KISA CHA MTU NA WANAWE
Palikuwa na mtu mmoja akaoa mke, akazaa watoto watatu wanaume. Na yule mtu hakuwa na kitu, rasilimali yake ilikuwa reale thelatha mia nazo kaziweka chini ya maliwato. Akakaa hata akapatwa na ugonjwa wake akafikiri kuwa mimi nina watoto watatu na mke hawa ndio warithi wangu na fedha hii haiwatoshi hawa. Afadhali niwarithishe kwa akili, kila, mtu asijue kuwa nimemrithisha mwenzake. Akamwita mke akamwambia, "Bibi, mimi siwezi, uhai wangu haba kuliko mauti na akiba yangu ni reale thelatha mia, na warithi ni wewe na wanao. Lakini nataka watoto wasirithi, sharti kwanza wakamrithi Sultani wa Mrisi (Mauritius), wakirudi huko ndipo warithi fedha."
Akakaa, hata hatimaye akamwita mwanawe mkubwa, akamwambia, "Mwanangu, mimi siwezi, naona uhai ni haba, na mauti mengi, lakini nikifa, mimi rasilimali yangu ni reale thelatha mia tu, nazo ziko chini ya maliwato, huo ndio urithi wako, wala usiwaambie nduguzo. Lakini nakutafadhalisha neno moja, usirithi kwanza mpaka uende ukarithi mali ya Sultani wa Mrisi."
Akakaa, akamwita mwanawe wa pili, akamwambia maneno kama yale aliyomwambia mwanawe mkubwa. Kisha akamwita mwanawe wa tatu, akamwambia maneno kama yale aliyowaambia wengine kwa siri.
Basi tena akawaacha kila mmoja anajishuku kuwa mimi napendwa kuliko wengine. Hatimaye baba yao akafa, wakamzika, wakakaa matanga wakaisha. Walipokwisha, yule mkubwa akaondoka usiku akaenda hata chini ya maliwato akafukua akaziona kama aliyosema baba yake, akazichukua. Na yule wa pili akaenda kufukua asizione, akaudhika sana, akasema, Kumbe baba kanihadaa Akarejea nyumbani. Na yule wa tatu vile vile akaenda akafukua asione kitu, akaudhika sana, akasema, Kumbe mze kanihadaa ila kwa hakika fedha ilikuwapo sijui aliyekwiba. Akarejea nyumbani akalala.
Hata asubuhi akawaambia wenziwe, "hamna habari? Baba aliniambia ya kuwa penye maliwato pana fedha reale thelatha mia. Nami nimekwenda tazama, sikuona kitu."
Na yule wa pili akasema vile vile, na mkubwa naye akasema vivyo hivyo. Yule mdogo akanena, "Lakini baba alisema tena fedha hii isirithiwe mpaka tukamrithi Sultani wa Mrisi. Basi aliyechukua yote ni batali, maana hakushika usia."
Basi wakapatana wote kutoka kwenda kumrithi Sultani wa Mrisi.Wakatengeneza mikate yao, na bisi, na vibuyu vya maji, walipokuwa tayari wakaondoka, mkubwa mbele, wa pili kati, mdogo nyuma.
Na vijana hawa walikuwa wamesoma vema sana wote watatu. Basi walipokuwa katika kwenda yule mkubwa akaona unyayo wa mnyama. Akasema, "Unyayo wa mnyama huu, na mnyama mwenyewe ngamia."
Wapili akasema, "Na ngamia huyu katwikwa pau za chuma." Wa tatu akasema, "Na ngamia mwenyewe amepita zamani yapata saa nzima."
Wakaenda hata mbele wakakutana na mtu, akawauliza,
"Je! wakina bwana, hamkunionea mnyama wangu?" Mkubwa akajibu, "mnyama gani?Ngamia, nini?"
Mtu akajibu, "Naam, ngamia."
Wa Pill akasema, "Na ngamia mwenyewe ametwikwa pau za chuma?"
Akaambiwa, "Ndiye hasa."
Wa tatu akasema, "Na ngamia huyo kapita zamani, yapata saa nzima?"
Yule mtu Akajbu, "Naam, ndiye."
Wakasema, Tumemwona hukoo.
Wakashika njia wakaenda zao.
Hata mbele chini ya mti wakaona alama. Mkubwa akasema, "Kitako hiki, nacho cha mtu."
Wa Pili akanena, "Na mtu huyu mwanamke."
Wa tatu akanena, "Naye ana mtoto mgongoni."
Walipofika mbele wakakutana na mtu.
Akawauliza, "Je, wakina bwana, huko mnakotoka hamkunionea mtu wangu?"
Mkubwa’ akajibu, "Mtu mke, nini?"
Akaambiwa, "Naam.
Wa pili akasema, "Ana kekee ya dhahabu?"
Akaambiwa, Eh! bwana mdogo."
Wa tatu akanena, "Ana mtoto mgongoni?"
Akajibu, "Hasa."
Wakanena, Huyoo! tumemwacha huko.Wakaenda zao.
