KISA CHA MAJUHA WAWILI WANAWAKE
Hapo zamani za kale palikuwa na maskini katika mji mmoja. Maskini huyo alioa mke na akazaa naye mtoto mmoja wa kike. Alikuwa na ng’ombe mmoja jike na ndiyo ilikuwa rasilimali yake pekee. Na kazi yake ilikuwa ni kulima makonde uko nje ya mji.
Kila siku wakati wa kuingia mjini huchukua majani ya ukoka kama chakula cha ng’ombe wake. Bibi na mtoto hubaki nyumbani. Hata siku moja alipokuwa yule mtoto ametimia miaka saba umri wake, aliota ndoto usiku.
Na ndoto yake ilikuwa ameota kaolewa tena amezaa mtoto mwanamke mzuri sana. Asubuhi baba yake akaamka akaenda kondeni kwake. Yule mtoto alipoamka akaangua kilio akalia, "mama wee! Mama wee mtoto wangu yuko wapi?"
Hata mama mtu akasikia kilio akaenda chumbani akamwuliza, "je mwanangu walilia nini asubuhi yote hii?"
Mtoto akamjibu mama yake kuwa, "nimeota ndoto usiku mmenioza mume, kisha nikazaa mtoto mwanamke mzuri, sasa naamka simwoni, ndiyo maana nalia, umemchukua wewe mama." Akasema hivi na huku analia.
Mama mtoto aliposikia habari ya mtoto aliyezaliwa usiku na kumwona mwanaye analia, naye akaangua kilio akalia. Ikawa kelele moja kwa moja, hata majirani mtaani wakasikia vilio wakaja nao kusikiliza kuna nini? Mama mtu akawaelezea watu mambo yote ya ndoto, majirani wakacheka sana wakanena, "Haya mambo! Hatujapata kuona sisi watu kulia kwa sababu ya ndoto." Lakini wale wenyewe wamekazana kulia,
Jirani mmoja mzee alipoona hawa ni wapumbavu, na kelele zikazidi akataka kuwanyamazisha akaenda kumwambia yule mama, "bibi hapana maana kukaa kitako ukilia, kama mtoto aliyezaliwa usiku amekufa, iliyobaki ni kuweka matanga nakuondoa.
Lakini aliyekufa kwa kuwa ni mtoto mdogo fanyeni chakula tu mpate kuondoa msiba."
Yule mke wa maskini akasema, "hayo ni mashauri mazuri lakini nitafanyaje mume wangu hayupo, naye ndiye mwenye mashauri ya mapesa."
Yule jirani akamwambia, "huna hata kikuku ukachinja?"
Akajibu, "nyumbani hamna kitu ila ngombe wa bwana naye anampenda sana. Akaambiwa, "utafanyaje basi, nawe una sharti ya kuondoa msiba huu, usipoondoa itakua uchimvi utakufa wewe au mume wako."
Yule mwanamke aliposikia vile akafanyiza hofu, akaona afadhali amchinje huyu ng’ombe maana sina kitu kingine.Akaita watu akagiza wamchinje ng’ombe.
Watu wakachekelea sana wakajua leo ndio kufaidi. Wakamchukua ng’ombe wakamchinja, wakamchuna upesi upesi. Wakatwaa mguu wakaenda wakabadili kwa mchele, wakatwaa nyama nyingne wakabadili na vitakataka vingine vya kupikia, Mara upishi ukasimama ukapikwa wali hata ikipata saa saba chakula tayari
Akaitwa mwalimu kuja kusoma hitima. Watu wengi wakaja kula chakula ikawa tena kila aliiyesikia akaja na wote waliokuwa wakija wakapata chakula. Hata habari ikaenea mji mzima kwa maskini kuna hitima, na wakisifu chakula kwa wingi wakati huu wote mume yupo shamba analima hana habari za hitima nyumbani kwake, Kasikia kwa watu waliokuwa wakitoka mjini kwenda shamba lakini hakutia moyoni maana hali ya nyumbani kwake anaijua mwenyewe. Akakaa hata saa zake za desturi akang’oa ukoka wake, akashika safari taratiibu kwenda zake mjini.
Wakati huu kule nyumbani wale watu wamekwisha ondoka, maskini akafika nyumbani kwake mkewe akamlaki juu kwa juu, karibu bwana karibu. Yule maskini kimya akaongoza njia moja kwa moja mpaka zizini, akatua mzigo wake aingie ndani ya zizi ng’ombe hayumo!
Akashangaa, "ng’ombe wangu yuko wapi?"
Mara mkewe akaja akamwambia, "Mume wangu twende ndani nikakupe habari za mkasa ulionipata, na nikuelezee ng’ombe wako yupo wapi."
