Siku ile usiku Bwana George alitusimulia habari za safari yake. Kwa uchache ilikuwa hivi: miaka miwili nyuma alitoka mji wa Sitanda kujaribu kufika milima ya Sulemani.
Ile barua niliyompa Jim hakuipata, wala hakupata habari zake mpaka leo hivi. Lakini alisikia habari kwa wenyeji wengine.
Hakujaribu kufika kwenye maziwa ya Sheba bali alifuata njia ile nyingine tuliyorudia sisi, yaani njia iliyo bora kuliko ile iliyoandikwa katika ramani ya mzee Silvestra.
Yeye na Jim walipata taabu nyingi katika jangwa lile, lakini kwa bahati walifika hapa pahali penye majani na maji, ndipo Bwana George alipopatikana na ajali. Siku moja alikuwa kakaa kando ya mto na Jim alipanda juu kujaribu kutafuta asali.
Alipokuwa akifanya hivi, jiwe kubwa lililegea likaporomoka likamwangukia likamvunja mguu vibaya sana.
Basi tokea siku ile hakuweza kwenda vizuri, ikawa hawezi kwenda mbele wala kurudi nyuma, akaazimia kukaa pale pale.
Waliweza kupata chakula cha kutosha, maana walikuwa na risasi nyingi na wanyama huja penye majani na maji yale usiku usiku kila siku. Basi huwapiga wanyama, nakula nyama, na ngozi walizitengeneza ziwe nguo zao.
Basi Bwana George akamaliza kusimulia hadhithi yake, akasema, ‘Basi hapa tumekaa kwa muda wa karibu miaka miwili tukitumai kuwa labda wenyeji watapita na kutusaidia, lakini hawakuja.
Hivi jana usiku tulifanya shauri kuwa Jim aniache hapa naye ajaribu kufika mji wa Sitanda na kupata watu watusaidie. Tulikata shauri kuwa aondoke kesho, lakini hakika sikutumai kuwa ataweza kurudi tena.
Na sasa wewe, ambaye katika watu wote duniani sijakutumainia kabisa, wewe niliyekufikiri kuwa umenisahau na kukaa Uingereza kwa raha, umekuja bila ya kukutarajia.
Ni jambo la ajabu, tena bahati sana.’
Basi alipokwisha kusema, Bwana Henry akaanza kusimulia habari za mambo muhimu katika safari yetu, tukakaa sana usiku ule tukizungumza.
Nikamwonyesha almasi zile nilizopata, akasema, ‘Lo! Kweli mmepata kitu katika taabu zenu, si kama mimi nisiyestahili hata kuhesabiwa sasa.’
Bwana Henry akacheka, akasema, ‘Almasi hizi ni mali ya Quatermain na Good. Hivyo ndivyo tulivyopatana, ya kuwa watagawana mali yoyote tutakayo ipata.’
Basi, maneno yale yalinitia katika fikra, na nilipokwisha kumshauri Bwana Good, nilimwambia Bwana Henry kuwa sisi sote wawili tunataka hata na yeye ashirikiane nasi katika kugawanyana zile almasi, na kama yeye hakubali, basi sehemu yake tutampa ndugu yake aliyevumilia taabu nyingi kuliko sisi katika kujaribu kuzipata.
Mwisho akakubali namna tulivyopatana, lakini Bwana George hakupata habari mpaka baada ya siku nyingi. Basi, hapo nadhani nitamaliza hadithi yangu.
Safari yetu ya kuvuka jangwa mpaka mji wa Sitanda ilikuwa safari ya taabu nyingi, hasa kwa sababu ilitupasa kumsaidi sana Bwana George ambaye mguu wake wa kulia ulikuwa dhaifu sana, na ukamfanyia matata.
Lakini tulivuka, na kusimulia habari zake ingekuwa kukariri hadithi ile niliyokwisha isimulia.
Tulifika Sitanda, tukaona bunduki na vyombo vyetu vingine vipo salama, lakini nadhani Yule mzee aliyekuwa akivitunza hakupenda kutuona tena.
Baada ya miezi sita tulifika kwangu, katika mji wa Durban, na ndipo ninapokaa sasa na kuandika habari hizi. Na sasa nakupeni Kwaherini nyote mliosafiri pamoja nami katika safari hiyo ndefu na ya ajabu kuliko zote nilizosafiri.
MWISHO.