Tanzania Railways Corp
Govt Institution
- Mar 23, 2018
- 292
- 690
Wananchi wa Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma wajitokeza kushiriki zoezi la utwaaji wa ardhi ili kupisha ujenzi wa kambi ya mkandarasi Mradi wa Kimkakati wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha saba kutoka Uvinza hadi Malagarasi.
Zoezi hilo ambalo limesimamiwa na timu kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRC) limefanyika katika shule ya msingi ya Mumnyika iliyopo kata ya Luhita wilayani Kasulu ambapo jumla ya takribani hekari ishirini na tano (25) zimetwaliwa kwa wananchi hao.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kasulu Bi. Theresia Mtewele alisema zoezi hilo limefanyika kwa kufuata taratibu za kisheria na kwa ushirikiano kati ya viongozi wa serikali na wananchi wa maeneo husika na alieleza kuwa lengo la hatua hiyo ni kuhakikisha utekelezaji wa mradi unaendelea bila vikwazo huku haki na taratibu za ulipaji fidia zikizingatiwa ipasavyo.
“Muhimu wananchi wasiwe kikwazo katika utekelezaji wa mradi huu ili tuweze kufurahia matunda haya ambayo serikali imetuletea”alisema Bi. Theresia.
Kwa upande wake, Mthamini kutoka TRC Bw. Ahsante Shadrack alifafanua kuwa tathmini ya ardhi na mali zilizopo imefanyika kwa weledi ili kuhakikisha wananchi wanaopisha mradi wanapata haki zao stahiki kwa mujibu wa sheria na miongozo ya tathmini pia lisisitiza kuwa mchakato wa uthamini ulizingatia viwango vilivyowekwa na mamlaka husika.
Naye Mwenyekiti wa mtaa wananchi Mumnyika Mchungaji Raphael Chandaro alieleza kuwa wananchi wameonyesha ushirikiano katika kufanikisha zoezi hilo, na akibainisha kuwa mradi wa SGR ni wa kimkakati na utaleta manufaa makubwa ya kiuchumi na kijamii kwa wakazi wa Wilaya ya Kasulu na maeneo jirani hata hivyo, alitoa wito kwa jamii kuendelea kutoa ushirikiano na pia kuwa na subira wakati utekelezaji wa mradi ukiendelea.
Mradi wa SGR kipande cha saba Uvinza - Malagarasi unaendelea kama sehemu ya juhudi za serikali za kuboresha miundombinu ya usafiri wa reli nchini, kwa lengo la kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo na abiria pamoja na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika ukanda wa Magharibi.