Hadithi: Penzi la Kiziwi

Hadithi: Penzi la Kiziwi

Episode Four

Nilitamani asubuhi ipambazuke ili nikamilishe kile ambacho nimekipanga. Basi usiku ulikuwa mrefu sana, sikuacha kuwaza namna gani nitamuingia? Namna gani nitazungumza naye? Namna gani nitampa sikio.

Mungu si Athumani, kile ambacho nilikuwa nakisubiri sasa kikatia nanga. Kwa bahati nzuri asubuhi ilikuwa imepambazuka na anga ikang’aa vyema, nami nikasema hakuna muda wa kusubiri napaswa kumtafuta Jane kwa namna yoyote ile. Kwanza nikaenda kuongea na Judy ambaye nilimwambia kwamba kuna sehemu nitaenda.

Nilimfahamu Judy hakuwa mtu wa maswali mengi sana ndio maana kwa siku hii nilimshirikisha lakini ajabu ni kwamba aliniuliza maswali yake. Nikachukia.
“Unaenda wapi?”
“Nimekuja kukuaga ili ujue nataka kuondoka”
“Sawa unaondoka, unaenda wapi?”
“Kuna sehemu tu, naenda mara moja halafu narudi”
“Okay, unarudi saa ngapi maana unahitajika na Baba baadaye kuna mambo anataka kuongea na wewe”
“Nitarudi muda wowote ila haiwezi kuwa usiku”
“Mmh! Sawa” alinielewa nami niliondoka.

Safari yangu ilienda kutua maeneo ya Nanenane, kwa bahati nzuri nilifanikiwa kumuona mpiga mbira akiwa amekaa katika gogo huku mbele yake kukiwa na kiroba ambacho aliweka karanga za kukaanga ambazo alikuwa anauza. Jane alikuwa amevaa gauni ambayo imechanika, kanda mbili ambazo zilikuwa na kitobo katika maeneo ya visigino huku nywele zikiwa timu timu.

Kwa mara ya kwanza katika maisha yangu nikaingiwa na huruma, sikuwahi kufanya hivi hapo kabla dhidi ya masikini. Lakini mbele ya binti huyu moyo wangu ulizididimia kwa muda kidogo. Wakati najiandaa kushuka katika gari, kuna mtu alikuja na kupiga teke karanga zake. Alikuwa ni mgambo nahisi maana aliongea kwa ukali mno.

Sikuona Jane akiwa anajaribu kumfukuza mtu yule, kwanza alimtazama na mwisho aliokota karanga na kusogeza kiroba eneo jingine kisha alipanga kama mwanzo na kuanza kuuza lakini macho yake yakauacha kumdondoka machozi. “Am sorry! Miss” nilijiambia ndani ya moyo wangu huku nikimwangalia yule mtu ambaye alikuwa mbali hivi sasa.

Basi nilishuka katika gari hadi karibu yake, nikachuchumaa na kumtazama usoni. Alikosa furaha, hakuwa na amani kabisa. Aliponiona uso wake ukaweka tabasamu lakini halikuwa lile ambalo nililiona siku za nyuma wakati nampatia pesa.
“Habari” nilimuuliza kwa makusudi ili kupima kama kweli anasikia ama lah? Nilichokutana nacho hakikuwa kingine bali ni kile ambacho ameniambia Anna kuwa Jane hasikii.

Sasa nilijikuta nikiwa njia panda mno, nilijikuta nikirudia kumsalimia zaidi ya mara tano lakini hakuna hata moja ambayo aliitikia. Naye alipoona nimemsalimia sana, alinigusa katika eneo la moyo kabla ya kupeleka mikono yake sikioni. Sijui hata alikuwa akimaanisha nini? Lakini niliona akibeba mbira yake na kuanza kupiga.

Watu ambao walikuwa wakipita barabarani sasa walisimama kumtazama. Jane alikuwa ni mtaalamu wa kupuliza mbira, alikuwa ni fundi na hakika Mungu alimpa kipaji cha kipekee sana. Upulizaji wake ulileta wateja mbalimbali ambao walianza kununua karanga zake. Lakini miongoni mwa wateja hao alikuja Baba pamoja na Mama ambao walisimamisha gari pembeni na kusogea hadi sehemu ile.
“Tuondoke” Mama alianza kwa kufoka akiwa ananishika mkono.
“Mama, tunaenda wapi?”
“Sitaki kurumbana na wewe, twende”
“Okay, hakuna shida” nilitoa laki moja mfukoni na kumpatia Jane. Nilifanya hivi sababu ndani ya pesa hizi kulikuwa na namba ya simu pamoja na majina yangu yote mawili huku nikiimani kuwa angenipigia kwa siku ile.

Niliondoka na wazazi wangu ambao hawakuacha kunikaripia, walinigomba kana kwamba mimi ni mtoto mdogo na sijui nini nafanya.
“Jack unataka kuleta fedhea Ikulu, unataka kuleta vituko si ndio?”
“Baba, lipo wapi kosa langu?”
“Tumekuambia nini kuhusu yule chizi?”

“Lakini nilikuja kumtazama, napenda jinsi ambavyo anapiga mbira”
“Unaondoka Ikulu unadhani Judy amependa? Mwenzako unamweka katika wakati mgumu, anataka kuchukua maamuzi magumu na utakuja kuweka roho ya mwenzako rehani”
“Sawa baba, nisamehe” Nilijishusha maana sikutaka tuendelee kurumbana.

Nakumbuka tuliendelea na safari pasi hata kusemeshana, mimi nilikuwa na hasira na hii ndio ilikuwa kawaida yangu. Kama ukinigomea basi fahamu kwamba umevunja mawasiliano na mimi kwa muda huo. Nakumbuka hadi tunafika Ikulu wote tulikuwa kimya.

Majira ya saa 10, Judy alikuja chumbani kwangu na kukaa kando yangu. Alinitazama usoni, nilihisi kama kuna jambo ambalo linaendelea katika kichwa chake. Nilimuuliza
“Tupo sawa Judy?”
“Unajua unachokifanya”
“Nafanya nini tena?”
“Kumbuka nimetoka wapi ili kukufuata, usije sababisha kila mmoja akaongea vibaya dhidi ya maamuzi ambayo nataka kuyachukua kama mtoto wa Rais” aliondoka katika kile chumba. Sikujua alikuwa amemaanisha nini maana hakusema tatizo.

Puuzo la nguvu lilinifikia, nilimpuuza Judy na kuona anataka kunichanganya. Basi, muda wa chakula ulipofika Anna alikuja kuongea na mimi, sababu siku hii watu wote walikula kivyao kutokana na nyumba kuanza kuharibika katika upande wa mawasiliano.
“Unapenda hii hali?”
“Ipi?”
“Hivi ambavyo kila mmoja anazungumza kuhusu wewe?”
“Kwani kuna nini kinaendelea?”
“Unajifanya hujui si ndio?”
“Sio kwamba najifanya bali sijui kabisa”
“Unatakiwa kufikiria maamuzi yako, utakuja kuweka watu pabaya”
“Kivipi?”
“Kama hujui lolote ni kwamba Judy ameenda kule ambako wewe umetoka, tena amechukua askari. Kazi kwako na huenda watamuua kama ambavyo unamjua Judy.” Anna aliondoka.

Kichwa changu kilianza kuchanganikiwa vilivyo, hata ladha ya chakula ikaniisha kabisa. Niliwaza kuhusu Jane, niliwaza kuhusu Judy amekwenda kumfanya nini mwanamke yule ambaye hakuwa na kosa bali kosa lilikuwa upande wangu… ITAENDELEA
 
Episode Five

Siku iliyofuata nilifunga safari hadi Nanenane ili kutazama kama Jane alikuwa bado yupo pale na yupo salama katika upande wa Afya. Masikini Jane, alijuta kwanini alijuana na mimi. Nilijuta kwanini nimemzoea binti wa watu na kumweka katika wakati mgumu.

Kwanza alikuwa amepigwa hasa maeneo ya kichwani, kibanda ambacho walikuwa wanaishi wote watatu kilibomolewa huku mbira yake ikiharibiwa. Yote haya yalifanywa na Judy, kibaya ni kwamba Jane aliponiona hakuwa hata na hamu na mimi. Alinichukia na alikuwa na hasira ambazo zilipelekea hadi kunishikia kisu, alitaka kuniua. Alinifukuza kwa ishara akitaka nitoke huku akilia kabisa.
“Sio mimi Jane! Sijafanya haya lakini” nilijaribu kujilalamisha ila nani wakunitetea ikiwa Mama yake mlezi haoni labda angenitetea, ndugu yake ni bubu hakuwa na uwezo wa kuongea hata yeye mwenyewe alikuwa ni Kiziwi ambaye hata kuongea kulikuwa na shida.

Nilibaki nikidondosha machozi, niliumia moyoni hadi mwilini. Nikashikwa hasira dhidi ya Judy, niliona napaswa kwenda kumkalipia. Nakumbuka niliondoka pale nikiwa nimempatia Tsh laki mbili lakini aliitupa chini na kusigina. Hasira zilimuongoza, nami sikuikotoka ile hela. Niliamua kuiacha nikiimani kuwa angeiokota.

Safari yangu ilitua hadi Ikulu ambapo nilikuta kukiwa na kikao cha familia kimekaa yaani Baba, Mama, Mama Judy pamoja na Rais. Niliingia moja kwa moja katika kikao na kumchomoa Judy, kwa hasira.
“Ebu njoo kwanza unieleze”
“Niachie Jack”
“Sikuachi hadi uje useme nani ambaye alikuambia kuvunja kile kibanda” hili lilikuwa ni kosa kwangu, my daddy and mommy walikuja juu. Walikuja juu na kuanza kuniwakia.
“Huna akili wewe? Unakili nakuuliza?”
“Baba! Sio kwamba sina akili lakini Judy amevunja mbira ya Jane, anategemeaje?”
“Unadhani napenda unavyonitesa kihisia?”
“Lakini wote hawa ambao waliopo hapa wanajua ukweli kuwa sikupendi”
“Unipendi si ndio?”
“Ndio sikupendi na sina hata hisia na wewe, ni vile baba na Mama waliamua kutufanya tuwe pamoja lakini sio kweli kwamba nakupend—”
“Mtoto mjinga sana wewe” Baba alinipiga kofi nzito huku akinitusi, nilimtazama Baba kwa hasira kisha niliondoka na kuelekea chumbani kwangu nikiwa nimefuraha kwa hasira.

Huu ndio ukawa mwanzo wa Mimi kususa kila kitu katika Ikulu, kwanza nilishikwa na hasira. Hakuna mtu ambaye alidiliki kuniongesha kwa zaidi ya siku mbili. Nilikuwa nawaza kwanini naishi maisha yake? Kwanini namfanya Jane anateseka ikiwa sijui anaishi katika nini?

