Hadithi: Ndoto ya Alinacha

Hadithi: Ndoto ya Alinacha

Lycaon pictus

JF-Expert Member
Joined
Jan 31, 2021
Posts
9,189
Reaction score
16,128
Pia unaweza kuisoma hadithi hii na nyingine nyingi bure ndani ya maktaba app(by pictus). install toka playstore.

KISA CHA NDUGUYE KINYOZI WA TANO​

MIMI ni Kinyozi na nina ndugu sita. Hiki ni kisa cha ndugu yangu wa tano, Alnacha. Katika siku alizokuwa hai baba yetu, Alnacha alikuwa mvivu sana, hata kule kufanya kazi ya kujipatia chakula chake mwenyewe kulimshinda ikawa kila jioni kuomba, na vile alivyokuwa akipewa alikuwa akiviweka ili ale siku ya pili yake. Hata baba yetu alipokufa kwa uzee, aliacha reale mia saba, tukagawana, na kila mtoto alıpata mia mia. Alnacha, ambaye katika maisha yake yote hakupata kuwa na fedha nyingi kama zile, akawa anahangaika nazo asijue la kuzifanya. Mwishowe akaona ni afadhali anunue vioo, na chupa, na vitu vinginevyo vya namna kama hiyo.

Alipokwisha kununua vitu vyake akatoka kwenda kutafuta duka dogo lililo zuri, akakaa kitako mbele ya mlango wa duka lake ila vyombo vyake ameviweka ndani ya kapu wazi mbele yake akingojea wanunuzi wanaopita njia.

Basi akakaa katika hali hiyo huku amelikodolea macho lile kapu, lakini mawazo yake yalikuwa mbali kabisa. Na bila ya kufahamu mwenyewe akaanza kusema kwa sauti kuu, hata yule mshoni alayekuwa na duka mlango wa pili wa duka lake, alimsikia waziwazi aliyokuwa akisema. Alinacha alisema hivi: Kapu hili limenigharimu reale 100, na hizo ndizo zote nilizokuwa nazo. Na maadam sasa nauza rejareja hivi vilivyomo kapuni huenda nikapata reale 200, na katika hizi mia mbili nitanunua tena vioo ambavyo vitanizalia reale 400, na kwa njia hii muda wa siku chache nitakuwa na reale 4000 ambazo zitajiongeza zenyewe mara mbili kwa urahisi. Hata hapo nitakapopata reale 10,000 (elfu Kumi), nitaacha biashara ya vioo niwe mwuzaji wa jonari, na wakati wangu wote utakuwa katika biashara za lulu na almasi na mawe mengineyo ya thamani.

Mwisho, kama nikishatosheka na utajiri wangu, nitanunua nyumba nzuri sana ya shamba, kisha ninunue na farasi wengi halafu nitaishi Maisha ya raha na kuwakaribisha rafiki zangu katika karamu zangu zote nitawaita wapigaji vinanda na pia wachezaji kutoka miji ya karibu, ili waje kuwafurahisha Rafiki zangu. Walakini sitaitupa kazi ya biashara mpaka nipate mali nyingi kama reale laki moja za fedha, na hapo niwapo mtu wa kuheshimiwa sana nitamposa binti ya waziri mkuu nitamwambia babaake kuwa nimesikia habari zinazopendeza juu ya sifa za uzuri na akili ya binti yake. Na kwa hivyo siku ya harusi yetu nitakuwa tayari kulipa reale elfu za dhahabu na kama waziri akiyakataa haya ninayokusudia (lakini naona haitakua vigumu) nitamshika ndevu zake nimvute mpaka nyumbani kwangu.
 
Lakini hapo nitakapooa, nitamwekea binti yake matoashi kumi walio mahodari kumtumikia. Halafu nitavaa joho langu zuri lenye katarizwa uzi wa zari nyekundu, nipande farasi wangu mwenye tandiko la dhahabu safi na kanda za hatamu yake ziking’aa kwa lulu na almasi huku nikifuatwa na kikosi cha watumishi. Nitakwenda mwenyewe kwenye jumba la waziri mkuu, na wakati nikipita watu wanainamisha macho tena wanisujudie. Hata nikifika kwenye ngazi ya jumba la waziri mkuu nitashuka juu ya farasi, na watumishi wangu watashuka kwa safu upande wa kulia na wa kushoto, nami nitapanda ngazi za jumba lake na mwisho wake nitamkuta waziri mkuu ananingojea kunipokea. Hapo atanikumbatia kwa kuwa ni mkwewe, tena atanipa na kiti chake na yeye mwenyewe atajiweka chini yangu. Haya yakishafanyika watumishi wangu wawili wataingia ndani, hata kila mmoja amechukua kifuko cha reale eflu za dhahabu. Kimoja nitampa yeye nimwambie ‘Hizi hapa reale elfu za mahari ya binti yako, na hizi,’hali naendelea katika kusema na huku nimeshika kifuko cha pili.’Reale elfu zingine za kukuonyesha kuwa mimi ni mtu mwenye utu.’ Baada ya yeye kuuona ukarimu kama ule, hata hiyo dunia haitanena neno jingine.

Baadae nitarudi kwangu kwa fahari ile ile niliyokwenda nayo, na mke wangu atamleta jemedari wa kunisindikiza kwa vile nilivyo kwenda kumtembelea baba ake, na huyo jemedari nitamvika heshima kwa kumpa vao la mali na zawadi nzuri. Lakini kama yeye akiniletea zawadi, hata moja, nitaikataa nimfukuze aliyeileta.

