Wawindaji wale walipiga kelele kama mbwa mwenye shangwe ya kugundua mnyama alipo. Kino akashika kisu chake mkononi barabara akiwa tayari kwa lolote. Alijua alichotakiwa kufanya; kama wawindaji wale wakigundua sehemu aliyofagia nyayo atatakiwa kumrukia mpanda-farasi, kumuua na kuchukua bunduki yake. Hiyo ndiyo nafasi pekee ya kujiokoa aliyokuwa nayo. Walipozidi kukaribia ndivyo Kino alivyozidi kujiweka tayari, akijiandaa kuruka bila wao kutegemea.
Kwenye maficho yao Juana akasikia sauti ya kwato za farasi, na wakati huohuo Koyotito akatoa kelele za kugumia. Haraka Juana akamchukua na kufunga kwa mtandio kisha akampa ziwa anyone, Koyotito akanyamaza.
Wawindaji walipokaribia Kino aliweza kuona miguu yao tu, na miguuu ya farasi. Wawindaji walisimama kwenye lile eneo alilofagia, walilichunguza huku mpanda-farasi akiwa kasimama pembeni. Farasi alipiga kelele kama ya chafya. Wawindaji wakageuka kumuangalia farasi, wakiangalia masikio yake.
Kino akazidi kutulia kimya, alibana pumzi, misuli yake ikazidi kukaza na jasho likamtiririka usoni. Wawindaji wale walisimamam pale kwa muda mrefu, kisha wakaoanza kusogea mbele wakichunguza ardhini. Mpanda-farasi aliwafuata nyuma. Kino alijua kwamba watarudi, watachunguza huku na huko lakini mwishowe watarudi pale alipofagia nyayo.
Alirudi kwenye maficho yao. Safari hii hata hakujihangaisha kuficha alama zake, alikuwa ameacha alama nyingi asizoweza kuzificha. Pale jiwe lilikuwa limeng’oka, hapa matawi yamekatika, kule eneo limevurugwavurugwa. Na zaidi ya yote, alikuwa amehamaki, kitu kilichokuwa kichwani mwake ni kukimbia tu. Alijua kuwa wawindaji wale watayapata mapito yake, na alijua hakuna njia ya kujiokoa zaidi ya kukimbia. Juana alimuangalia mume wangu kwa uso uliojaa maswali.
“Wawindaji, tuondoke haraka.” Alisema Kino.
Lakini ghafla ghafla huzuni na kukata tamaa vikamjaaa Kino. Akasema, “Pengine labda ni vyema nikajipeleka wanikamate.”
Haraka juana akasimama na kusema, “Unafikiri watakurudisha ukiwa hai ukawatuhumu kukupora lulu? Tuondoke haraka.”
Lakini Kino akawa anasita. Juana akasema tena, “Unafikiri wakikukamata wataniacha mimi hai? Unafikiri watamuacha mtoto hai?”
Hoja za Juana zikafanya akili na ujasiri vimrudie. Akauma midomo na macho yake yakawa makali. “Twende. Tutaelekea milimani, pengine tutawapoteza huko.”
Haraka haraka, akakusanya kibuyu, mkoba mdogo walioweka vitu vyao; alivishika kwa mkono wa kushoto huku mkono wa kulia akiwa ameshika kisu chake kikubwa. Alifungua vichaka ili Juana aweze kupita na kisha wakaanza safari kuelekea magharibi, kwenye milima mirefu ya mawe. Walikimbia kidogokidogo kupita kwenye vichaka vifupi. Kino hata hakuhangaika kujaribu kuficha alama za walimopita, walikuwa wamehamaki. Walipokuwa wanakimbia waling’oa mawe hapa na pale na kuangusha majani ya miti. Jua la utosi lilipiga nchi bila huruma. Mbele yao ilikuwepo milima ya mawe, ikiwa na kilele kimesimama wima. Kama wanyama wanaokimbizwa hufanya; Kino alikuwa akikimbia kuelekea kwenye muinuko.