Yule maskini akasema, "siendi popote mpaka nimwone ng’ombe wangu kwanza, Mkewe akamwambia, Bwana twende ndani nikakueleze."
Lakini yule madjini akasisitiza, "nieleze hapa hapa." Yule mkewe tena akaona hana budi kumweleza mambo yaliyopita akamweleza yote. Maskini aliposikia kuwa ng’ombe wake amechinjwa kwa ajili ya ndoto, akaduwaa, asijue la kutenda, akaingia ndani akakaa kimya, mkewe akamletea chakula asiweze kula.
Hata usiku Yule maskini akamwambia mkewe, "tangu kuzaliwa sijapata kuona juha kama wewe. Ilikwendaje wewe kusikiliza maneno ya ndoto? Basi sasa nifanyizie mikate nataka nisafiri nataka niende mbali nitafute mtu mwingine aliye juha kama wewe. Nikimwona utakuwa mke wangu hivi hivi. La sikumwona nitakuacha."
Asubuhi mkewe akamtengenezea mikate akafunga akachukua na karatasi na bahasha na wino. Akaondoka akaenda zake msitu na nyika hata zikatimia siku saba akafika katika mji mmoja mkubwa. Na yeye kwa kuwa alikuwa na mashauri yake moyoni hakuingia mjini, akafika katika kibanda cha kizee mmoja mwanamke. Yule mwanamke hakukasirika akamkaribisha, akamfanyizia na chakula.
Yule mgeni akauliza sana habari za mjini, na habari za wakubwa wa mji, kizee mwanamke akamwambia, "mwanangu, je, una haja nao hata ukawauliza hivyo?"
Akanena, "naam, shughuli kubwa." Hata ilipofika usiku kizee akamwuliza, "je utakwenda mjini leo au utalala hapa leo?" Akanena, "Ningependa nilale hapa, asubuhi niingie mjini."
Yule kizee akamwambia, "karibu mwanangu, ipo nafasi tele hapa." Akapewa chumba cha pili katika kibanda chake. Yule mgeni akafurahi sana alipoingia chumbani kwake akafunga mlango wake akatoa karatasi zake, akakaa kitako akaandika barua zake, moja kwa Sultani, moja kwa binti Sultani moja kwa waziri, moja kwa mke wa waziri.
Akazifunga katika bahasha kila barua bahasha ya peke yake.
Asubuhi akamwuliza Yule kizee nyumba za watu hawa aliowaandikia barua ziko wapi?
Yule kizee akajibu, "Nyumba za watu hawa wote zipo pwani forodhani, ila nyumba ya Binti Sultani iko nje ya mji si mbali kwa kutoka hapa." Akauliza namna ilivyokaa, na alama zake akaambiwa zote, basi alipokwisha pata habari zote alizozitaka akaaga akasema, "kwa hapa mama sina budi kwenda mapema nikamuwahi kila mtu nyumbani kwake niwape barua zao."
Akaondoka akaenda akishika njia akaingia mjini akafika panapo ile nyumba ya binti Sultani. Akatazama huku na huko akaona tanuru ya chokaa na ile tanuru inaelekea penye dirisha la binti Sultani. Akachimba chini ya ile chokaa. Akangoja mpaka alipoona sasa ni sa tatu akajifukiza pale penye chokaa kwa kichwa chake, na huku anapiga kelele, "Eeh! Jamani nifaeni mwenzenu natoka, mbali mimi, shime jamaa." Mara akachungulia mtumishi dirishani akaona chokaa inatutumuka na kichwa cha mtu kinatokeza, akaenda akamwita bibi yake akamwambia tazama chini, "Kitu gani kile?"
Akachungulia chini akaona mtu anaotokeza penye chokaa na huku akipiga kelele. Mara binti sultani akamwita mtumishi mwana mume akamwambia, "Uledi nenda upesi ukamtazame mtu yule ana nini?"
Mara Uledi akaenda akamwuliza, "wewe ni shetani au binadamu?"
Yule mgeni akasema, "mimi ni mtu lakini natoka ahera nimetumwa kuja kuleta barua za watu hapa mjini. Je sasa mimi nipo wapi hapa?"
Uledi akamwambia, "hii nyumba inayokukabili ni nyumba ya binti Sultani." Yule mgeni akasema, "ooh! vema sana ninayo barua yake hapa."
Uledi akamshika mkono akatoka katika ile chokaa, akampeleka uani, akapewa maji akaoga, akapewa na chakula, na wakati wa kula akistaajabu. "Hivi ndiyo chakula cha ulimwenguni wa siku hizi?" Anafanya kasahau maana yake katoka ahera. Alipokiwsha wakampeleka kwa bibi, kufika tu yule mtu akamwamkia bibi, akatoa barua akampa, akamwambia, "barua yako hii yatoka ahera kwa mjomba wako, naye anakusalimu pamoja na bwana."
