Hadithi ya mashimo ya mfalme Sulemani

SURA YA NANE

Mchana kutwa tulisafiri na tulifuata njia ile nzuri. Infadus na Skraga walifuatana nasi, lakini watu wao walitangulia.

Baadaye kidogo nilimuuliza Infadus, ‘Nani aliyetendeneza njia hii? Akajibu, ‘Ilitengenezwa zamani sana na hayupo anayejua wakati gani au kwa namna gani ilivyotengenezwa, hata Kizee Gagula aliyeishi kwa vizazi kumi hajui.

Hapana anayeweza kutengeneza njia kama hii sasa.’Nikamuuliza, ‘Na maandishi na picha zile katika pango lile nani aliye chora?’

Akajibu, ‘Bwana wangu, mikono iliyotengeneza njia hii ndiyo iliyochora picha zile. Hatujui nani aliyechora.’ Nikamuuliza tena, ‘Wakukuana walikuja katika nchi hii wakati gani?’ Akajibu, ‘Bwana wangu, kabila hili lilikuja kama kuvuma kwa dhoruba zama za kale miaka elfu na elfu nyuma.

Walitoka nchi ile iliyo kaskazini, Babu zetu walisimulia kama hawakuweza kwenda mbele zaidi kwa sababu ya milima mirefu inayozunguka nchi.

Na Kizee Gagula, mwanamke mwenye busara, anasema hivyo hivyo. Nchi hii ilikuwa ya neema, basi wakakaa wakazaana wakapata nguvu, na sasa hesabu yetu ni kama punje za mchanga wa pwani, na mfalme Twala akiwaita askari wake wakutanike, huenea huwandani mpaka upeo wa macho.’

Nikamuuliza, ‘Je, na kama nchi imezungukwa na milima, majeshi watapigana na adui gani?’ Akajibu, ‘Nchi yetu imezungukwa na milima ila upande wa kaskazini, na mara kwa mara adui hutoka upande huo kama mawingu kutoka nchi tusioijua, nasi tunawaua. Tokea vita vya mwisho miaka ishirini tu imepita, na elfu nyingi za watu walikufa, lakini tuliwaua wale waliokuja kutula sisi.

Basi tangu siku hizo hakujakuwa na vita tena.’ Nikasema, ‘Basi ikiwa ni hivi Infadus, askari wenu watakuwa wamechoka kwa kukaa bure tu!’ Akajibu, ‘La, bwana, tangu vita vile, vita vingine viliingia vilivyokuwa vikali, lakini vilikuwa vita kati yetu sisi wenyewe; yaani mbwa kula mbwa.

Ikawa hivi: Ndugu yangu aliyekuwa mfalme alikuwa na ndugu yake waliyozaliwa pamoja, yaani, walikuwa pacha. Katika nchi yetu ni desturi tusiwaache wote wawili waishi, Yule aliye dhaifu huuawa.

Lakini mama alimficha Yule mtoto aliyekuwa dhaifu ambaye alizaliwa mwisho, maana alimpenda sana, na Yule mtoto ni Twala, mfalme wa sasa.

Mimi mdogo wake nilizaliwa na mama mwingine. Baba yetu aliitwa Kafa, naye alipofariki, ndugu yangu Imotu alitawala mahali pake, akazaa mtoto. Yule mtoto alipopata umri wa miaka mitatu, ukawa wakati ule wa mwisho wa vita vikubwa.

Wakati huo watu hawakupata nafasi kulima, na njaa kali iliingia katika nchi na watu wakaanza kunung’unika, wakageuka kama simba watafutao kitu cha kurarua. Ndipo alipotokea Yule mchawi mwanamke Gagula ambaye hafi kabisa, akasema, ‘Huyu mfalme Imotu si mfalme.’

Na wakati huo Imotu alikuwa amelala anaugua majeraha, amekaa katika nyumba yake hajiwezi kabisa.

Basi Gagula alikwenda katika nyumba akamtoa Twala, ndugu yake, ambaye alimficha katika mapango na miamba tokea wakati aliozaliwa, akamvua shuka akawaonyesha Wakukuana alama tukufu ya nyoka aliyochanjwa kiunoni, alama ambayo amechanjwa mwana wa kwanza kuzaliwa na mfalme, akapaaza sauti yake na kusema, ‘Tazameni, huyu ni mfalme wenu, nimemwokoa mpaka hivi leo kwa ajili yenu!’

Basi, watu ambao walikuwa kama wana wazimu kwa sababu ya njaa wakapiga kelele, ‘Mfalme! Mfalme!’Lakini mimi nilijua ya kuwa siyo mfalme, maana Imotu ndiye aliyekuwa wa kwanza kuzaliwa katika wale pacha, naye ndiye mfalme wa kweli.

Basi kelele zilipozidi, mfalme Imotu akatoka nyumbani ingawa alikuwa mgonjwa, ameshikwa mkono na mke wake, naye amefuatwa na mtoto wake mdogo, Ignosi, yaani kwa tafsiri yake ni ‘Umeme

Akauliza, ‘Kelele hizo za nini? Mbona mnaita ‘Mfalme! Mfalme!’ Basi hapo Twala aliyekuwa ndugu yake waliozaliwa na mama mmoja pacha, akamkimbilia akamshika nywele na kumchoma kisu cha moyo.