Siku ya tatu nilimuita Judy na kuzungumza naye, ilikuwa ni chumbani kwake ambapo yeye alikaa kwenye kiti huku mimi nikiwa nimekaa katika sofa.
“Unamtesa mwenzako, unadhani bado una mapenzi ya dhati?”
“Nawe unanitesa mimi unategemea nini?”
“Sikupendi, kwani unanilazimisha?”
“Mbona hukusema mapema nikatafuta mzungu wangu huko marekani nikaishi vizuri?”
“Waliokuwa nyuma yako wanajua nini kinaendelea”
“Basi nawe utajua nini kitaendelea jifanye kuwa mbishi. Nina nguvu, nina mamlaka na baba yangu ni Rais, lolote lile ambalo naamua basi lazima litimie” Judy alisisitiza.

Taarifa za sintofahamu yetu ilimfikia Rais ambaye alishikwa na hasira sana, basi jioni moja aliniita. Nami nilienda kumsikiliza.
“Mwenzako anateseka na tulikubaliana kwa kila kitu”
“Ni kweli Mtukufu Rais lakini kwa sasa nimebadilisha maamuzi, nampenda mtu mwingine”
“Unadhani upo sahihi?”
“Hata kama utaniona sipo sahihi lakini niheshimiwe kwa hili”
“Binafsi sitataka kukuona ukiishi Ikulu, utatafuta makazi mengine hadi pale ambapo utaamua kurudi kwa mwanangu”
“Ahsante na samahani kwa makosa haya” Nilikuwa tayari kutoka katika jengo ambalo linaheshimiwa mchini lakini yote yakiwa ni sehemu ya mapenzi kwa Jane.

Basi taarifa hii ilifika kwa Baba pamoja na Mama, hawa walinijia juu. Walikuwa tayari kunipa radhi, walikuwa wamechukia sana. Baba hakuacha kufoka, nami kama kawaida yangu. Alipofoka basi nilijinunisha, nikitaka kuondoka katika lile jengo lakini wao hawakuacha kunisisitiza nimuoe Judy.


Baba ilifika hatua alikuwa ananipiga vibao mbele ya Anna ambaye hakuwahi kuniona nikipigwa. Nilipatwa na hasira, damu yangu mwilini ilichemka maana sikuwa napenda dharau kama hizi. Nilimtazama Baba huku nikiwa nimekunja ngumi, naye alisisitiza kwa kusema.
“Nipige si unanipangia ngumi, nipige sasa” Nilimuomba sana Mungu kupoza hasira zangu, kwa bahati nzuri hasira zilipoa. Kwakuwa nilichukia basi niliamua kuondoka katika eneo lile, nilienda kubeba vitu vyangu ikiwemo begi na kutoka nalo nje.

Nilienda kuweka katika gari tayari kwa kuondoka lakini Mama na Baba walikuja na kuchukua funguo wakisema.
“Umeshakuwa na una uwezo wa kufanya maamuzi yako binafsi bila kutumia mali zetu, nenda. Acha hizi mali, hazikuhusu” Mwanaume ambaye ni baba yangu ndio alitoa maamuzi haya. Kwakuwa nilikuwa na hasira, niliamua kuondoka na sikutaka kurudi tena.

Lakini nyuma Judy alilia sababu alikuwa ananipenda, aliona kabisa anaenda kumpoteza mwanaume wa ndoto zake yaani kuolewa na mimi. Kila mmoja katika Ikulu alidhani kwamba nimerogwa, kila mmoja aliniona mjinga lakini binafsi niliweka msimamo wangu.

Niliimani kuwa chaguo langu alikuwa ni Jane na kile ambacho amefanyiwa hakikuwa kitu cha kiungwana, napaswa akuwajibika kama sehemu ya watu waliomsababishia matatizo. Nakumbuka niliondoka nyumbani huku mvua inanyesha, nilitembea kwa miguu hadi nilipofika Nanenane ambako huko mvua ilikuwa kubwa mno.

Nilikuta kina Jane wakiwa wamepanga miti na kuweka turubai juu. Walikuwa akiishi kwenye kibanda kidogo ambacho hata hakikuwekwa hata udongo wala fito kwa chini. Hapa ndipo walikuwa wakifanya nyumba ya kulala. Hawakuwa na makazi tena tangu walipobombolewa, nilijaribu kuongea na Jane lakini bado msimamo wake ulikuwa ule ule kwamba hayupo tayari kwa lolote. Alinifukuza kwa mara ya pili.

Mwisho nikaamua kuchukua maamuzi kama mwanaume, nilichukua panga na kuingia msituni ambako nilitafuta miti ili niweze kujenga kibanda nao wapate
 
Episode Six

Nilipomaliza kukata miti, nilirudi na kuanza kujifanya kufunga fito ili kibanda kisimame vizuri lakini hata hakikukaza. Kibanda kilikuwa kimeregea mno kama mtu angekuja na kusukuma kidogo tu, basi kingedondoka chini si unajua nilikulia ushuwani. Kwahiyo, mambo kama haya nilikuwa hata siyawezi.

Kwa bahati nzuri Jane alikuwa ni mtaalamu mzuri sana wa kufunga. Alinisaidia kufunga huku akinitaka niwe nashikia fito ili ziweze kukaza. Nilifanya hivyo hadi tulipomaliza, ilikuwa ni muda ambao mvua imeacha kunyesha sasa. Kila mmoja akaweka tabasamu, nilifurahia moyoni kuona Jane ameanza kushirikiana na mimi katika kujenga kibanda kile.

Basi, alinielekeza nini ambacho kinafuata ambapo ilikuwa ni kuziba udongo katika kibanda, mwanzo nikajifanya mbwembwe. Nilijua wanaweka udongo wowote ule, si nikachota wa chini uliolowa na kujaribu kuziba.

Niliona Jane akiangua kicheko kisha alinipa alinipa jembe na kunielekeza natakiwa kuchimba shimo ambalo udongo ungetoka. Sikuwa naweza hii kazi ila katika kujifanya kwamba nami sio mchache nilifanya, shimo lilikuwa kubwa na udongo ulipatikana.

Kwa mara ya kwanza niliweza kuona namna gani nyumba ya udongo inavyotengenezwa. Mwanzo nilishangaa lakini Jane alinifundisha kwa ishara na niliweza kwa haraka mno. Kwahiyo tulikandika hadi pale ambapo tulimaliza, nakumbuka ilikuwa ni jioni kama ya saa 12 ila nilikuwa hoi. Mikono ilikuwa na marengerenge, mwili ulichoka kana kwamba nimetoka kupigana.
“Unaitwa nani?” alikuwa ni Mama Jane ananiuliza wakati tupipata sijui ndio niite kifungua kinywa ama kilaza kinywa.
“Jack Charles”
“Wewe ndio mtoto kutoka Ikulu?”
“Ndio mwenyewe”
“Oh! Unapaswa kurudi nyumbani maana Mpenzi wako alikuja hapa ametufanyia vurugu hata kama sikumuona lakini niliambiwa na watu”
“Nisameheni mimi”
“Kwanini upo hapa na kwanini hurudi kwenu?”
“Siwezi kurudi sababu tayari nimeshafukuzwa, nimefukuzwa kwa ajili ya Jane. Nipo tayari kuanza naye maisha hapa” nilimweleza Mama Jane.

Mwanzo alikuwa mbishi lakini mwanaume nilitumia mbinu nyingi, nilizungumza naye kwa uzuri kabisa hadi alikuja kunielewa. Alinipa idhini ya kukaa pale lakini akiwa na onyo kali sana, onyo kuhusu usalama wao nami nilihakikishia kwamba kila kitu kitaenda sawa.

Usiku ulipoingia tulilala kwenye kidogoro kidogo maarufu kama ulimi wa Mbwa, wote wanne tulilala katika kidogoro hichi huku tukijifunika nguo ambazo zikikuwa mbichi ingawa tulizikamua kidogo na kuziweka juani. Haki tena sikuwahi kuoina dhiki katika maisha yangu kama hii, niliteswa na mbu. Nikateswa na baridi, nilitamani kurudi nyumbani ila nilijipa moyo acha nibakie hapahapa nitajua nini nafanya.

Mwanga mdogo wa kibatari ulisukuma usiku wote, hatimaye kulipambazuka nasi tukaliona jua. Kwa mara ya kwanza nikajua kwamba hakuna utofauti kati ya masikini na Tajiri katika kulala. Jane alikuwa ni mtu wa Mungu sana, kwani baada ya kuamka niliona akitoa salamu katika rozali yake na aliondoka ila sikujua alikwenda wapi?

Mwanaume uvivu ukanivaa, bado nilibakia katika kigodoro kwani bado usingizi ulikuwa mwilini. Nje nilisikia sauti za watu wakiwa wanazungumza na Mama Jane, nilitoka ili kuzungumza nao. Walikuwa ni majirani zao ambao mara kadhaa walikuwa wanawasalimia na leo hii walikuja kwa ajili ya salamu.

Baada ya kusalimia waliondoka, nami nikaenda kukaa kando na Mama jane ambaye alikuwa akipika uji. Kwanza nilishangaa anapikaje uji ikiwa hana uwezo wa kuona? Ila Mungu ana maajabu yake jamani.
“Kumbe huku watu huwa wanasalimiana hivi?”
“Ndio, kwani hujazoea?”
“Hapana, sisi huwa hatuna majirani wa kusalimiana nao”
“Basi huwa tunasalimiana, tunatembeleana na kupeana pole na hongera na mambo mengine mengi”
“Napenda haya maisha”

“Lakini wazazi wako watakufuata”
“Nitawaambia kama watakuwa tayari basi niondoke na Jane”
“Haha! Mpiga mbira, mtoto wa kimasikini ambaye hana thamani. Nani ambaye atamtaka”
“Lakini anapiga vizuri”
“Kipaji chake kinatumiwa hovyo, watu wanamdhurumu kila siku”
“Natamani kusaidia”
“Wapi?”
“Nitaangalia endapo akinipa nafasi. Kwanza yupo wapi?”
“Huwa anawahi kuuza karanga”
“Mbona amewahi?”
“Masikini halali”
“Kwanini?”
“Anatafuta kitu ambacho hakilali, ukiona masikini amelala basi hajui kama pesa hazilali. Anatakiwa kwenda nazo sambamba hadi akizipata ndio alale” Kauli hii ilinifanya kuangua kicheko lakini ndio ilikuwa mwanzo wa sisi kuzoeana zaidi.

Uji ulipoiva tulikunywa pamoja na binti ambaye ni ndugu wa Jane aliyekuwa hazidi miaka 12, aliitwa Janeth. Alikuwa ni mweupe ingawa hakufanana sana na Jane ila kama ungewaona kwa mara ya kwanza usingepata kigugumizi kutambua kwamba watu hawa walikuwa ni ndugu.