Hata mbele wakamkuta mtu amechinjwa, hana kichwa, kimebaki kiwiliwili tu.
Mkubwa akasema, "Mtu huyu kachinjwa, naye mwanamume."
Wa pili akasema, "Naye ana sharafa ya ndevu."
Wa tatu akasema, "Mtu mwenyewe kizee, umri wake yapata miaka sabini au themanini."
Wakaenda hata mbele wakakutana na mtu, naye ni mwanawe yule aliyechinjwa. Akawaambia, "Je! Wakina bwana hamkunionea mtu wangu huko mtokako?"
Mkubwa akasema, "Mtu mume, nini?"
Akaambiwa, "Naam."
Wa pili akasema, "Naye ana sharafa njema ya ndevu?" Akajibu, "Naam, ndiye."
Wa tatu akasema, "Naye mzee sana, bwana, apata umri wake miaka sabini, themanini hivi?"
Akanena, "Naam, ndiye hasa."
Wakanena, "Huyoo, anakwenda huko.
Kumbe yule mtu kwenda mbele amkuta mzee wake amechinjwa
Akanena, "kumbe! wale wamemwua mzee wangu."
Na wale vijana watatu wakashika njia mpaka wakafika kwa Sultani wa Mrisi. Sultani akawakaribisha vizuri, akawapokea kwa mikono miwili Akawapa nyumba wakakaa. Hata kwa Siku ya tatu Sultani akataka kuwakirimu wageni wake. Akatuma mtu kwenda shamba kwa msimamizi kuchukua mpunga, na mbuzi aliye nona.
Ukaja mpunga ukatwangwa, na mbuzi akachinjwa. Ukapikwa wali mwema. Wakaenda wakaitwa wageni kwa Sultani. Wakapewa maji wanawe ili wale chakula.
Mkubwa akasema, "Wali huu unawalakini."
Wa Pili akasema, "Hata kitoweo kina Walakini."
Wa tatu akasema, "Hata Sultani mwenyewe naye ana Walakini."
Watwana waliosikia maneno haya wakaudhika, wakaenda wakamwambia bwana wao maneno haya, na ya kuwa hawakula chakula. Sultani akaudhika sana, akaona, vijana hawa hawana adabu. Juu ya kuwakirimu namna hii, bado wananitukana.
Akanena, "Kawaiteni hawa vijana."
Wakaitwa wakaja, akawaambia, "Namna gani hii mliyofanyiza ninyi? Mimi nimewakirimuni na ninyi mwanitukana?"
Wale vijana wakajibu, "Tumekutukanaje, Sultani?" kabla Sultani hajawajibu mara yakaja mashtaka ya yule mtu mwenye ngamia njiani waliyekutana naye njiani. Akashtaki kwa Sultani ya kuwa watu hawa wamekwiba ngamia wangu. Na Sultani akawaambia, "Kwa nini ninyi mmekwiba ngamia wa huyu?"
Wale vijana wakanena, "Tumemwibaje, Sultani?
Ametuona naye?"
Mwenye ngamia akasema, "kwa sababu waliniambia alama zake zote. Basi wamezijuaje hao kama hawakumwona?"
Sultani akasema, "mmesikia basi jibuni sasa, mmezijuaje alama za ngamia, nanyi hamkumwona?" wakajibu hivi:
mkubwa, "Mimi nilimjua huyu ni ngamia kwa nyayo zake ,nyayo za ngamia hupotea?"
Wa pili akasema, "Mimi nalijua kuwa amechukua pau za chuma kwa kuwa nyayo zake zilikwenda chini sana. Nikajua huyu kachukua kitu kizito, na hapana kizito kama pau ya chuma."
Wa tatu akasema, "Mimi nalimjua kuwa alipita zamani, kwa kuwa nyayo zake zilikanyagwa, saa nzima, kwa kuwa nyayo zake zilikanyagwa na watu waliokuja nyuma na watu wenyewe tuliwaona njiani, huko nyuma kabisa lakini ngamia hatukumwona."
Sultani akanena, "Hakika hawa hawakuiba ngamia wako nenda zako."
Akaja yule mwenye mke naye akashtaki, akasema, "Bwana, hawa wamenichukulia mke wangu."
Sultani akanena, "Mnasikia ninyi, kwa nini kuchukua mke wa watu?"
Wale wakanena, "Hasha, bwana, sisi hatukumchukua mke wa mtu."
Mwenye mke akasema, "Mbona basi wameniambia alama zote za mke wangu, ikiwa hawakumwona?"
Mkubwa akasema, "Mimi naliuliza tu mtu mwenyewe mtu mke? Huko ni kuiba, bwana?"
Wa Pili ikasema, "Mimi nalijua kuwa huyu mwanamke, maana naliona kekee ya dhahabu kule alikokaa chini ya mti, lakini sikuigusa."
Wa tatu akasema, "Mimi nalijua kuwa ana mtoto mgongoni, maana asingeondoka hana kekee yake, ila alimpa mtoto wake uichezea, ikamponyoka, mama yake hana habari."