Na watu wote walipiga makofi na kelele, ‘Twala ni mfalme, sasa tunajua kuwa Twala ndiye mfalme’ maana walikuwa dhaifu kabisa.

Nikamwuliza Infadus. ‘Je, na Yule mke wake na mtoto Ignosi, Twala aliwaua vile vile?’ Akajibu, ‘Hapana, bwana wangu. Malkia alipoona kuwa bwana wake ameuawa alimshika mkono mtoto wake akakimbia huku analia.

Baada ya siku mbili alikwenda nyumba moja akaomba chakula, lakini kwa vile bwana wake aliyekuwa mfalme amekwisha kufa hapana aliyekubali kuwapa chakula wala maziwa.

Lakini usiku ulipoingia, mtoto mmoja mdogo mwanamke akatoka akampa chakula, mama akamshukuru Yule mtoto, akashika safari kwenda milimani kabla jua halijapanda mbinguni, na humo hakosi alipotea, maana hapana aliyemwona yeye wala Yule mtoto Ignosi mpaka leo hivi.’ Nikasema, ‘Basi, na kama huyo mtoto Ignosi yu hai, ndiye Mfalme wa kweli wa Wakukuana?

Akajibu, ‘Naam, bwana, nyoka mtukufu amechanjwa kiunoni mwake. Kama yu hai, yeye ndiye mfalme. Lakini amekufa zamani.

Tazama bwana, nyumba ile ni nyumba ambayo mke wa Imotu alionekana mara ya mwisho pamoja na mtoto Ignosi. Ndipo tutakapolala usiku, yaani ikiwa nyinyi mabwana mnalala duniani.’

Basi nikajibu, ‘Rafiki yangu Infadus, tunapokaa pamoja na Wakukuana, basi tutafuata desturi za Wakukuana.’

Basi hapo niligeuka kuongea na Bwana Good aliyekuwa anafuata nyuma amechukia sana kwa kuvaa shati tu, maana lilikuwa likipeperuka katika upepo. Nikashtuka, maana niligongana na Umbopa, nikaona kuwa alikuwa akinifuata karibu sana ili asikie maongezi ya Infadus na mimi, nikaona uso wake kama mtu anayejaribu sana kukumbuka mambo yaliyokwisha pita.
 
Kabla hatujaondoka, Infadus alikuwa amepeleka mtu kutangulia amepeleka mtu kutangulia apeleke habari mjini.

Mtu huyu alikwenda mbio sana, maana watu wote wa kabila lile walizoezwa kwenda mbio sana, Sasa tukaona matokeo ya habari alizopeleka, maana tulipokaribia mjini, tuliona vikosi vingi vya askari wakitoka katika milango ya mji.

Bwana Henry akanishika mkono akasema kuwa labda tutapokewa vibaya. Lakini sauti yake ilimwonyesha Infadus kuwa tuna shaka, akasema, ‘Mabwana wangu, msiwe na hofu, hapana hila katika moyo wangu.

Hivyo vikosi ni askari wangu mimi, nao wanataka amri yangu ili wawapokee kwa heshima.’ Tulipokaribia zaidi tuliona kuwa vikosi vimejipanga kwa safu. Kila kikosi kilikuwa na watu mia tatu, na vilikuwa vikosi kumi na mbili. Ilikuwa vizuri sana kuwatazama askari namna walivyokuja mbio na kujipanga kwa nidhamu katika mahali pao.

Tulipofika kwenye kikosi cha kwanza tuliona namna walivyokuwa wanaume. Wote walikuwa watu wazima, na hapana mmoja aliyepungua urefu wa futi sita, na wengine walikuwa futi sita na inchi nne.

Walikuwa wamejipamba na manyoya marefu meusi vichwani, na kiunoni na chini ya goti la kulia walikuwa wamefungwa mikanda meupe ya ngozi ya ng’ombe na katika mkono wa kushoto wameshika ngao ndogo ya duara. Ngao hizo zilitengenezwa kwa namna ya ajabu sana, maana viunzi vyake vilikuwa vya chuma, na juu yake imetandwa ngozi ya ng’ombe nyeupe.

Silaha zao zilikuwa mikuki mifupi, na visu vyao vilikuwa vipana kadiri ya shubiri moja. Mikuki hii haitupwi, ila hutumika kwa kumchoma adui wanapopigana karibu karibu. Tena kila mtu alikuwa na visu vikubwa vitatu.

Kisu kimoja kilichomekwa katika mkanda uliofungwa kiunoni, na viwili vingine vilichomekwa kwa nyuma ya ngao. Askari aliye hodari aliweza kuvitupa kadiri ya hatua sitini kwa shabaha kamili.

Ni desturi kuwatupia adui mfululizo wanapokaribiana.
Watu wa vikosi vyote walisimama imara kama masanamu mpaka tulipowafikia, na mara mkubwa wao aliyevaa ngoziya chui alitoa amri, na kila mtu aliinua mkuki wake na wote wakasema kwa sauti kubwa, IKoom.’