Nchi hii ilikuwa ni kame isiyo na maji, ilijaa mimea ya miba ambayo ilikuwa na uwezo wa kutunza maji, ikiwa na mizizi mirefu iliyoweza kwenda chini sana kusaka maji. Ardhi yake ilikuwa si udongo bali mwamba. Nyasi chache dhaifu zilimea kwenye nyufa za mwamba huu. Vyura wadogo walikuwa wakishangaa familia ya Kino ilipokuwa ikipita na mara chache waliona sungura walioshtushwa na ujio wao wakiruka na kujificha. Jua kali lilikuwa likipiga jangwa hili, mbele yao mlima ule ulionekana kama ni eneo salama na baridi..
Kino alizidi kukaza mwendo. Alijua kitakachotokea. Alifahamu kuwa baada ya mwendo kidogo wawindaji watatambua kuwa wamepotea njia, na watarudi wakiitafuta kwa makini. Muda si mrefu watayapata maficho yao, na kutoka hapo haitakuwa kazi tena kuwafuatilia. Mawe yaliyong’olewa barabarani, majani ya miti yaliyoangushw, matawi yaliyoinama na maeneo ambayo yamekwanguliwa baada ya mguu kuteleza yataonyesha kila kitu. Akilini Kino aliweza kuwaona wawindaji wakifuata alama walizopita kwa shauku huku mpanda-farasi akifuata nyuma. Alifahamu kuwa Mpanda-farasi ndiye atakamilisha kazi kwa bunduki yake, hatathubutu kuwarudisha mjini. Muziki wa uovu ukazidi kuimba kwa sauti kubwa masikioni mwa Kino. Uliimba pamoja na sauti za nchi inayopigwa joto na kelele za nyoka wa jangwani.
Muinuko ukazidi kuwa mkali na mawe yakazidi kuwa makubwa. Lakini sasa umbali wake na wa windaji ulikuwa mkubwa hivyo wakapumzika. Alipanda juu ya jiwe kubwa na kuangalia alikotoka. Hakuweza kuwaona wawindaji, hata mpanda-farasi hakuonekana. Juana yeye alikaa kwenye kivuli cha jiwe lile na kuanza kumnywesha Koyotito maji; ambaye kwa kiu aliyokuwa nayo alikunywa kwa pupa. Japo Juana alikuwa amechoka lakini macho yake yalionyesha nuru. Kino akashuka, Juana akamuona akimuangalia miguuni ambapo alikuwa na majeraha kutokana na mawe na vichaka hapa na pale. Alifunika miguu yake kwa sketi yake haraka na kumpatia Kino kibuyu cha maji lakini Kino alitikisa kichwa kukataa na kulamba midomo yake mikavu kwa ulimi.
“Juana,” alianza kusema Kino. “Wewe utajificha. Mimi nitawaongoza, na wakifika mbali kunifuatilia wewe utaondoka kuelekea kaskazini. Nenda Loreto au Santa Rosalia. Kama nikiweza kuwatoroka nitakufuata huko. Hii ndiyo njia pekee ya kuwa salama.”
Juana alimuangalia Kino machoni kama vile anamshangaa, kisha kwa msisitizo akasema, “Hapana, tutakwenda na wewe.”
“Nikiwa peke yangu ninaweza kwenda kasi zaidi. Ukifuatana nami utamuweka mtoto hatarini.”
“Hapana,” aliendelea kukataa Juana.
“Itakubidi ufanye hivyo. Ni jambo la busara na mimi nimeamua hivyo,” akasema Kino
“Hapana,” akajibu Juana.
Kino akamuangalia mke wake usoni lakini alikutana na uso shupavu. Macho ya Juana yaling’aa. Kino akaishia kutingisha mabega tu asijue la kufanya, lakini mke wake alikuwa amempa nguvu. Walipoanza safari tena haikuwa kwa kukimbia kwa hamaki kama hapo mara ya kwanza.
Kadri walivyokuwa wakizidi kupanda ndivyo nchi nayo ilivyozidi kubadilika, tena haraka. Sasa miamba mikubwa ilichomoza ikiwa na makorongo marefu kati. Kino alijitahidi kutembea juu ya miamba kadri alivyoweza, ilikuwa si rahisi kuacha alama juu ya miamba hivyo alijua hilo litawachelewesha wale wawindaji kuyapata mapito yake. Hakupanda mlima moja kwa moja bali alitembea zigi-zag. Mara nyingine alielekea kusini na kuacha alama na kisha kueleka mlimani tena, akipita juu ya mawe bila kuacha alama. Mlima ulizidi kuwa mkali, alivuta pumzi kwa shida kadri alivyokuwa akipanda.
