Pengine unaweza kujiona upo salama kwa kudhani ngumi za mtaani ni kwa wapiga debe, bodaboda, au watu wa tabaka fulani tu. Ukweli ni kwamba, mtu yeyote anaweza kujikuta kwenye hali hii, tulichotofautiana ni viwango tu, Unaweza ukawa unajenga nyumba yako mmepishana kauli na fundi kiasi cha kutwangana, Makazini mnaweza kupishana kauli mkapigana, Jela ni kawaida sana kupigana lasivyo unakuwa target, Hata watu wazima huwa kuna kuoneana kuna muda itabidi ujitetee, n.k.
Ni bora zaidi kuzuia pambano pigana ikiwa hakuna mbadala
Ulimi ni moja ya kiungo makini sana katika kuepusha ugomvi, neno dogo kama samahani mkuu linaweza epusha mengi, jaribu kusuluhisha mzozo kidiplomasia au kwa kuondoka eneo hilo. Kupigana inapaswa kuwa chaguo la mwisho kabisa. Kupigana kunaweza kusababisha madhara makubwa kama vile majeraha makubwa, kuua mtu kwa bahati mbaya na visasi vya kikatili. Aidha, kunaweza kuwa na athari kubwa za kisheria kama kufungwa jela.
Kufikiri Kuna Sheria
Ni kosa kuingia kwenye mapambano ya mtaani ukidhani kuna sheria za kufuatwa. Hii sio boxing, hakuna mwamuzi, hakuna muda wa kupumzika, na mara nyingi, hakuna huruma. Kufikiri kwamba mpinzani wako atafuata kanuni ni kosa kubwa. Mapambano ya mtaani mara nyingi hayana heshima, na ni muhimu kuelewa kuwa usalama wako unapaswa kuwa kipaumbele.
Kutokukimbia Kisu au Silaha inapotolewa
Kuna mikoa kama Arusha ugomvi huambatana na visu hawawezi kuzichapa kavu, Unapoona kisu kwenye pambano, jambo bora zaidi unaloweza kufanya ni kukimbia, Kiburi cha kuendelea kupigana kwa hofu ya kuonekana muoga waweza poteza uhai wako. Mapambano dhidi ya mtu mwenye silaha ni hatari sana na mara nyingi huishia kwa madhara makubwa. Kisu hakihitaji nguvu nyingi ili kusababisha majeraha mabaya, na kukabiliana nacho kunaweza kuwa kosa la maisha.
Kutohifadhi Nguvu
Watu wengi hutumia nguvu zote kwa mpigo ndani ya zile sekunde 30 za mwanzo, matokeo yake huchoka haraka kwa kutumia nguvu nyingi mwanzoni mwa pambano, Hii ni advantage kubwa kwa mtu unaepigana nae alietunza nguvu atakudonoa sana ukiwa huna nguvu, Ni vema kutumia nguvu kwa sekunde 10 za mwanzo ukiona adui bado anastahimili ni muda wa kujitafakari kutunza nguvu zako.. Ni muhimu kugawa nguvu zako ili usiwe rahisi kushindwa.
Kujitamba na Kuongea Maneno mengi (Kupiga Bla Bla)
Ni pambano la kimwili sio kuchambana kwa mdomo, Usiongee sana kabla ya pambano, Anza kuongea ukiingia kwenye pambano na dalili zinaonesha unammudu, Kuchimba mkwara au kujigamba kuhusu kile utakachofanya huchochea hasira za mpinzani na kumpa nafasi ya kujipanga jinsi ya kukushushia kipigo. Kimya na umakini ni silaha bora za akili wakati wa mapambano ya mtaani.
Kujaribu Kuiga Mapigo ya Kwenye Filamu
Mapambano ya kwenye filamu ni ya kubuni na mara nyingi hayahusiani na hali halisi. Kujaribu kuruka au kufanya miondoko ya kushangaza kama unavyoona kwenye filamu kunaweza kukuweka kwenye hatari zaidi. Badala yake, elewa hali halisi na tumia mbinu za msingi.
Kufikiri Kuzuia / Kublock ngumi ni Rahisi Kama Kwenye Game
Katika hali halisi, kuzuia ngumi sio rahisi. Badala ya kujaribu kuzuia ngumi zote, ni bora zaidi kurudi nyuma au kuendelea kumshambulia mpinzani. Kuwaza kuwa unaweza kuzuia kila ngumi kama kwenye game ni kosa litakalo kugharimu.
Kutoshusha Kidevu Chini
Kidevu kilichoinuliwa huacha uso wazi na rahisi kushambuliwa kwa uppercuts na vifuti. Kuweka kidevu chini ni mbinu ya msingi ambayo inapunguza hatari ya kupata pigo kubwa kwenye uso. Hakikisha unalinda kichwa chako vizuri.
Kuacha baada ya Kumwangusha Mpinzani
Baada ya kumwangusha mpinzani, usidhani pambano limeisha na kugeuza mgongo kuondoka. Wengi wao huweza kusimama tena na kuendeleza shambulizi. Hakikisha unadhibiti hali na kuwa tayari iwapo atajaribu kushambulia tena. Usimpe nafasi ya kukushambulia unapogeuka.
Kumsukuma Mtu Baada ya Kusukumwa
Kusukuma hakutatatua chochote. Ikiwa umesukumwa, jibu kwa ngumi badala ya kurudisha msukumo. Hii inakupa nafasi ya kujilinda na kushinda pambano kabla mpinzani hajapata nguvu ya kushambulia tena.
Kupigana na Mtu Mwenye Mwili Mkubwa au Mrefu
Kupigana na mtu mwenye nguvu nyingi, mwili mkubwa, au mrefu ni hatari zaidi. Watu hawa mara nyingi wana faida ya kimwili inayoweza kukuangamiza kwa urahisi. Badala ya kupigana, tafuta njia ya kuzuia au kujiepusha kabisa.
Kutaka kuendelea Kulinda Heshima baada ya kushushiwa kipigo
Kutaka kuendelea kupigana kwa sababu ya kiburi au kujaribu kuokoa heshima mara nyingi hupelekea madhara makubwa. Ikiwa umeona hali ni mbaya umeshushiwa kipigo hevi ni bora zaidi kukubali kushindwa au kutoroka. Hakuna aibu katika kuokoa maisha yako.
Kurudia Mbinu Zisizozaa Matunda
Ikiwa mbinu fulani haifanyi kazi kwa mpinzani, kuendelea kujaribu hakuwezi kubadilisha matokeo. Badala yake, kuwa mbunifu na badilisha mkakati wako. Kurudia makosa yale yale kunaongeza tu nafasi ya kushindwa.