Hadithi ya Kweli: Jini wa Daraja la Selander

Hadithi ya Kweli: Jini wa Daraja la Selander

sorry ep.21 imefutika....

IIPOISHIA;
“Ewe mwanadamu, acha kumkosea heshima mtukufu mfalme, kila utakalojibu tanguliza neno mtukufu mfalme.” Mkuu wa watwana alimkumbusha tena Brighton.
“Ndiyo mtukufu mfalme.”
“Vizuri, Balkis.”
“Mtukufu Mfalme.”

“Unajua sababu ya kukutuma duniani?”
“Ndiyo mtukufu mfalme.”
“Mbona imekuwa kinyume?”
“Mtukufu mfalme nimekwisha kujibu kila kitu.”
“Bado hujanibu.”

“Unataka jibu gani mtukufu mfalme?”
“Sababu kuu ya kukutuma huko, hujanijibu.”
“Ni kweli mtukufu mfalme shida kubwa ni kuongeza familia yetu.”
“Sasa kwa nini umekaidi amri yangu, nakuomba urudi duniani akaifanye kazi niliyokutuma.” SASA ENDELEA...

“Mtukufu mfalme, kupitia huyu mwanadamu nitapata mtoto unayemtaka. Nina imani tatizo lilikuwa damu zetu kukosa virutubisho. Lakini damu ya mwanadamu huwa ina virutubisho vingi.”
“Hatutaki mtoto mchanganyiko.”
“Lakini mtukufu mfalme si atakuwa mwanangu?”
“Sipo tayari kuchanganya damu.”

“Mtukufu mfalme, nami sipo tayari kumpoteza mpenzi wangu.”
“Tunabishana?” mfalme Barami alikuja juu.
“Baba hatubishani, ila ukweli ni huo.”
“Mwana wa mfalme mwite mtukufu mfalme si baba,” mtwana mkuu, Kulani alimwambia Balkis aliyekuwa amemvunjia heshima baba yake na kusimama wima.

“Wewe nani unayeingilia mazungumzo na baba yangu? Nani kakupa ruhusa ya kunikemea. Huna heshima, kibaraka mkubwa wee,” Balkis alimfokea mkuu wa watwana.
“Balkis umekosa heshima?” mfalme Barami alimfokea mwanaye.
“Sijakosa baba, natetea haki yangu.”

“Kulaniiii, wachukueni mkawaweke kwenye chumba cha giza haraka.”
Mfalme Barami alisema kwa sauti ya juu baada ya kumuona mwanaye amemvunjia heshima. Kulani na wenzake waliwabeba juu juu na kwenda kuwafungia katika chumba cha giza.

****
Suzana alishtuka siku ya pili na kujikuta akiwa amelala kwa mara nyingine kitandani kwake. Alijiuliza kuwa pale kitandani ni kweli au anaota, kumbukumbu zake zilimkumbusha kuwa jana yake alitoka nyumbani na kwenda ofisini na kisha alitoka.

Breki yake ya kwanza ilikuwa ofisini kwa shoga yake Sharifa na kumuelezea yaliyomsibu baada ya kulala kwa mpenzi wake Brighton, lakini ajabu siku ya pili alijikuta kitandani kwake. Alikumbuka baada ya kumuelezea shoga yake alimpa ushauri kabla ya kufanya lolote aende kwa Brighton kupata ukweli kama ni ndoto au kweli.

Suzana akiwa bado amekaa kitandani aliendelea kuvuta kumbukumbu ya mambo aliyoyafanya jana yake. Alikumbuka baada ya kushauriana na Sharifa aliaga kazini na kwenda moja kwa moja kwa mpenzi wake. Alipofika Brighton alionesha kubabaika hata majibu yake yalikuwa kama mtu aliyemfumaniwa.

Baada ya hapo hakumbuki kilichoendelea mpaka alipoamka na kujikuta tena kitandani kwake. Tukio la kujikuta kwake tena wakati anaamini jana asubuhi alikwenda kwa Brighton lilizidi kumchanganya akili.
Kabla hajafanya lolote simu yake iliita alipoangalia ilikuwa ya Sharifa, aliipokea na kuzungumza.

“Haloo Sharifa.”
“Eeh, Suzy vipi, ndiyo ukaondoka kimoja na simu ukazima. Lakini hiyo ni tabia gani ukiwa na tatizo tuko pamoja likikuishia ananisahau?” Sharifa alilalamika upande wa pili.
“Najua utanilaumu bila kujua.”
“Suzy hata kama ulichokifuata kimekwenda vizuri, kwa vile uliniacha na mimi na maswali ulitakiwa kunijulisha.”

“Sharifa nashindwa sijui nikuambie nini?”
“Uniambie nini Suzy? Kitendo cha kukosa uungwana kwa kweli siyo kizuri hasa tukiwa watu wa karibu.”
“Kabla sijakuambia kitu naomba nikuulize swali?”
“Uliza tu. ”

“Ni kweli jana nilikuja ofisini kwako asubuhi?”
“Mbona unaniuliza hivyo?”
“Shoga yangu nina maana kubwa sana ya kukuliza hivyo naomba unijibu usinidanganye.”
“Ni kweli ulikuja.”

“Si nilikuja kukueleza maajabu yaliyonitokea nilipolala kwa mpenzi wangu na kujikuta kitandani kwangu?”
“Ndiyo.”
“Ni kweli asubuhi sikufanya kazi nilikuaga nakwenda kwa Brighton.”
“Ndiyo.””Basi dada yangu yaliyonitokea juzi kuamkia jana ndiyo aliyonitokea jana kuamkia leo.”

“Una maana gani kusema hivyo?”
Suzana alimweleza yote aliyokutana nayo na siku ya pili alipoamka na kujikuta kitandani kwake.
“Suzana usiwe unachanganya mambo, pengine ulipotoka hapa badala ya kwenda kwa Brighton ulikwenda kwako ukalala na kupitiwa na usingizi mzito?”

“Sijafikia huko kiasi cha kupoteza kumbukumbuku hivyo, nilipotoka ofisini nilikwenda moja kwa moja kwa Brighton. Jamani hata kama nilirudi nyumbani asubuhi ile ndiyo nilale nishtuke asubuhi ya siku ya pili?”
“Mmh! Suzana kuna tatizo.”

“Yaani huwezi kuamini sasa ndiyo inajidhilisha kuwa kuna kitu kinanichezea akili.”
“Kwani Brighton yeye anasemaje?”
“Lazima na yeye atakuwa na tatizo, siku mbili hizi simwelewi kabisa, amekuwa kama mtu aliyechanganyikiwa.”

“Suzana umezidi ubishi kila kitu nilikueleza, lakini hutaki kuamini wacha yakukute.”

Suzana yupo njia panda anataka kujua yaliyomzunguka ni kweli au ni ndoto.
 
JINI LA DARAJA LA SALENDA........EP.23






“Tuache masihara, hebu nipelekwe kwa huyo mtaalamu, kilea kidonda mwisho kukatwa mguu.”
“Leo ndiyo unagundua, nilikueleza toka mwanzo kuwa majini wana hadaa inayokuchanganya na mwisho wa siku wanakuingiza sehemu mbaya.”
“Sharifa huu si wakati wa kunilaumu, nahitaji msaada wako la sivyo nitachanganyikiwa.”
“Kama upo tayari, twende pamoja Bagamoyo.”

”Lini?”
“Leo hii.”
“Saa ngapi?”
“Safari yetu itakuwa saa tatu?”
“Basi shoga tutakuwa wote hali inatisha.”

Walikubaliana kwenda wote Bagamoyo, baada ya kukata simu Suzana alinyanyuka kitandani ili kujiandaa na safari ya Bagamoyo.
Baada ya maandalizi waliingia kwenye gari kwenda nyumbani kwa Sharifa kumpitia kwenda kwa mganga Bagamoyo. Njiani alijitahidi kumpigia simu Brighton simu yake haikuwa hewani, aliachana naye na kuendelea na safari yake mpaka kwa Sharifa.

Aliwakuta wameisha jiandaa wakimsubiri, walipomuona tu hawakutaka kupoteza muda.
“Jamani tutatumia magari yote?” Suzana aliuliza.
“Hakuna haja ya kutumia magari yote, moja tu linatosha”
“Hakuna tatizo.”

Walikubaliana kwenda kwenye usafiri mmoja walipanda kwenye gari la Sharifa na kuelekea Bagamoyo. Walitumia dakika arobaini na tano kufika Bagamoyo, walipofika waliuliza wenyeji sehemu aliyopo mganga Njiwa Manga.
“Samahani kaka,” Sharifa alimuuliza kijana mmoja aliyepita karibu na mlango wa gari lake.
“Bila samahani dada yangu,” kijana yule alijibu huku akisogea karibu.
“Habari za saizi?”

