao, lakini kila mmoja alifahamu kuwa lulu ile haina thamani yoyote.”
“Lakini labda walipangana mapema”
“Kama ni hivyo basi sote tumekuwa tukitapeliwa maisha yetu yote.”
Wengine wakasema kuwa pengine ilikuwa ni jambo jema kwa Kino kuchukua zile peso elfu moja na miatano. Hiyo ni pesa nyingi, nyingi kuliko alizowahi kuona. Pengine Kino anakuwa mjinga na kichwa ngumu. Fikiria akienda makao makuu na kukuta hakuna mnunuzi aliyetayari kununua lulu yake?
Mtu mmoja muoga-muoga, “Na sasa kwa sababu amewakatalia walanguzi, hawatataka tena kufanya naye biashara. Pengine Kino amejikata kichwa na kujiharibia.”
Wengine wakasema, Kino ni mtu jasiri na shupavu; yupo sahihi kufanya alivyofanya. Na sisi tunaweza kufaidika na ujasiri wake. Watu hawa ni wale waliokuwa wakisifa kitendo cha Kino.
Ndani ya nyumba yake Kino alichuchumaa kwenye mkeka wake wa kulalia akitafakari. Alikuwa tayari ameifukia lulu yake kwenye figa moja. Alikuwa ametulia akishangaa jinsi mkeka wake ulivyosukwa. Ndani yake alikuwa amejawa na uoga. Katika maisha yake hajawahi kuwa mbali na nyumbani. Aliogopa dubwana linaloitwa makao makuu. Lilikuwa liko mbali kuvuka maji na milima, umbali wa maili zaidi ya elfu moja na kila maili ikiwa na kila namna ya hatari. Lakini ulimwengu wa zamani wa Kino ulikuwa umepotea, hakuwa na budi kuukabili ulimwengu mpya. Mipango yake ilikuwa ni halisi, na hakuna cha kuiharibu, alijisemea “Nitakwenda,” na hapo jambo hilo likawa halisi. Kuwa na nia ya safari na kuisema ilikuwa ni kwenda nusu ya safari.
Juana alimuangalia alipokuwa akifukia lulu yake. Baada ya muda akatengeneza keki za mahindi kwaajili ya chakula cha usiku.
Juan Tomas alifika nyumbani kwa Kino na kuchuchumaa pembeni yake, walitulia kimya bila kusemezana kwa kitambo kirefu, mwishowe Kino akasema.
“Unafikiri ningefanya nini? Wale ni matapeli.”
Juana Tomas alitikisa kichwa chake tu. Yeye ndiye alikuwa mkubwa na kino alikuwa akimtegemea kwa ushauri. “Si rahisi kujua,” alisema Juan Tomas. “Tunachojua ni kuwa tumekuwa tukidanganywa toka tunazaliwa, gadi tunapouziwa majeneza yetu kwa bei ya kitapeli. Lakini pamoja na yote, bado tunaishi. Hujasimama dhidi ya walanguzi tu, bali mfumo mzima. Juu ya utamaduni wote. Nina wasiwasi juu yako.”
“Kitu gani cha kunitisha zaidi ya njaa?” alisema Kino.
Lakini Juan Tomas alitikisa kichwa polepole. “Wote tunaogopa hilo. Lakini fikiria labda upo sahihi. Kwamba lulu yako ni kweli ina thamani kubwa, unafikiri huo ndiyo utakuwa mwisho wa haya?”
“Unamaanisha nini?”
“Sifahamu.” Juana Tomasa alisema, “Lakini nina wasiwasi juu yako. Ni nchi mpya unayotembea, nawe hufahamu njia.”
“Nitakwenda. Nitakwenda haraka iwezekanavyo,” alisema Kino.
“Sina pingamizi na hilo, “ alisema Juan Tomas. “Wasiwasi wangu ni iwapo utakuta hali ya makao makuu ni tofauti na hapa. Hapa walau una rafiki zako na mimi kaka yako, huko hautakuwa na mtu yeyote.”
“Sasa nifanyaje?” alisema Kino….mwanangu anatakiwa kupata fursa. Na hicho ndicho wanachotaka kunipora. Rafiki zangu watanilinda.”