Tena sitamwachilia mke wangu kutoka chumbani mwake kwa udhuru wowote bila ya ruhusa yangu.

Hakuna neno litakalokuwa thabiti kama langu na siku zote nitatahadhari katika kuvaa mavazi: kwa kadiri inavyostahili cheo changu. Usiku tunapoingia vyumbani mwetu nitakaa mahali pa heshima, na sura zangu zitakuwa za haiba, tena nitakuwa nikitazama mbele yangu sawasawa, na mke wangu aliye mzuri kama mwezi arobataashara, anaposimama kwa unyenyekevu mbele ya kiti changu nitajifanya kama simwoni. Halafu watumishi wake wataniambia: ‘Ewe, Bwana wa mabwana, mkeo aliye mjakazi wako amesimama mbele yako kungojea umwangalie. Kweli twajua kwamba amekutia uchungu sana hata hutaki kumwangalia, lakini mhurumie kwani amechoka kwa kusimama sana. Na hivi twakusihi, umwambie akae.’ Ama kwa kweli sitaonyesha hata dalili ya kusikiliza maneno yao, na kwa hivyo wataona haya sana. Basi kisha watajitupa chini ya miguu yangu kwa vilio na mwisho wake nitainua kichwa changu nimtupie jicho la kejeli halafu nirudie hali yangu ile ile ya kwanza. Watumishi wake watadhani kuwa labda sikupendezewa na nguo za mke wangu na kwa hivyo watamwondoa kwenda kumvisha nguo nzuri zaidi, na mimi kwa upande wangu nitaondoka kwenda kubadili zile nilizovaa nivae zingine zilizo nzuri zaidi. Basi wakiisha kumvisha nguo zake watarudi tena, lakini safari hii itachukua kitambo sana kabla hawajaweza kunifanya nimwangalie mke wangu.
 
Lakini mambo haya yote ni heri yaanze siku ile ile ya harusi yangu, maana nakusudia kuendelea na mengi zaidi katika hizo siku za mbele za maisha yetu.

Siku ya pili yake atamshtakia mamake kwa haya aliyotendewa na mashtaka hayo yatafanya moyo wangu kujaa furaha. Mamaake atakuja kunitafuta, na akiniona, ataniamkia kwa kunibusu mikono yangu kwa heshima tupu, aseme: ‘Bwana wangu (maana hatothubutu kujitia katika hatari ya kuniudhi kwa kuniita mkwe’ Kama tunajuana sana) nakusihi usikatae kumwangalia au kumkaribia binti yangu, kwani haja yake ni kukupendeza tu na anakupenda kwa moyo wake wote.’

Lakini sitayasikiliza maneno ya mkwe wangu kama vile nilivyoyasikiliza maneno ya wale watumishi. Atanisihi tena nimsikilize maombi yake, na wakati huo atajitupa chini ya miguu yangu lakini yote ni bure. Halafu atatwaa bilauri aitie mvinyo ampe binti yake akimwambia: ‘Twaa umpelekee mwenyewe mmeo hawezi kuwa mkatili hivyo hata akatae kupokea kila anachopewa.’ Basi mke wangu ataipokea bilauri anipe kwa kutetemeka na machozi yakimchiririka machoni; lakini mimi sitamwangalia kamwe, ila nitageuka niangalie kando upande mwingine. Hivi itamfanya alie zaidi na hali ile bilauri kaishika mkononi mwake, aseme: ‘Mume wangu nikupendae sana, sitaacha kukusihi mpaka unifanyie jamala upokee unywe.’ Lakini maneno hayo yatanigadhibisha. Ndipo hapo nitakapompiga jicho la hasira nimvurumishie ngumi ya shavu na teke la nguvu, hata apepesuke kutoka chumbani akaangukie kitanda kidogo cha ukumbini.’

Ama kwa hakika, ndugu yangu alishughulika sana kwa mawazo yake, hata akatupa teke kweli na kupiga lile kapu lake la vioo.

Yule jirani yake mshoni, aliyekuwa akimsikiliza maneno yake alipoona vile, akaangua kicheko akacheka sana. Akamwambia, 'E, baa wee! Hata haya huna unamtenda hivyo mkeo naye hakukosa kitu? Bila ya shaka wewe mtu mbaya kwani hata machozi yake na maombi yake hayakukutia huruma. Na laiti kama mimi ningekuwa waziri mkuu, ningeamrisha upigwe mijeledi mia, kisha utembezwe mjini huku mpigaji mbiu, akikunadishia uovu wako.’

Sasa ile hasara ya uchumi wake wote, ikamtia akili ndugu yangu akaona kuwa hasara ile yote imetokea kwa ajili ya majisifu yake yasiyo maana, ikawa kurarua nguo zake na kung’oa nywele zake huku akilia kwa uchungu mno, hata wale watu wapitao njia walisimama kumsikiliza. Kwani siku hiyo ilikuwa Ijumaa, na watu wanaopita njia walikuwa wengi mno zaidi ya siku zote. Wengine walimsikitikia Alnacha, lakini wengine walimcheka tu, na yale majivuno yake yote aliyokuwa nayo yalimtoka pamoja na kapu lake la vioo, akawa analia kwa upumbavu wake.
 
1642817370516.png
 
Back
Top Bottom