“Nzuri tu dada.”
“Eti, Njiwa Manga anaishi wapi?”
“Njiwa Manga! Yupi, yule mganga?”
“Eeh, huyo huyo.”
“Unaona hii barabara kubwa?”
“Ndiyo.”

“Ifuateni, acha barabara ndogo mbili zinazokatisha kulia, ya tatu ufuate nenda moja kwa moja mpaka mbele utaona kuna nyumba ina bendera nyekundu hapo hapo kwa mzee Njiwa Manga.”
“Asante,” Sharifa alishukuru huku akimpa elfu mbili.
“Nashukuru dada yangu.”

Waliachana na yule kijana na kufuata maelekezo yake, walipofika barabara ya tatu inayoingia kulia waliifuata na kwenda mwendo kidogo mpaka kufika kwa mganga Njiwa Manga. Walipaki gari sehemu iliyo salama na kutelemka, ilikuwa sehemu yenye eneo kubwa lililokuwa na nyuma kubwa moja na pembeni kulikuwa na mabanda madogo.
“Karibuni,” binti mmoja aliyekuwa amevalia gauni refu na kitambaa kichwani aliwakaribisha.
“Asante,” waliitikia kwa pamoja.

“Karibuni kwenye benchi hapo chini ya mti.”
“Asante,” walikwenda wote kukaa chini ya mti kusubiri maelekezo.
Ilipita zaidi ya saa nzima bila kupata maelezo yoyote zaidi ya kukaribishwa kana wageni wengine na kuonesha sehemu ya kukaa.

“Samahani dada,” Sharifa alimwita yule msichana aliyewakaribisha na kuendelea kuwakaribisha wageni wengine kama watatu, mmoja alikuja na gari na wengine wawili walikuja kwa miguu kuonesha walikuja na usafiri wa daladala.
“Bila samahani,” alisema huku akisogea kuwasikiliza.
“Eti mganga tumemkuta?”

“Yupo, kama asingekuwepo nisingewaacha mkae mpaka muda wote huu.”
“Kwa hiyo tutaonana naye saa ngapi?”
“Mmh! Sijajua ila si muda mrefu, leo hakuna wagonjwa wengi.”
“Wengine wapo wapi?”
“Wapo ndani, wakipungua nanyi mtaingia.”

“Haya,” waliachana na yule msichana aliyerudi sehemu yake kusubiri wateja wengine.
Baada ya nusu saa waliitwa ndani, wakati huo ilikuwa imefika saa tatu na nusu asubuhi. Waliongozana wote watatu mpaka kwenye sebule kubwa iliyokuwa imetandikwa zuria bila kiti. Baada ya kuketi msichana aliyewafuata aliingia chumbani na kuwaacha wasubiri.

Ilipita kama robo saa tena waliitwa ndani, waliingia wote watatu. Chumbani kulikuwa na mzee wa makamo aliyeonekana kula chumvi nyingi kutokana na kuenea mvi sehemu kubwa ya nywele zake. Alionekana ni mtu wadini kutokana na mavazi yake ya kanzu iliyokuwa nyeupe sana na juu alivalia kilemba cheupe. Pembeni yake kulikuwa na msahafu.
“Asalamu aleykum,” mama Sharifa alimsalimia mganga.

“Waleyku msalamu, karibuni.”
“Asante,” waliitikia kwa pamoja.
“Shikamoo,” Sharifa na Suzana walimwamkia mganga.
“Marahaba mabinti zangu, karibuni.”
“Asante.”
“Haya, mna shida gani?”

“Kuna vitu vimewatokea mabinti zangu, mpaka sasa vinawachanganya, japo kuna sehemu tulikwenda na kuelezwa tatizo lao, mmoja hakuwepo na mwisho wa yote ilionesha tatizo lile kwa upande wake ni zito hivyo alituelekezwa kuja kwako,” mama Sharifa alitoa maelezo mafupi.
“Mmh, nimekupateni, nipe majina yao.”

Nini kitaendelea, watapata msaada kwa mganga Njiwa Manga?
 
JINI LA DARAJA LA SALENDA........EP.25.

LIPOISHIA:
“Nina imani mmebahatika kumuona Balkis jinsi alivyo mwanamke mzuri sana, ambaye hakuna mwanaume atakayemtaka akamkataa. Mchumba’ako akaingia kichwa kichwa kumtaka kimapenzi, kana kwamba hana shida na mumeo, alipoonesha dalili za kumtaka alimuuliza maswali ya mitego, kama angekuwa na akili angetambua kuwa yule si mtu wa kawaida. SASA ENDELEA...

Lakini kutokana na kuchanganyikiwa na mapenzi, hakupata muda wa kujiuliza, Balkis alimuuliza maswali kuhusiana na uhusiano wenu, hakushangaa mtu kuonana naye mara ya kwanza kumuulizia vitu ambavyo hata watu wenu wa karibu hawajui.

Alipomuulizia kuhusu kumtaka yeye wakati wewe ni mchumba wake, mwenzio alikukana na kusema kuwa wewe ni mpenzi wake si mke wake. Alipoulizwa kama yupo tayari kuoa mwanamke mwingine na kuachana na wewe, kutokana na kiwewe cha mapenzi alikubali kuwa yupo tayari na kuusema udhaifu wako.

“Alipoulizwa tena yupo tayari kumuoa yeye Balkis alikubali. Aliutumia udhaifu wa mchumba wako kujenga uhusiano wa haraka na kutaka kuwa naye siku ile, pia alikubali. Walikubaliana kwenda nyumbani kwa mchumba wako, ili kutowagonganisha, mchumba wako alitaka kukupigia simu ili usiende, lakini Balkis alimzuia asikupigie simu na kukueleza uende na ulipokwenda ulimuona jinsi alivyobabaika baada ya kuingia na kwenda moja kwa moja chumba cha wageni alichokuwa ameingia Balkis muda ule ule. Ulishtuka baada ya kumuona ameingia ghafla chumbani, ni kweli?”

“Ni kweli,” Suzana alijibu kwa sauti ya chini huku akiwa anaona muujiza mkubwa kutokana na maneno ya mganga ambayo mwanzo aliyaona kama simulizi ya kusisimua isiyo na ukweli. Lakini swali lile lilikuwa kama kitu kilichomtoa kwenye bumbuwazi.

“Basi kitendo cha kuingia na kwenda moja kwa moja kilimtia wasiwasi mkubwa mchumba wako kwa kujua lazima utamkuta Balkis na kumfumania. Hata lugha zenu ziligongana kitu kilichokushangaza. Kingine kilichokushangaza kilikuwa kwa mpenzi wako kuwa tofauti na siku zote kukujibu kwa ukali jambo la kawaida.

Baada ya kumuona humuelewi, ulikwenda chumba cha kulala, yeye alirudi hadi chumba cha wageni na kushangaa kumkuta Balkis akiwa amejaa tele kitandani. Alipotaka kujua alikuwa wapi alimwambia akuwahi chumbani ili akurudishe kwenye hali ya kawaida.

Baada ya kuingia chumbani, penzi alilokupa ndilo lilikuchanganya na kusahau yaliyotokea muda mfupi. Usiku jini Balkis alikuja kukuchukua ukiwa usingizini na kukurudisha kwako na yeye kulala na mchumba wako mpaka asubuhi. Wote mlipoamka mlishtuka lakini hakuna aliyejua ukweli wa tukio la usiku ni kama ndoto au kweli.

Ulipokwenda kwake asubuhi ya jana kupata uhakika kwa kilichotokea, ndani walikuwa mchumba wako na Balkis, ndiye aliyemweleza ujio wako. Ulipofika alikuwa mule mule chumbani amelala kitandani. Wewe hukumwona ila mwenzako alimwona kama kawaida, kitu kile ndicho kilichompa kigugumizi.

Hali ile ilikuchanganya na kumuona kama mtu mwenye matatizo, wakati huo Balkis alimwambia mchumba wako kwa sauti ya juu ya kumkemea kuwa akikuuliza useme hukuja jana ili ujue kilichotokea si kweli bali ni ndoto.

Lakini kwa yeye kuwepo pembeni ya kitanda karibu na Balkis aliyekuwa amelala pembeni yako bila wewe kumuona, ilizidi kumchanganya.

Mchumba wako alipatwa na kigugumizi kwa kujua utanamuona Balkis, kubabaika kwake kulikufanya umtilie wasiwasi na kumuuliza swali ambalo lilimchanganya pale ulipotaja jina la Balkis kama jini, jina ambalo lilikuwa la mpenzi wake, kumtaja kama jini ilimuudhi sana Balkis na kukupuliza upepo uliokufanya upoteze fahamu.

Kitendo kile mchumba wako alikiona na kumpandishia na kutaka kujua amekufanyia nini, Kauli ile ilimfanya Balkis kukasirika na kuondoa nguvu za kiume za mchumba wako na kutaka nawe kukutoa kizazi.”