Baada ya kupata chakula, nilipewa mwingine katika bakuli kubwa ya udogo ili nimpelekee Jane. Basi, niliondoka na Janeth tulienda hadi sehemu ambayo Jane anauza karanga. Nami nikakaa pembeni kutazama namna ambavo alikuwa anauza huku Janeth akirudi.

Nakumbuka tulikaa pale hadi kufikia saa nane mchana, hakukuwa na mteja ambaye alikuwa amenunua. Wote walikuwa wakizipita na kwenda kununua sehemu nyingine. Nilipatwa na hasira, kwanini wasinunue kwetu? Hapo matusi moyoni hayakukauka, niliwatusi vizuri tu. Mwisho nikapata majibu kwamba Jane alikuwa aitilishii wateja kama wafanyavyo wenzake.

Basi niliingia mzigoni mwenyewe, nilianza kuuza kutangaza kwa kila mtu ambaye alikuwa anapita. Wapo ambao walikuwa wakiniona mimi ni chizi na wapo ambao walikuwa wananiona ni mtu ambaye nilikuwa na akili timamu. Nilinadisha hadi pale ambapo wateja walianza kuja.

Tabasamu katika uso wa Jane lilirudi upya, alitabasamu na kufurahia. Alinitazama usoni, nikasema ndio ndio! Naona unakuja sasa. Basi, tuliuza na jioni ilipofika tulikuwa tumepata kiasi kadhaa ingawa Karanga zilibakia lakini hazikuwa nyingi sana. Tuliondoka nazo na kuelekea eneo lingine ambako kulikuwa na watu kidogo.

Eneo hili ndio Jane alikuwa akikaa na aliunganisha mbira yake na kutaka kuipiga lakini haikuweza kutoa sauti. Niliona akidondosha machozi, niliumia sana moyoni. Nikatoa simu yangu na kuitazama, nikajiambia kwamba napaswa kufanya kitu kwa ajili ya kurudisha tabasamu la Jane kupitia mbira maana ndio kitu alikuwa anakipenda…. ITAENDELEA
 
Episode Seven

Mara baada ya kurudi nyumbani sikutaka mambo mengi sana, nilienda mjini ambako nilimtafuta mwanachuo na kumuuzia simu yangu kwa bei ya laki sita. Iliniuma sema nilijiambia kwamba simu ni muhimu lakini haikuwa na thamani kuliko tabasamu la Jane. Kumfurahisha Jane kwa kumnunulia Mbila huenda ndio ikawa sehemu ya tabasamu langu.

Nakumbuka nilienda kununua mbila na kurudi nayo nyumbani, ilikuwa ni mbila ambayo mpya na ya kisasa tofauti na ya kwake ambayo ilikuwa imechoka kupitiliza. Tabasamu katika uso wa Jane lilirudi upya, Jane alitabasamu. Akafurahi kwa kuruka ruka huku akinikumbatia. Hakuamini kama nimempatia kitu ambacho anakipenda. Niliona akinishukuru mara mbili mbili.

Tabasamu lake lilinipa maswali kadhaa kuhusu yeye, kuhusu ndugu yake na mtu ambaye alikuwa anamlea. Niliomba kujua machache kuhusu mwanamke huyu na familia yake. Wakati Jane akiwa ndani, mimi nilikuwa nje na Mama yake tukifanya mazungumzo.
“Jane ni nani?”
“Mtoto wa kimasikini ambaye amezaliwa Songea”
“Amefikaje Dodoma sasa?”
“Niliwaokota wakiwa wadogo sana”
“Uliwakota?”
“Ndio”
“Wakiwa katika hali hii?”
“Ndio, Janeth ulimi wake umekatwa.”
“Na nani?”
“Inaonekana kuna kitu watu wameficha”
“Mungu wangu! Na vipi kuhusu Jane?”
“Huyo ni mlemavu, amezaliwa akiwa hivyo”
“Mmmh! Kati ya hao hakuna ambaye anaweza kusoma?”
“Jane mbona anajua kusoma, kwani hujawahi kumuongelesha?”
“Naona anapenda sana kutumia ishara? Nimejaribu kumuandikia mara kadhaa lakini hajajibu”
“Si mtu wa kuzoea wanaume mapema hasa mtu mgeni”
“Lakini kwa muda wote ambao naishi hapa ameshindwa kunizoea?”
“Labda anakuogopa”
“Kwahiyo anajua kusoma vizuri tu?”
“Na kuandika anafahamu vizuri na anaweza kukuandikia historia yake, yeye ni nani? ingawa kuna mambo hataki kusema”
“Uwi! Nitajaribu kumdadisi, ahsante kwa taarifa” Niliona Mama Jane amenirahisisha jambo sana, sababu dhumuni langu lilikuwa linaenda kutimia.

Kuanzia siku hii ndio nilikuwa nikiwasiliana na Jane kupitia maandishi, kuna muda nilikuwa naandika chini. Muda mwingine katika kikaratasi, hii kidogo ilinisaidia sana. Niliweza kufahamu Jane alikuwa anapenda nini? Anachukia nini? Nani ambaye alimfunza mbila ambapo aliniambia ni Mama yake mlezi.

Nakumbuka siku moja ilikuwa jioni nakumbuka vizuri. Nilimtoa Jane na kwenda naye nje kabisa ya mji ambako kulikuwa na eneo watu wanateka maji. Niliamua kutoka naye ili kuangalia mazingira lakini pia tuweze kuzungumza kwa urahisi tukiwa wawili.

Tukiwa huko tuliangalia mazingira vizuri, tuliweza kuona miti. Tuliweza kuona ndege wakiwa wanaruka pamoja na sisi wenyewe kila mmoja kuweka tabasamu.
“Mimi ni Jack” Nilimwandikia chini, akasoma na kujipiga kifuani kwa kutumia kidole cha shahada cha mkono wa kulia kisha alifuta nilichoandika. Naye aliandika cha kwake.
“Mimi ni Jane, kwanini upo na sisi?”
“Kwa sababu nimependa kuwa na wewe! Kwani ni vibaya?”
“Hapana ila wewe unaishi katika jumba kubwa, kuna ulinzi huoni tunakutesa kwenye kibanda chetu?”
“Wewe huteseki?”
“Nimezoea, tazama sura yako ilivyokuwa nyeusi sasa”
“Nami nitazoea kama ambavyo wewe umezoea?”
“Mimi nimekulia kwenye shida tangu nilipotoka kabla ya Mama ajakufa tulikuwa tunalala chini”
“Pole sana, yote maisha yatakwisha lakini niko hapa kupambana na wewe hadi ufanikiwe”
“Kweli?”
“Ndio au hutaki?”
“Hapana nataka sababu umenipa mbila nzuri sana, hakuna mtu alifanya vile. Mungu akubaliki”
“Ahsante! Nawe pia”
“Sawa, ila unaonekana una moyo wa kusaidia wengine. Una sura nzuri sana” Nilisoma neno hili hadi moyo wangu ukahisi umetua mzigo mzito.

Nilimtazama Jane usoni, niliona akikwepesha macho pembeni kabla ya kuinamia chini. Aibu ilikuwa mbele yake na hakupenda niwe namtazama usoni. Nilirudi tena katika kuandika
“Nawe pia ni mzuri, napenda unavyopiga mbila. Natamani siku moja unifundishe”

“Unataka kuwa kama mimi?”
“Ndio”
“Lakini inaumiza mikono”
“Kuna siku wewe utachoka nami nitakusaidia au hutaki nikusaidie?”
“Hapana nataka halafu yule aliyekuja na kuvunja mbila yangu ni nani?”
“Judy”
“Ndio nani?”
“Ni mtoto wa Rais”
“Mungu wangu! Sikujua, nilimsukuma”
“Ndio maana alipatwa na hasira lakini unajua kwanini niko hapa na wewe?”
“Hapana”
“Kwa sababu nakupenda na nataka uwe mama wa watoto wangu” nilimtazama Jane ambaye aliweka mikono usoni, akaficha sura. Aibu ilimkumbata.

Namna ya kuendeleza mazungumzo yetu ndio palikuwa na mziki, mwisho nilimuomba tuondoke huku nikiwa na imani kuwa nimempata utangulizi ambao unaweza kumweka sawa. Basi tuliporudi nyumbani, Jane alimsimulia Mama yake ambaye alicheka sana. Akaja kunielekeza kuhusu Jane kwamba hakuwahi kuwa na mwanaume yoyote katika maisha yake.

Alinisisitiza kama niko na nia ya kweli na Jane basi niwe naye karibu, jambo hili niliahidi nitalifanya vizuri. Mbele yetu kukawa na maisha ya raha sasa, maisha ya Mimi na Jane kucheka na kutabasamu. Ilikuwa tukiamka asubuhi ni mwendo wa kuandaa karanga kisha tunafunga na kwenda kuuza sehemu yetu huku Jane anapiga mbila nami sikuacha kuimba. Sikuwa naimba yanayoeleweka lakini itoshe kusema kwamba ilikuwa ni sehemu ya kuwavutia wateja.

Mama Jane akanitafutia eneo lingine la Mimi na Jane kuishi maana tulishaanza kuwa wapenzi sasa, lilikuwa ni eneo nzuri tu ambalo alitupa kiwanja na kujenga kibanda hapo. Tuliishi wote mimi na Jane huku tukicheka, kufurahi na kupeana matumaini kwamba kesho yetu ingekuja kuwa bora. Kuhusu nyumbani sikuwa najisumbua hata mara moja, sio simu wala meseji yangu ilienda kuwapigia. Ingawa Jane alisisitiza twende, nahisi ni kwa sababu aliona mali yaani Ikulu.

Kuna siku moja nakumbuka nilienda na Jane kazini kwetu kama ilivyokuwa kawaida, siku hii karanga kidogo zilichelewa kuisha. Ilifika hadi saa moja hatujauza na kupata pesa ambayo inaeleweka. Nikamwambia Jane nataka kwenda nyumbani kuchukua kibatari ili tuuze na usiku, alinielewa.

Nami nilirudi nyumbani ambapo nilipika na ugali kisha nikaweka katika hotpoti sijui ndio vibesi vya plastiki na kurudi nao katika eneo la biashara lakini sikuamini. Katika eneo lile nilikuta mbila zikiwa zimevunjwa na Jane hakuwa mahala pale.

Licha ya kuwaulizia watu ambao walikuwa karibu ila hakuna hata mmoja ambaye alituambia Jane alikuwa wapi…? Wakati mgumu ukawa mbele yangu katika kumtafuta Jane popote pale alipo. Wazo la kwanza lilikuwa ni kwa Judy, nilifunga safari hadi Ikulu lakini sikubahatika kumkuta Jane ingawaje Judy alikuwa pale… ITAENDELEA
 
Episode Eight

Nilikuwa kwenye kipindi kigumu katika maisha yangu, nilikuwa kwenye kipindi ambacho nilihitaji msaada zaidi ili niweze kumpata Jane lakini hakuna mtu ambaye aliweza kunisaidia. Kuanzia Ikulu ambako nilimuomba Baba lakini aliniambia hawezi kuingia vita yangu na maisha ya watu wengine. Nimuache maana nilikuwa mbishi

Nikarudi kwa watu wachache ambao nilikuwa nafahamiana nao lakini nako hakuna hata mmoja ambaye alikuwa tayari kunisaidia katika kumpata Jane. Wengi walitaka hela nami sikuwa na pesa, nilijiona naenda kumpoteza Jane.