Na mara tulipokwisha pita walifuata nyuma yetu. Basi ikawa vivyo hivyo mpaka tulipokwisha kupita vikosi vyote na vyote vilifuata nyuma yetu wakikanyaga nchi mpaka ikatetemeka.

Tulipofika kwenye mji tuliona kuwa umezungukwa na handaki pana, na ng’ambo ya handaki boma la miti minene yenye nguvu limejengwa. Daraja ya kupitia iliwekwa mlangoni mwa mji, nayo iliweza kuinuliwa na kushushwa tena..

Basi tuliona kuwa mlinzi wa mlango amekwisha shusha daraja tayari, tukapita ndani. Mji ulikuwa umetengenezwa kwa mpango mzuri, maana katikati ilikuwepo njia pana na kila upande wa njia nyumba zilipangwa kwa miraba, na kila mraba ni wa kikosi kimoja.

Nyumba zilikuwa za udongo nazo ziliezekwa vizuri kwa majani. Kila nyumba ilizungukwa na baraza upana wake hatua sita, na chini ilipigiliwa na chokaa mpaka kuwa ngumu kabisa.

Wanawake wengi walikuwa wamejipanga kila upande wa njia wamekuja kututazama. Walikuwa wazuri sana. Wote walikuwa warefu na wenye maumbo mazuri. Nywele zao zilikuwa fupi za kuviringana, si za kipilipili, na midomo yao haikuwa minene sana.

Basi tulipofika katikati ya mji, Infadus alisimama mbele ya nyumba kubwa iliyozungukwa na nyumba ndogondogo, akasema, ‘Ingieni, Wana wa Nyota, mpumzike katika nyumba ndogo yetu.

Chakula kidogo kitaletwa ili msiwe na haja ya kukaza mikanda yenu kwa ajili ya njaa, asali kidogo na maziwa, na ng’ombe wawili watatu; si kingi, Mabwana wangu, lakini ni chakula.’

Nikamjibu, ‘Ahsante, Infadus, tumechoka kwa kusafiri katika dunia zilizo angani; na sasa tupumzike.’ Basi tuliingia ndani ya nyumba tukaona kuwa imetengenezwa vizuri ili kutupokea kwa heshima. Vitanda vyenye ngozi laini vilikuwa tayari, na maji ya kuoga yalikuwa yamewekwa tayari.

Baadaye kidogo tulisikia sauti za watu nje, tukaenda mlangoni na tukaona wanawali wakileta maziwa na bisi na asali katika vyungu.

Na nyuma ya wanawali tuliona vijana wanaume wanaleta ng’ombe aliyenona sana. Tulipokea zawadi, na mara kijana mmoja akatwaa kisu chake akamchinja Yule ng’ombe, na katika muda wa dakika kumi alikuwa tayari amechinjwa na kugawanywa vizuri.

Nyama iliyo bora iliwekwa mbali, na iliyobaki niliwapa askari waliokuwepo, nao wakaitwaa wakaigawanya wakasema kuwa ni ‘Zawadi ya mabwana weupe.’

Umbopa alianza kutupikia chakula katika chungu cha udongo, na mwanamwali mzuri alimsaidia. Chakula kilipokuwa tayari tulipeleka mtu kuwakaribisha Infadus na Skraga waje wale pamoja nasi. Wakaja tukakaa juu ya viti vidogo, maana Wakukuana hawakai chini kama wanavyokaa Amazulu.

Yule mzee alitupendeza sana namna alivyotuheshimu, lakini tuliona kuwa Yule kijana alitushuku, akawa anatutilia shaka.

Yeye pamoja na wenzake alistaajabu alipoona weupe wetu na uchawi wetu; lakini alipoona kuwa tuna kula na kunywa na kulala kama wanavyofanya wanadamu wengine, basi hofu aliyokuwa nayo ilianza kumtoka kidogo.

Tulipokuwa tukila, Bwana Henry akaniomba nijaribu kuwauliza kama wanazo habari za ndugu yake; lakini nilifikiri ni afadhali tungoje mpaka wakati mwingine. Baada ya kula tulikaa tukavuta tumbako, na Infadus na Skraga wakashangaa, maana Wakukuana hawakuwa na habari za matumizi ya tumbako. Tumbako inaota katika nchi yao lakini hawavuti, hunusa tu.

Halafu nilimuuliza Infadus tutaendelea lini na safari yetu? Akaniambia ya kuwa safari imekwisha fungwa nayo itakuwa asubuhi siku ya pili na tarishi amekwisha tangulia kumpa habari mfalme Twala ya kuwa tunakwenda.

Twala alikuwa anakaa katika mji wake mkubwa ulioitwa Loo. Naye alikuwa akitayarisha karamu kubwa ya siku kuu iliyokuwa katika mwezi wa juni.

Katika karamu hiyo ni desturi kwa jeshi zima kuhudhuria mbele ya Mfalme ila wale tu wanaolinda miji, na tena ndio wakati wanapohudhuria wachawi wote walio katika nchi, lakini nitasimulia habari zake zote baadaye.


Infadus alitwambia kuwa tutaondoka kutakapo pambazuka tu, na njiani tutalala usiku mmoja tu, yaani ikiwa mito haina maji mengi.