“Mama yangu!” Suzana alishtuka na kushika mdomo kusikia vile.
“Usiogope, hakukutoa kizazi baada ya mchumba wako kumuomba msamaha na kuwa tayari kumuoa baada ya kumkataa kutokana na vitendo vyake visivyo vya kawaida. Baada ya Balkis kumsamehe aliamua kuondoka naye kwenda kuishi chini ya bahari.”

“Mamaaa!” Suzana alipiga mayowe ya mshtuko.
“Mungu wangu unataka kutuambia Brighton yupo ujinini?” Mama Sharifa aliuliza.
“Ndiyo, lakini kwa sasa yupo katika matatizo.”
“Matatizo! Matatizo gani tena jamani?” Suzana aliuliza kwa huzuni.

“Baada ya kufika katika mji wa majini, baba mzazi wa Balkis alishtuka kuona mwanaye amekwenda na mwanadamu akimsema ndiye mume wake badala kupeleka alichotumwa.
Hapo palitokea kutoelewana kati ya Balkis na baba yake, baba akitaka mwanaye arudi duniani kuendelea kutafuta vizazi zaidi vya wanawake ili apate dawa ya kuweza kupata ujauzito ili aolewe na jini mwenzake.

Lakini Balkis hakuwa tayari kuolewa na jini mwenzake baada ya kuonja penzi la mwanadamu. Yeye aliamini kuolewa na mwanadamu kusingekuwa na haja ya kuendelea kuwatoa uzazi wanawake. Kwani angekutana kimwili na mwanadamu angeweza kupata bila kutumia dawa hiyo.

Hapo ndipo palipozuka mvutano wa mtoto na baba, Balkis aliamini kwa vile anapendwa sana na baba yake atakubaliwa, lakini baba yake hakuwa tayari kuchanganya damu ya jini na mwanadamu. Baada ya kuona mtoto wake amemkosea adabu, alimuamuru mkuu wa Watwana anaitwa Kulani, Jini mweusi lakini mwenye nguvu. Kumchukua Balkis na mchumba wako kuwapeleka katika chumba cha giza.”

“Kwa hiyo ndiyo harudi tena?” Suzana aliuliza.
“Anaweza kurudi lakini mpaka atoke sehemu aliyofungwa.”
“Bila ya hivyo hawezi kutoka?” Sharifa aliuliza.

“Inategemea na uamuzi wa mfalme wa bahari kumtoa.”
Mambo yanazidi kuwa mazito. Je, Brighton atapona au atauawa katika mji wa majini? Mganga njiwa Manga atawasaidia?
 
Ilipoishia:
“Bila ya hivyo hawezi kutoka?” Sharifa aliuliza.
“Inategemea na uamuzi wa mfalme wa bahari kumtoa.”Sasa endelea:


“Hawezi kumuua?” Suzana aliuliza kwa sauti ya kukata tamaa.
“Hawezi, nina imani atatoka tu, kinachotakiwa ni kuvuta subira.”
“Mmh! Na mimi tatizo langu?” Sharifa aliuliza.

“Wewe tatizo lako limepata bahati moja kubwa ambayo sawa na bahati ya mtende.”
“Bahati gani?” Sharifa aliuliza huku akijiweka sawa.
“Kitendo cha kufungiwa Balkis katika chumba cha giza, kimewawezesha kuja huku bila ya matatizo.
“Una maana gani?” Sharifa aliuliza.

“ Majini ni viumbe wasiokubali kuona wanavurugiwa mipango yao, Balkis kama angekuwa hajafungiwa lazima angeizuia safari yenu.”
“Angeizuia kivipi?”
“Mngekutana na vitu vya ajabu njiani hata kupinduka na gari lenu.”
“Si tungekufa?”

“Msingekufa, mngeumia tu ili msiweze kumfuatilia.”
“Na bahati nyingine?”
“Bahati nyingine wakati wa kufanya dawa ya kurudisha kizazi chako hakutakuwa na upinzani wowote. Wala kazi yako haitahitaji vitu vingi vya kufanya na itaanza leo saa sita za usiku baharini.”
“Kama angekuwepo?”

“Mmh! Pangechimbika, waganga wengi wamepoteza maisha kwa ajili ya kutaka kuvuruga mipango ya majini. Pia tungehitaji vitu vya gharama ili kumdhibiti hapo kazi ingetakiwa kufanyika saa nane za usiku baharini katika maji ya shingo.”
“Mmh! Sasa akitoka si ataweza kutuua?”

“Balkis ni jini lenye huruma sana, katika maisha yake hapendi kufanya vitu vibaya, hata kuolewa ilikuwa ni shinikizo la wazazi wake tu ambao walimlazimisha kutafuta vizazi vya wanawake ili aweze kupata tiba ya matatizo yake ya kushindwa kupata ujauzito.

“Mwanzoni alikataa katakata lakini aliahidiwa kupewa zawadi kubwa kama atapata mtoto hasa wa kiume. Alikubali kuifanya kazi ile kwa shingo upande, lakini moyoni mwake hakupenda hata siku moja kutenda kitendo chochote kibaya kwa wanadamu, siku zote aliwaza kuishi duniani na kuolewa na binadamu.

“Hata kazi ya kutoa vizazi ilimchukua muda mrefu sana, kitu kilichowafanya wazazi wake kumleta duniani moja kwa moja ili aweze kupata vizazi hivyo kwa muda mfupi, bila kujua Balkis hakupenda kuifanya kazi ile.

“Siku Suzana alipoona sherehe ya ajabu juu ya bahari, hiyo ndiyo ilikuwa siku rasmi ya kuja duniani kwa Balkis kusaka vizazi vya wanawake na kuvipeleka baharini. Aliandaliwa jini mwingine ambaye kazi yake ilikuwa ni kuvipokea vizazi hivyo juu ya bahari katika eneo lile la Daraja la Salenda na kuvipeleka kwenye stoo chini ya bahari.

“Lakini ilikuwa tofauti na walivyotegemea wazazi wake, tangu Balkis alipofika rasmi duniani kwa kazi hiyo, kwa siku moja alipeleka vizazi vinne tu na chako kikiwa kimojawapo.
Kazi aliyotumwa alisahau baada ya kuvutiwa na uzuri wa mchumba wa Suzana na kujikuta akianzisha uhusiano wa siri bila mwenzako kujua.

“Katika harakati za kuhakikisha anamdhibiti mchumba wako, muda mwingi aliutumia kuhakikisha anamchukua jumla badala ya kuifanya kazi aliyotumwa.
“Aliweza kuwagonganisha kwa kuziua nguvu za kiume za mchumba wako na usiku ulipoingia alizirudisha ili afaidi yeye.

“Hali ile ndiyo iliyowasukuma kutafuta suruhu ya tatizo lenu, alipoona mmeanza kupata mwanga aliwachanganyeni kwa kuzirudisha kitu kilichokufanya uone kama hakuna tatizo.Balkis alipofanikiwa kumnasa mchumba wako kwenye mtego wake, hakupanga kuondoka naye mapema.
“Mngeendelea kushea mapenzi bila wewe kujua mpaka angeshika ujauzito.
“Kosa alilolifanya mchumba wako ni kwenda kinyume na yale aliyokuwa akielekezwa na Balkis.

“Kubabaika kwake kulipelekea wewe kuingia wasiwasi na kutamka neno lililomchukiza Balkis na kukupulizia hewa iliyokupoteza fahamu.
Hali ile ilimfanya Balkis aone mpango wake umeharibika mapema, ili asiweze kumpoteza mpenzi wako aliamua kuondoka naye kwenda chini ya bahari.

“Kutokana na huruma yake aliamini kama ataolewa na binadamu atakuwa ameokoa tatizo la wanawake kutolewa vizazi. Lakini ilikuwa tofauti na walivyotegemea wazazi wake ambao wao walimtuma kuishi duniani ili kufanikisha kupatikana kwa vizazi vingi vya mwanamke vitakavyomuwezesha kupata dawa ya kushika ujauzito ili aolewe na jini mwenzake.

“Walishangaa kumuona akiwa na mwanaume wa kibinadamu na kumtambulisha kwao kama ni mume wake. Kitendo kile kiliwaudhi sana, naye hakutaka kukubali.Baada ya mvutano Balkis na mchumba wako waliwekwa kwenye chumba cha giza.”
“Sasa kama unasema wazazi wake hawakukubali wataweza kumtoa salama Brighton?” Suzana aliuliza.

“Hapa inaonesha maisha yake yapo zaidi ya hapo, Kwa hiyo hawezi kuuawa.”
“Kama umeona anaweza kuendelea kuishi, itakuwa wapi duniani au kuendelea kufungwa kwenye chumba cha kiza?” Suzana alikuwa na shauku kutaka kujua hatma ya mchumba wake.
“Kwa kweli haioneshi ataishi wapi ila kuna maisha marefu ya mchumba wako.”
“Vipi kuhusu kazi yangu ya kurudisha kizazi kuna vitu vinatakiwa kwenda kununua?” Sharifa aliuliza.