Niliangaika kila sehemu, nilipita kila eneo kumtafuta Jane lakini sikuweza kumpata. Kwa zaidi ya wiki nilikuwa ni mtu ambaye naamka asubuhi halafu naingia mtaani kumtafuta kipenzi changu. Lakini safari zote nilizozifanya zilikuwa ni safari za pwagu, Jane hakuweza kurudi nyumbani. Jane sikuweza kumtia katika mikono yangu.
“Mama hakuna mtu ambaye unajuana naye ili atusaidi kumpata Jane?”
“Najuana na nani mimi baba yangu, sina ambaye najuana naye”
“Nani sasa ameondoka na Jane, nani?”
“Mwenyewe nachanganikiwa, Jane sijui amekwenda wapi?”
“Mwanzo nikajua ni kina Judy lakini sio wao”
“Pambana pengine unaweza kumpata, pita ukiomba msaada”
“Mama, hakuna sehemu ambayo nimepita na sijaomba msaada. Kila sehemu nimepita. Polisi wenyewe wameniambia watanipa majibu lakini wiki ya pili hii, Jane hayupo na sisi”
“Basi tumshkuru Mungu na kumuomba, kama Jane atakuwa wa kurudishwa basi utamuona” Mama mkwe aliniambia wakati tukiwa tumekaa kibarazani.

Maneno yake hayakufua dafu, bado nilihitaji Jane. Kwakuwa Janeth alikuwa anaona basi niliamua kuongozana naye kila napopita ningebeba karanga pamoja na picha ya Jane, ningeuliza kwa watu lakini bado mafanikio hayakuonekana. Siku moja nilijitoa ufahamu, nakumbuka ilikuwa ni jioni. Nilienda na Janeth Soko Kuu la Job Ndugai.

Tulikaa pale kwa muda kama dakika 40 hivi huku nikisoma mazingira. Nakumbuka kuna gari jeusi lilikuja na kusimama mnele yetu, kutokanana na msongo wa mawazo sikulipa umakini gari hili. Macho yangu yalikuwa yanatazama mbele ila niliweza kumuona mzee wa miaka kama 59 ambaye sikujua ni nani? Niliona Janeth akinyoosha kidole, sikuelewa alikuwa anamaanisha nini? Nilijaribu kumuongelesha kiishara lakini bado nilishindwa kumwelewesha vizuri.

Dakika 10 mbele Mzee alipanda katika gari nyingine na kuondoka, mi niliendelea na mambo yangu sababu nilikuwa katina upepelezi lakini sikufanikiwa kumuona mtu ambaye nilikuwa namtafuta. Basi, nilirudi nyumbani lakini wakati tunakula. Alikuja jirani yetu ambaye alikuwa akiitwa Mama Natalia.
“Umefanikiwa kumuona?”
“Hapana Mama Natalia yaani nachanganikiwa mno”
“Polise wanasemaje?”
“Hakuna taarifa yoyoye ile, sina lolote hapa maana walisema watanipigia simu lakini hadi muda huu hakuna chochot”
“Kuna mtu amepatikana amekufa nyuma kidogo ya stand ya mabasi”
“Jinsia gani?”
“Waliomuona wanasema ni mwanamke maana amechinjwa na kichwa hakipo. Nenda kamtazame labda utaweza kujua kitu” Habari hii kwangu ilikuwa ni mbaya, niliumia sana moyo huku nikiomba Mungu nama nikiende basi asiwe ni yeye.

Sikutaka kuchelewa, niliondoka hadi nilipofika katika eneo lile. nilikuta mwili umechukuliwa na askari lakini watu wa pale walitaka nitoe sifa za mtu ambaye nilikuwa namtafuta, niliwatajia.
“Dah! Labda useme alivaa gauni gani”
“Batiki tu ilishonwa kama dera then kiremba juu”
“Mmh! Mwenyewe huyo”
“Aise! Ndio mwenyewe kabisa”
“Rangi kama ya kijivu hivi halafu ina unjano si ndio then mapambo ya Sambusa?”
“Ndio”
“Hauna bahati, ndio mwenyewe watu wameshamchinja” Waliniambia na kunichanganya zaidi.

Kichwa changu kilikuwa ni kizito, nilitamani hata kukitoa maana sikuwa na jambo ambalo nililifikiria na kukaa kichwani kwa muda mrefu. Katika kuthibitisha maneno yao, niliondoka moja kwa moja hadi polisi ambako walikuwa na taarifa yangu kuhusu kupotea kwa Jane.


Siku hii niliwabwatia sana maana haiwezekani waone mauaji halafu wasinipigie simu hadi napewa taarifa na watu wengine. Masauti yangu ama kubwata kwangu hakukusaidia kitu zaidi ni kwamba walinitaka twende chumba cha maiti ili kutazama kama kweli yule aliyechinjwa ni yeye ama lah.

Nikiwa ni mwenye woga, nilioneshwa maiti. Niliifungua na kutazama vizuri, mwili ulikuwa umeharibika kiasi lakin sio cha kushindwa kutambua yule alikuwa ni nani? Ndio alikuwa ni mke wangu, alikuwa ni mwanamke ambaye nampenda. Alikuwa ni Jane ndio namuona katika jokofu amehufadhiwa akiwa hana kichwa.

Nilipata kuthibitisha kwamba Jane amechinjwa pale ambapo niliona nguo zake, ilikuwa ni zenyewe kabisa hasa pale waliponipatia kiremba ambacho alipenda sana kujifunika kichwani. Sikuwahi kulia kama ambavyo nililia hii siku, sikuwahi kutokwa na machozi pamoja na makamasi kama ambavyo nilitokwa hii siku. Sikuamini kama kweli Mke wangu amefariki, kama kweli mwanamke aliyenifanya kutoka Ikulu ili kupata penzi lake ameaga dunia.

Basi, nilichukua mwili na kurudi nao nyumbani lakini wakati huo sikuwa mimi kabisa. Nilikuwa ni binadamu mwingine, nilikuwa ni mwanaume ambaye hafahamu lolote kuhusu kesho yake. Nilipofika nilimpa taarifa Mama kabla hata ya Janeth
“Jane wangu! Nini kimekukuta Mama yangu, Jane amka basi mbona unaniachia mtoto ambaye sijui namleaje Jane. Amka Jane wangu, amka bhana mume wako anakuhitaji” Mama Jane alilia akiwa amekumbatia kitambaa cha mtoto wake.

Wanasema vipofu wanamacho ya pua, kunusa harufu na kujua vumba hili la nani? Ni jambo la kawaida sana, kutokana na yeye kuthibitisha kwamba kweli hata ile nguo ilikuwa ya Jane. Sikuwa na namna nyingine zaidi ya kukubali ukweli kwamba Jane amefariki na natakiwa kujiandaa na mazishi. Lakini nilikuwa kwenye msongo wa mawazo ambao ulitamani nami nife kuliko kuendelea kuishi duniani.

Janeth naye hakuwa mtu, chozi lilimdondoka akimtaka Dada yake. Alitamani aongee lakini uwezo wa kufanya hivyo hakuwa nao, alitamani aniambie lolote lile juu ya kile ambacho anapitia lakini bado hakuweza kusema lolote. Maumivu yaliendelea kumtafutana, maumivu yalimfanya kuzidi kudondosha machozi...... ITAENDELEA
 
Episode Nine.

Nashkuru Mungu, niliukubali msiba wa Jane kama ilivyokuwa misiba mingine ingawa nafsi yangu iliumia. Nilishirikiana na Watu wa mahala pale kwakuwa hatukuwa wengi sana, tulifanya mazishi lakini wakati tunazika Janeth alikuja na kunikabidhi picha. Zilikuwa ni picha mbili ambazo ni tofauti. Moja ilikuwa ni yeye pamoja na Dada yake. Nyingine walikuwa ni watu ambao sikujua ni nani? Lakini walikuwa ni mwanamke na mwanaume ambao walifanana umri na wazazi wangu.

Picha ya Mwanamke ilikuwa ikioneshwa sana na Janeth, kidole chake ilitua katika picha hii kuliko picha ya mwanaume. Kqa bahati mbaya sikuwa mtaalam wa kusoma ishara na lugha za mabubu labda ningeelewa nini alikuwa akimaanisha?

Nilitazama zile sura vizuri sana, zilikuwa zimefanana na kina Janeth hasa mwanamke. Hii ilinitafakarisha sana, nilikaa na picha hadi mazishi yalipomalizika na kurudi nyumbani. Usiku ulipoingia kichwa changu kilipokea maswali kibao kuhusu ile picha. Nilijiambia kutakapopambazuka basi niwahi kwa mtaalamu yoyote ambaye angewaelewa vizuri mabubu ili anitafsirie.

Nashkuru Mungu, asubuhi ilipoingia nilimchukua Janeth na kuelekea mjini ambapo tulibahatika kumpata mwalimu wa watu wa mahitaji maalamu. Kwa muda wa dakika zisizopungua 10, yule mwalim aliweza kuzungumza na Janeth kwa uhuru kabisa. Walichokakiongea mimi nilienda kukichukua kama sehemu ya majibu.
“Anasema kwamba hizi picha ni Shangazi yake na mjomba yake”
“Kumbe wana ndugu hapa mjini?”
“Hilo halitoshi, wao ndio waliua wazazi wao. Ndio maana alikuwa anakuonesha kwa msisitizo”
“Mungu wangu! Kwahiyo wapo wapi?”
“Anasema familia yao ilikuwa na pesa, kwao wanautajili wa kutupwa lakini mali zinagombaniwa na ndio sababu ya wao kukimbia na kuja Dodoma lakini bado walitakiwa uuawa.”
“Ok, kwahiyo hadi muda huu nini kinaendelea?”
“Walikuwa wanatafutwa kwa ajili ya kuwaua kwa muda tu na ndio sababu alikuwa anamkataza Dada yake kutopiga Mbila maana angekuwa maarufu na mwisho wangejulikana wapi wapo”
“Inaonesha bado hao watu wapo?”
“Aliniambia kuna siku aliwahi kumuona na alikuonesha lakini hukujali”
“Wapi?”
“Sokoni” Mwalim alipoweka kituo hapa, ndio nikapata kujua kumbe kulikuwa na mchezo kweli unafanyika.

Sasa ile sura ya kwenye picha niliiunganisha vizuri, nikajua hakuwa tofauti na yule Mzee. Nilimeza funda kubwa la mate na kumtazama Janeth na kumuuliza kama yule ndio mtu wa siku ile ambaye anamuogopa kila siku? Aliniambia ndio, basi nilimshkuru yule Mwalim na kuondoka katika eneo lile.

