Lengo kuu la HakiElimu ni kuchangia katika kuhakikisha kuwa kila mtoto nchini Tanzania - bila ubaguzi wa aina yoyote ile- anapata haki yake ya elimu bora ya msingi na sekondari. Hapa tunasisitiza kuwa si elimu ya aina yoyote tu, bali ile inayokuza utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu, demokrasia na uzalendo wa dhati ikiwa ni pamoja na uraia unaotambua na kuzingatia haki na wajibu wake na kuweza kuhoji pale haki hizo zinapokiukwa. Kwa mtazamo wetu shule nzuri ni ile inayomjali mtoto, yenye kujali na kuheshimu haki na usawa wa kijinsia (angalia maelezo kuhusu Shule Nzuri ni Ipi (Kuweza kusoma faili hili, unahitaji Acrobat Reader Bonyeza hapa). Shule ni mahali ambapo watoto wanakua na kujifunza kufikiri mambo kwa undani na kuwa wabunifu, ni mahali wanapopata stadi za maisha na kujenga hali ya kujiamini na ambapo wanaheshimiwa na kujifunza kuwaheshimu wengine.
Maono au dira hii ndiyo sababu ya msingi ya kuanzishwa kwa HakiElimu. Uchambuzi wa hali halisi uliotolewa katika sehemu iliyopita unaelezea uchaguzi wa mkakati wetu wa kufikia dira hii. Utaratibu na mbinu yetu katika utekelezaji wa azma hii unaondokana kabisa na dhana ya kuendesha programu yetu kama shughuli ya hisani (welfare) au mradi. Hatuamini kuwa itasaidia sana kuanzisha miradi midogo midogo ya kutoa huduma za kuboresha shule bila kwanza kushughulikia tatizo la msingi linalosababisha kuzorota kwa elimu. Badala yake, tukizingatia uchambuzi wetu, HakiElimu inaelekeza jitihada zake katika kuwezesha na kuimarisha zaidi ushiriki wa wanaume, wanawake na watoto katika utawala wa elimu nchini Tanzania. Tunaamini kuwa kufufua na kuimarisha utawala bora ni jambo muhimu sana katika kuleta mageuzi katika elimu, ikiwa ni pamoja na kufanikiwa kwa Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu (ESDP).
HakiElimu inaendesha shughuli zake ili kufikia lengo hili katika ngazi tatu za kimkakati kama inavyoainishwa hapo chini.
1. Utawala wa Jamii: HakiElimu inawezesha wadau katika ngazi ya chini kabisa kuwa na usemi wakati wa kufanya maamuzi na kubadilisha shule zao kwa kuwezesha ushiriki wao kamilifu katika utawala wa shule na jamii zao. Kwa kuanzia kazi hii inatekelezwa katika wilaya mbili na hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2003 itakuwa ikitekelezwa katika wilaya nne ambazo zinaonekana kuwa na mfumo duni wa elimu na ambazo HakiElimu imeweza kufikia makubaliano nazo kuhusu namna ya kushirikiana ili kuleta maendeleo. HakiElimu imeweka waraghibishi wawili wa jamii katika kila wilaya ili kuratibu kazi hiyo. Mafunzo yanayojitokeza katika utekelezaji wa kazi hiyo yanawekwa katika kumbukumbu na kuchapishwa kwa namna ambayo itakuwa rahisi kuwafikiwa watu wengi zaidi na hatimaye kusambazwa Tanzania nzima hivyo kuwa na matokeo makubwa zaidi.
Lengo la msingi ni kuchochea na kuhimiza demokrasia katika kamati za shule, hii ni katika muundo wake (wajumbe wake nk) na utekelezaji wa majukumu yake. Umuhimu wa kipekee unawekwa katika kuyahusisha makundi ambayo yanawekwa pembezoni na kunyimwa haki zao za kimsingi, ikiwa ni pamoja na watoto, vijana, watu wenye ulemavu, wanawake na masikini, na kuhimiza usawa wa kijinsia. Kamati zinasaidiwa ili ziishirikishe zaidi jamii na kuzifanya ziwajibike zaidi kwa jamii zao, ikiwa ni pamoja na kusikiliza na kushughulikia maoni na hata kero zinazotolewa na wanajamii husika.