“Anatakiwa njiwa mwekundu tu, kwenye mabanda yangu anapatikana.”
“Na mimi kumpata mchumba wangu utanisaidiaje?”
 
LIPOISHIA;
“Sasa kama unasema wazazi wake hawakukubali wataweza kumtoa salama Brighton?” Suzana aliuliza.

“Hapa inaonesha maisha yake yapo zaidi ya hapo, kwa hiyo inamaanisha hawezi kuuawa.”
“Kama umeona anaweza kuendelea kuishi, itakuwa wapi duniani au kuendelea kufungwa kwenye chumba cha giza?” Suzana alikuwa na shauku kujua hatima ya mchumba wake.

“Kwa kweli haioneshi ataishi wapi ila kuna maisha marefu ya mchumba wako.”
“Na kuhusu kazi yangu ya kurudisha kizazi kuna vitu vinatakiwa kwenda kununua?” Sharifa aliuliza.
SASA ENDELEA...

“Anatakiwa njiwa mwekundu tu, kwenye mabanda yangu atapatikana.”
“Na mimi kumpata mchumba wangu utanisaidiaje?”
“Kama akitoka kwenye chumba cha giza tutampata, lakini kumtoa kule ni kazi ngumu, haonekani kila nikimtafuta.”

“Kwa hiyo utanisaidia vipi?”
“Kwa vile kazi ya mwenzako ni nyepesi ngoja tuifanye usiku wa leo, ya kwako itabidi nichimbe sana kuona kama kuna uwezekano wa kumtoa hata akiwa chumba cha giza.”
Walikubaliana kuifanya kazi ile usiku wa siku ile, mganga aliwaruhusu wakapate chakula na kupumzika ili kuvuta muda.
***
Majira ya saa sita usiku Sharifa alisimamisha gari lake pembeni kabisa na bahari maeneo ya pwani ya Bagamoyo, sehemu aliyoelekezwa na Mganga Njiwa Manga. Hali ya hewa ilikuwa giza la wastani, kwa mbali ilionekana miale ya moto ya wavuvi wa usiku.
Baada ya kusimamisha gari hakuteremka walisubiri maelekezo ya mganga. Mganga Njiwa Manga alianza kuteremka kisha aliwaita, wote walitoka nje ya gari.

Baridi la ufukweni lilikuwa kali, kila aliyekuwepo pale lilimchonyota hadi kwenye mifupa. Mganga alitoa vifaa vya kufanyia kazi, njiwa wa kazi alikuwa ameshikiliwa na Sharifa.

Wote walikuwa kimya wakimsikiliza mganga ambaye alikuwa akitembea kuelekea baharini, mawimbi muda ule hayakuwa makali sana yalipiga taratibu. Mganga aliingia majini usawa wa maji ya mafuti na kumwaga vitu huku akizungumza maneno kwa sauti ya juu.
“Ewe jini la bahari nakuletea zawadi hii ili bahari iwe tulivu, pia nimekuletea zawadi ya njiwa ili kuniruhusu niifanye kazi yangu bila kikwazo.”

Baada ya kusema vile aligeuka bila kutoka ndani ya maji na kumwita Sharifa.
“Kavue nguo zote kisha ujifunge upande wa kanga halafu uingie ndani ya maji na njiwa wako.”

Sharifa alifanya kama alivyoelekezwa na mganga, aliingia ndani ya maji na kuwaacha mama yake na Suzana wakiwa wamesimama huku wakiendelea kupigwa na baridi kali ya upepo utokao baharini. Aliingia ndani ya maji ya baridi huku akiwa na hofu ya kutojua mganga anataka kumfanya nini hasa akiwa amejifunga upande wa kanga bila kitu chochote mwilini.

Alipomfikia mganga alisogea naye mbele hadi maji ya shingo njiwa wake akiwa amemnyanyua juu. Baada ya kufika kimo kile cha maji, mganga alimwambia Sharifa amuweke kichwani, naye alifanya vile. Mganga alimshika sikio la kushoto na kuanza kuomba kwa lugha ya kiganga.

Aliomba kwa kuzungumza maneno haraka haraka bila kumeza mate kwa zaidi ya nusu saa. Baada ya robo saa Sharifa alianza kusikia vitu vikikoroga tumboni, Sharifa alishindwa kufanya kitu kutokana na mikono kuwa kichwani amemshikilia njiwa.

Mganga aliendelea kuzungumza maneno ya kiganga akiwa bado amemshikilia sikio, tumbo nalo liliendelea kumkoroga huku mwili ukizidi kupungua nguvu. Mara alianza kuona kiza mbele na kuangukia ndani ya maji na njiwa wake mkononi.

Mganga aliwahi kumdaka na kujitahidi kumsimamisha lakini miguu haikuwa na nguvu, alipiga kelele kuomba msaada kwa mama Sharifa na Suzana waliokuwa nje ya maji. Nao walijikuta wakiingia kwenye maji na nguo zao bila kujijua kuwahi kutoa msaada kwa mganga.

Walipofika ndani ya maji ya shingo walimsaidia mganga kumsogeza ufukweni, walipofika ilionesha kama Sharifa amepoteza fahamu.
“Mganga mbona hivi?” Mama Sharifa aliuliza.
“Ni kawaida kuna kitu kilikuwa mwilini mwake kimetoka lakini baada ya muda atakuwa katika hali ya kawaida.”

Pamoja na Sharifa kupoteza fahamu mganga aliwaomba wambebe hadi ndani ya maji ili aendelee na tiba yake.
“Sasa baba si unamuona alivyo kwa nini tusisubiri arudiwe na fahamu kisha uendelee na tiba?” Mama Sharifa aliuliza akiwa amejawa na wasiwasi juu ya hali ya mwanaye.
“Mama unanifundisha kazi?” Mganga alimuuliza kwa sauti ya ukali.
“Samahani baba.”

“Sipendi kufundishwa kazi kama ulikuwa unajua kwa nini mlimleta kwangu?”
“Nisamehe baba yangu.”
“Basi naomba kila utakachokiona hapa ukae kimya.”
“Nimekuelewa baba yangu nisamehe sana.”
“Haya mbebeni muda unakwenda.”

Mama Sharifa na Suzana walimbeba Sharifa mpaka maji ya chini ya mafuti mganga alimuomba Suzana akae chini ili ampakate mgonjwa. Suzana alifanya kama alivyoelezwa na mganga kisha Sharifa alilazwa chali juu ya Suzana. Mama yake alimshika sehemu ya kichwani ili kisiingie kwenye maji. Baada ya kulazwa mganga aliendelea na tiba yake kwa kuendelea kusema maneno ya kiganga kwa zaidi ya nusu saa. Huku njiwa aliyekuwa amelowana akimshikilia kwenye tumbo la Sharifa.

Baada ya muda mganga alinyamaza ghafla na kupita kimya kizito kikifuatiwa na upepo mkali. Baada ya muda upepo ulikoma. Suzana na mama Sharifa kila mmoja aliingiwa na wasiwasi kutokana na hali iliyojitokeza mle baharini. Kila moja alimuomba Mungu kimoyomoyo.

Baada ya upepo kutulia ilisikika sauti ya Sharifa ikiita.
“Mama...mama...mama.”
Mama Sharifa hakuitikia alimuangalia mganga aliyekuwa bado akitazama upepo ulipotokea na kunyanyua mkono.
 
ILIPOISHIA:
“Nipo mimi” Suzana alijibu.
“Haya fanyeni haraka mkimaliza mniite.”
Walimbeba Sharifa ambaye hakuwa na nguvu hadi ndani ya gari na kumbadili nguo zake kisha walimwita mganga ili waondoke kurudi nyumbani.
SASA ENDELEA...

Mganga aliingia kwenye gari, Suzana aliliendesha mpaka nyumbani kwa mganga, walipofika walimteremsha Sharifa ambaye alitembea kwa tabu. Walipomfikisha sebuleni walimlaza kwenye mkeka na kumsuburi mganga aliyekuwa amemshika njiwa aliyekuwa tayari ameshamchinja tangu baharini.

Mganga alimwomba mkewe awape nguo za kujifunga wateja wale kutokana na nguo zao kulowana na maji ya bahari walipokuwa wakimtoa Sharifa kwenye maji. Baada ya kubadili nguo alimpa mkewe yule njiwa na kumweleza amnyonyoe na kumchemsha. Mkewe alimchukua na kuondoka naye na kuwaacha kina Suzana sebuleni.

Majira ya saa kumi za usiku mganga alimwamsha Sharifa na kumpa dawa ya njiwa aliyechemshwa kwa ajili ya kumla akiwa katika sufuria ile ile aliyochemshiwa.
“Mle njiwa wote na unywe na supu yake,” mganga alimwambia Sharifa ambaye bado mwili wake ulikuwa hauna nguvu.