Siku hii niliweza kupata mwangaza, niliweza kujua kwanini Jane ameuwa. Kwahiyo napaswa kufanya juu chini ili nijue nampataje mtu ambaye amemuua Jane. Basi, nilirudi nyumbani na kumwambia Mama Jane juu ya nini ambacho kinaendelea.
“Kwahiyo umeamuaje?”
“Nitajua nampataje”
“Mmmh! Inaonekama Janeth anajua vingi”
“Ndio maana ukasema alikatwa ulimi, sasa jioni nitaondoka na kwenda kumtafuta mtu huyu. Atakuja kuniambia amempeleka wapi Jane wangu” Nilikula kiapo hichi, pasi hata kuwa na woga.

Usiku ulipofika nilimchukua Janeth wangu maana nilifohia kumuacha nyumbani, naye ikatokea kama ya dada yake. Tuliingia Mjini Dodoma kuwatafuta wale watu tukiwa na picha na picha zao. Sikutaka kutumia nguvu nyingi sana, nilienda kuteka katika maeneo yangu ambayo nilikuwa nayajua ikiwemo katikati ya Mji ambapo kulikuwa na mzunguko mkubwa.

Kwa bahati nzuri, upande wa mashariki niliona gari likija na kusimama. Janeth alisisimka mwili na kunionesha kwa ishara, nilitambua kwamba pale ndipo lilikuwa lenyewe, nilijifanya kuondoka katika eneo lile. Gari nalo lilianza kunifuata, nikatafuta njia ndogo kisha nilizama na kutokea upande wa pili. Sasa mimi ndio nilikuwa nyuna ya lile gari nikitazama.

Nilikuwa nimewapoteza, nao walipotaka kunipata basi walishuka katika gari na kwenda kuulizia sehemu. Niliwatazama vizuri sana, niliona wakielekezwa namna ambavyo sisi tulikuwa tumetembea. Baada ya maelekezo waligeuza na kurudi kule sisi tuliko.

Kitu cha kwanza ilikuwa ni kukariri Plate number, mambo mengine ningejua mimi nafanyaje.

Tulirudi nyumbani kwenye kama saa sita hivi huku tukiwa hoi, tulilala lakini binafsi nilikuwa na mawazo mengi sana. Kwanini wale watu wanazidi kuwatafuta kina Janeth? Je, ni kweli Jane amepoteza maisha. Niliendelea kuwaza hadi palipopambazuka.

Jambo la kwanza lilikuwa ni kuondoka hadi katika makazi ya Baba, nilikuwa natambulika pale. Bado nilikuwa na nafasi, niliingia ndani ambapo nilimkuta Judy. Niliamua kumwelekeza ukweli wa mambo na nini napitia.
“Msaada wako unaweza kumweka huyu binti sehemu huru”
“Hilo gari unalijua”
“Niko na Plate number”
“Lakini kwanini nawe uliingia mtaani?”
“Nilifukuzwa”
“Ulikataa ndoa na mimi, nahisi umejitakia haya”
“Kila linalokuja linamjia mtu, nisaidie you never know” Judy hakuwa na hiyana. Aliniambia kwamba angeweza kurahisisha zoezi lakini kwa sharti moja tu. Endapo akipatikana mtu ambaye anatafutwa basi nirudi Ikulu na kufunga naye ndoa.

Kwakuwa nilijua kwamba tayari Jane amefariki basi nilimkubalia. Nilimhakikisha yaani kila kitu kitakamilika endapo atanikamilishia. Naye alinihakikishia hakuna shida naweza kukifanikisha kwa wakati mwafaka tu.
“Ondoa shaka”
“Sasa ole wako hawa watu wapatikane halafu usinioe”
“Haki nakuoa Judy, nisaidie hilo” Nilimthibitishia.

Nakumbuka siku hii ndio niliweza kuzungumza na Baba yangu, Anna, Mama pamoja na Rais bila kusahau mke wake. Walinilaumu kwa maamuzi ambayo niliyachukua lakini kuna nyakati ilibidi wakubaliane na mimi. Walinielewa sababu waliona pale kilichokuwa kinaniendesha ni hisia.

Niliweza kulala Ikulu kisha asubuhi ilipopambazuka niliondoka na kurudi nyumbani lakini kufikia majira ya saa tisa mchana. Zilisimama gari mbili nyeusi, zote zilitoka Ikulu. Nikajua kuna namna maana niliona akianza Judy, akafuatia Mama, akafuatia Baba na mwisho alikuwa nani. Magari mengine yalikuwa na walinzi wa Binti wa Rais
“Panda gari tuondoke” Judy aliniambia
“Tunaenda wapi?”
“Unaogopa nini? Una kila sababu ya kuondoka na mimi, twende”
“Sawa” Nilimuitikilia lakini nilikuwa na mashaka ndani yake sababu sikujua alikuwa ananiitia nini? Ingawa moyoni nilijipa imani kuwa huenda ni wale watu wamepatikana.....

Tutaendelea
 
Episode 10

Niliondoka na Judy hadi tulipofika Ikulu na kuingia ndani, nilikaribishwa vizuri sana siku hii hadi nikashangaa kuna nini? Sikuzoea tangu nilipotoka. Walinipeleka hadi katika chumba ambacho Rais hupendelea kukaa kisha waliniacha nao walitoka nje.

Nilishangaa kwanini nimeletwa kukaa na Rais tukiwa wawili tu, jambo ambalo sikuwahi kulifanya ama halikuwahi kutoka katika maisha yangu. Mara zote nilipozungumza na mtu huyu basi kulikuwa na walinzi nyuma, ila leo hii haikuwa hivyo.
“Jane yupo hai” Rais alinieleza na kunifanya nishangae, nilishikwa na butwaa sababu ni mimi ndio nilimzika Jane kwa macho yangu halafu wao wananiambia kwamba Jane yupo hai. Nilibaki njia panda.
“Tuliomzika ni nani?”
“Hakuwa Jane! Tazama kule” nilioneshwa upande wa pili ambako kulikuwa na runinga kubwa hivi.

Tukio la mwanamke ambaye alifanana na Jane akiuawa na kuchinjwa lilionekana kisha alivishwa nguo ambazo Jane alikuwa amevaa. Kichwa chake kikachukuliwa na watu waliovaa mizura na kuondoka. Baada ya dakika nne, runinga ilizimwa. Macho yakarudi kwa Rais.
“Alitakiwa kusafirishwa na tayari alishakuwa border”
“Kwahiyo mjomba yake ndio alifanya hivyo?”
“Akishirikiana na Shangazi yake”
“Kwanini?”
“Ndio maana walibuni kifo chake ili iwe rahisi kumsafirisha bila watu wengine kujua”
“Shangazi yake ni nani?”
“Ni mafia mmoja ambaye bado tunaendelea kumtafuta”
“Kwahiyo Jane amepatikana?”
“Ndio”
“Yupo wapi?”
“Ongozana na Anna atakuonesha wapi Jane yupo?”

Niliongozana na Anna hadi katika chumba ambacho nilimkuta Jane wangu akiwa mzima wa afya hana. Jane hakuwa na mchubuko wowote katika mwili wake, sikuamini kama kweli yule ambaye namuona mbele yangu alikuwa ni yeye. Nilipiga hatua nikiwa na woga sana maana wasiwasi kwamba huenda angekuwa ni msimu bado nilikuwa nao katika mwili wangu.

Ni kweli alikuwa Jane, ni kweli alikuwa mwanamke ambaye nilimpenda kupitiliza. Mwanamke ambaye nilikuwa silali kwa raha endapo nikijua kwamba yupo eneo sio salama. Nilimkumbatia nikiwa natokwa na machozi, naye hakuacha kulia.

Kwakuwa nilitaka kufahamu ukweli basi nilitafuta kidaftari, na peni kisha nilikaa naye pembeni na nilianza kuwasiliana naye kama ilivyokuwa ada yetu.
“Nani alikuteka?”
“Shangazi, alimuua Baba miaka nane iliyopita”
“Kwanini alikuteka?”
“Unajua kuna mali nyingi sana baba yangu kabla ya kuuawa alikuwa akimiliki, mali ambazo hadi leo zinamilikiwa na Shangazi kwa njia sio sahihi. amejilimbikizia”
“Oh! Pole kwahiyo?”
“Nasikia kwamba kuna mtu alikufa na kudhaniwa ni mimi?”
“Ndio na tulizika kabisa”
“Walimuua mtu mwingine, wakamvisha kila kitu kinachofanana na mimi lengo ni kuzuga kuwa nimekufa, sikuwa mimi”
“Kwanini walifanya hivi?”
“Walitaka kunisafirisha niende China, ningeishi huko kama mtumwa. Nisingerudi tena huku”
“Sawa”
“Ila nina taarifa nzuri baby”
“Ipi tena?”
“Nina ujauzito wako” Sikuamini kile ambacho nimekisoma.

Nilimtazama Jane mara mbilimbili, uso wake uliweka tabasamu akiwa anachezea tumbo lake. Tukiwa tunaendelea kutazamana, alikuja Judy na kukaa pembeni yetu. Alinitazama usoni, sura yake ilionekana kuwa na hasira lakini tulipotazama kwa muda mrefu aliweka tabasamu. Akaniambia kwa sauti ya kitetemeshi
“Unakwenda kuitwa Baba”
“Umejuaje?”
“Tumeshafanya vipimo muda tu lakini hili haliwezi kutengua ahadi yangu mimi na wewe! Ndoa ipo palepale” aliondoka akiwa anatokwa na machozi. Nilimfuata hadi nje, nikamsimamisha na kuzungumza naye.
“Judy, najua nimekukosea na niliweka ahadi ya kweli kwako lakini kwasasa hivi sipo tayari. Nataka kuendelea kuishi maisha yangu na Jane”
“Huwezi kucheza na hisia zangu kiasi hichi Jack! Huwezi kabisa”
“Upo sahihi lakini lazima ukubali ukweli”
“Hata kama naumia”
“Always ukweli huwa unaumiza, niache nibakie na Jane ili nilee mimba yangu?”

“Kuhusu hilo sahau, au nilifanya makosa kushirikisha Baba ili kufuatilia hili” Judy alinieleza na kuondoka.

Nilikuwa katika wakati mgumu sana, nilikuwa katika kipindi ambacjo sikujua ipi ingekuwa hatima ya penzi langu na Jane. Ipi ingekuwa mwisho wa sisi kuwa sehemu moja kama mke na mume maana kila kitu kilikuwa kimeharibika. Kibaya ni kwamba Judy alikuja na kunisisitizia kwamba niache ukaribu na Jane otherwise angeweza kumuua.