HakiElimu inasaidia pia wadau wengine muhimu, hususan wanafunzi na walimu kuanzisha au kujiunga na vyama vyao katika maeneo yao. Ujenzi wa mitandao, upashanaji habari na mafunzo ni mambo yanayohimizwa na kuendelezwa ndani ya wilaya na baina ya wilaya moja na nyingine. Mbinu za uwezeshaji shirikishi na matumizi ya michoro na vielelezo mbalimbali (animation) zinatumika wakati wote ili kuondoa vikwazo vya mfumo wa kufanya maamuzi wenye urasimu na ngazi nyingi za madaraka. Azma ya HakiElimu ni kuimarisha uwezo wa taasisi za wananchi katika maeneo yao ili kuwezesha kufuatilia kwa makini na kuwa na usemi kuhusu utoaji wa huduma ya elimu, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha uwajibikaji wa viongozi katika jamii husika na uwazi katika matumizi ya fedha.
2. Ushiriki wa umma: HakiElimu inachangia katika kuanzisha na kuendeleza harakati za kitaifa aa mabadiliko ya kielimu na kijamii kwa kuchochea na kuhimiza ushiriki mpana zaidi wa jamii, upashanaji habari, kuanzisha na kukuza uanachama na kujenga mitandao ya wanachama. Kazi hii inatekelezwa Tanzania nzima, na ina vipengele vikuu viwili:
Kipengele cha kwanza kinahusu kuibua na kuhamasisha mjadala wa umma kuhusu masuala muhimu katika elimu ya msingi kwa kutumia machapisho mbalimbali, vyombo vya habari vyenye ubunifu na mikutano na makongamano ya umma. Mjadala huu umeanza kwa kuangalia kero au mambo ambayo jamii zingependa yashughulikiwe lakini pia unaingia kwa undani zaidi na kuangalia masuala ya msingi kama vile 'nini malengo ya kwenda shule' na 'mtoto aliyeelimika ni yupi'. Aidha, mjadala huu unaangalia pia masuala mbalimbali yenye mkanganyiko, mathalan, 'iwapo elimu ni muhimu, kwa nini tunawatendea walimu vibaya na kutowathamini'. Mbinu inayotumika ni ile ya kuuliza maswali na kuchochea mijadala badala ya kuhutubia au kuhubiri na kutoa majibu. Umma unahimizwa kuchambua hali mbaya inayoikabili elimu na hatimaye kupendekeza utatuzi wake.
Kipengele cha pili, ambacho pengine ni kipengele cha mkakati wa HakiElimu chenye malengo makubwa sana, ni kujenga msingi imara na kupanua wigo wa uanachama wake miongoni mwa watu binafsi na taasisi zinazojali maendeleo ya elimu kutoka sehemu zote nchini, katika chombo kinachoitwa 'marafiki wa elimu'. Msisitizo unawekwa katika ushiriki kamilifu wa wanawake, wanaume, watoto na vijana. Marafiki wa Elimu wanaweza kuchangia maoni yao na mambo wanayoyatilia shaka na kupatiwa majibu haraka kwa maswali mahsusi wanayoyauliza. Aidha, wanapatiwa taarifa za mara kwa mara kuhusu masuala ya kisera na maoni kuhusu mambo yanayoweza kufanyika ili kuinua elimu katika jamii yao. HakiElimu inawaunganisha marafiki na kuwapatia fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu, kujifunza na kuchukua hatua za pamoja. Vyama vya wananchi na mitandao yao iliyo na isiyo rasmi, itasaidiwa ili kuinua zaidi hamasa na mwamko wao kuhusu elimu nchini. Baada ya muda marafiki wanachama watakuwa ni chombo kikubwa cha wananchi wenye ufahamu wa hali ya juu, waliojiunga pamoja, wanaoweza kuwaelimisha wengine na kutoa shinikizo la kijamii kwa mamlaka zinazohusika na utoaji wa elimu. 3.Uchambuzi wa Sera na Utetezi: HakiElimu inajitahidi kupata fursa ya kutoa mchango wa mawazo na ushauri katika uundaji na utekelezaji wa sera za kitaifa kuhusu elimu na masuala mengine yanayohusiana nayo, na kuinua kiwango cha ushiriki wa umma katika utayarishaji wa sera kwa kupitia programu za utafiti, uchambuzi, utetezi na kujenga mitandao. Hii inajumuisha uchambuzi wa athari za sera za kitaifa katika elimu na kuelimisha umma na wote wanaohusika katika utengenezaji wa sera kuwa demokrasia na elimu bora ni mambo ya msingi kabisa katika kazi ya kuondoa umasikini, kuleta usawa wa kijinsia na utawala bora.