Sharifa alianza kumla njiwa na kunywa supu yake kwa shida kwa vile alichemshwa bila kuwekwa chumvi, alipomuona kama anamshindwa kutokana na kutokuwa na kiungo hicho aliuliza.

“Mbona hana chumvi?”
“Huyo hawekwi chumvi, jitahidi umle vivyo hivyo, tena una bahati njiwa ni mdogo, watu wanakula kuku mzima bila chumvi.”

Sharifa hakuongeza neno alimuinamia njiwa wake na kuendelea kumla taratibu mpaka alipommaliza, wakati huo Suzana na mama yake walikuwa wakikoroma. Baada ya kumaliza kumla njiwa aliruhusiwa kuendelea kulala na wenzake ambao walikuwa hawajitambui kwa usingizi.

Wote waliamshwa alfajiri kwa ajili ya tiba ya mwisho ya kuoga maji ya bomba yaliyochanganywa na yale ya baharini. Baada ya kuoga waliingia kwenye chumba cha mganga kwa ajili ya mazungumzo ya mwisho kabla ya kuruhusiwa kwenda nyumbani.

Wote walikaa kwenye mkeka baada ya mganga kutulia kwa muda huku akipitia maelezo kwenye karatasi nyeupe iliyoandikwa kwa wino mwekundu kisha alisema kwa sauti ya chini:
“Nina imani kazi yetu imekwenda vizuri sana tofauti na nilivyofikiria, shughuli kama hii niliifanya siku za nyuma kwa muda wa wiki nzima, tena nikiwa na majeraha mengi kutokana na kushindana na jini.”

“Unataka kuniambia nimepona?” Sharifa aliuliza.
“Umepona.”
“Kwa hiyo nina uwezo wa kushika mimba?”
“Bila shaka.”

“Nashukuru sana mzee wangu,” Sharifa alinyanyuka kwa lengo la kumpigia magoti.
“Hapana mama kaa tu, wakushukuriwa ni Mungu yeye ndiye mwenye kukubali au kukataa maombi yetu.”

“Ina maana kama Balkis angekuwa hakufungwa kazi isingeisha leo?” Suzana aliuliza.
“Kazi ya kushindana na majini ni ngumu msione imekwenda kirahisi kiasi kile, kama Balkis angekuwa hajafungwa vita ingekuwa kubwa asingekubali tuchukue kizazi katika stoo yake. Lazima ingetakiwa niwe na vijana wangu wa kazi na katika kumdhibiti wangetakiwa mbuzi wekundu wawili, shuka nyekundu mbili na vitu vingine vingi.”

“Kutokana na kauli za mganga wa awali kuwa matatizo mengi ya tumbo yanatokana na jini Balkis kuchukua vizazi vya wanawake, lakini mbona ni wanawake wengi wana matatizo tofauti na idadi ya vizazi vilivyoko kwenye stoo ya Balkis?” Sharifa aliuliza.

“Kama nilivyowaeleza majini wanaishi kama wanadam, jinsi matatizo yetu yanavyofanana basi na ya majini huwa ni vivyo hivyo. Majini wengi wenye matatizo ya kukosa uzazi hutumwa duniani kuifanya kazi kama ya Balkis, hivyo vita si vyake peke yake ni kwa majini wengi.”

“Mungu wangu sasa tutapona vipi?” Suzana aliuliza.
“Kupona inategemea na wewe kuonana na watu wenye uwezo kama sisi au kusimama katika imani yako.”
“Kusimama kwenye imani una maana gani?” Sharifa aliuliza.

“Kila anayesimama katika imani humtanguliza Mwenyezi Mungu mbele kwa kila jambo, kabla ya kulala huomba ulinzi wake na baada ya kuamka humshukuru kwa kumvusha usiku salama, kisha humuomba tena amlinde na mchana wote.”
“Mbona tunafanya hivyo?” Alisema Suzana.

“Unaweza kuwa unafanya kutimiza wajibu wa maombi lakini imani yako si kamili, siku zote imani husimama kwa matendo siyo kwa maneno.”
“Unataka kuniambia aliyesimama kwa imani ya matendo mema hawezi kupatwa na tatizo hili?’

“Litaingilia vipi wakati Mungu ndiye mlinzi wake, hata hao majini wanamuogopa na kumuabudu yeye.”
“Kutokana na maelezo yako sasa hivi nimepona kabisa?” Sharifa aliuliza.
“Umepona na wala haitakutokea tena.”
“Kwa mfano Balkis akitoka gerezani, akijua nimerudishiwa kizazi changu si litakuwa tatizo?”

“Tatizo litabakia kwake, wewe utakuwa salama kuanzia asubuhi hii.”
“Ile hali ya tumbo kuvurugika nilipokuwa pale baharini ilitokana na nini?”
“Kizazi chako kilikuwa kikirudi sehemu yake.”

“Baba tunashukuru kwa msaada wako,” mama Sharifa alisema kwa niaba ya mwanaye.
Nini kiliendelea?
 
ILIPOISHIA;
Uso wake ulionesha huzuni kitu kilichomtisha mumewe ambaye alitaka kujua kulikoni.
“Vipi mahabuba wangu?”
“Mambo yameharibika.”
“Kivipi?”

“Mpango wetu umeingia kwenye mtihani wa kwanza.”
“Mtihani upi?”
“Kizazi kimoja kimechukuliwa.”
“Tufanye haraka kabla hakijarudishwa kwa mwenyewe tumtume Kulani akaifanye kazi hii kabla hakujapambazuka.”

“Tumechelewa tayari kimeisharudishwa kwa mwenyewe.”
“Umejuaje?”
“Damu ya sehemu kilipotoka nilipoigusa imeganda kidoleni.”

“Ooh! Nani anataka kuchezea himaya yangu lazima nimkomeshe,” Mfalme Barami Hudirud alisema kwa hasira.
“Hebu kaniletee damu ya sehemu iliyotoka kizazi ili nimjue ni nani?”
SASA ENDELEA...

Malkia Huleiya alikwenda hadi kwenye chumba cha siri na kurudi na damu ya sehemu iliyochukuliwa kizazi cha Sharifa na kumpelekea mumewe.
“Naomba niilambe.”
Malkia Huleiya alimlambisha mumewe, mfalme alitulia kwa muda kisha alisema:
“Nimeishamjua, nitamtuma Kulani akishindwa nitakwenda mwenyewe.

Lazima nitamuonesha mimi ni nani.”
“Umemgundua ni nani?”
“Kuna mshenzi mmoja anataka kushindana na nguvu zangu, nataka mpaka kutakapopambazuka awe amebakia jina.”

“Kulaniiiiii,” aliitaka kwa sauti ya juu ambayo kama mwanadamu angeisikia basi angepasuka ngoma za masikio.
Kulani aliyekuwa mbali alikuja mbio na kupiga magoti mbele ya mfalme.
“Rabeka mtukufu mfalme.”
“Nataka uende duniani, damu hii itakuongoza mpaka kwa mtu huyu, nataka umfutilie mbali, sawa?”

“Sawa mtukufu mfalme.”
“Haya ondoka mbele yangu, usirudi mpaka umemfutilia mbali kiumbe huyo dhaifu anayetaka kucheza na nguvu zangu.”
Kulani alizama chini ya ardhi na kutoweka, baada ya muda alikuwa pembeni ya bahari eneo la Bagamoyo, aliilamba damu aliyopakwa kidoleni ambayo ilimuelekeza aende upande upi. Alitoka eneo baharini na kuelekea kwa Mganga Njiwa Manga.

Alitembea taratibu toka eneo la bahari akiwa katika umbile la kibinadamu, hakuchelewa kufika kwenye makazi ya watu. Aliilamba tena ile damu iliyokuwepo kidoleni mwake, kwa vile kulikuwa na giza, sehemu ya Mganga Njiwa Manga ikawaka mwanga wa taa.

Mwanga ule ulimuongoza hadi karibu kabisa na nyumba ya Mganga Njiwa Manga. Nia yake kubwa ilikuwa kwenda mpaka mlangoni na kugonga ili akifungua tu wakutane uso kwa uso na ammalize pale pale kisha aondoke kabla hakujapambazuka.

Alitembea kuelekea eneo la nyumba ya mganga, ajabu alipokaribia nyumba yake alishangaa kuona moto ukiwaka kuizunguka nyumba ile. Hali ile ilimshtua sana, aligeuka na kutimua mbio hadi baharini ambako alikunywa maji mengi na kurudi hadi kwenye eneo la nyumba ya mganga.

Alipoikaribia moto uliwaka tena, alilisogelea eneo la nyumba huku akimwaga maji aliyoyachukua baharini kwa lengo la kuuzima moto ule. Alifanikiwa lakini alipotaka kuingia kwenye himaya ile moto uliwaka tena. Alijikuta akifanya kazi ya kwenda baharini na kurudi, kila alipouzima moto na alipotaka kuingia uliwaka tena.