Nakumbuka siku hii nilikaa pale Ikulu ambapo niliona kukiwa na kikao, kikao ambacho Mama pamoja na Baba walienda kuzungumza na mke wa Rais kutaka kutobadilisha maamuzi ya Judy ambaye alitaka tubakie pale kwa muda wote.

Basi niliitwa kwenye kikao ambacho kilihusisha watu watano yaani Mimi, Jane, Mama, Mke wa Rais pamoja na Baba.
“Umeitia aibu taasisi nzima ya Rais, umetufanya humu ndani wote tuonekane wajinga. Huko nje sio wabunge wala Mawaziri ambao wanafurahia hili, wanatucheka muda wote” Mke wa Rais aliniambia
“Ni sawa na najua kwamba nimefanya makosa, basi naomba niondoke na mke wangu”
“Mkeo ni Judy pekee, hakuna mwingine ambaye tunamtambua”
“Jane ndio kiiini cha moyo wangu na mapenzi yangu yalipo, sio mtu mwingine”
“Sahau kuhusu Jane, ndoa itafungwa Ikulu muda wowote kuanzia sasa. Jiandae”
“Nitafanya juu chini lakini sitakuwa tayari kuwa na mahusiano na Judy” Niliwaambia huku nikisusia kikao chao.

Nilienda kwa Jane na kumweleza hali halisi, nilimwambia kuna moja mbili hadi tatu. Wakati tunazungumza mtumishi wa Rais alikuja na kuniambia kwamba nahitajika na Rais ifikapo saa 12 kwahiyo nijiandae maana kutakuwa na kikao kirefu huko mbeleni.

Nakumbuka ilipofika saa 12 jioni, nilifuatwa na Anna kunipeleka kwa Rais ambaye alinieleza kwamba uongozi umekaa na wameona kwamba hawawezi kutoa damu yoyote nje ya Ikulu. Maisha yangu yote kuanzia siku ile yangekuwa Ikulu, sio mimi tu hadi Jane hadi pale ambapo Jane angejifungua kisha angeondoka yeye pasi kuchukua damu yake lakini mimi nilingebaki.
“Kwanini? Sitaki hili suala”
“Tunafahamu mengi kuliko wewe, ulikuwa nje ya Ikulu sio kwamba hakuna watu walikuwa hawakufuatilii. Kila nyanyo yako ulipokanyaga majasusi walikuwa nawe bega kwa bega. Ungekuwa kama sio kuhatarisha Ikulu” nilijaribu kupinga kadri ambavyo nilikuwa najua lakini bado sikuweza kubadilisha ukweli.

Walinirudisha Ikulu nikiwa kama mtumishi, mtoto na familia ya muda mrefu katika jengo hili lakini sikuruhusiwa kuonana na mtu yoyote kwa upande wa Jane kuanzia Mama yake, Janeth ambaye sikujua anaendeleaje? Watu niliokuwa naruhusiwa kuonana nao ni ndugu zangu yaani Baba, Judy, Rais, Mke wake na vijakazi wengine ambao walikuja ndani ya Ikulu na kuondoka…
 
Episode 11

Nilijitahidi kadri ambavyo najua kumshawishi Rais ili nionane na Jane lakini ilikuwa ni ngumu. Alimiambia siwezi na Jane yupo katika uangalizi wa hali ya juu na hatoweza kudhurika kwa lolote hivyo miache mawenge. Basi, Maisha yangu yalibadilika kabisa, nilikuwa ni mtu ambaye ratiba yangu ni fupi na isiyoeleweka. Mara nyingi nilikuwa ni mtu wa ndani nikidondosha machozi.

Muda wote niliwaza kuhusu Jane, niliwaza kuhusu kiumbe ambaye alikuwa tumboni mwake. Huyu ndio alikuwa akiniumiza kichwa zaidi maana sikuwa tayari kumpoteza. Hatimaye siku zilisonga taratibu, ilifika wiki kisha mwezi na sasa miezi miwili.

Sikuweza kumuona Jane, sikujua Jane alikuwa wapi licha ya mimi kukesha Ikulu kila siku. Sasa ukaribu wangu na Jane ukafa huku ukizaliwa ukaribu na Judy ambaye alinipeleka maeneo mbalimbali ya starehe.

Tulikuwa tunaweza kusafiri wiki nzima tukiwa nje ya nchi, mara tulikuwa Moroco, Canada na maeneo mengine. Safari zote hizo ni uongozi ndio ulikuwa unalipia na kila tulipoenda tulipokelewa kama watoto wa Rais na watu walituchukulia kama mke na mume. Kwahiyo hakukuwa na namna nyingine ya kumkwepa Judy katika kufanya naye mapenzi.

Nilikuwa nafanya naye lakini moyoni niliumia, nilikuwa na maumivu kuona namsaliti mtu ambaye hata hakuwahi kunionesha dalili yoyote ya usaliti. Nilikuwa naumia kuona nimebadilika kimaisha kabisa.

Nilianza kunywa na pombe, sio kwa kupenda bali ni stress na mawazo kuhusu Jane, kuhusu kichanga aliyoko tumboni mwake. Siku moja tukiwa kwenye hotel ya kimataifa Nchini Spain, Judy aliniuliza
“Bado unakuwa hauna furaha ukiwa na mimi?”
“Umekuwa refa mbaya dhidi ya maisha yangu, kwanini unanifanyia hivi?”
“Ni wewe ndio ulienda kinyume, tulishakuambia nini la kufanya na wapi tunatakiwa kuwepo?”
“Lakini nilishabadilisha maamuzi, sikukupenda. Unanilazimisha tu”
“Hilo la kukulazimisha halitoshi, kizuri ni kwamba fahamu nina ujauzito wako kama ilivyokuwa kwa Jane” Nilihisi kuchanganikiwa, nilitamani kumpiga makofi mbele za watu lakini sikuwa na uwezo wa kufanya hivi.

Tulikaa Spain kwa zaidi ya miezi miwili yani ilikuwa ni mwendo wa kula bata, tunatumia pesa vile ambavyo tulikuwa tunataka. Miezi yetu ya kuishi katika hii nchi ilipoisha tulirudi Tanzania.

Taarifa kwamba Judy ana mimba zilitapakaa kila sehemu ndani ya Ikulu, Rais alifurahi sana na kutununulia gari la kutembelea ambalo lilikuwa lingine. Kiukweli sikuyapenda haya maisha maana niliona kama nakuwa mtumwa lakini bado nilikosa nafasi ya mimi kuamua.

Nikiwa mezani nimekaa na Baba, niliamua kumfungukia ukweli
Nilimweleza juu ya kile ambacho napitia.
“Huyu ambaye unamuona hapa sio Jack, sio mimi kabisa”
“Unatakaje?”
“Nipeni uhuru wa mimi kufanya maamuzi, kwanini mnaniteda hivi?”
“Uhuru gani sasa unataka? Hakuna uhuru wowote”
“Mkishindwa kuchukua maamuzi basi nami nitachukua maamuzi yangu” nilimwambia na kuondoka pale nilipokuwa nimekaa.

Siku iliyofuata asubuhi na mapema, alinijia Anna na kuniambia kitu ambacho kiliniogopesha kama sio kunitisha
“Ikulu sass hivi inawaka moto na kuna hatihati Jane atatolewa na kwenda kutupwa huko nje”
“Unamaanisha nini?”
“Judy ana ujauzito na amesema hataki mwanamke mwingine mwenye mimba azae kabla yake. Kwahiyo jana kikao kilikaliwa watu watatu yaani Judy, Mama yake na Rais kujadili kuhusu hatima ya Jane”
“Waliamua nini?”
“Judy hajaniambia, ni muda wako kwenda kumuuliza labda atakueleza” Nilishindwa la kufanya zaidi ni kumtafuta Judy.

Nilienda kufanya naye mazungumzo juu ya yale ambayo yalikuwa yanaendelea.
“Hawezi kuishi hapa, tumepanga kumtoa. Atajua anakwenda kuishi wapi?”
“Kama mnataka kumfukuza basi namimi naomba niondoke, muacheni Jane wangu”
“Huna sauti mbele ya mamlaka, hata hivyo tumemsaidia baadhi ya mambo. Kwahiyo, ataweza kwenda kujiandaa na uzazi huko mbeleni”


“Kwanini mnakuwa na roho hii? Kipi amewakosea Jane? Kama makosa ni yangu”
“Ukilijua hilo linatosha, acha uongozi uamue” niliona Judy ananichanganya.

Nilienda kwa Mama kuzungumza naye lakini huyu ndio alikuwa hasikii lolote, msimamo wake ulikuwa mkali dhidi ya Jane. Mama hakupenda, hakumhitaji wala kumjali Jane.
“Anatoka Ikulu ataenda kuungana na Omba omba wengine hukp nje”
“Mama kumbuka Jane ni binadamu ana haki ya kulindwa, kupendwa na kutunzwa”
“Lakini sio ndani ya Ikulu hii, sio hapa labda huko kwengine”
“Kwanini mnamfanyia hivi? Kwanini mnamtesa Jane? Kosa lake haswa ni lipi?”
“Maswali yote hayana majibu” Mama alisisitiza

Siku iliyofuata nilishuhudia Jane akitolewa Ikulu, ilikuwa ni majira ya saa sita usiku. Sikujua walikuwa wanampeleka wapi? Kibaya ni kwamba Anna alikuwa hamfahamu lolote kuhusu hili, hapa ndipo nilimpoteza Jane wangu. Nilimkosa Jane pamoja na kiumbe aliyekuwa tumboni kwake.... ITAENDELEA
 
Episode 12

Maisha yaliendelea mara baada ya Jane kutimuliwa ndani ya Ikulu, mwanzo nilikuwa ni mtu wa kumuwaza sana lakini kadri siku zilivyozidi kwenda ndivyo nikaanza kupoteza baadhi ya vitu hasa kumhusu mrembo huyu.

Nikawa ni mtu ambaye sijui nini kinaendelea juu yake zaidi ni kwamba Rais alinisisitizia kuhusu suala la ndoa.
“Mtoto akishajifungua tu, utakaa mwezi mmoja kisha mtafunga ndoa”
“Kwanini isiwe hivi sasa?”
“Lazima tufuate sheria, lakini harusi itakuwa kubwa na haijawahi kufanywa hapa nchini”
“Oh! Sawa”
“Baada ya hapo mtaangalia wapi mnataka kuishi kama hapa Tanzania au nje ya hapa basi uamuzi utakuwa juu yenu”
“Hakuna shida” nilimuitikilia lakini kiukweli mpango wa kwenda kuishi nje ya Tanzania sikuwa nao.

Nilichokuwa nakihitaji ni mimi kuishi hapahapa ili nitumie muda mwingi kumtafuta Jane ama ndugu yake ili nikimuona basi maisha yawe kama mwanzo. Hata kama ningeshindwa kumshawishi Jane kuwa na Mimi kwa mara nyingine lakini nisikose kumuona. Nakumbuka ulipitia mwezi wa pili, kisha tatu, nne na tano tangu Jane aondoke. Ukapita pia mwezi wa sita na saba.

