- Source #1
- View Source #1
Kumekuwepo na picha kadhaa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii, hususan Facebook, zikionyesha hali ya viwanja vya michezo vilivyotumika katika mashindano ya AFCON nchini Gabon mwaka 2017 vikiwa katika hali mbaya ya uharibifu na kutelekezwa. Katika baadhi ya picha zinazoonekana kwenye picha hizo, miti imeota ndani ya viwanja hivyo, jambo linaloashiria kuwa havitumiki kwa muda mrefu na havifanyiwi matengenezo ya mara kwa mara.
je taarifa hizo zina usahihi kiasi gani ?
je taarifa hizo zina usahihi kiasi gani ?
- Tunachokijua
- Mwaka 2017 Gabon ilikuwa mwenyeji wa Kombe la Mataifa ya Afrika 2017 (AFCON), yaliyofanyika kuanzia tarehe 14 Januari hadi 5 Februari 2017. Gabon ilichaguliwa kuwa mwenyeji mbadala na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) mwezi Aprili 2015 baada ya mwenyeji wa awali, Libya, kujiondoa kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Karibuni baadhi ya kurasa mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii zimekuwa zikichapisha picha zinazoonesha hali ya uwanja wa mpira wa miguu unaoonekana kutelekezwa na kutokuonekana kufanyika kwa shughuli yoyote katika uwanja huo ambapo unadaiwa kuwa ni miongoni mwa viwanja vilivyotumika katika michuano ya AFCON 2017. Wafuasi wa soka wameonesha kusikitishwa kutokana na hali inayooneshwa katika picha huku lawama zikitupwa kwa mamlaka za soka nchini humo.
Je, ni upi uhalisia wa uwanja huo?
Inaelezwa uwanja huo unaojulikana kama "stade omar bongo" wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 40,000 uliojengwa mwaka 1976 ulipangwa kufanyiwa ukarabati kwa ajili ya michuano ya AFCON ya mwaka 2012 iliyofanyika katika nchi za Gabon na Equatorial Guinea hata hivyo, haukukamilika kabla ya mashindano hayo kumalizika.
Vilevile tovuti ya "Africa Top Sports" inabainisha kuwa kazi za ukarabati zilianza mwaka 2010 lakini hazikukamilika hata kabla ya AFCON ya 2017, ambayo pia iliandaliwa na Gabon. Tangu wakati huo, uwanja huo umeachwa bila kukamilika, kwa sehemu kutokana na kuondoka kwa kampuni ya Uhispania iliyokuwa ikisimamia na kutekeleza kazi za ukarabati
Aliekuwa waziri wa michezo wa Gabon Franck Nguema, aliwahi kunukuliwa na Africa Top Sports akisema “Mradi wa ukarabati wa Omar Bongo Omnisports Stadium, ambao ulianza wakati wa maandalizi ya ushirikiano wa kuandaa Africa Cup of Nations 2012, ni mradi ambao lazima ukamilishwe kwa vyovyote vile,”
Aidha kupitia Google Earth, inaonesha mandhari ya uwanja huo kwa picha zilizopigwa mwaka 2024.
Je, uwanja huo ulitumika kwenye meche za AFCON 2017?
Ufuatiliaji wa JamiiCheck umejiridhisha kuwa uwanja huo haukuwa miongoni mwa viwanja vilivyoorodheshwa na shiriki la soka barani Afrika kutumika katika michuano hiyo. Kwa mujibu wa CAF Oktoba 19, 2016 ilibainisha viwanja vinne vilivyokuwa tayari kutumika kwa mashindano hayo ambavyo ni
"Stade de l’Amitié, Stade de Franceville, Port Gentil Stadium, na Oyem Stadium"
Stade Omar Bongo uliopo jijini Libreville haukuandaa mechi zozote wakati wa michuano ya 2017 kutokana na ukarabati kutokukamilika kwa wakati, ingawa uwanja huo ulikuwa umepangwa kuwa moja ya viwanja vya mashindano hayo.
Kupitia taarifa iliyochapishwa Julai 22, 2016, kuelekea AFCON 2017, aliyekuwa Katibu Mkuu wa CAF, Hicham El Amrani, aliiambia BBC Sport kuhusu utayari wa mji wa Libreville kutumia viwanja viwili wakati wa fainali za mashindano hayo, ambapo aliutaja uwanja wa Stade Omnisports Omar Bongo, ambao awali ulipangwa kuandaa mechi ya fainali lakini ukakosa nafasi hiyo kutokana na kuchelewa kwa ukarabati.
Hata hivyo, uwanja huo unaobeba jina la rais wa zamani Omar Bongo, aliyelitawala taifa la Gabon kuanzia mwaka 1967 hadi 2009, unaweza kuwa mwenyeji wa mechi ya fainali takribani miaka mitano baadaye.
“Huenda Stade Omnisports Omar Bongo, ambayo ina uwezo mkubwa zaidi wa kuchukua watazamaji, ikatumika kwa mechi ya ufunguzi na fainali, lakini hayo bado ni majadiliano tunayoendelea nayo hakuna kitu kilichoamuliwa rasmi bado,” alisema El Amrani.