Programu hii ina vipengele vikuu vitatu, kipengele cha kwanza kinahusika na ujenzi na uimarishaji wa uwezo wa HakiElimu katika kufanya utafiti na uchambuzi madhubuti, ikiwa ni pamoja na kuwa na maktaba inayojitosheleza yenye nyaraka zote muhimu. Matokeo ya tafiti mbalimbali na uchambuzi huo wa sera yanawasilishwa katika taarifa ya kila mwaka itakayoitwa- Hali ya Elimu Tanzania- na katika nyaraka maalumu kuelezea msimamo wa kisera.
Kipengele cha pili ni kile cha kuwezesha ushiriki wa wahusika wengi kwa kadiri iwezekanavyo katika utayarishaji wa sera za kitaifa na ufuatiliaji wa utekelezaji wake. Hii ni pamoja na kuwezesha uwasilishwaji wa mawazo na maoni ya wananchi kutoka katika ngazi ya chini kabisa na umma kwa ujumla katika michakato muhimu ya kufanya maamuzi ya kisera, na katika kuuliza maswali muhimu kuhusu mambo ambayo kwa sasa hayashughulikiwi kikamilifu.
Kipengele cha tatu kinahusu uundwaji wa programu shirikishi na za kibunifu za utetezi na ushawishi kwa lengo la kuhimiza mabadiliko ya kijamii katika elimu. Programu hii inalenga katika kujenga ushirikiano maalumu wa kimkakati na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali, taasisi za utafiti, wanaharakati wa masuala ya kijamii, vyama vya wafanyakazi, viongozi wa serikali na jamii wenye uchungu na hali ya elimu nchini, vyombo vya habari na wadau wengine. HakiElimu inaanzisha ushirikiano na kampeni mbalimbali za kitaifa na kimataifa, mathalan, kampeni ya kuzingatia masuala ya jinsia katika utayarishaji bajeti, Elimu kwa Wote na Jubilee 2000 yenye lengo la kuzishawishi nchi tajiri kuzifutia madeni yote nchi masikini. Msisitizo unawekwa katika kuwapa taarifa wabunge na viongozi wengine wa kuchaguliwa. Aidha, utaratibu unawekwa wa jinsi ya kushughulikia haraka na kwa ufanisi masuala na fursa mbalimbali zitakazojitokeza.
Kwa pamoja vipengele hivi vitatu vinaiwezesha HakiElimu kuwa 'kurunzi' makini katika sekta ya elimu. Jukumu hili la kufuatilia kama mambo yanakwenda sawa na kubainisha pale penye matatizo ni muhimu sana katika uendeshaji jamii kidemokrasia, hususan, katika zama hizi ambapo masuala mbalimbali ya kijamii yanashughulikiwa kisekta, kama ilivyo kwa Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu ambao fedha za wafadhili kusaidia sekta hiyo zinatolewa moja kwa moja kwa serikali.
Uhusiano unajengwa kati ya programu tatu za HakiElimu - Utawala wa Jamii/Umma, Ushiriki Umma na Uchambuzi wa Sera na Utetezi ili kuwezesha wahusika wote kujifunza kutoka kwa kila mmoja na kujiimarisha kimkakati katika ngazi zote. Vipengele vikuu vya mkakati na uhusiano baina yao vinaelezwa kwa kifupi katika kielelezo kifuatacho.