Kulani alijikuta akitumia muda mwingi kwenda baharini kuchukua maji na kurudi huku moto ukizimika na kuwaka. Mpaka kulipokuwa kunakaribia kupambazuka hakuweza kuingia katika himaya ya Mganga Njiwa Manga. Kwa upande wake aliiona kazi imekuwa ngumu au maji yalikuwa marefu na kuamua kurudi chini ya bahari, aliogopa kutokana na kauli aliyopewa na Mfalme Barami Hudirud kuwa asirudi chini ya maji mpaka ahakikishe amemmaliza Mganga Njiwa Manga.

Kulani alijikuta kwenye wakati mgumu katika kazi ile, tofauti na zilizotangulia ambazo alizifanya kwa muda mchache. Lakini ile ilikuwa ngumu kwake, baada ya kukutana na kikwazo cha moto.
Aliamua kurudi hadi baharini akiwa katika umbile lile la kibinaadamu, alisubiri jua litochomoze ili aweze kwenda jirani kwa mganga na kumsuburi akitoka ammalize.

Jua lilipotoka na watu kuwa wengi kujaa ufukweni kwa ajili ya kununua samaki na wengine wakipanda ngarawa kwenda kuvua.
Kulani alijichanganya na watu bila ya kujulikana kama ni jini. Baada ya pwani kuchanganya na watu kuongezeka, alijitoa eneo la bahari na kwenda kwa mganga kwa kutembea kama mtu wa kawaida.

Kila aliyemuona hakumdhania vibaya, aliacha eneo la bahari na kuingia makazi ya watu, alipokaribia maeneo ya nyumba ya mganga aliuona moto ukiwaka tena. Alikwenda kwenye nyumba ya jirani na kuomba kupumzika, kutokana na kuonekana kama mstaarabu, alikaribishwa na kupewa kiti. Mwenyeji wake hakujishughulisha naye aliendelea na shughuli zake na kumuacha Kulani akitupia jicho njia ya kutokea kwa Mganga Njiwa Manga.
Jini Kulani ataweza kutimiza azma yake ya kumuua Mganga Njiwa Manga?
 
ILIPOISHIA:
Kila aliyemuona hakumdhania vibaya, aliacha eneo la bahari na kuingia makazi ya watu, alipokaribia maeneo ya nyumba ya mganga aliuona moto ukiwaka tena. Alikwenda kwenye nyumba ya jirani na kuomba kupumzika, kutokana na kuonekana mstaarabu alikaribishwa na kupewa kiti. Mwenyeji wake hakujishughulisha naye aliendelea na shughuli zake na kumuacha Kulani akitupia jicho njia ya kutokea kwa Mganga Njiwa Manga.
SASA ENDELEA...

Muda ulikwenda bila mganga kuonekana, kila alipopata wazo la kwenda kwenye nyumba ile alishangaa kuuona moto ukiwaka, lakini ulipotulia nyumba ilikuwa katika hali ya kawaida. Alijikuta yupo kwenye wakati mgumu akiamini kabisa ngoma ile ni nzito kwake kuchezeka.

Kilichomchanganya zaidi ilikuwa ni kauli ya mfalme Barami Hudirud ya kuhakikisha anammaliza mganga ndipo arudi, japo muda aliopewa ulipita.
Kulani alipata pigo baada ya mwenyeji wake kutaka kuondoka, akiwa bado kichwa kinamuuma alimwambia:

“Samahani kaka.”
“Bila samahani.”
“Nataka kuondoka kwenda pwani.”
“Hakuna tatizo funga mlango wako mimi niache hapa nimekaa baada ya muda nitaondoka.”
“Hapana kaka sikujui nimekukaribisha kibinadamu, lakini siwezi kukuamini kukuachia nyumba yangu, dunia haiaminiki siku hizi.”

“Sawa.”
Kulani alikubali kuondoka pale, lakini sehemu iliyokuwa nzuri kupaona kwa mganga ilikuwa kwenye nyumba ile iliyokuwa ikitazamana na ya mganga. Aliondoka kwa kuzunguka nyumba ile na kujigeuza haraka kuwa mjusi. Aliupanda ukuta haraka na kwenda kujificha chini ya bati bila kuonekana.

Mwenye nyumba ile alishtuka na kuzunguka nyuma ili kupata uhakika kama kweli yule mgeni atakuwa ameondoka. Lakini ajabu alipozunguka nyuma ya nyumba iliyokuwa na uwazi mkubwa wa kumuona mtu kama anatembea kutoka pale, hakumuona mgeni wake. Alijiuliza kwa sauti:

“Sasa atakuwa amekwenda wapi, mtu azunguke sasa hivi asionekane, mmh! Lisiwe jini lile, Mungu aniepushie mbali.”
Kulani alimtazama na kutulia akiwa amejilaza kwenye ukuta chini ya bati. Baada ya kusema yale mwenye nyumba ile aliondoka na kumwacha Kulani palepale nyumbani bila kujua.

Baada ya kuondoka, Kulani aliendelea kumsubiri mganga palepale ukutani chini ya bati katika umbile lile lile la mjusi kama atatokea Mganga Njiwa Manga amvae na kumuulia mbali. Alisubiri kwa saa kumi mpaka jioni ilipoingia ndipo alipomuona akiwa anamsindikiza mmoja wa wateja wake.

Jini Kulani aliteremka na kurudi katika umbile la mwanadamu na kumfuatilia kwa nyuma bila ya mganga kujua. Nia yake ilikuwa kukutana naye wakati anarudi ili amvae. Taratibu alitembea kumfuata kwa nyuma mganga aliyekuwa mbele akitembea huku akizungumza na wateja wake.

Njiani Mganga Njiwa Manga alianza kuhisi kama ardhi inatetemeka na mwili kuwa mzito, kitu kile kilichomfanya ageuke na kutazama nyuma. Alishtuka kukiona kiumbe cha ajabu kwa mbali kikija taratibu. Kwa haraka alichutama chini na kushika michanga huku akilikemea jitu lile ambalo liligundua limejulikana.

Wakati Kulani akijitayarisha kumvaa Mganga Njiwa Manga baada ya kugundua amejulikana, kabla hajamfikia alirusha vumbi la mchanga lililomuingia machoni na kumpofua macho. Alipiga kelele za maumivu na kujipiga chini kwa hasira na kusababisha kishindo kizito kilichotikisa eneo kubwa la Bagamoyo.

Kishindo kile kilisababisha watu waliokuwa karibu na sehemu kilipotokea waanguke na kupoteza fahamu. Nyumba nyingine zilipata nyufa kutokana na kushindo cha Kulani kupasua ardhi na kupotea. Baada ya robo saa hali ya eneo la Bagamoyo ilirudi kuwa ya kawaida.
Baada ya kurudi hali ya utulivu Mganga Njiwa Manga alinyanyua alipokuwa ameangukia baada ya kurushwa na udongo uliotoka kwenye shimo alilozama jini Kulani baada ya kupofuka macho. Alimtuma mtu kwenda nyumbani kumletea dawa ambayo alikunywa na kujimwagia kichwani.

Baada ya kuyafanya yale alikwenda hadi kwenye shimo lililokuwa limechimbika kama kumelipuka bomu. Sehemu ile aliweka dawa kisha aliondoka na kurudi nyumbani kwake. Alipofika nyumbani mwili ulikuwa umechoka sana, hakuweza kuendelea na kazi ya matibabu, aliwaomba wagonjwa wake apumzike baada ya kunusurika kifo toka kwa jini ambaye hakujua ametoka wapi.

Siku ile hakufanya kazi yoyote, alilala mpaka siku ya pili huku akiviona viungo vyake vikipoteza nguvu. Hata alipolala hakuweza kujigeuza mpaka siku ya pili, kwake ulikuwa upinzani mkubwa katika kazi yake. Mara nyingi upinzani uliishia nje ya ngome yake, lakini hakikuwahi kiumbe chochote cha ardhini majini au angani kilichoweza kumdhuru.

Pia katika kazi yake haikuwahi kutokea kiumbe kilichowahi kumvizia njiani kwa ajili ya kumdhuru. Wengi walivamia sehemu aliyokuwa akifanya kazi na kukutana na vikwazo. Lakini uwezo wa kinga yake ya mwili ndiyo uliomsaidia, bila hivyo angemalizwa na jini yule.
***

Jini Kulani baada ya kuzama chini ya ardhi kwa kujipigiza kwa hasira, aliibukia pembeni ya bahari. Alitembea taratibu huku akipapasa ili kuingia majini. Baada ya kutembea kwa muda alibahatika kuyakanyaga maji. Pale pale alizama chini.
Mfalme wa bahari alishangaa kumuona Mkuu wa Watwana Kulani amesimama mbele yake akiwa haoni.

“Kuna nini tena kimekusibu mtwana wangu mtiifu?”
“Mtukufu mfalme, safari yangu imekuwa mbaya.”
“Kulani umefanya makosa, kwa nini jana hukurudi?”
“Niliogopa mtukufu mfalme kurudi bila kutimiza ulichonituma.”
“Umekitimiza?”