Alipokwisha kutwambia hayo, akatuaga; nasi tulilala, ila tulimweka mtu mmoja akeshe atulinde tusishambuliwe kwa ghafla. Tukajitupa vitandani tukalala usingizi mtamu.
 
SURA YA TISA

Hapana haja ya kusimulia habari za mambo yote yaliyotokea katika safari yetu mpaka kufika mji wa Loo.

Ilikuwa mwendo wa siku mbili kufuata Njia Kuu ya Sulemani iliyopita katikati ya nchi ya Wakukuana. Yatosha kusema kuwa tulipozidi kuingia katika nchi tuliona kuwa inazidi kuwa nzuri, na mashamba na nyumba zilizidi kuwa nyingi.

Miji yote ilijengwa kufuata taratibu ile iliyotumiwa katika kujenga lile kambi la askari, na kila mji ulilindwa na kikosi cha askari.

Maana katika nchi yao Wakukuana hufuata desturi ile wanayofuata Amazulu, na Wadachi, na Wamasai, yaani kila mtu mzima ni askari, na kwa hivyo nguvu zote za taifa ni tayari wakati wa vita, vikiwa vya kushambulia au kujitetea. Tulipokuwa tukisafiri tuliona askari elfu nyingi wanakwenda mbio Loo kwenye siku kuu ile ya mwaka, nao walikuwa wa kupendeza sana.

Jioni ya siku ya pili tulipumzika kidogo juu ya kilima, tukatazama chini na tukaona mji’ wa Loo katika uwanda.

Mji ulikuwa mkubwa na kuuzunguka ni mwendo wa maili tano, na kwa nje miji midogo iliyotumika kwa askari wakati wa siku kuu ilionekana. Mji ulikaa vizuri sana, na katikati yake mto ulipita uliogawanya mji sehemu mbili.

Infadus aliona kuwa tunatazama mji akasema, ‘Njia inaishia huko kwenye milima ile mitatu inayoitwa Vichawi Vitatu.’ Akaonyesha` kwa mkono mahali penyewe, Nikamuuliza, ‘Mbona inaishia hapo?’ Akajibu, ‘Nani anayejua? Milima imejaa mapango na katikati lipo shimo linalokwenda chini sana.

Ndipo wale watu wa zamani waliokwenda kupata waliyojia kuyapata, ndipo tunapowazika wafalme wetu sasa, yaani ni Mahali pa Mauti.’ Nikamuuliza, ‘Wale watu walikuja kutafuta nini?’ Akajibu, ‘Sijui, nyinyi mabwana mlioshuka kutoka nyotani hamkosi kujua.’

Akanitazama macho upande. Nadhani alijua mambo zaidi lakini hakutaka kuniambia. Nikajibu , ‘Ndiyo, umesema kweli, katika nyota twafundishwa mambo mengi. Nimesikia kuwa wazee wale wenye busara wa zamani walikuja hapa milimani ili watafute mawe yanayong’aa, mawe mazuri mno, na chuma chenye rangi ya kimanjano.’

Akasema, ‘Bwana una akili nyingi. Mimi ni mtoto tu, siwezi kuongea nawe juu ya mambo hayo. Afadhali useme na Kizee Gagula katika jumba la Mfalme, ndiye mwenye akili kama zako bwana.’ Akaondoka na mara niliwaonyesha wenzangu ile milima nikasema, ‘Mashimo ya Almasi ya Sulemani ni kule.’

Umbopa aliyekuwa kasimama anafikiria kama ilivyokuwa desturi yake, alisikia maneno yangu akasema, ‘Ndiyo, Makumazahn, almasi zipo kweli, nawe utazipata maadam nyinyi watu weupe mnapenda michezo na fedha.’

Nikamuuliza , ‘Unajuaje hayo Umbopa?’
Alicheka akasema, ‘Niliota ndoto usiku.’ Akageuka akaondoka.

Bwana Henry akasema, ‘Je, rafiki yetu ana nini? Yeye anajua mambo mengi lakini hapendi kuyasema. Hayo ni dhahiri. Lakini, Quatermain, ulimuuliza kama amesikia habari za ndugu yangu?’ Nikajibu, ‘Hajasikia hata kidogo, amemuuliza kila mtu anayemjua lakini wote wanasema kuwa hapana mtu mweupe aliyefika katika nchi hii.’


Bwana Good akasema, ‘Unadhani kama alifika hapa? Maana sisi tulifika kwa miujiza tu; yeye angaliwezaje kufika hapa bila ramani?’ Bwana Henry akasema, ‘Sijui, lakini nadhani tutamwona.’ Na sauti yake ilionyesha huzuni.

Basi jua lilishuka na giza likafunika nchi kama wingu, lakini giza halikuficha nchi kwa muda mrefu, na mara mwezi ulitoka na mbalamwezi ikazagaa kila mahali.

Tulisimama tukatazama nchi namna ilivyokuwa nzuri mno, na Infadus akaja akasema, ‘Ikiwa mabwana mmekwisha pumzika tushike safari yetu kwenda Loo, ndipo kulipotengenezwa nyumba ya kukaa usiku huu. Sasa mbalamwezi inaangaza nchi hamwezi kujikwaa njiani.’

Tukakubali, na baada ya saa moja tulikuwa tumefika mpaka wa mji, na mioto ya kambi ilikuwa haihesabiki kwa wingi wake.

