Hakuna biashara kichaa kama kuwekeza kwenye mpira duniani kote kwani pesa inaanza kurudi sio chini ya miaka mitano tangu senti ya kwanza iwekezwe na wakati mwingine inaweza isirudi kabisa. Matajiri wengi wanaowekeza kwenye mchezo wa mpira wa miguu ni kwa sababu ya mapenzi yao kwenye mpira wa miguu tu na suala la faida huja baadae sana.
Kama ingekuwa ni rahisi kuwekeza kwenye mpira leo Vodacom na Serengeti Breweries wangekuwa na timu zao kwenye ligi kuu na hata timu za TBL (Plisner Dar na Ndovu Arusha) zingekuwa bado zipo na zinacheza ligi kuu. Lakini makampuni yote hayo (Voda na TBL) yaliona ni rahisi kudhamini ligi kuu na Serengeti waliona ni rahisi kudhamini timu ya taifa na si kudhamini vilabu kwani ni gharama kubwa sana.
Napata shida kumwelewa mtu anayesema ni lazima wawekezaji wawe watatu (3) katika asilimia 49. Je akipatikana mmoja tu au wawili tu huo uwekezaji hautaruhusiwa? Kuna makosa yaliwahi kufanyika kwa mkubwa mmoja kufuta michezo mashuleni ilituchukua zaidi ya miaka 10 kurudisha hali ilivyokuwa kabla japo kwenye riadha imeshindikana kabisa kurudi tulipokuwa. Hili la uwekezaji badala ya kuwavutia wawekezaji tunawafukuza sijui itatuchukua miaka mingapi kuwavutia wawekezaji na je wakati huo wawekezaji wenye wazimu na mpira dizaini ya MO watakuwepo?
Kwa sheria ya namna hii na matamko ya hivi karibuni kuwa Mo akaanzishe timu yake ni rasmi kuwa soka la bongo linaenda kaburini kwani sidhani kama wawekezaji makini watakuja kuwekeza kwenye vilabu vyetu na hivyo ligi itadorora na mwisho wa siku hata mdhamini wa ligi atakosekana. Hao wavurugaji wote hawajui kuwa baada ya Simba kufanya vizuri chini ya MO ligi yetu imeaanza kufuatiliwa na watu wengi sana Afrika na nje ya bara la Afrika. Na si hivyo tu wachezaji wazawa na wa kigeni zaidi ya kumi wameuzwa/wamepata vilabu nje ya nchi na hata baadhi ya mawakala wakubwa wa wachezaji wameanza kuiona Tanzania kama chimbo jipya la wachezaji wanaofaa kuuzwa sehemu mbalimbali duniani.
Kwa wanaojua mpira kiukweli Mo alijilipuwa sana kuwekeza kwenye mpira lakini vikwazo alivyowekewa vinatosha. Waliaanza asimiliki asilimia 51 akakubali baadae wamebadilisha kibao eti hiyo asilimia 49 wawe watatu. Aliye karibu na Mo amwambie aachane sasa na Simba pesa akawape tu watoto yatima atapata baraka kwa Mungu na atalipwa thawabu kuliko hizi figisu anazofanyiwa. Timu amuachie Kilomoni na genge la watu walimtanguliza mbele waendeshe timu ila wajue tu mshahara wa Kagere ni milioni 10 kwa mwezi na kuiendesha Simba kwa mwezi haitapungua millioni 300 kwa mwezi kwa hiyo zikiisha pesa za CAF 1.5 billioni wanazozipigia mahesabu itabidi waingie mifukoni mwao kuendesha timu.
Narudia tena aliye karibu na Mo amwambie aachane na soka la bongo atapata presha bure apeleke pesa zake kwa watoto yatima atapata thawabu kwa Mungu. Kichekesho watu wana asilimia 51 hawajaweka hata shilingi moja benki, hawajui timu anasafiri vipi, timu inakula nini, mishahara inalipwa vipi, fedha ya usajili inalipwa vipi eti wamekomaa Mo weka bilioni 20 benki wanasahau kuwa Mo ni mwekezaji mwenza na sio mnunuzi hivyo walitakiwa wao wawe wa kwanza kuweke japo hata billioni 5 tu. Wabongo tupo serious kweli?
Yaani nasikitika sana kuona kuwa ligi yetu itakapokosa msisimiko. Tutarudi tena kufuatilia ligi za wenzetu. Viwanja vitakosa watazamaji, soka letu litaporomoka kwani itakuwa sasa Boxer wa Yanga anamkaba Rashid Juma wa Simba badala ya boxer wa Yanga kumkaba Kagere. Mmiliki wa viwanja Tanzania atapoteza mapato kwa kiasi kikubwa sana n.k. Anyway kwa kuwa ndio tumeamua hivyo twendeni tu.