MKJJ na Mkuu Field Marshall mnawachanganya hata hawa. watanzania wa bongo..
Maziko ya Balali utata
2008-05-22 12:47:07
Na Simon Mhina na Restuta James
Wakati taarifa za kifo cha aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Dk. Daudi Ballali, zimethibitishwa na serikali kupitia BoT, mazishi ya kiongozi huyo yamebaki kuwa na utata juu ya mahali atakapozikiwa.
Habari kutoka kwa wanafamilia zinaonyesha kuwa wamegawanyika kuhusu mahala pa kumzika, Marekani ama hapa Tanzania huku akisubiriwa mkewe atoe umauzi wa mwisho.
Wakati hayo yakitokea, Ubalozi wa Marekani umesisitiza kuwa licha ya kifo cha kiongozi huyo, wanachosubiri ni kuona ripoti ya uchunguzi wa BoT ikianisha matokeo ya kashfa iliyopoteza zaidi ya Sh. bilioni 133 zilizo kwenye akaunti ya madeni ya nje (EPA), kupitia nyaraka za kughushi na vielelezo feki.
Hali ya utata wa maziko ya Dk. Balali, ulianzia jana kwa Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu, Bw. Salva Rweyemamu, ambaye aliwaeleza waandishi wa habari kwamba hakuna utata kuwa Bw. Balali amefariki dunia.
Hata hivyo, Mkurugenzi huyo alisema mtu ambaye angeweza kutoa taarifa juu ya suala hilo ni serikali kupitia Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) Bw. Kassim Mpenda.
``Suala hili sio la Ikulu ni la serikali, tafadhali ngoja niwaitie Mzee Mpenda aweze kuwajibu maswali yenu,``alisema Bw. Rweyemamu.
Baada ya muda mrefu, Bw. Mpenda alikuja na kuwaeleza waandishi kwamba habari alizonazo ni kuwa kweli msiba huo umetokea.
Hata hivyo, alisema wamekubaliana kwamba BoT ndiyo itatoa taarifa kamili juu ya msiba huo.
``Tumekubaliana kuwa mzungumzaji katika jambo hili ni Benki Kuu,`` alisema.
Alipoulizwa kuwa ni vipi BoT wawe wasemaji wa kifo cha Balali, wakati alishafukuzwa kazi kwenye taasisi hiyo ya fedha, Bw. Mpenda alisema hiyo haiwezi kuwa sababu ya kuzuia chombo hicho kutoa taarifa zake kwa vile ni makubaliano yaliyoafikiwa na serikali.
Kundi la waandishi lilipofika BoT saa 7:00 mchana maofisa wa benki hiyo walisema taarifa kamili zitatolewa saa 8:30 na Mkurugenzi wa Itifaki na kuwataka wanahabari kuondoka na warejee muda huo.
Muda ulipotimu waandishi wa vyombo mbalimbali walirejea, maofisa hao waliwataka wasubiri hadi saa 9:00 alasiri. Waliendelea kusubiri na kuelezwa kuwa vigogo wako kwenye kikao nyeti kinachohusiana na mambo ya bajeti.
Waandishi hao waliambiwa waendelee kusubiri kwa dakika 45 kwa maelezo kwamba mkutano hujaisha.
Hatimaye muda wa saa 10:15 jioni, Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa BoT Bw. Emmanuel Mwero, aliibuka na taarifa fupi ya maandishi ya tangazo la kifo cha Dk. Balali.
Hata hivyo, ofisa huyo kabla ya kugawa tangazo hilo, alitahadharisha kwamba hatojibu maswali yoyote ya waandishi kwa vile taarifa hiyo imetolewa na Gavana wa Benki Kuu, Profesa Beno Ndulu, yeye alitumwa tu kuigawa.
``Jamani sitasema lolote, kama kuna mtu mwenye swali anatakiwa kuwasiliana na Gavana, sikuja kuzungumza bali kuwapa hii taarifa kama nilivyoelekezwa na bosi wangu,`` alisema.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo fupi ya mistari nane yenye picha ya Dk. Balali akiwa ametabasamu, ilisema alifariki Ijumaa iliyopita jijini Boston nchini Marekani.
