Skraga akapunga mkuki wake mara moja, mara ya pili, akapiga. Aah! Umempiga, umetoka upande wa pili kadiri ya futi moja.
Akanyosha mikono yake juu akaanguka, akafa. Basi yamekwisha; pale maiti amelala, nasi bado hatujatambua vema mambo yaliyotokea. Bwana Henry akaruka juu na kupiga ‘Lahaula,’ lakini mara alikaa tena, maana kila mtu alikaa kimya.
Mfalme akasema, ‘Lilikuwa pigo zuri sana. Haya, mwondoe.’ Na watu wanne wakatoka katika kikosi wakamwinua Yule mtu aliyeuawa wakamchukua. Hapo tulisikia ile sauti ndogo tena ya Yule kama nyani, ‘Futeni alama ya damu, futeni. Amri ya mfalme imetekelezwa.’
Mwanamwali mmoja akatoka amechukua chokaa katika kapu akainyunyiza juu ya alama ya damu. Huku nyuma Bwana Henry alishikwa na ghadhabu kuu; nikamzuia kwa shida asisimame, nikamnong’oneza, ‘Kaa, kaa usisimame au tutapoteza maisha yetu.’ Akakubali akakaa.
Twala alikaa kimya mpaka alama zile za damu zimekwisha futwa, ndipo aliposema, ‘Watu weupe mmetoka wapi, mmekuja kutafuta nini?’ Nikajibu, ‘Tumetoka katika nyota, usituulize kwa namna gani, Tumekuja kutazama nchi hii.’
Akasema, ‘Mmesafiri kutoka mbali ili kuja kutazama kitu kidogo. Je, na Yule ametoka katika nyota vile vile?’ (akamwonyesha Umbopa.) Nikamjibu, ‘Hakika hata watu wa rangi uliyonayo wewe wapo mbinguni; lakini Mfalme Twala haifai kuuliza mambo ambayo huwezi kuyafahamu.’
Akajibu, na sauti yake iliyochukiza sana, ‘Nyinyi watu wa nyota mnasema kwa sauti na maneno ya kiburi sana, afadhali mkumbuke kuwa nyota ziko mbali, na nyinyi mpo hapa. Je, itakuwaje nikikufanyeni kama Yule waliye mchukua?’
Nikacheka sana, lakini katika moyo wangu sikuwa na kicheko, nikajibu, ‘Ee Mfalme, tahadhari sana, nenda pole pole juu ya mawe ya moto usije ukaunguza nyayo zako; uushike mkuki kwenye mpini usije ukakukata mkono.
Ukigusa hata unywele mmoja wa vichwa vyetu utaangamia papo hapo. Je, huyu Infadus na Skraga hawajakwambia sisi ni watu gani? Umepata kuwaona watu kama sisi?’ (Nikamwonyesha Bwana Good, maana nilijua hakika kuwa hajaona mtu kama yeye.) Mfalme akamtazama Bwana Good akasema, ‘Ni kweli, sijaona.’
Basi nikaendelea nikasema, ‘Hawajakwambia namna tunavyoweza kuwaua watu kwa mbali?’ Mfalme akajibu, ‘Wameniambia, lakini sisadiki. Nataka nione kwa macho yangu ukimuua mtu. Muue mtu Yule anayepita kule, nami nitasadiki.’ Akaonyesha mtu aliyekuwa akipita upande mwingine wa mji.
Nikajibu, ‘La, sisi hatumwagi damu ya watu wasio na hatia lakini ukitaka kuona, basi amuru mtu alete ng’ombe, na kabla hajaenda hatua ishirini nitamuua Yule ng’ombe.’ Mfalme akacheka, akasema, ‘Hapana, ukimuua mtu ndipo nitakapo sadiki.’
Nikajibu, ‘Vema’ wewe nenda upite uwanjani na kabla hujafika mlangoni utakuwa maiti; au kama hupendi kwenda wewe mwenyewe, basi mpeleke mwanao Skraga.’ Basi kusikia hayo tu, Skraga akalia sana akaondoka akakimbilia nyumbani. Twala akakunja uso akasema, ‘Leteni ng’ombe.’
Mara watu wawili walikwenda mbio kuleta ng’ombe, nikamwambia Bwana Henry, ‘Sasa Bwana Henry ni juu yako kumpiga ng’ombe, maana nataka mfalme ajue kuwa si mimi tu ninayeweza kupiga bunduki.’