Katika miezi yote hiyo nilikuwa namtafuta Jane kwa siri sana ambapo nilituma baadhi ya watumishi wengine katika Ikulu huku nikiwapa na picha ya Jane lakini hakuna hata mmoja ambaye aliniletea taarifa kwamba Jane yupo hai. Hata nilipowaulizia kuhusu ndugu zao wengine nao pia nilipewa jibu hawapo, hata pale walipokuwa wanaishi inasemekana walishaondoka muda tu.

Nilichanganikiwa na habari zao, nikawa katika wakati ambao unanipa mawazo mno. Kuwaza Jane atakuwa amekufa ama yupo hai ndio kitu kiliniumiza kichwa.
“Itakuwa amekwenda wapi?” bado nilikosa jibu. Nakumbuka siku moja kulikuwa na sherehe ya ngoma za Asili, ilikuwa inafanyika Jijini Mbeya ambapo watu mbalimbali walitakiwa kwenda kumwakilisha Rais.

Miongoni mwa hao alitakiwa kwenda Judy akiwa na mpenzi wake ambaye ni Mimi, basi tuliondoka hadi Mbeya na siku ya shughuli ilipofika. Watu ama watumbuizaji mbalimbali niliwaona wakiimba miongoni mwa hao kulikuwa na mwanamke ambaye alipiga mbila vizuri sana.

Ufundi wake ulifanana mno na Jane, nilimtazama yule mwanamke kwa makini. Naye aliponitazama hakuonesha kama alikuwa ananijua. Hii ikanipa mashaka, nikamnong’oneza msaidizi wangu.
“Nitahitaji kujua huyu anaishi wapi”
“Sawa”
“Mfuatlie”
“Hakuna shida” aliondoka na kumfuatilia yule mwanamke.

Jioni ilipofika nililetewa taarifa kuwa hakuwa Jane bali ni mwanamke ambaye anaishi Jijini Mbeya kwa muda tu. Taarifa hii ilinikosesha amani sana maana nilitegemea kwamba angekuwa katika eneo lile.

Wakati tunajiandaa kurudi Dodoma, hali ya Afya ya Judy ilianza kuwa sio. Haraka simu ikapigwa Ikulu na amri ikatolewa kwamba anatakiwa kuwahi Dar es salaam kwa ajili ya kujifungua.
“Hakikisheni mnampeleka Mhimbili muda huu”
“Lakini alibakiza mwezi mmoja”
“Mtakuwa mkiishi Ikulu ya Dar es salaam na akishajifungua basi mtarudi hapa kwa ajili ya ndoa” Mama Judy hakuacha kusisitiza.

Maneno yake yalikuwa ni sheria, nilitekeleza ambapo tuliondoka hadi Dar na kufanya vipimo vya awali. Majibu yalikuja kuwa mtoto alikuwa anajipindua lakini amebakiza siku chache ili aweze kujifungua. Tulirudi nyumbani kusubiri siku ili Judy ajifungue
“Natumaini nitakuletea mtoto mzuri”
“Hata mimi pia”
“Kweli?”
“Ndio”
“And Daddy anasema kila kitu kuhusu ndoa kipo tayari”
“Oh! Lakini binafsi nisingependa kuwa mbali na wazazi wangu”
“Kwanini? Mimi nilidhani tungeenda kuishi hata France maana Baba alishanunua nyumba huko?”
“Hapana, nataka kubakia hapa”
“Mmmh! Sawa” niliamua kumzuga Judy naye alinielewa.

Tarehe ya kujifungua ilipofika Judy alijifungua na nilikwenda na Maua hospital, alikuwa amejifungua mtoto wa kiume ambaye nilimuita Johnson. Johnson alifanana na mimi kuanzia macho, pua, masikio na hata rangi pia.

“Hongera mke wangu”
“This is for you, nawe pia hongera. Mchukue mwanao” kwa mara ya kwanza ndio nilishika damu yangu.

Nilihisi fahari, nilihisi amani ndani ya moyo lakini baadaye yakazaliwa maumivu mengine. Maumivu ambayo yalinikumbusha kuwa, kuna damu yangu ipo sehemu na sijui inaendeleaje. Natakiwa kumtafuta Jane popote alipo ili nijue kama amejifungua tayari ama lah!

Miezi miwili mbele mara baada ya Judy kujifungua, ilifanyika harusi kubwa tena ya kimataifa naweza sema kwani vyombo mbalimbali vya habari kutoka nchi tofauti tofauti iliripoti harusi yetu. Kila kona ya nchi watu walizungumza kuhusu sisi, wasanii mbalimbali walituburudisha.
“Nitakuzawadia Benz mpya” Mama mkwe alituambia wakati wa sherehe
“Utachukua hisa aslimia 20 za kampuni yetu” Baba naye aliniahidi

Wazazi walikuwa na furaha, nasi pia kwa upande wetu tulikuwa na furaha. Tulifurahi kuona tumeungana na kuwa mwili mmoja.
“Nafurahi kuwa na mwanaume anayejali kama wewe Jack”
“Hata mimi Judy, nisamehe kwa pale ambapo nilikukosea”
“Hapana, hukukosea Jack. Naomba tutazame mbele na kumtunza mtoto wetu”
“Sawa” Nilihakikishia Judy na tuliianza safari ya maisha ya ndoa ambapo Baba yake aliniita na kunipa ushauri.
“Johnson huenda atakuchukia endapo akijua kwamba Mama yake humpendi ama ulikuwa humpendi. Sisi hatutakuwa tayari kusimulia historia mbaya ya upatikanaji wake, hivyo basi hakikisha kuwa unajibadilisha kitabia. Mpende Judy na mchukulie kama mke wako” Maneno ya Baba yaliniingia.

Kuanzia siku hii ndio nilifuta kumbukumbu kamili kuhusu Jane, niliamua kuwa mtu bora. Niliamua kuwa Baba bora kwa Johnson na kuwa mume bora kwa Judy. Sikutaka tena kumfuatilia Jane, sikutaka tena kujihusisha juu ya jambo lolote linalohusu Jane…. ITAENDELEA
 
-

Episode 13

Mwaka wa kwanza ukakatika huku tukiendelea kumkuza Johnson katika mazingira mazuri, tulimlea kama wazazi wenye mapenzi ya dhati kwa mtotop wao. Ukaingia mwaka wa pili wa Johson, wote kwa pamoja tukamhakikishia malezi ambayo yalikuwa mazuri sasa.

Mwaka wa tatu ukaingia nao haukukaa sawa uliondoka na kuukaribisha wa nne mwaka huu ulikuwa ndio mwaka wa uchaguzi ambapo Rais alitakiwa kurudi tena madarakani. Kwahiyo pale nyumbani kulikuwa na pirika pirika za hapa na pale. Ikulu muda wote waliingia watu mbalimbali na kutoka.

Judy akaniambia kwamba haoni kama wanapaswa kuishi pale, labda tutafute sehemu nyingine ya kwenda kuishi.
“Tutaenda wapi na unajua sisi ni watu ambao tumelelewa hapa”
“Ishu sio kulelewa lakini unapenda mtoto awe anakutana na watu mbalimbali?”
“Mmmh! Kwahiyo umeamuaje?”
“Nataka kwenda Masaki then nitaishi huko”
“Unamaanisha Dar?”
“Ndio! Kule ambako viongozi wastaafu wanakaa, nasi tutakuwa huko”
“Ok, hakuna shida” nilimkubalia.

Basi mwezi mmoja mbele tulihama na kuingia Jijini Dar es salaam huku tukiwa na ulinzi wa kutisha kama sio askari. Maisha yetu yakawa ni watu wa ndani tu, tumetoka sana labda ni kuangalia maisha katika nchi nyingine na sio kuzunguka sana. Kwakuwa nilishayazoea maisha haya sikuwa naona kuna kipingamizi chochote.
“Johnson anasema hapendi pale anaposoma?”
“Anataka kusoma wapi sasa?”
“Kasisitiza tumbadilishie shule”
“We unaona shule gani inaweza kumfaa?”
“Nakusikiliza ukiwa kama baba?”
“Kwanini asisome nje?”
“Nitakuwa nakosa muda wa kumuona mtoto wangu”
“Lakini mazingira ya shule za hapa kwetu unazijua”
“Hata kama ila sipo tayari”
“Ok basi chagua wewe nimekupa uhuru au ngoja kesho nitafuatilia halafu nitakuambia”
“Sawa”

Asubuhi ilipopambazuka niliingia mtandaoni na kutafuta baadhi ya shule kwa bahati nzuri niliona, nikatazama mazingira yake na kumuonesha Judy. Aliyapenda mazingira ila alinisisitiza kuwa ni vyema kama ningeenda kutazama vizuri na kuangalia hali ya ulinzi wa mahala pale ili niweze kujua kama ni salama ama lah
“Halina shida nitalifanyia kazi” nilimuonesha John pia mazingira ya eneo lile kama ameyapenda. Naye aliniambia ameyapenda. Basi kazi ikabaki upande wangu kufuatilia zaidi.

Siku iliyofuata nilifunga safari hadi sehemu shule ipo, nilizungumza na uongozi wa pale kuhusu mazingira. Walinipa maelezo ambayo nilikubaliana nayo kuanzia katika ulinzi hadi namna ya ufundishaji wao. Basi, nilirudi nyumbani na kumpa maelekezo Judy.
“Mazingira yapo poa”
“Ulinzi je?”
“Wana hadi CCTV Camera halafu security yake ya kisasa kabisa”
“Kesho tutampeleka, wote kwa pamoja”
“Hakuna shida” niliitika na kwenda chumbani kwa Johson.

Nilikuta akiwa anacheza game, nilienda kumkumbatia huku nikikaa kando yake ili kumpa kampani.
“Tuone nani atashinda sasa?”
“Haha! Nashindwaaaaa”
“Ndio unashindwaaaaaa” Judy naye alikuja chumbani na kumpokonya pad Johnson kisha alikaa na tulianza kucheza. Sasa Johnson alibakia kama mshangiliaji.

Haya ndio yalikuwa maisha yetu, haya ndio yalikuwa maisha ambayo tumeyachagua. Kwetu furaha ilipatikana muda wowote, hakukuwa na kitu ambacho kinatupa mawazo kwakweli. Basi, siku iliyofuata tulifunga safari hadi shuleni na kumuacha Johnson. Nasi tulirudi nyumbani.
“Kwanini tusipitie hotel kupata chakula?”
“Unataka tule hotel leo?”
“Ndio mume wangu! Hata hivyo kuna Birthday ya Kelly itakuwa next week”
“Yule mtoto wa Waziri mkuu?”
“Yah! Itafanyika hapahapa Dar na kasema tusikose”
“Ok, ni la muhimu hilo” Nilimwambia Judy na tulienda hotelini ambako tulipata chakula na kurudi nyumbani.