Sultani akanena, "Kweli maneno yao, hawakumwona hawa."
Akaja Kijana aliyechinjiwa baba yake, akanena, "Hawa wamemchinja baba yangu." Sultani akanena, "Jibuni ninyi, mmemuuaje baba yake huyu?"
Wale vijana wakanena, "Hatukumwua, bwana."
Yule kijana akanena, "imekuwaje basi kunipa wasifu wake wote?" Mkubwa akasema, "alikuja huyu bwana kututuliza akina bwana mmenionea mtu wangu? Mimi nikamwambia mtu gani, bwana?Mtu mume? Akanena, naam, huko kuuwa bwana?"
Wa pili akasema, "Mimi nalimjua kuwa ana sharafa ya ndevu kwakuona manyoya mengi kifuani, nikajua kuwa hakosi kuwa n sharafa ya ndevu, maana hii ni maujudi."
Wa tatu akasema, "Mimi nalimjua kuwa ni mzee wa miaka sabini au themanini kwa kuona damu yake. Ilikuwa haina nuru tena, ina maji nikajua kuwa hii ni damu ya mzee."
Sultan akasema, "Kweli maneno yao, hawakumwua hawa, nenda zako."
Sultani akashangaa kwa akili zao wale vijana, lakini bado hawajajitakaSa. Imebaki habari ya Sultani mwenyewe.
Sultani akawaambia, "Ehe! Sasa nawauliza mimi, Kwa nini mkafanya wali wangu kuwa na Walakini, na mnbuzi kuwa na Walakini, na mimi kuwa na Walakini?"
Mkubwa akasema, "Mimi nimejua kuwa wali una walakini, kwa kuwa mchele wake mrefu, mnene. Nikajua mpunga huu ulipandwa makaburini, maana ndipo penye rutuba sana. Basi chakula cha makaburini hakinaWalakini?"
Wapili akasema, "Nalijua kuwa nyama ina Walakini kwa kuwa nyama yake ilinona sana, nikajua kuwa mbuzi huyu malezi yake si ya mbuzi wengine."
Wa tatu akasema, "Mimi nimejua kuwa Sultani una Walakini, kwa sura."
Basi Sultani akakasirika sana. Akamwita nokoa, akamuuliza habari za mpunga. Akanena, "Naam, bwana, mpunga huu ulipandwa makaburini, wala si uongo."
"Na habari ya mbuzi je?"
Akasema, "Naam, mbuzi yule mama yake alikufa alipokuwa mdogo akanyonya maziwa ya punda!"
Sultani akaona kweli, mbuzi huyu kama punda. Kisha akamwita mama yake akamfunga panapo nguzo akampiga akamwambia, "Sharti uniambie kweli. Hawa wanasema mimi nina Walakini, namna gani? Wewe ndiye unayejua."
Mama yake akamwambia Kweli, "mwanangu, wewe ni mtoto wa mume wangu wa kwanza aliyekuwa Baniani, si mtoto wa marehemu Sultani."
Sultani akaona vijana hawa wana akili wala hawana mfano wao. Mahali pa kuwafunga akawapa zawadi nyingi, akawaruhusu kwenda zao. Lakini pamoja na hayo ndani ya moyo wake hakutaka kuwaacha wale watoto warudi kwao wazima kwa vile walivyomfedhehi kumtambua kuwa yeye si mtoto wa marehemu Sultani.
Alitaka kuwaua, ila hakutaka kuwaua kwa dhahiri. Basi wakati wa kuondoka akatwaa majoho mekundu akawavika wote watatu. Kisha akatwaa majoho meusi akawavika wanawe watatu, akawaambia, "Nendeni muwasindikize wageni." Akawaacha kwenda zao. Mara nyuma akatuma askari.
Akawaambia, "Nendeni zenu, wafuateni wale wageni, mkiwakuta, waueni vijana watatu wenye majoho mekundu."
Kumbe! wale vijana walipokwenda mbele wakatambua kuwa pana neno hapa. Wakawaambia watoto wa Sultani wa Mrisi, ya kuwa, "Baba yenu ameharibu. Majoho mekundu ni rangi ya kifalme si majoho ya kuvaa sisi. Majoho meusi ni ishara ya msiba, ndiyo yanayotuelekea sisi tuliofiwa na mzee wetu karibu. Basi yafaa tubadili."
Wakabadilisha yale majoho. Wale watoto Sultani wakavaa majoho mekundu. Na wale askari waliambiwa kuwa mkiwakuta wale vijana waueni wenye majoho mekundu.
Basi askari walipowakuta wakatimiza amri yao wakawauawenye majoho mekundu. Kumbe! ndio watoto wa Sultani. Na wale vijana watatu, wakawarudisha kwa Sultani. Sultani alipowaona wanakuja wamevaa majoho meusi, akajua kuwa werevu wao.
Akawapa tena malinyingi mno.
Wakatimiza maneno ya baba yao.Wakamrithi Sultani wa Mrisi kwanza, kabla hawajarithi mali ya baba yao. Kisha wakarudi kwenda kurithi mali ya baba yao.