Basi tukakaa kimya kidogo, halafu tukaona ng’ombe anakuja mbio, na mara alipoona wale watu wengi, akasimama.
Nikamwambia Bwana Henry. ‘Haya sasa piga.’ Na pale pale akaelekeza bunduki akapiga. Mara ile ile ng’ombe alilala kafa. Basi hapo watu wote walishangaa wakazuia pumzi; nikageuka nikamwambia mfalme, ‘Je, mfalme nimesema kweli?’
Mfalme akajibu, na sauti yake ilikuwa ya mtu anayeogopa sana, ‘Ndiyo, mtu mweupe, umesema kweli.’
Basi nikaendelea nikasema, ‘Sikiliza, Twala. Umeona sasa unaweza kusadiki kuwa sisi tumekuja kwa amani wala si kwa vita. Tazama.’ Nikamwonyesha ile bunduki tuliyomletea.
‘Huu ndio mwanzi utakaokupa nguvu kuua kama sisi tunavyoua, lakini naweka sharti hii, usimuue mtu. Ukiielekeza kumpiga mtu, utajiua wewe mwenyewe.
Ngoja, nitakuonyesha. Mwambie mtu mmoja apime hatua arubaini kisha achomeke mkuki katika ardhi na bamba lake lituelekee sisi.’
Akaamuru ikafanywa, nikasema, ‘Sasa tazama utaona kuwa nitalivunja nikapiga bunduki.
Risasi ikalipiga lile bamba la mkuki likavunjika vunjika vipande. Tena watu wote walizuia pumzi kwa kushangaa, nikasema, ‘Sasa Twala, twakupa mwanzi huu, na baadaye nitakufundisha namna ya kuutumia, lakini uangalie sana usiutumie uchawi huu wa nyota kumdhuru mtu wa duniani.’
Nikampa ile bunduki. Mfalme akaitwaa kwa kuiogopa akailaza miguuni pake. Alipokuwa akiiweka, Yule kama nyani akatamani kutoka kivulini mwa nyumba. Alitambaa kwa miguu na mikono, lakini alipofika mahali alipokuwa kakaa mfalme, akasimama, akafunua uso wake ambao ulikuwa wa kutisha mno.
Alikuwa mwanamke kizee sana sana, na uso wake umekunjika mno kwa uzee hata kuwa kama uso wa mtoto mchanga wenye mikunjo mingi.
Kinywa chake kilikuwa kama ufa katika mikunjo hiyo, na chini ya ufa, kidevu chake kilitokeza kama ncha. Alikuwa na pua ndogo na kama macho yake yasingelioneka , uso wake ungalikuwa kama uso wa maiti iliyokauka kwa kuwekwa juani.
Lakini macho yake yaling’aa kama mwenye akili nyingi. Kichwa chake kilikuwa kipara, hana nywele kabisa, na ngozi ya utosini iliyokunjana ikimeta kama ngozi ya nyoka.
Mtu huyu alitufanya kutetemeka kwa hofu.
Alisimama kimya kidogo, kisha akaweka mkono wake uliokuwa na makucha marefu sana, juu ya bega la mfalme Twala, akasema kwa sauti nyembamba na kali, ‘Sikiliza, Ee Mfalme! Sikilizeni, Ee Mashujaa!
Sikilizeni, Ee milima na nyanda na mito, na nchi ya Wakukuana! Sikilizeni, Ee mbingu na jua, Ee mvua na dhoruba na ukungu! Sikilizeni, Ee wanaume na wanawake, Ee vijana na wanawali, na nyinyi watoto msiozaliwa bado! Sikilizeni, vitu vyote vyenye uhai vitakavyokufa! Sikilizeni, vitu vyote vilivyokufa vitakavyofufuka na kufa tena! Sikilizeni, nami nitabashiri. Sasa nabashiri, nabashiri!’
Sauti yake ilififia na watu wote walishikwa na hofu kuu. Kizee huyu alitisha mno. Akaendelea. ‘Damu! Damu! Damu! Mito ya damu; damu pote pote. Naiona, naisikia, naionja ina chumvi! Ni nyekundu juu ya nchi! Inanyesha kutoka mawinguni. Nyayo! Nyayo! Nyayo! Nyayo za watu weupe watokao mbali. Zinatikisa nchi; nchi inatetemeka mbele ya bwana wake.
