JINI WA DARAJA LA SALENDA.......EP.5.
ILIPOISHIA:
Kwa vile Brighton alikuwa amekwishaoga, Suzana naye alikwenda kuoga na kujumuika wote kitandani. Kama kawaida walisafiri katika meli ya wapendanao, safari ya kwanza ilianza vizuri kila mmoja alifurahia safari ile.
Baada ya safari ya kwanza kwisha, Suzana hamu ilikuwa bado haijamuisha, alitaka asafiri safari moja zaidi ndipo wapumzike.
Ajabu kila alipomgusa mwenzake, jogoo alikataa kuwika kitu kilichomshtua Suzana.
“Vipi mpenzi mbona hivi?”
“Hata mimi nashangaa.”
SASA ENDELEA...
“Au umeanzia kwa mwingine?”
“Lakini kwa nini kila linapotokea tatizo unanifikiria vibaya kuwa nilikuwa na wanawake? Siku hizi sina kazi, kazi yangu kutembea na wanawake,” Brighton alilalamika.
“Mbona leo imekuwa hivi?”
“Hata mimi nashangaa.”
Suzana alijitahidi kumkanda mpenzi wake kumrudisha kwenye hali ya kawaida lakini hakukuwa na mabadiliko, jogoo alikataa kuwika. Aliamua kumwacha ajipumzishe waendelee baadaye. Alijilaza pembeni ya Brighton aliyeonekana mwingi wa mawazo.
Suzana akiwa amejilaza alikuwa na yake aliyokuwa akiwaza, ghafla mazungumzo yake na Sharifa yalijaa kichwani na kuyakumbuka maneno aliyoelezwa juu ya tatizo la mume wake.
“Basi shoga, siku ile niliporudi nyumbani nilikutana kimwili na mume wangu kama kawaida mzunguko wa kwanza ulikwenda vizuri, ajabu wa pili hakuwa na nguvu kila alivyojitahidi, nguvu za kiume ziligoma.”
Sauti ile ilijirudia kichwani mwake na kumfanya atishike na kuamini huenda tatizo la Sharifa limempata na yeye. Bila kujielewa, alijikuta akikaa kitako na kumshtua Brighton aliyekuwa katika dimbwi la mawazo.
“Brighton,” alimwita kwa sauti ya juu japo alikuwa pembeni yake.
“Unasemaje?”
“Hali hii imekutokea mara ngapi?”
“Suzana swali gani hilo, toka niwe na wewe hali hii imeshanitokea?”
“Hapana, basi utakuwa na tatizo la muda mrefu.”
“Lakini siamini huenda ni uchovu ngoja nipumzike kidogo tutaendelea,” Brighton alimtoa hofu Suzana.
“Mmh! Sawa,” Suzana aliguna akiwa na wasiwasi na maneno aliyoelezwa na Sharifa ya mpenziwe kuwa amekufa nguvu za kiume.
Kila mmoja alilala upande wake, mchana waliamka na kwenda kupata chakula cha mchana. Wakiwa wamekaa wanakula, Brighton akamsifia Suzana kwa usafi aliofanya na kuifanya nyumba ipendeze.
“Mpenzi umetumia muda gani kufanya usafi ule?”
“Usafi gani?”
“Wa nyumba,” kauli ile ilimshtua Suzana na kuamini kabisa tayari nyumba yao imeingia kwenye tatizo lakini hakutaka kulikubali mara moja ili kuficha kila anachokiwaza, alijikuta akikubali pongezi zisizo zake.
Baada ya kupata chakula walirudi nyumbani kupumzika, kwa vile kila mmoja alikuwa na hamu na mwenzake baada ya kuoga walipanda kitandani kujiachia kwa raha zao. Lakini hali ilikuwa mbaya zaidi Brighton hakuwa na nguvu za kiume.
Hali ile ilizidi kumweka Suzana kwenye hali mbaya, hakukubaliana nayo, aliendelea kumsaidia mpenzi wake lakini hali ilikuwa ile ile.
Suzana alijikuta akiangua kilio kitu kilichomshtua Brighton na kuhoji:
“Suzana mbona unalia?”
“Brighton unajiona upo sawa?”
“Sijajua nikujibu nini?”
“Hujioni haupo sawa?”
“Hali ya leo inanishangaza hata mimi si kawaida yangu.”
“Inawezekana kuwa ndiyo yenyewe,” Suzana aliropoka.
“Yenyewe nini?”
“We acha tu, kesho nitakwenda kumweleza Sharifa.”
“Kumweleza nini?” Brighton alizidi kuyashangaa maneno ya mpenzi wake.
“Naomba leo tuachane na hilo.”
“Kwani umegundua nini kuhusu tatizo langu?”
“Brighton sijagundua lolote.”
“Mbona unasema utanijibu kesho?”
“Sijajua nini tatizo, linafanana na la Sharifa.”
“Sharifa ana tatizo gani?”
“Brighton tutazungumza kesho, naomba niondoke.”
“Si ulisema utalala?”
“Kwa hali hii siwezi kulala niache tu niwahi nyumbani.”
Brighton hakuwa na la kusema zaidi ya kumruhusu Suzana akalale kwao. Suzana akionekana amechanganyikiwa, aliwasha gari na kurejea kwake. Alijikuta akilia njia nzima juu ya hali ya mpenzi wake huku akijiuliza kama itakuwa hivyo mpenzi wake amekufa nguvu za kiume atafanya nini? Alipoingia ndani kwake alijitupa kitandani hata usingizi ulivyomchukua hakujua.
Suzana alishtuka siku ya pili, alijiandaa kwenda kazini huku akiwa na shauku ya kuonana na Sharifa kumwelezea yaliyomsibu kama yake. Alipofika kazini kiti alikiona cha moto, hakukaa, alikwenda moja kwa moja ofisini kwa Sharifa. Sharifa alipomuona alishtuka na kumkaribisha:
“Mmh! Dada mbona asubuhi asubuhi?”
“Wee acha tu, ukiona hivyo ujue kuna jambo.”
“Karibu, mi ndo naingia sasa hivi hata vumbi sijafuta kwenye kompyuta.”
“Yaani wee acha tu,” Suzana alisema huku akiketi kwenye kiti.
“Mh, kuna kipi kipya?”
“Kuna mapya! Yale yaliyokutokea yamefika na kwangu.”
“Yapi hayo tena?”
“Si yaliyomtokea mume wako.”
“Unamaanisha jogoo kushindwa kuwika?”
“Ndiyo.”
“Ehe!”
Suzana alimwelezea Sharifa yaliyomkuta, baada ya kumsikiliza alishusha pumzi na kusema:
“Unajua unaweza kuona nakutania .”
“Kwa kipi?”
“Jana usiku nilipokutana na mume wangu huwezi kuamini, nimefurahia tendo kama kawaida.”
“Wewee! Mara zote?”
“Tena ajabu lilikuwa penzi tamu ajabu hata asubuhi nimeamka nilihisi kama siku ya kwanza kuonana na mume wangu.”