“Hali yangu kama unavyoniona.”
“Tatizo nini?”
“Nimepofuka mtukufu mfalme.”
“Lakini hujanijibu, umemmaliza?”
“Sikuweza, yule mtu hata wewe sikushauri uende.”
“Kwa nini?”

“Amejidhatiti, ana nguvu za ajabu sijawahi kuona, ameizindika ngome yake haiingiliki, na yeye mwenyewe alichonifanya sitasahau mpaka nakufa.”

Jini Barami Hudirud, mfalme wa bahari atakubali ushauri wa Kulani kuachana na Mganga Njiwa Manga?
 
Hapana lazima niende, hawezi kushindana na nguvu zangu.”
“Mtukufu mfalme, bado himaya ya chini ya bahari inakuhitaji lazima atataka kutumia nguvu za ziada kukumaliza. Nashukuru sikugusana naye ningeweza kupoteza maisha.”
“Kwa hiyo tuwaache wanadamu watuchezee?”

“Hapana, ila nguvu zinazidiana, yule mwanadamu ana nguvu za ajabu sana, nilijitahidi kuuzima moto alioutega kwenye himaya yake, nilishindwa kila nilipouzima na nilipotaka kuingia uliwaka tena nikajikuta kukipambazuka bila ya kuweza kuingia kwenye himaya yake. Ndiyo sababu ya kuchelewa kurudi na kuamua kubaki ili nihakikishe nammaliza akitoka kwake. Lakini haikuwa hivyo matokeo yake nimekuwa kipofu.”

“Mmh! Nimekuelewa, basi mpelekeni akapate tiba.”
Watwana wengine walimchukua Kulani na kwenda kumpatia tiba ya macho, baada ya kuondoka, mfalme alimgeukia mkewe aliyekuwa kimya akimuangalia Kulani kwa huruma.
“Mke wangu umeona hali ilivyo, unanishauri nini kutokana na hali aliyorudi nayo Kulani?”

“Mmh! Mume wangu hali inatisha, inaonesha wazi vita ni nzito, tukifanya mchezo tutakwisha, mpaka Kulani kusema hivyo ujue kuna kazi. Kwa nini tusiachane na mpango wa kumfuatilia huyo mwanadamu?”
“Lakini mke wangu si unajua uwezo wangu? sijawahi kushindwa na kitu,” Mfalme alijitapa.

“Naujua vizuri, hata Kulani anaujua lakini mpaka kakukueleza vile naomba umsikilize huenda kuna kitu amekiona kinaweza kukupotezea maisha kama utashindana na yule mwanadamu.”
“Lakini kumbuka jini ana nguvu kuliko mwanadamu?’
“Lakini mwanadamu ndiye kiumbe mwerevu kuliko viumbe wote wa Mungu?”
“Hilo nalijua lakini bado hawawezi kushindana na sisi.”
“Mume wangu majini sisi hatuna ushirikiano, kuna majini wengine huwakinga mwanadamu na kuwafanya kuchanganya nguvu za kijini na akili ya kibinadamu lazima tu atakushinda.”
“Kwa hiyo tufanye nini?”
“La muhimu tuachane na mpango huo.”

“Na suala la Balkis kuolewa na jini mwenzake?”
“Hilo nalo ni gumu, tuendelee kumshawishi aweze kubadili mawazo na kuendelea na kazi ya kukusanya vizazi vya wanadamu na kutengenezewa dawa.”
“Mimi nina hasira, jaribu kuongea naye wewe.”

“Nitafanya hivyo jioni nitazungumza naye.”
Walikubaliana mke wa mfalme azungumze na Balkis ili aweze kubadili uamuzi wake wa kung’ang’ania kuolewa na mwanadamu.
****
Baada ya kuamka siku ya pili, Mganga Njiwa Manga bado mwili wake haukuwa na nguvu, wagonjwa wengi waliofika siku ile hawakupata huduma kutokana na hali yake. Ilibidi siku ile na yeye kutumia dawa za kujifusha na kunywa ili kujirudisha katika hali ya kawaida, baada ya kukumbwa na upepo wa jini Kulani.

Kilichomshangaza kilikuwa rangi ya jini yule, alikuwa mweusi kama rami tofauti na majini wote aliowahi kukutana nao. Siku ya pili tangu akutane na dhahama nzito ya jini Kulani, aliendelea na kazi ya kutoa huduma kwa wagonjwa wanaotoka mbali.

Baada ya kuingia katika chumba chake kutoa huduma, alitulia kwenye mkeka kisha aliweka ubani kwenye kitezo na kutulia kwa muda ili ajiandae kwa matibabu ya wagonjwa waliokuwa wameongezeka kutokana na kusimama kwa huduma yake.

Ilikuwa ajabu baada ya moshi wa ubani kupanda juu, ulimfuata mbele ya uso wake na akaanza kuona picha asiyoielewa. Alikiona kiumbe cha ajabu kikitoka kwenye maji na ghafla kiligeuka na kuwa mwanadamu, kisha kilitembea taratibu toka kwenye ufukwe na kuingia maeneo ya watu.

Baada ya kiumbe kile kilichojigeuza kuwa binaadamu kukaribia ngome yake, kilijigeuza umbile na kurudia lile alilotoka nalo chini ya maji. Ajabu kilipotaka kuingia kwenye himaya yake aliona moto ukiwaka kuzunguka eneo lake, ghafla kiumbe kile kilitoka mbio kurudi baharini na kuchota maji kisha kuja kuzima moto.

Kiliendelea kuzima moto mpaka kulipopambazuka, kila kilichoendelea alikiona mpaka kupambana na jini lile. Hapo ndipo alipogundua jini lile lilitoka wapi, alicheka na kuona kinga aliyokuwa nayo ndiyo iliyomsaidia bila hivyo angekufa vibaya.
Taratibu moshi ulipungua na hali ya ndani ikarudi kuwa ya kawaida, Mganga Njiwa Manga aliendelea kuweka tena ubani uliotoa moshi wa kawaida bila kuwepo na kitu kisichokuwa cha kawaida. Alimtuma msaidizi wake kuwaita wagonjwa.

Nini kiendelea baada ya mganga kuonekana kudhibiti nguvu za kijini? Je, nini hatma ya Brighton katika chumba cha giza?
 
CHINI YA BAHARI
Malkia Huleiya, mama mzazi wa Balkis alikwenda hadi chumba cha giza na kuomba Balkis atolewe, baada ya kutolewa alimpeleka kuoga na kukaa naye kwenye pwani ambayo huitumia kupumzika familia ya kifalme. Muda wote Balkis alikuwa akibubujikwa na machozi.
Baada ya kukaa kimya kwa muda malkia Huleiya alimwita mwanaye.
“Balkis”

“Abee mama.”
“Najua utatuona sisi wazazi wako makatili lakini unajua kabisa ubaya wa wanadamu na pia ni aibu jini kutoka katika ukoo wa kifalme kuzaa na mwanadamu.”
“Mama kabla ya kuzungumza lolote naomba mumtoe mpenzi wangu na kama hamtaki awe huku naomba mumrudishe duniani.”

“Hakuna tatizo.’ Alitumwa mtu kwenda kumtoa Brighton kwenye chumba cha giza na kumpa maji ya kuoga kisha kuwekwa kwenye chumba kizuri. Baada ya hatua zile mazungumzo yaliendelea.
“Nina imani imefurahi?” Mama yake alimuuliza.
“Siwezi kufurahi kwa vile sijatimiza dhamira yangu.”
“Ipi?”

“Ya kuolewa na mwanadamu.”
“Hilo ndilo baba yako hataki kusikia.”
“Lakini kumbuka tunachokifanya hakimpendezi Mwenyezi Mungu.”
“Kipi hicho.”

“Cha kuwafanya wanawake matasa.”
“Ni kweli, lakini tunafanya hivyo kwa ajili yako.”
“Kama unaona kufanya vile ni dhambi kwa nini msiniache na mpenzi wangu aliyekuwa tayari kukaa huku hata watoto wangezaliwa wangekuwa wetu.”
“Mwanangu hujui vita ya wanadamu ni kubwa, huwezi kuamini kizazi kimoja kimechukuliwa. Kama kizazi kimechukuliwa je, mwanadamu watakubali aishi huku?”
“Mwanadamu kanipenda mwenyewe wala sikumlazimisha.”

“Lakini si ana mchumba wake?”
“ Alimkana mbele yangu na kuwa tayari kunioa.”
“Kwa sababu hakujua kuwa wewe ni jini.”
“Hata alipojua alikubali ndiyo maana nimekuja kuishi nae huku.”
“Lakini kumbuka baba yako alikuwa akikutegemea sana, ulichokifanya kimemchanganya sana.”