Bila kueleza sababu za kifo chake taarifa hiyo ilifafanua kwamba BoT ilipata taarifa za kifo cha Gavana wake wa zamani juzi usiku.
Taarifa hiyo haikuonyesha imetolewa na nani wala maradhi yaliyokuwa yanamsumbua licha ya kusema wana-BoT wamestushwa na kifo hicho.
``Ofisi ya Gavana ilipata taarifa za kusikitisha jana usiku (juzi) kuwa Gavana wa zamani, Dk. Balali, amefariki dunia Ijumaa nchini Marekani,`` ilisema taarifa hiyo na kuongeza: ``BoT tunaungana na familia ya marehemu na kuomboleza msiba huo na kumuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi, amina.``
Kwa mujibu wa taarifa hiyo marehemu Balali alijiunga na BoT Julai 14, 1998 hadi Januari 8, 2008 alipotimuliwa kazi na Rais Jakaya Kikwete kwa tuhuma za ubadhirifu kupitia akaunti ya madeni ya nje ya EPA.
Katika kashfa hiyo, inadaiwa kuwa Sh. bilioni 133 zililipwa kinyemela kwa makampuni yasiyo na stahili yaliyotumia vielelezo feki na nyaraka za kughushi.
Wakati hayo yakiendelea, nyumbani kwa marehemu Masaki Dar es Salaam, palikuwa na ulinzi mkali ulioshirikisha askari kanzu.
Mmoja wa wanafamilia wa marehemu huyo, ambaye aliomba jina lake lisitajwe, alisema amelazimika kulia kutokana na mazingira ya kifo cha mzee wao kilivyotokea.
Alisema licha ya kuhuzunishwa na kifo hicho, lakini ametafakari milima na mabonde na majaribu makubwa ambayo Dk. Balali ameyapitia kabla mauti hayajamfika.
``Ngoja mzee akapumzike. Mzee amepata shida sana siku za hivi karibuni. Ugonjwa, majaribu fitina na kila aina ya kusemwa vimemkabili hali akiwa kitandani,`` alilalamika.
Alipoulizwa habari za maziko, alisema kwamba kumetokea utata mkubwa kwamba ni wapi Dk. Balali azikwe.
``Hata taarifa za kifo chake kuchelewa kutangazwa, zimetokana na mkanganyiko huo,`` alisema.
Alisema kuna watu wanasisitiza kwamba azikwe nchini Marekani na wengine arejeshwe.
Lakini akasisitiza kwamba mke wa marehemu, ndiye anatarajiwa kutoa uamuzi wa mwisho.
Alisema taarifa alizonazo ni kwamba upande wa serikali unataka Dk. Balali arejeshwe kwa vile inaona hatua yoyote ya kumzika nje, itachukuliwa kwamba kuna kitu kinafichwa.
Kwa upande mwingine, Ubalozi wa Marekani ambao marehemu Balali anadaiwa atazikwa nchini humo, umesema hauna taarifa zake mbali na kuzisoma katika vyombo vya habari.
Ofisa Uhusiano wa Ubalozi huo, Bw. Jeffery Salaiz, akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu alisema kinachongojewa ni taarifa ya uchunguzi kuhusu ufisadi ndani ya BoT licha ya Balali aliyehusihusishwa na kashfa hiyo kufariki dunia.
Alisema Ubalozi hauna taarifa kuhusu mtuhumiwa huyo marehemu kwa kuwa haukuwahi kuombwa na serikali kusaidia kupata taarifa zake au kufuatilia mwenendo wake huko Marekani.
``Sijui alikokuwa anaishi, sifahamu alikuwa amelazwa hospitali gani kwa vile hatujaombwa kusaidia kumtafuta Balali,`` alisema.
Kuhusu maelezo ya kuwa na uraia wa mataifa mawili ya Tanzania na Marekani na kama nchi hiyo ina taarifa za marehemu huyo kuwekeza vitega uchumi vikubwa nchini humo, Bw. Salaiz, alisema mengi yamesemwa kuhusu Balali lakini nchi hiyo ilimfutia haki ya kuwa raia wa Marekani mwanzoni mwa mwaka huu na asingependa kuzungumzia masuala ya uwekezaji.