Tulifika upesi kwenye daraja ya kuvukia, tukaona askari analinda zamu. Infadus alitaja neno la kujulisha kama tu rafiki, tukapita katika njia kuu ya katikati ya mji.

Baada ya mwendo wa nusu saa tulipokuwa tukipita katika majumba, Infadus alisimama mbele ya mlango uliokuwa umekabili nyumba chache zilizopangwa kuzunguka kiwanja kilichopigiliwa mawe na chokaa, akatuambia ya kuwa hizo ni nyumba zetu.
Tuliingia tukaona kuwa kila mtu amewekewa nyumba yake.

Nyumba hizo zilikuwa bora kuliko nyumba zozote tulizo ziona. Katika kila nyumba kilikuwamo kitanda kilichotandikwa ngozi zilizolainishwa na majani mabichi.

Chakula kilikuwa kimepakuliwa tayari, na mara tulipokwisha nawa mikono, wanawali wazuri walituletea nyama iliyookwa, na bisi zilizowekwa vizuri juu ya sahani za mbao, wakatupa kwa unyenyekevu.

Tukala tukanywa, kisha tukaagiza vitanda vyetu tuhamishiwe katika nyumba moja, tukajitupa vitandani tukalala usingizi wa watu waliochoka kabisa. Tulipoamka tuliona kuwa jua limekwisha panda mbinguni, na wanawali wako nje tayari wameamrishwa kuja kutusaidia tukijitayarisha kuvaa.


Bwana Good akasema, ‘Kujitayarisha nitawezaje nami nina shati moja na viatu tu! Bwana Quatermain, tafadhali waombe waniletee suruali zangu.’ Nikaomba, lakini niliambiwa kuwa zimekwisha chukuliwa kwa mfalme, naye anataka kutuona adhuhuri. Basi tuliwatoa nje wanawali wale tukajitengeneza kadiri tulivyoweza.
 
Bwana Good akanyoa tena upande wa uso wake, lakini tulimwambia asinyoe upande wa pili, maana sasa ndevu nyingi zimekwisha ota.

Tulioga tukachana nywele. Nywele za Bwana Henry zikawa ndefu sana , sasa hata zikafika kwenye mabega yake.

Tulipokwisha kufungua kinywa, tukavuta tumbako, na baadaye kidogo Infadus akaja akatwambia kuwa mfalme Twala yu tayari kutupokea. Lakini tulimwambia kuwa sisi hatuna haraka, tutangoja mpaka jua lipande juu kidogo.

Tulifanya hivi ili asije akafikiri kuwa anaweza kutuita apendavyo yeye. Basi tulikaa muda wa saa nzima tukitengeneza zawadi katika vitu tulivyokuwa navyo, yaani bunduki ile iliyokuwa ya marehemu Ventvogel, na shanga kidogo.

Ile bunduki na risasi zake tulinuia kumpa mfalme, na shanga zile tulitaka kuwapa wake zake na wafuasi wake.

Tulikuwa tumekwisha wapa Infadus na Skraga kidogo wakafurahi sana, maana hawajaona shanga namna zile. Basi baadaye kidogo tulisema kuwa sasa tupotayari, tukaongozwa na Infadus, na Umbopa aliyechukua bunduki na shanga. Baada ya kutembea hatua mia na hamsini tulifika kwenye kiwanja kama kile tulichopewa sisi lakini kikubwa zaidi.

Nyumba nyingi zilipangwa kuzunguka boma la nje, nazo lilikuwa nyumba za wake zake mfalme, Jumba kubwa lilikabili mlango wa kiwanja, nalo ndilo jumba la mfalme. Katikati ya kiwanja kulikuwa wazi yaani hapana nyumba, ila kulijaa vikosi vya askari, na askari walipata elfu saba au nane.


Askari hao walikuwa wamesimama kimya kama masanamu.
Tukapita katikati yao. Siwezi kueleza jinsi walivyokuwa wazuri. Wote walivaa manyoya vichwani, na mikononi walikuwa wameshika ngao ndogo na mikuki iliyong’aa katika mwangaza wa jua.

Palikuwa na nafasi mbele ya jumba na viti vimepangwa tayari. Infadus alituashiria, tukakaa vitini na Umbopa alisimama nyuma yetu. Infadus alisimama mbele ya mlango wa jumba.

Muda wa dakika kumi tulikaa hivi kimya kabisa, lakini tulijua kuwa macho elfu yalitutazama na ikawa ni hali ya kutisha mno, lakini tulifanya kama si kitu.

Halafu mlango wa jumba ulifunguliwa na jitu kubwa sana, likatoka. Lilikuwa limevaa ngozi ya chui begani na limefatwa na Yule kijana Skraga na kitu kilichoonekana kuwa kama nyani kimefunikwa nguo za ngozi yenye manyoya.

Lile jitu lilikaa kitini, na Yule kijana Skraga alisimama nyuma yake, na kile kitu kama nyani kikakaa kitako; ikawa kimya kabisa.