“Lakini mama tatizo nini, kutafuta vizazi vya wanawake na kuzaa bila vita na wanadamu kipi bora, ona kama ulivyoniambia mkuu wa watwana Kulani kawa kipofu, kwa nini tusiachane na vita na wanadamu ili hamu ya mtoto apatikane bila kupata madhara zaidi.”
“Uamuzi wako umemuweka baba yako katika wakati mgumu, kumbuka anakupenda kuliko kitu chochote, hakuota hata siku moja utamkosea heshima.”

“Ni kweli najua baba ananipenda lakini alitakiwa kunisikiliza kuliko kuchukua maamuzi mazito, ona katumia nguvu nyingi matokeo yake Kulani kawa kipofu.”
“Balkis mwanangu hakuna jini anayekubali kushindwa na mwanadamu.”
“Ni kweli lakini kuna wanadamu nao huamini kabisa majini hawawawezi, kama wameweza kuchukua kizazi kimoja wanashindwa nini kuvichukua vyote?”

“Balkis mwanangu kama ungekwenda kwa kitu tulichokutuma, nina imani kazi yako ingekuwa nyepesi sana kuliko ulichokifanya cha kuanzisha uhusiano na mwanadamu.
“Kitendo kile kilituchanganya sana hasa baba yako, hata kuzungumza na wewe alishindwa na kunituma mimi. Anaamini hata matatizo ya Kulani chanzo ni wewe.”
“Chanzo ni mimi kwa vipi? Wakati niliwakataza tuachane na vita na wanadamu lakini mkawa wabishi.”

“Balkis mwanangu naomba uifanye kazi tuliyokutuma, tunaamini wewe ni mtoto mwenye heshima na usikivu. Nakuomba chonde chonde mwanangu msikilize baba yako.”
“Mamaa kwa nini msinikubalie, kwani kuna ubaya gani?”
“Kumbuka baba yako ni mfalme wa majini, ni aibu kwa mwanaye kuolewa na mwanadamu, ndiyo maana alikutuma kutafuta kizazi cha mwanamke ili kuhakikisha unapata tiba na kuolewa na jini mwenzako.”

“Kwa hiyo nimrudishe Brighton duniani?”
“Ikiwezekana.”
“Mbona unasema ikiwezekana.”
“Lazima tumuulize baba yako ataamua nini juu ya mwanadamu aliyejua siri yetu.”
“Sasa naona unataka kuharibu mazungumzo, mmenikataza kuolewa na mwanadamu basi nimrudishe kwao.”

“Lakini si atakuwa amejua siri yetu?”
“Sasa mnataka kumfanya nini?”
“Sijajua mpaka tupate maelekezo ya baba yako.”
“Sikiliza kama nimekubaliana na uamuzi wenu wa kuachana na mwanadamu ili niendelee na kazi yangu ya kutafuta vizazi vya wanawake, naomba kwenye suala la kurudi kwao mpenzi wangu msiniingilie.”

“Lakini kumbuka mwanangu chini ya bahari hii mwenye sauti ya mwisho ni baba yako.”
“Hata awe na sauti gani uamuzi wowote tofauti na kumrudisha duniani hatutaelewana.”

Nini hatima ya Brighton? Je, ataruhusiwa na mfalme kurudi duniani baada ya kuijua siri ya majini
 
“Mbona umefika mbali, ngoja nimpelekee taarifa hizi, atafurahi sana kusikia kuwa umekubali kurudi dunia kutafuta vizazi vya wanawake. Pia nitamueleza suala la mpenzi wako la kurudishwa duniani. Siamini kama atakuwa na maamuzi mazito ya kukuumiza.”
“Mmh! Haya basi naomba nafasi ya kuzungumza na Brighton.”
“Mmh! Basi ataletwa huku ili baba yako asijue chochote.”

Baada ya kusema vile, Huleiya aliondoka na kumuacha Balkis akiwa amejilaza kwenye kiti cha uvivu. Japo moyo ulimuuma kumuacha Brighton mwanaume aliyeamini ndiye mume wa maisha yake. Bado hakuamini kama anaweza kutoa siri za majini. Lakini aliamini hakuwa akijua lolote katika siri za chini ya bahari kutokana na kufikia kwenye chumba cha giza.

Baada ya muda Brighton alifikishwa bustanini na kukutana na Balkis, baada ya kukutana Balkis alimueleza hali halisi na yeye kuwa tayari kumrudisha duniani. Kwa upande wake Brighton alijikuta akizama kwenye dimbwi la mahaba ya Balkis na kumuomba atafute njia yoyote ili asirudishwe duniani.

“Mpenzi kwa nini usimbembeleze baba yako ili tuishi pamoja?”
“Hilo ndilo lilikuwa lengo langu lakini limeleta mtafaruku mkubwa ndani ya familia. Kwa hiyo nakuomba ukubali kurudi duniani ila sitakuwa mbali nawe.”

“Mmh! Sawa lakini nitalikosa penzi lako.”
“Ni kweli, lakini lazima nikubaliane na matakwa ya wazazi wangu.”
“Sawa, sina jinsi,” Brighton alikubali kwa shingo upande.

Malkia Huleiya baada ya kuzungumza na mwanaye alipeleka taarifa ya kikao kwa mumewe mfalme Barami. Alipofika alimkuta akimsubiri kwa hamu.
“Karibu malkia wangu.”

“Asante mfalme wangu.”
“Mh, nijuze yaliyojiri huko?”
“Mmh! Namshukuru Mungu yamekwenda vizuri.”
“Kakubali?”

“Ndiyo.”
“Ooh! Afadhali.”
“Lakini..”
“Lakini nini tena malkia wangu?” Mfalme alishtuka.

“Kuhusu yule mpenzi wake.”
“Ana nini?”
“Anataka arudishwe duniani.”

“Ina maana hajui sheria yetu mwanadamu anayejua siri zetu huwa harudi tena duniani?”
“Hapo ndipo penye tatizo.”
“Tatizo gani?”
“Mwanao anataka amrudishe duniani.”
“Haiwezekani.”
“Amesema iwe isiwe lazima tumrudishe duniani.”

“Yeye ni nani anayetaka kutulazimisha tufanye anavyotaka, siwezi kuwa na sauti mbili katika himaya yangu ya chini ya bahari.”
“Lakini mume wangu..”
“Hakuna cha lakini, aendelee na kazi ya kutafuta vizazi tena tutampangia kwa siku moja alete vingapi ili awahishe kutimiza lengo la kuolewa tuondokane na adha hizi.”
“Mume wangu si vyema kila wakati kutumia nguvu, ifike wakati mwingine uwe unawasikiliza walio chini yako.”

“Siwezi, nasema kauli yangu ni ya mwisho na maamuzi yangu yaheshimiwe,” mfalme alikuwa mkali.
“Mume wangu hii itakuwa vita nyingine, kwa jinsi nilivyomsikiliza mwanao hawezi kukubali hili.”
“Nitakachomsikiliza ni kumuacha hai, lakini si kumrudisha duniani.”
“Mwanao amesema kwa hili hamtaelewana.”
“Hebu kamlete hapa,” mfalme alisema kwa hasira.

Alitumwa kijakazi kumfuata bustanini, Balkis alifika mbele ya baba yake kusikiliza kile alichoitiwa.
“Abee mtukufu mfalme,” Balkis aliitikia akiwa amesimama mbele ya baba yake.
“Kwanza nimefurahi kusikia umeweza kubadili uamuzi wako ila umeniudhi kwa kunilazimisha nifanye utakavyo.”
“Baba kukulazimisha kitu gani?”
“Kuhusu kumrudisha mwanadamu duniani.”

“Sasa tatizo liko wapi? Mmemkataa asinioe sasa si nimrudishe nilipomtoa.”
“Ina maana hujui sheria za majini, kama mwanadamu atajua siri zetu?”
“Nazijua lakini huyu nimemleta miye hakujileta mwenyewe, wala hakuletwa kwa lipizo.”
“Sheria za huku mwanadamu yeyote atakayeingia huwa hatoki salama, lakini kwa heshima yako hatutamuua bali ataishi huku milele.”

“Kwa hilo baba sitakubali hata kwa kukatwa kichwa, ni mimi ndiye niliyemlazimisha kuja huku iweje mumshikilie?”
“Hiyo ndiyo sheria ya huku kamwe haibadiliki.”
“Nasema kwa hili itabadilika.”
“Tunabisha?”

“Hatubishani ukweli ndiyo huo, ikifanywa kinyume nikiondoka hapa sitarudi tena.”
“Sooba,” alimwita mtwana msaidizi wa Kulani kwa sauti ya juu.
“Rabeka mtukufu mfalme,” Sooba aliitika na kusimama imara mbele ya mfalme.

“Mpeleke huyu kwenye chumba cha giza.”
Balkis alichukuliwa tena na kurudishwa kwenye chumba cha giza.
Nini kiliendelea?
 
Back
Top Bottom