Binti sultani akafungua barua akasoma nayo imeandikwa hivi:
"Saalam mjomba, mimi huku ahera sijambo, na jamaa wote waliopo wazima ila mimi nina dhiki ya deni, nilikopa fedha za watu nami sina cha kuwalipa, basi tafadhali mpe huyu niliyemtuma rupia elfeeni aniletee nilipe deni za watu. Salaam Wakatabahu Mjomba wako."
Yule binti Sultani aliposoma ile barua alisikitika sana akaenda zake moja kwa moja mpaka chumbani akafungua bweta akatoa rupia elfeeni ndani ya mifuko miwili akaenda. Kwenye sanduku la nguo akatoa kanzu ya hudhurungi safi na kanzu melimeli iliyo safi, na kanzu ya doria iliyo safi. Akatoa na buraa Muskati moja, na kitambi cha debwani iliyo njema, na kofia nyeupe ya kazi nzuri.
Akatwaa na vitu vingine vidogo vidogo kama miski, na halundi akatafuta kileso kikubwa cha Hariri akafunga pamoja na vitu hivi vyote. Kisha akaandika barua kwa mjomba wake ahera akaandika hivi:
Salaam mjomba, waama baada ya salam barua yako imewasili. Nami nimefurahi kuniletea huyu mtu wa kunipasha habari ya kuwa wewe mzima, na vitu ulivyoagiza nimempa huyu mtu, nimempa rupia elfeeni, na nguo maana nasikia nguo adimu sana huko.
Salaam, mimi Binti Sultani.
Akampa bahasha Yule mtu wa ahera na barua hii. Akamwambia, "mchukulie mjomba mwambie bwana hukumkuta, ungepewa zaidi ya hivi." Binti Sultani akaendelea kusema, "je nikupe mtu akuchukulie mizigo?"
Yule maskini akanena, "itanilazimu kuchukua mwenyewe maana ahera haendi mtu ila aliyekufa. Basi kwa heri, bibi sina budi kwenda upesi maana jua linapanda na sisi watu wa ahera jua linaatuathiri."
Yule mgeni wa ahera alipotoka nje akaona haina haja ya kupeleka zile barua nyingine.
Akatazama huko na huko akaona mahali njia inapita kwenda vichakani akachagua njia hii, akashika njia kwenda zake. Njiani akapita akasema kimoyo moyo, "Ah! Kumbe majuha wapo wengi nikadhani ni mke wangu tu Kumbe hata katika watu wakubwa wamo majuha!"
Akashika njia akaendda zake upesi upesi, akaviisha vile vichaka akatokea katika mashamba. Alikua anakwenda hivi upesi kwa kuwa alishuku kuwa atafuatwa. Alipofika mle shambani akamkuta mzee mmoja analima, akamwambia, "eeh baba umepta habari za mjini leo?"
Yule baba akasema, "la! Sina habari, kumetokea nini?"
Yule mtu wa ahera akajibu, "imetoka amri kwa Sultani watafutwe vizee vya shamba wote wauawe iwe kafara ya nyumba moja ya Sultani inayojengwa, basi mimi kwa hisani yangu napenda uvae hii kanzu yangu, na mimi unipe nguo zako za kulimia unipe na jembe lako nilimie, na wewe panda juu ya mnazi huu utazame juu njia ya mjini utaona mtu anakuja."
Sasa turudi kwa binti Sultani baada ya kuondoka huyu mtu wa ahera mara bwana mume wa binti sultani akarudi nyumbani, akamkuta mkewe ana majonzi akamwuliza, "je bibi una nini?"
Yule bibi asiseme neno akatwaa ile barua akampa mumewe akaisoma. Alipokwisha soma akamwuliza mkewe jinsi yalivyokwenda mambo haya, mkewe akaleza yote jinsi alivyokuja mtu wa ahera akaleta barua hii, na yakuwa amempa mjomba wake wa ahera haja aliyotaka na zawadi nyingine.
Yule mume akakasirika sana akamwuliza mkewe, "wewe una wazimu! Sasa niambie huyu mtu kaenda njia gani?" Akaambiwa kapita ile njia ya vichakani, mara akaagizwa atandikwe farasi akavaa nguo zake, joho, kilemba na upanga mkononi. Akapanda farasi ili kumfuata huyu mwizi mkubwa lakini akamwambia mkewe, "fahamu mimi namfuata huyu mtu maneno yake yakinielea vema utakuwa mke wangu lakini ukiwa ni upuuzi wako na wazimu nitakuacha."
Akatoka akaenda zake kwa kasi. Basi alipokuwa anakuja mbio, Yule mjumbe wa ahera akasema, "je sikukwambia miye?" Mara yule mpanda farasi akafika pale akamkuta Yule hasimu wake analima. Akadhani huyu ni baba shamba tu, akamuuliza, "hukumwona mtu anapita hapa na bahasha?"