Sasa Yule mtu mkubwa alisimama akavua ngozi ile ya chui, akawa wa kutisha mno. Alikuwa mkubwa kabisa na sura yake ilichukiza kupita sura zote tulizoziona. Midomo yake ilikuwa minene mno, pua yake imebonyeka, na alikuwa na jicho moja tu linalong’aa. Jicho lingine hana ila tundu tu.

Sura yake ilionyesha ukali na uovu kupita kiasi. Kichwani alivaa manyoya ya mbuni marefu meupe, na mwilini nguo za minyororo miembamba ya chuma iliyofumwa pamoja, na kiunoni na magotini amefungwa mikia meupe ya ng’ombe.

katika mkono wa kulia ameshika mkuki mkubwa sana, na shingoni amevaa mkufu wa dhahabu, na juu ya kipaji cha uso almasi kubwa iliyong’aa sana ilikuwa imefungwa.
Hata sasa ilikuwa kimya; lakini si kwa muda mrefu, Mara Yule mtu, maana ndiye mfalme, akainua mkuki wake.

Mara ile mikuki elfu nane iliinuliwa na sauti nene nane elfu zikajibu amkio la mfalme, ‘Koom.’ Mara tatu walisema hivi, na kila mara sauti ilifanya nchi kutetemeka. Ikawa kama mlio wa ngurumo.

Ndipo tuliposikia sauti kali iliyotoka kwa Yule aliyekuwa kama nyani, ‘Mfalme Mtukufu, ni Mfalme.’ Na mara sauti kubwa zilitoka kwa askari wale elfu nane, ‘Ni Mfalme, Mfalme Mtukufu, ni Mfalme.’

Ikawa kimya kabisa tena, lakini mara askari mmoja aliyesimama upande wa kushoto ngao yake ilimtoka mkononi, ikapiga chini kwa kishindo . twala akamgeukia na kumwambia, ‘Njoo hapa wewe.’

Kijana mzuri akaja akasimama mbele yake. Twala akasema, ‘Mbwa wewe usiyeangalia, ngao yako ndiyo iliyoanguka? Wataka kuishusha heshima yangu mbele ya wageni hawa waliotoka kwenye nyota? Je, unalo la kusema?’ Yule kijana alisawajika akasema kwa sauti ndogo, ‘Sikukusudia, Ee Ndama wa Ng’ombe Mweusi .’


Twala akasema, ‘Umenifanya mpumbavu mbele za watu hawa; jiweke tayari kufa.’
Akajibu kwa sauti ndogo, ‘Mimi ni ng’ombe wa mfalme .’ Twala akasema kwa sauti kubwa, ‘Skraga, hebu nione ustadi wako wa kutumia mkuki.

Niulie huyu mbwa.’ Skraga akasimama mbele huku kakenua, akainuka mkuki wake. Yule masikini kijana akaweka mkono mbele ya macho yake, akasimama kimya. Na sisi tulikuwa kama tumegeuka mawe.
 
Skraga akapunga mkuki wake mara moja, mara ya pili, akapiga. Aah! Umempiga, umetoka upande wa pili kadiri ya futi moja.

Akanyosha mikono yake juu akaanguka, akafa. Basi yamekwisha; pale maiti amelala, nasi bado hatujatambua vema mambo yaliyotokea. Bwana Henry akaruka juu na kupiga ‘Lahaula,’ lakini mara alikaa tena, maana kila mtu alikaa kimya.

Mfalme akasema, ‘Lilikuwa pigo zuri sana. Haya, mwondoe.’ Na watu wanne wakatoka katika kikosi wakamwinua Yule mtu aliyeuawa wakamchukua. Hapo tulisikia ile sauti ndogo tena ya Yule kama nyani, ‘Futeni alama ya damu, futeni. Amri ya mfalme imetekelezwa.’

Mwanamwali mmoja akatoka amechukua chokaa katika kapu akainyunyiza juu ya alama ya damu. Huku nyuma Bwana Henry alishikwa na ghadhabu kuu; nikamzuia kwa shida asisimame, nikamnong’oneza, ‘Kaa, kaa usisimame au tutapoteza maisha yetu.’ Akakubali akakaa.

Twala alikaa kimya mpaka alama zile za damu zimekwisha futwa, ndipo aliposema, ‘Watu weupe mmetoka wapi, mmekuja kutafuta nini?’ Nikajibu, ‘Tumetoka katika nyota, usituulize kwa namna gani, Tumekuja kutazama nchi hii.’

Akasema, ‘Mmesafiri kutoka mbali ili kuja kutazama kitu kidogo. Je, na Yule ametoka katika nyota vile vile?’ (akamwonyesha Umbopa.) Nikamjibu, ‘Hakika hata watu wa rangi uliyonayo wewe wapo mbinguni; lakini Mfalme Twala haifai kuuliza mambo ambayo huwezi kuyafahamu.’

Akajibu, na sauti yake iliyochukiza sana, ‘Nyinyi watu wa nyota mnasema kwa sauti na maneno ya kiburi sana, afadhali mkumbuke kuwa nyota ziko mbali, na nyinyi mpo hapa. Je, itakuwaje nikikufanyeni kama Yule waliye mchukua?’

Nikacheka sana, lakini katika moyo wangu sikuwa na kicheko, nikajibu, ‘Ee Mfalme, tahadhari sana, nenda pole pole juu ya mawe ya moto usije ukaunguza nyayo zako; uushike mkuki kwenye mpini usije ukakukata mkono.

