Basi, tulivuka daraja dogo, tukapita katika mlango mwembamba katika ukuta wa boma tukaingia katika bustani nzuri sana.
Katikati ya kiwanja mbele ya nyumba, tuliuona ule mti mrefu, na Bwana Mackenzie alituambia kuwa ni mnara wake wa kuangalia nchi yote, kisha, akasema, ‘’Lakini hamkosi mnaona njaa, basi haya twendeni.’’
Tulipokwisha kula, tuliviwasha viko vyetu vya tumbako, na Sir Henry akasimulia habari za safari yetu, na mkarimu wetu alisikiliza kwa fadhaa.
Akasema, ‘’Ni dhahiri ya kuwa wale Wajivuni waovu wanawafuata, nami nashukuru sana kuwa mmefika nyumbani kwangu salama.
Nadhani hawatadhubutu kuwashambuli hapa. Lakini ni bahati mbaya, maana karibu watu wangu wote wamekwenda pwani kupeleka pembe za ndovu na vitu vingine.
Wako watu mia mbili katika msafara huo, na kwa hivi wamebaki watu ishirini tu wanaoweza kulilinda boma letu ikiwa watatushambulia.
Lakini hata hivyo, nitatoa amri kadha wa kadha ili tusije tukatokewa ghafla.’’ Akamwita mtu mmoja aliyekuwa amesimama nje katika bustani, akamwambia maneno kwa Kiswahili. Yule mtu alisikiliza, kisha, alipiga saluti akaondoka.
Bwana Mackenzie alipokaa tena, nilimwambia, ‘’Natumaini sana ya kuwa hatutawaletea misiba, basi ni afadhali twende mbele na kubahatisha ajali yetu, kuliko kuwaletea wale watu waovu hapa.’’
Akajibu, ‘’Hapana kabisa, hamwendi sasa. Wajivuni wakija, basi watakuja, lakini nadhani nitaweza kuwapokea kwa namna itakayofaa. Mimi siwezi kumwondoa mgeni aende zake hata kama Wajivuni wote wa duniani wakija.’’
Nikasema, ‘’Sasa nakumbuka, Bwana Balozi wa Lamu alituambia kuwa alipata barua kutoka kwako, ambayo kwayo ulimpa habari ya kwamba mtu mmoja alifika toka mbali akasema ameona watu weupe mbali sana ndani ya nchi. Je, unasadiki habari alizokuambia?
Nauliza kwa sababu mara mbili tatu katika, maisha yangu nimesikia tetesi ya habari hizo kwa wenyeji waliotoka kaskazini mbali sana, ya kuwa taifa la watu hao lipo.’’
Bwana Mackenzie asijibu kwanza, ila alitoka chumbani, kisha alirudi tena amechukua upanga wa namna.
Ulikuwa mrefu, na bamba lake ambalo lilikuwa nene na zito lilikuwa limetiwa temsi lote hata kufika karibu na makali yake, na kazi yake ilipambwa kwa dhahabu. Akasema, ‘’Je, umepata kuuona upanga kama huu?’’
Sote tuliutazama sana, tukavitikisa vichwa vyetu.
Akaendelea akasema, ‘’Nimeuleta kuwaonyesha kwa sababu Yule mtu aliyesema ameona watu weupe ndiye aliyeuleta pamoja naye tena, kwa sababu unafanya habari alizozisema kuwa kama kwamba ni kweli.
Kama asingaliuleta nisingalimsadiki. Tazameni; nitawaambieni habari zote kadiri ninavyozijua, lakini si nyingi.
Siku moja jioni nilikuwa nimekaa barazani, na maskini mtu aliyedhoofu sana alikuja akichechemea, akaketi mbele yangu.
Nikamuuliza ana habari gani, akaanza kuniarifu habari kama yeye ni mtu wa kabila linalokaa mbali sana kaskazini.
Na jinsi kabila lake lilivyoangamizwa na watu wa kabila jingine, na yeye pamoja na watu wengine wachache waliosalia, walifukuziwa kaskazini zaidi kupita ziwa liitwalo Laga.
Kutoka huko, alikwenda mpaka ziwa jingine lililoko juu ya mlima, akaliita ‘ziwa lisilo na mwisho kwa kwenda chini.’
Na huko mkewe na ndugu yake wakafa kwa ugonjwa wa kuambukiza labda ndui na kwa hivi watu wa huko walimfukuzia jangwani atoke katika miji yao.
Akatangatanga kupita juu ya milima muda wa siku kumi, kisha, akaingia katika gongo la mwitu wa miti yenye miiba.
Na siku moja akaonekana huko na watu weupe wengine waliokuwa wakiwinda, wakamchukua mahali ambapo watu wote ni weupe, wakaao katika nyumba za mawe.
Alikaa hapo muda wa juma moja amefungiwa katika nyumba, mpaka siku moja mtu mwenye ndevu nyeupe, aliyemtambua kuwa ni mganga, akaja kumtazama, kisha akaongozwa kupita katika mwitu wa miti yenye miiba mpaka jangwani, akapewa chakula na upanga huu, ndivyo alivyosema, akaachwa huru.’’
Sir Henry alikuwa akisikiliza sana habari hizi, akasema, ‘’Ndiyo, halafu alifanya nini?’’
Bwana Mackenzie akasema, ‘’Kadiri alivyosema, alipatikana na taabu na maumivu yasiyo na idadi, akaishi siku nyingi anakula mizizi na matunda ya porini, na vinyama alivyoweza kuvikamata na kuviua.
Mradi aliweza kuishi, na kwa mwendo wa Pole pole alisafiri akijia kusini mpaka akafika hapa.
Sikupata simulizi ya mambo yote ya safari yake, nilimwambia arudi kesho yake, nikamwamuru mmojawapo wa wanyapara amtunze usiku ule.
Yule mnyapara alimchukua, lakini Yule maskini alikuwa na upele mwingi hata mke wake mnyapara asikubali aingie ndani asije naye akapata upele pia. Basi alipewa blanketi akaambiwa alale nje.
Ikatokea ya kuwa wakati huo, simba mmoja alizoea kutembeatembea karibu, na kwa bahati mbaya alisikia harufu ya Yule msafiri maskini, akamrukia, akamuuma kichwa hata karibu kutoka kabisa.
Wale waliokuwamo nyumbani hawakuwa na habari, na huu ulikuwa ndio mwisho wake na wa hadithi yake juu ya watu wale weupe na **** habari hizo ni kweli ama si kweli, siwezi kuwaambia.
Je, wewe Bwana Quatermain waonaje?’’
Nilitikisa kichwa changu, nikajibu, ‘’Mimi sijui.
Yapo mambo mengi ya ajabu yaliyofichika katikati ya kochi hii kubwa, nami sipendi kusema kuwa ni kweli, Ama si kweli.
Lakini liwalo lolote na liwe, tumekaza nia kujaribu kuvumbua habari,. Tumenuia kusafiri mpaka Lekakisera, na kutoka huko tutaenda kule kwenye Ziwa Lagana kama wako watu weupe wanaokaa kupita hapo, basi tutajaribu tuwezavyo kuwagundua.’’
Bwana Mackenzie akasema, ‘’Ninyi watu ni jasiri sana.’’ Akacheka kidogo, tukaziacha habari zile.