Akamjibu, "sikumwona bwana lakini tazama huko juu mnazini, kuna mtu: huyo ndiye aliyekuja kutoka huko mjini, alipofika hapa akapanda juu ya mnazi, nilipomwuliza akasema anaogopa basi sijui kama ndiye unayemtafuta."
Yule bwana akamwuliza yule mtu kama anajua kupanda mnazi, yule akasema, "la bwana sijui." Yule mwarabu akawa ameshikwa na uchungu, akawa anataka kumwua yule aliyekuwa juu ya mnazi, basi akavua nguo zake kanzu na joho na kilemba na jambia akampa yule mgeni wa ahera amshikie pamoja na farasi. Yeye akapanda juu ya mnazi. Alipokuwa akipanda akawa anasema, "utanitambua leo mwizi mkubwa wewe, leo kutoka yangu au yako."
Na yule aliyekuwa juu akaona kuwa maneno ya yule mgeni wa ahera kuwa ya kweli. Akadhani huyu anakuja kuniua kwa habari ya amri iliyotoka. Basi naye akamwambia, "haya njoo nami nikuoneshe kazi kama sikukupiga na mundu wangu, yule mwarabu akawa anapanda tu, wala hatazami chini.
Yule mjumbe wa ahera kule chini akaenda akatwaa bahasha yake akafunga juu ya farasi. Akatwaa na zile nguo za mwarabu akazifunga juu ya farasi akampanda, Huyooo! Akaenda zake. Yule mkulima aliye juu ya mnazi akamwambia mwarabu, "Ela! Ebu tazama chini yuko wapi farasi wako?"
Akatehemu, kwenda juu hawezi, kushuka chini hawezi. Kisha akaona hana hila ila kushuka apate hakika ya maneno yale. Akamwambia yule mzee, "shuka chini tupate kuulizana vema. Yule mzee akakataa kushuka mpaka mwarabu alipomwapia kuwa hatamuua. Basi wakadhuka wote. Walipofika chini mwarabu akamwambia, "nipe habari ya yule habithi." Mkulima akampa habari yote tangu mwanzo, alivyokuja na aliyosema, na kumtisha kwa amri ya mfalme iliyoko mjini. Hata ikajiri kubadilishana nguo na yeye kupanda juu ya mnazi, hata kutokea yeye mwarabu.
Yule mwarabu aliposikia kisa hiki, badala ya kukasirika akacheka sana. Na yule mkulima naye akanwambia mwaarabu, "Ela na mimi nieleze ilivyokwenda huko mjini." Mwarabu akamweleza habari zote za barua ya ahera, na vitu alivyopewa. Wote wawili wakakauka kwa vicheko.
Yule mkulima akamuuliza mwarabu, "sasa ukienda nyumbani, Utakwenda kusemaje?"
Yule mwarabu akasema, "Sina la kusema ila nitakwenda kumwambia bibi kuwa nimemkuta yule mtu, nami niliposika habari za ahera moyo wangu ukaingia huzuni sana, hata sikuweza kustahimili nikampa farasi wangu na nguo zangu zote awachukulie watu wa ahera. Je! waonaje kizee?"
Kizee akasema, "Kwell maneno yako. Mana ukisema kuwa umenyang'anywa utachekwa sana. Mwarabu akarudi mjini na kikoi chake na Jambia lake mkononi. Kisha akafika kwa mkewe.
Mkewe akamuuliza, "jinsi gani bwana nguo zako na farasi viko wapi?"
Akamwambia, "kweli maneno yako bibi. Habari za ahera nilizosikia kwa yule mjumbe wa ahera zimenitia huzuni sana, hata nimempa farasi na vitu vyangu vyote kuongezea vile uilivyompa wewe."
"Bai sasa Bibi na tukae. Lakini pamoja na hayo akija mtu mwingine kutoka ahera usimpe kitu mpaka unishauri."
Sasa tumrejee yule mjumbe wa ahera. Baada ya kupata farasi akamwendesha kasi, akaenda mwendo Wa siku chache kuliko alivyokuja maana sasa kapanda farasi. Akafika hata kwa mkewe, amechoka kwa kwenda mbio. Akamfungua farasi mzigo wake akaimweka katika lile zizi la ng’ombe wake. Na mzigo akauweka ndani.
Alipokwisha pumzika na kula chakula akamweleza mkewe mambo yote ya safari yake. Akamwonyesha na fedha. Akanena Sasa na tukae kitako mke wangu nimekwisha muona aliye juha kuliko wewe. Lakini Pamoja na hayo ukitokea tena Upuzi wa ndoto wajibu uningoje unieleze tufanye shauri pamoja. Wakakaa raha mustarehe.