JINI LA DARAJA LA SALENDA........EP.23
“Tuache masihara, hebu nipelekwe kwa huyo mtaalamu, kilea kidonda mwisho kukatwa mguu.”
“Leo ndiyo unagundua, nilikueleza toka mwanzo kuwa majini wana hadaa inayokuchanganya na mwisho wa siku wanakuingiza sehemu mbaya.”
“Sharifa huu si wakati wa kunilaumu, nahitaji msaada wako la sivyo nitachanganyikiwa.”
“Kama upo tayari, twende pamoja Bagamoyo.”
”Lini?”
“Leo hii.”
“Saa ngapi?”
“Safari yetu itakuwa saa tatu?”
“Basi shoga tutakuwa wote hali inatisha.”
Walikubaliana kwenda wote Bagamoyo, baada ya kukata simu Suzana alinyanyuka kitandani ili kujiandaa na safari ya Bagamoyo.
Baada ya maandalizi waliingia kwenye gari kwenda nyumbani kwa Sharifa kumpitia kwenda kwa mganga Bagamoyo. Njiani alijitahidi kumpigia simu Brighton simu yake haikuwa hewani, aliachana naye na kuendelea na safari yake mpaka kwa Sharifa.
Aliwakuta wameisha jiandaa wakimsubiri, walipomuona tu hawakutaka kupoteza muda.
“Jamani tutatumia magari yote?” Suzana aliuliza.
“Hakuna haja ya kutumia magari yote, moja tu linatosha”
“Hakuna tatizo.”
Walikubaliana kwenda kwenye usafiri mmoja walipanda kwenye gari la Sharifa na kuelekea Bagamoyo. Walitumia dakika arobaini na tano kufika Bagamoyo, walipofika waliuliza wenyeji sehemu aliyopo mganga Njiwa Manga.
“Samahani kaka,” Sharifa alimuuliza kijana mmoja aliyepita karibu na mlango wa gari lake.
“Bila samahani dada yangu,” kijana yule alijibu huku akisogea karibu.
“Habari za saizi?”
“Nzuri tu dada.”
“Eti, Njiwa Manga anaishi wapi?”
“Njiwa Manga! Yupi, yule mganga?”
“Eeh, huyo huyo.”
“Unaona hii barabara kubwa?”
“Ndiyo.”
“Ifuateni, acha barabara ndogo mbili zinazokatisha kulia, ya tatu ufuate nenda moja kwa moja mpaka mbele utaona kuna nyumba ina bendera nyekundu hapo hapo kwa mzee Njiwa Manga.”
“Asante,” Sharifa alishukuru huku akimpa elfu mbili.
“Nashukuru dada yangu.”
Waliachana na yule kijana na kufuata maelekezo yake, walipofika barabara ya tatu inayoingia kulia waliifuata na kwenda mwendo kidogo mpaka kufika kwa mganga Njiwa Manga. Walipaki gari sehemu iliyo salama na kutelemka, ilikuwa sehemu yenye eneo kubwa lililokuwa na nyuma kubwa moja na pembeni kulikuwa na mabanda madogo.
“Karibuni,” binti mmoja aliyekuwa amevalia gauni refu na kitambaa kichwani aliwakaribisha.
“Asante,” waliitikia kwa pamoja.
“Karibuni kwenye benchi hapo chini ya mti.”
“Asante,” walikwenda wote kukaa chini ya mti kusubiri maelekezo.
Ilipita zaidi ya saa nzima bila kupata maelezo yoyote zaidi ya kukaribishwa kana wageni wengine na kuonesha sehemu ya kukaa.
“Samahani dada,” Sharifa alimwita yule msichana aliyewakaribisha na kuendelea kuwakaribisha wageni wengine kama watatu, mmoja alikuja na gari na wengine wawili walikuja kwa miguu kuonesha walikuja na usafiri wa daladala.
“Bila samahani,” alisema huku akisogea kuwasikiliza.
“Eti mganga tumemkuta?”
“Yupo, kama asingekuwepo nisingewaacha mkae mpaka muda wote huu.”
“Kwa hiyo tutaonana naye saa ngapi?”
“Mmh! Sijajua ila si muda mrefu, leo hakuna wagonjwa wengi.”
“Wengine wapo wapi?”
“Wapo ndani, wakipungua nanyi mtaingia.”
“Haya,” waliachana na yule msichana aliyerudi sehemu yake kusubiri wateja wengine.
Baada ya nusu saa waliitwa ndani, wakati huo ilikuwa imefika saa tatu na nusu asubuhi. Waliongozana wote watatu mpaka kwenye sebule kubwa iliyokuwa imetandikwa zuria bila kiti. Baada ya kuketi msichana aliyewafuata aliingia chumbani na kuwaacha wasubiri.
Ilipita kama robo saa tena waliitwa ndani, waliingia wote watatu. Chumbani kulikuwa na mzee wa makamo aliyeonekana kula chumvi nyingi kutokana na kuenea mvi sehemu kubwa ya nywele zake. Alionekana ni mtu wadini kutokana na mavazi yake ya kanzu iliyokuwa nyeupe sana na juu alivalia kilemba cheupe. Pembeni yake kulikuwa na msahafu.
“Asalamu aleykum,” mama Sharifa alimsalimia mganga.
“Waleyku msalamu, karibuni.”
“Asante,” waliitikia kwa pamoja.
“Shikamoo,” Sharifa na Suzana walimwamkia mganga.
“Marahaba mabinti zangu, karibuni.”
“Asante.”
“Haya, mna shida gani?”
“Kuna vitu vimewatokea mabinti zangu, mpaka sasa vinawachanganya, japo kuna sehemu tulikwenda na kuelezwa tatizo lao, mmoja hakuwepo na mwisho wa yote ilionesha tatizo lile kwa upande wake ni zito hivyo alituelekezwa kuja kwako,” mama Sharifa alitoa maelezo mafupi.
“Mmh, nimekupateni, nipe majina yao.”
Nini kitaendelea, watapata msaada kwa mganga Njiwa Manga?