Siku zilienda hatimaye siku ya Birthday ya Kelly ilifika, tuliondoka hadi kwenye moja ya Hotel kubwa ambako ndio shughuli hii ingefanyika. Kwanza haikuwa party ya kitoto, watu mbalimbali waliarikwa katika party hii.

“Kuna mtu wa muhimu Kelly amesema atamtambulisha” alininong’oneza Judy wakati tukiwa tumekaa katika kiti
“Nani?”
“Sijajua lakini amesema itakuwa surprise kwahiyo tujiandae tu”
“Mh! Sawa” niliitikia.

Watu walizidi kumiminika na muda wa sherehe ulipofika, alitambulishwa mke wa Kelly kwa mara ya kwanza kila mmoja alimpongeza. Muda wa kurudi nyumbani ulipofika tuliongozana kurudi nyumbani lakini tukiwa njiani, nilimuona mtu akiwa barabarani anapiga mbila huku pembeni yake kukiwa na mtoto ambaye alishika kopo.

Macho yangu yalitua kwa mtu yule ambaye alikuwa ni mwanamke, nilimtazama sana. Hakutofautiana kabisa na Jane, kila nilipokuwa namtazama ndivyo taswira ya Jane ilikuwa inarudi kichwani kwangu. Nikasema kwa namna yoyote yule atakuwa ni yeye na napaswa kumfuatilia zaidi.

Siku iliyofuata asubuhi na mapema nilimuaga Judy kuwa kuna sehemu nakwenda kufuatilia masuala ya kadi zangu za Bank baada ya hapo nitaingia ubalozi kujua baadhi ya mambo kisha ningerudi nyumbanni. Alinielewa ingawa ukweli haukuwa hivyo.

Nilikuwa nimepanga kwenda kumfuatilia yule mwanamke, nakumbuka nilifika hadi sehemu ambayo jana nilimuona. Lakini sikubahatika kumkuta, nikapatwa na wasiwasi wapi itakuwa amekwenda. Jibu likaja labda kuna sehemu, nilijaribu kuulizia watu?
“Huwa anatabia ya kuchelewa”
“Kama saa ngapi hivi?”
“Mara nyingi naanzia saa 10 kwenda juu, sasa hivi jau lakini kwenye mida ya jioni ndio uhakika” mmoja alinieleza.

Nikaona bora nipitie sehemu ambazo nilimweleza Judy hata kama kwa kugushi ili asijue nini kinaendelea. Basi nilifanya hivyo na jioni ilipofika, nilienda tena katika ile sehemu. Kwanza nilimkuta mtoto wa kike ambaye hakuzidiana sana na umri wa Johnson tofauti yao ilikuwa ni malezi tu.

Huyu kidogo alikuwa na mwili dhohofu, ngozi iliyosinyaa pamoja na nguo ambazo zilidhihirisha alikuwa anaishi kwenye nyumba ambayo ni kambi ya kunguni, nzi, mende, nge na wadudu wengine wabaya. Alikuwa amesimama mwenyewe kwa muda tu huku akiwa na bakuli la aluminium.

Nilianza kumfuata lakini niliona akinikimbia, sasa nikawa namsisitiza asimame ili nizungumze naye ila bado alizidi kukimbia. Nikasema ngoja nimfuate lakini ghafla nilishikwa mkono, nikageuka kutazama nani ambaye ananishika mkono. Macho yangu yakakutana na Jane akiwa na mtoto mdogo mgongoni…... ITAENDELEA
 
Episode 14 (mwisho msimu wa Season 0ne)

Nilihema juu juu, sikuamini kile ambacho nakiona mbele yangu. Ni kweli yule alikuwa ni Jane ama mwingine. Naye alinitazama huku akiwa na hasira mno, macho yake yaliingia ndani. Binti ambaye alikuwa anakimbia sasa alirudi na kumkumbatia Jane katika mapaja yake.

Sikuwa na jinsi ilinibidi nijishushe kwa Jane, nilijilalamisha ili aweze kunisamehe na kupata kuzungumza ili kujua nini ambacho kimetokea. Hatima ya mimba yake ni ipi? Mtoto ambaye alikuwa amembeba ni wa nani? pamoja na maswali mengine mengi ambayo nilikuwa nayo.

Nashkuru Mungu, Jane alinipa uhuru huo. Basi, nilimchukua na kwenda naye kwenye moja ya hotel kisha tuliweka makazi hapo. Tukaanza kuzungumza kwa kutumia maandishi, kila mmoja alikuwa anamtumia meseji mwenzake maana nilimpatia moja ya simu yangu.
“Mtoto yupo wapi?”
“Huyu ambaye unamuona anakula chakula” nilimtazama yule binti.

Sura yake ilikuwa ya Jane kabisa, walitofautiana vitu vichache sana. Jane alimwambia aje kuniamkia kwa kumuoneshea ishara, naye alifanya hivyo. Aliniamka kwa kuweka mkono kichwani kabla ya kurudi sehemu alipokuwa mwanzo.
“Mbona hajaongea?”
“Bubu”
“Bubu?”
“Ndio”
“Kwanini?”
“Acha tu”
“Kipi kilitokea nieleze?”
“Shangazi alinifuatilia tena miaka mitatu nyuma”
“Ikawaje?”
“Alinikuta nikiwa na huyu mtoto, aliamua kumkata ulimi”
“Mungu wangu! Kwanini anafanya haya?”
“Sijajua”
“Kwahiyo anaitwa nani?”
“Jessica”
“Umempa jina nzuri, na baba je?”
“Siwezi kufuta ukweli kuwa huyu ni damu yako, anaitwa Jessica Jack”
“Ahsante! Halafu huyo ambaye umembeba mgongoni ni mtoto wa nani?”
“Janeth”
“What! Inamaana Janeth ana mtoto?”
“Ndio”
“Yupo wapi mwenyewe?” swali langu lilimfanya Jane kuangua kilio.

Alitoa picha ya Janeth katika mkoba mdogo ambao alikuwa ameubeba kisha alinikabidhi. Niliitazama ile picha vizuri, ilimuonesha Jane akiwa ametobolewa macho. Nilipatwa na huruma kama sio hasira. Nilishika tena simu na kumtumia meseji.
“Amepatwa na nini?”
“Ndivyo alivyokuwa hivi sasa”
“Inamaana upo naye?”
“Ndio, naishi naye”
“Wapi?”
“Kwangu”
“Ok, unatakiwa kunipeleka na hili la shangazi yako kama yupo hai tutajua nini la kufanya” nilisisitiza.

Kiukweli nisiwe muongo katika siku ambayo moyo wangu uliumia ni hii, niliteseka sana moyoni kuona watu ambao nilikuwa nawapenda wakiwa katika mateso. Basi, tuliondoka na Jane hadi nyumbani kwake ambako alikuwa anaishi. Ilikuwa ni kwenye ghofu ambalo liliandikwa NYUMBA HAIUZWI EPUKA MATAPELI. Alikuwa akiishi hapo.

Tuliingia ndani na kumkuta Janeth akiwa amelala, muonekano wake ulikuwa tofauti kabisa. Maumivu ndani ya mwili wake yalikuwa mengi. Janeth alikonda, Janeth alikosa furaha, Janeth hakuwa na mvuto kama hapo awali.
“Huyu ndio Janeth wangu, natamani hata kumuua lakini naogopa dhambi. Lakini hana ambalo analijua, haoni furaha katika huu ulimwengu” niliisoma hii meseji huku machozi yakinitoka.
“Nani ndio baba wa huyu mtoto wake?”
“Sijui maana hata mimi nilimkuta mbezi akiwa na ujauzito wake”
“Nani ambaye alimsafirisha kutoka Dodoma hadi hapa?”
“Sijajua maana Mama alishafariki”
“Mama amekufa?”
“Ndio”
“Mungu wangu! Ilikuwaje?”
“Mungu aliamua kumtesa”
“Kwahiyo wewe unaishije?”
“Bado natafutwa ili kuuawa na Shangazi, bado maisha yangu yapo sehemu mbaya. Natoka jioni kutafuta riziki na mchana natumia kulala nikiwa na familia yangu” aliniambia Jane.

Siku hii tulizungumza mambo mengi sana, akaniulizia kuhusu familia yangu. Naendeleaje na maisha na mambo mengine kadha wa kadha ambayo nilimjibu, mwisho niliaga na kurudi nyumbani ambako nilimkuta Judy akiwa ni mwenye hasira maana nilikuwa nimechelewa kurudi.
“Ulikuwa wapi?”
“Kuna jambo nataka tuongee hata kabla ya kujua nilikuwa wapi?”
“Jambo gani?”
“Unakumbuka kama kuna mtu anaitwa Janeth”

“Usiniambie ulienda kwa Jane?”
“Kwanini unakuwa mkali hivyo?”
“Inamaana hadi leo unamfuatilia si ndio?”
“Hapana ila nilikutana naye njiani ikanilazimu nisimame. Tazama sasa hivi Janeth alivyo” nilitoa picha na kumuonesha Judy.

Nilimtazama Judy akiwa anatazama ile picha, macho yake yalianza kutoa machozi. Nikajua kwamba tayari kuna kitu kinamsumbua katika moyo wake, tayari alikuwa na huruma dhidi ya kile ambacho amekiona.
“Janeth anateseaka, Janeth hana macho, hasikii pia”
“Nani amefanya haya yote?”
“Ni yule ambaye alitaka kuwaua”
“Shangazi?”
“Ndio, binafsi nakuomba tuwasaidie hawa watu maana Dada yake anatafuta pesa ili kumpatia matibabu ndugu yake. Tuwasaidie hata kama watashindwa kuona ama kusikia lakini iwe kuwe na urahisi kimaisha. Jane anategemea Mbila ili kupata hela ya kuendesha maisha yake, hana ambalo analifahamu kwa sasa zaidi ya kunusa maumivu. Anahitaji msaada wetu” nilimwekea kituo hapa Judy.

Naye alivuta pumzi ndefu na kuiachia, macho yake yalikuwa yanaendelea kudondosha machozi huku akiwa anatetemeka na ile picha.
“Then baada ya kuwapa msaada nini kitaendelea?”
“Maisha yao yakiwa mazuri tu inatosha hayo mengine watapambana wenyewe”
“Hautarudiana naye?”
“Siwezi”
“Sawa! Nitafanya hilo” Judy alinipa uhakika nami nilimani kuwa ni kweli angeweza kufanya hili…... ITAENDELEA

Mwisho wa msimu wa kwanza, usikose kujua nini haswa kiliendelea katika msimu wa pili ambao utakujia hivi karibuni……….
 
Daah watoa hadithi wote wangekuwa kama wewe,ingekuwa safi sana. Umeshusha vipande bandika bandua mpaka raha yani. Big up sana Jon woka hauna lawama. Siku yoyote ukipata nafasi utatuwekea sizoni two.
 
Back
Top Bottom