Jua lilianza kuzama upande mwingine wa mlima ule. Kino akaanza kuelekea kwenye korongo moja lililokuwa limefunga kwa mimea. Alijua kuwa kama kuna sehemu ina maji basi itakuwa ni pale penye mimea iliyofungamana. Na kama kuna njia rahisi ya kuvuka korongo lile basi itakuwa ni pale pia. Kulikuwa na hatari kwa sababu wawindaji nao watatambua hilo, lakini alikuwa ameishiwa maji hivyo wazo hilo hakulizingatia sana. Jua lilipokuwa likizama, Juana na Kino walikuwa wakijikongoja kuelekea kwenye korongo lile kichovu.
Upande wa juu wa korongo lile kulikuwa na chemichemi ndogo ya maji ikibubujika. Chanzo chake ilikuwa ni theluji iliyokuwa sehemu isiyofikiwa na jua mlimani. Ilikuwa ikitoa maji baridi na masafi karibu muda wote, ni muda mfupi tu wa mwaka ilikuwa inakauka. Nyakati za mvua iliweza kuwa mapromoko makubwa ya maji yakishuka korongoni. Ilishuka na kutengeneza kidimbwi; nacho baada ya kujaa maji yakaporomokea kwenye kidimbwi kingine, kijito kilienda kwa mtindo huu kama ngazi hadi kilipopotea kwenye makorongo. Wanyama walitoka kila kona ya nyika ile kuja kunywa maji kwenye kijito hiki. Kondoo mwitu, puma, swala, panya na wengine wengi. Ndege nao walitoka sehemu mbalimbali kuja kweny kijito hiki. Pembeni ya kijito hiki mimea mbalimbali ilijishikiza popote ilipopata nafasi; zabibu-pori, michikichi pori na mingine mingi. Ndani ya vidimbwi walikuwemo vyura, minyooo na viumbe wengine, kitu chochote kilichopenda maji kilikuja mahali hapa. Paka waliwinda mahali hapa, walichafua maji kwa manyoya ya ndege waliowaua na kwa damu. Madimbwi haya madogo yalikuwa sehemu ya uhai sababu ya maji, na sehemu ya kifo sababu ya maji.
Wakati Juana na Kino wanafika sehemu ya maji jua lilikuwa limezama upande wa pili wa milima. Kutoka eneo hilo waliweza kuona sehemu kubwa ya jangwa hadi kwenye ghuba ya bluu iliyokuwa mbali mashariki. Walifika kwenye kidimbwi wakiwa wamechoka sana, Juana alipiga magoti na kumuosha Koyotito uso, kisha akajaza kibuyu maji na kumnywesha. Mtoto alikuwa amechoka sana hivyo alikuwa anasumbua sana, hadi Juana alipompatia ziwa ndipo akatulia. Kino alikunywa maji kidimbwini kwa muda mrefu, kisha akakaa kwa kuridhika akimuangalia Juana akimlisha mtoto. Baada ya kupumzika kidogo akaenda kwenye sehemu ambayo kijito kilikuwa kinaporomoka kwenda chini na kuanza kuangalia uwanda wa chini kwa makini. Macho yake yakaona kitu na akabaki amekikodolea. Mbali bondeni aliweza kuwaona wale wawindaji wawili; walionekana kama nukta tu au sisimizi, na nyuma yao alionekana sisimizi mkubwa zaidi.
Juana alikuwa akimuangalia mume wake na akaona jinsi mgongo wake ulivyojikaza.
“Wako umbali gani?” aliuliza
“Kufika jioni watakuwa hapa,” alijibu Kino.
“Inabidi tuelekee magharibi,” alisema Kino huku akiangalia upande ule yanakotokea maji. Aliona mapango yaliyotengenezwa na maji. Alivua ndala zake na kupamba kuyaelekea, alipoyafikia aliona kuwa yana ukubwa wa futi kadhaa tu, yakiwa na mteremko kidogo kuelekea ndani. Kino aliingia kwenye pango kubwa, aliona kuwa mtu akiwa nje hataweza kumuona. Alirudi haraka kwa Juana.
“Tukajifiche mule pangoni. Pengine hawatatuona.” Alimwambia mkewe.