“Watakulinda iwapo kufanya hivyo hakuhatarishi maisha yao au hali zao.” alisema Juan Tomas. Hapo alisimama na kusema, “Mungu awe nawe katika safari yako.”
Kino naye akajibu, “Mungu awe nawe pia,” lakini hakuinua uso kumuangalia kaka yake.
Baada ya kaka yake kuondoka Kino alibaki amekaa kichovu kwenye mkeka wake kwa muda mrefu akitafakari. Ilionekana kama njia zote mbele yake zimezibwa. Kichwani mwake ni muziki wa adui tu ndiyo ulisikika. Hisia zake zilikuwa chonjo lakini akili yake ilikuwa mbali kwa mawazo.
Juana alikuwa na wasiwasi juu ya hali ya Kino, lakini alimfahamu vizuri. Alijua kuwa njia pekee ya kumsaidia ni kukaa kimya na kuwa karibu naye. Alimbeba Koyotito mikononi na kumuimbia ili kufukuza mkosi, sauti yake ilikuwa ya kishupavu, ikikabiliana na muziki wa uovu.
Kino hakuinuka pale wala kudai chakula cha usiku. Juana alijua kuwa ataulizia iwapo atahitaji. Macho ya Kino yalionyesha mashaka makubwa aliyokuwa nayo. Alihisi kama kuna kitu kiovu nje ya nyumba yake kikimnyemeloea. Kikimwita kupambana naye. Alishika kisu chake kuhakikisha kama kipo na kisha akaelekea mlangoni. Juana alitaka kumzuia lakini sauti haikumtoka, aliishia tu kuinua mkono. Kino alisimama kidogo mlangoni na kisha akatoka nje gizani. Ghafla Juana akasikia purukushani kutoka nje, alishikwa na uoga mkubwa lakini ujasiri ukamuingia haraka. Akamuweka Koyotito chini na akachukua jiwe moja la mafiga na kukimbia nje. Lakini purukushani zilikuwa zimeshatulia, Kino alikuwa amelala chini akijaribu kuinuka, hakukuwa na mtu mwingine. Juana aliachia jiwe lake na kuzungusha mikono yake kwa Kino kumsaidia kuinuka. Alimshikilia kwenda ndani. Damu ilimvuja Kino kutoka kichwani na alikuwa na jeraha kubwa la kukatwa kutoka kwenye sikio hadi kidevuni. Ilionekana kuwa Kino hajitambui vizuri, alitingisha kichwa chake huku na huku, nguo ake zilikuwa zimechanika-chanika. Juana alimlaza mkekani na kumfuta damu iliyoanza kuganda usoni mwake kwa sketi. Baada ya hayo akamletea kikombe cha Pulque na kumuuliza:
“Ni nani?”
“Sijui,sijamuona.” Alijibu Kino.
Juana akaleta mtungi wa maji na kumuosha jeraha lililokuwa usoni pake huku akimkazia macho usoni.
“Kino mume wangu,” alisema Juana huku machozi yakimlengalenga. “Kino unanisikia?”
“Nakusikia,”
“Kino hii lulu ni mkosi. Tuiharibu kabla haijatudhuru. Tuiponde kwenye mawe. Au tuitupe baharini ilikotoka. Kino hii ni mkosi, mkosi kabisa!”
Alipokuwa akiongea hayo udhaifu ukamuisha Kino. Macho yake yaliwaka na misuli ikamkaza.
“Hapana,” alisema Kino. “Nitapambana hadi mwisho. Na nitashinda. Hii ndiyo fursa yetu, tutaitumia.” Alisema hayo huku akipiga ngumi mkeka wa kulalia. “Hakuna atakayetupora bahati yetu,”. Hapo macho yake yakaonyesha upole, akamshika Juana begani . “Niamini, mimi ni mwanaume.”
Juana akasema, “Kino, nina wasiwasi kuwa hata wanaume wanaweza kuuwawa. Tuitupe baharini.”
“Nyamaza,” alifoka Kino. “Mimi ni mwanaume, nyamaza.” Hapo Juana akakaa kimya, maana Kino aliongea kwa amri. “Mwanga wa kwanza ukitoka tu tutaanza safari. Unaogopa kwenda na mimi?”
“Hapana mume wangu.”
Hapo macho ya Kino yakaonyesha upole, alimshika mke wake mashavuni na kusema, “Basi na tulale kidogo.”