Ukigusa hata unywele mmoja wa vichwa vyetu utaangamia papo hapo. Je, huyu Infadus na Skraga hawajakwambia sisi ni watu gani? Umepata kuwaona watu kama sisi?’ (Nikamwonyesha Bwana Good, maana nilijua hakika kuwa hajaona mtu kama yeye.) Mfalme akamtazama Bwana Good akasema, ‘Ni kweli, sijaona.’


Basi nikaendelea nikasema, ‘Hawajakwambia namna tunavyoweza kuwaua watu kwa mbali?’ Mfalme akajibu, ‘Wameniambia, lakini sisadiki. Nataka nione kwa macho yangu ukimuua mtu. Muue mtu Yule anayepita kule, nami nitasadiki.’ Akaonyesha mtu aliyekuwa akipita upande mwingine wa mji.

Nikajibu, ‘La, sisi hatumwagi damu ya watu wasio na hatia lakini ukitaka kuona, basi amuru mtu alete ng’ombe, na kabla hajaenda hatua ishirini nitamuua Yule ng’ombe.’ Mfalme akacheka, akasema, ‘Hapana, ukimuua mtu ndipo nitakapo sadiki.’

Nikajibu, ‘Vema’ wewe nenda upite uwanjani na kabla hujafika mlangoni utakuwa maiti; au kama hupendi kwenda wewe mwenyewe, basi mpeleke mwanao Skraga.’ Basi kusikia hayo tu, Skraga akalia sana akaondoka akakimbilia nyumbani. Twala akakunja uso akasema, ‘Leteni ng’ombe.’


Mara watu wawili walikwenda mbio kuleta ng’ombe, nikamwambia Bwana Henry, ‘Sasa Bwana Henry ni juu yako kumpiga ng’ombe, maana nataka mfalme ajue kuwa si mimi tu ninayeweza kupiga bunduki.’

Basi tukakaa kimya kidogo, halafu tukaona ng’ombe anakuja mbio, na mara alipoona wale watu wengi, akasimama.

Nikamwambia Bwana Henry. ‘Haya sasa piga.’ Na pale pale akaelekeza bunduki akapiga. Mara ile ile ng’ombe alilala kafa. Basi hapo watu wote walishangaa wakazuia pumzi; nikageuka nikamwambia mfalme, ‘Je, mfalme nimesema kweli?’
Mfalme akajibu, na sauti yake ilikuwa ya mtu anayeogopa sana, ‘Ndiyo, mtu mweupe, umesema kweli.’

Basi nikaendelea nikasema, ‘Sikiliza, Twala. Umeona sasa unaweza kusadiki kuwa sisi tumekuja kwa amani wala si kwa vita. Tazama.’ Nikamwonyesha ile bunduki tuliyomletea.
‘Huu ndio mwanzi utakaokupa nguvu kuua kama sisi tunavyoua, lakini naweka sharti hii, usimuue mtu. Ukiielekeza kumpiga mtu, utajiua wewe mwenyewe.

Ngoja, nitakuonyesha. Mwambie mtu mmoja apime hatua arubaini kisha achomeke mkuki katika ardhi na bamba lake lituelekee sisi.’

Akaamuru ikafanywa, nikasema, ‘Sasa tazama utaona kuwa nitalivunja nikapiga bunduki.

Risasi ikalipiga lile bamba la mkuki likavunjika vunjika vipande. Tena watu wote walizuia pumzi kwa kushangaa, nikasema, ‘Sasa Twala, twakupa mwanzi huu, na baadaye nitakufundisha namna ya kuutumia, lakini uangalie sana usiutumie uchawi huu wa nyota kumdhuru mtu wa duniani.’


Nikampa ile bunduki. Mfalme akaitwaa kwa kuiogopa akailaza miguuni pake. Alipokuwa akiiweka, Yule kama nyani akatamani kutoka kivulini mwa nyumba. Alitambaa kwa miguu na mikono, lakini alipofika mahali alipokuwa kakaa mfalme, akasimama, akafunua uso wake ambao ulikuwa wa kutisha mno.

Alikuwa mwanamke kizee sana sana, na uso wake umekunjika mno kwa uzee hata kuwa kama uso wa mtoto mchanga wenye mikunjo mingi.

Kinywa chake kilikuwa kama ufa katika mikunjo hiyo, na chini ya ufa, kidevu chake kilitokeza kama ncha. Alikuwa na pua ndogo na kama macho yake yasingelioneka , uso wake ungalikuwa kama uso wa maiti iliyokauka kwa kuwekwa juani.


Lakini macho yake yaling’aa kama mwenye akili nyingi. Kichwa chake kilikuwa kipara, hana nywele kabisa, na ngozi ya utosini iliyokunjana ikimeta kama ngozi ya nyoka.
Mtu huyu alitufanya kutetemeka kwa hofu.

Alisimama kimya kidogo, kisha akaweka mkono wake uliokuwa na makucha marefu sana, juu ya bega la mfalme Twala, akasema kwa sauti nyembamba na kali, ‘Sikiliza, Ee Mfalme! Sikilizeni, Ee Mashujaa!