Damu ni njema, damu nyekundu hung’aa; hakuna harufu kama harufu ya damu iliyomwagwa kwa kiasi. Simba watailamba na kunguruma, tai wataoshea mbawa zao ndani yake na watalia kwa furaha.
Mimi ni mzee! Mimi ni mzee! Nimeona damu nyingi; ha,ha.! Lakini nitaona nyingi zaidi kabla sijafa, nitafurahi. Baba zenu walinijua, na baba zao walinijua, na baba za baba zao. Nimeona watu weupe, ninajua tama zao. Mimi mzee, lakini milima hii imenipita kwa uzee. Nani aliyetengeneza Njia Kuu, niambieni?’
Nani aliyechora sanamu zile juu ya miamba, niambieni? Nani aliyeumba wale Watatu walio kimya wanaotazama shimo, niambieni?’
Akaelekeza mkono wake kuonyesha kwenye milima ile mirefu. Akaendelea, ‘Hamjui, lakini mimi najua. Walikuwa watu weupe waliowatangulieni nao watakuja hapo nyinyi mtakapokwisha kutoweka, watawaleni na kuwaaharibuni.
Ndiyo! Ndiyo! Ndiyo! Na hao watu weupe walijia nini? Wenye kutisha, Wenye elimu ya uchawi na maarifa yote, wenye nguvu wasiochelea! Ee Mfalme, lile jiwe linalong’aa katika kipaji chako ni nini? Mikono ya nani ilifuma nguo hizo za minyororo unazovaa kifuani, Ee mfalme?
Hujui!, ila mimi najua. Mimi, mzee, mimi mwenye busara, mimi Isanusi, Kichawi.’ Akatugeukia akasema, ‘Nyinyi watu weupe wa Nyota mnatafuta nini? Mnatafuta mmoja wenu aliyepotea?
Hayupo. Hapana mguu mweupe uliokanyaga nchi hii tangu vizazi na vizazi vilivyopita ila mara moja tu, naye alipoondoka hapa aliondoka kwenda kufa tu.
Mmekuja kuchuma mawe yanayong’aa; najua, najua; damu itakapokwisha kukauka mtayaona; lakini je, mtarudi mtokako au mtakaa na mimi?
Ha!ha!ha! Na wewe, wewe mwenye ngozi nyeusi, mwenye udaha, nani wewe, unatafuta nini? Wewe hutafuti mawe yanayong’aa wala chuma cha dhahabu, hayo unawaachia watu weupe watokao kwenye Nyota.
Nadhani nakujua; nadhani naweza kusikia harufu ya damu iliyo katika moyo wako. Haya uvue mkanda ..
Basi hapo Yule kizee akawa amepandwa na pepo akaanguka chini na povu likamtoka kinywani, akachukuliwa ndani ya nyumba.
Mafalme akasimama anatetemeka, akapunga mikono. Mara moja vikosi vyote vikaanza kutoka kwa taratibu, na baada ya dakika kumi hapakuwa na mtu ila sisi na Mfalme na watumishi wachache.
Mfalme akasema, ‘Watu weupe, ‘ninayo nia ya kuwauweni, Gagula amesema maneno ya ajabu juu yenu. Mnasemaje?’ Nikacheka nikasema, ‘Angalia, Ee Mfalme, sisi si wepesi wa kuuawa.
Umeona kufa kwa Yule ng’ombe; wataka kuwa kama alivyo Yule ng’ombe?’
Mfalme akakunja uso akasema, ‘Si busara kujaribu kumtisha mfalme.’
Nikasema, ‘Hatujaribu kukutisha, tunayoyasema ni ya kweli.
Ukijaribu kutuua basi utatutambua’ Yule mfalme akaweka mkono kichwani akafikiri, kisha akasema, ‘Nendeni kwa amani.
Usiku wa leo kuna ngoma kuu. Mtayiona. Msiogope na kudhani labda nitajaribu kuwanasa. Kesho nitafikiri juu ya habari zenu.’ Nikajibu, ‘Vema, Ee mfalme.’ Kisha tukaondoka, tukafuatana na Infadus tukaenda nyumbani kwetu.