Sikilizeni, Ee milima na nyanda na mito, na nchi ya Wakukuana! Sikilizeni, Ee mbingu na jua, Ee mvua na dhoruba na ukungu! Sikilizeni, Ee wanaume na wanawake, Ee vijana na wanawali, na nyinyi watoto msiozaliwa bado! Sikilizeni, vitu vyote vyenye uhai vitakavyokufa! Sikilizeni, vitu vyote vilivyokufa vitakavyofufuka na kufa tena! Sikilizeni, nami nitabashiri. Sasa nabashiri, nabashiri!’

Sauti yake ilififia na watu wote walishikwa na hofu kuu. Kizee huyu alitisha mno. Akaendelea. ‘Damu! Damu! Damu! Mito ya damu; damu pote pote. Naiona, naisikia, naionja ina chumvi! Ni nyekundu juu ya nchi! Inanyesha kutoka mawinguni. Nyayo! Nyayo! Nyayo! Nyayo za watu weupe watokao mbali. Zinatikisa nchi; nchi inatetemeka mbele ya bwana wake.


Damu ni njema, damu nyekundu hung’aa; hakuna harufu kama harufu ya damu iliyomwagwa kwa kiasi. Simba watailamba na kunguruma, tai wataoshea mbawa zao ndani yake na watalia kwa furaha.


Mimi ni mzee! Mimi ni mzee! Nimeona damu nyingi; ha,ha.! Lakini nitaona nyingi zaidi kabla sijafa, nitafurahi. Baba zenu walinijua, na baba zao walinijua, na baba za baba zao. Nimeona watu weupe, ninajua tama zao. Mimi mzee, lakini milima hii imenipita kwa uzee. Nani aliyetengeneza Njia Kuu, niambieni?’


Nani aliyechora sanamu zile juu ya miamba, niambieni? Nani aliyeumba wale Watatu walio kimya wanaotazama shimo, niambieni?’

Akaelekeza mkono wake kuonyesha kwenye milima ile mirefu. Akaendelea, ‘Hamjui, lakini mimi najua. Walikuwa watu weupe waliowatangulieni nao watakuja hapo nyinyi mtakapokwisha kutoweka, watawaleni na kuwaaharibuni.


Ndiyo! Ndiyo! Ndiyo! Na hao watu weupe walijia nini? Wenye kutisha, Wenye elimu ya uchawi na maarifa yote, wenye nguvu wasiochelea! Ee Mfalme, lile jiwe linalong’aa katika kipaji chako ni nini? Mikono ya nani ilifuma nguo hizo za minyororo unazovaa kifuani, Ee mfalme?

Hujui!, ila mimi najua. Mimi, mzee, mimi mwenye busara, mimi Isanusi, Kichawi.’ Akatugeukia akasema, ‘Nyinyi watu weupe wa Nyota mnatafuta nini? Mnatafuta mmoja wenu aliyepotea?


Hayupo. Hapana mguu mweupe uliokanyaga nchi hii tangu vizazi na vizazi vilivyopita ila mara moja tu, naye alipoondoka hapa aliondoka kwenda kufa tu.

Mmekuja kuchuma mawe yanayong’aa; najua, najua; damu itakapokwisha kukauka mtayaona; lakini je, mtarudi mtokako au mtakaa na mimi?


Ha!ha!ha! Na wewe, wewe mwenye ngozi nyeusi, mwenye udaha, nani wewe, unatafuta nini? Wewe hutafuti mawe yanayong’aa wala chuma cha dhahabu, hayo unawaachia watu weupe watokao kwenye Nyota.

Nadhani nakujua; nadhani naweza kusikia harufu ya damu iliyo katika moyo wako. Haya uvue mkanda ..

Basi hapo Yule kizee akawa amepandwa na pepo akaanguka chini na povu likamtoka kinywani, akachukuliwa ndani ya nyumba.

Mafalme akasimama anatetemeka, akapunga mikono. Mara moja vikosi vyote vikaanza kutoka kwa taratibu, na baada ya dakika kumi hapakuwa na mtu ila sisi na Mfalme na watumishi wachache.

Mfalme akasema, ‘Watu weupe, ‘ninayo nia ya kuwauweni, Gagula amesema maneno ya ajabu juu yenu. Mnasemaje?’ Nikacheka nikasema, ‘Angalia, Ee Mfalme, sisi si wepesi wa kuuawa.

Umeona kufa kwa Yule ng’ombe; wataka kuwa kama alivyo Yule ng’ombe?’
Mfalme akakunja uso akasema, ‘Si busara kujaribu kumtisha mfalme.’
Nikasema, ‘Hatujaribu kukutisha, tunayoyasema ni ya kweli.

Ukijaribu kutuua basi utatutambua’ Yule mfalme akaweka mkono kichwani akafikiri, kisha akasema, ‘Nendeni kwa amani.


Usiku wa leo kuna ngoma kuu. Mtayiona. Msiogope na kudhani labda nitajaribu kuwanasa. Kesho nitafikiri juu ya habari zenu.’ Nikajibu, ‘Vema, Ee mfalme.’ Kisha tukaondoka, tukafuatana na Infadus tukaenda nyumbani kwetu.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…