KUSAJILIWA KWA TANU ABDUL NA ALLY SYKES WALIMSUBIRI NYERERE MTAA WA KIPATA
Mwalimu wangu aliyenifunza mbinu za kufanya mijadala marehemu Sheikh Haruna Fakir alikuwa heshi kutueleza, ''Haleti mtu matusi katika mjadala ila ameghadhibika na huku kughadhibika husababishwa na kushindwa akawa hana uwezo tena wa kushindana basi hapo nafsi huingia katika fadhaa na matokeo yake ndiyo hayo matusi.''
Wakati ujumbe wa umoja wa mataifa ulipofika Tanganyika, TANU ilikuwa bado haijasajiliwa na serikali.
TANU ilipata tasjila yake tarehe 30 Desemba, 1954 baada ya kuzishinda hila nyingi na vizingiti vilivyowekwa na serikali za kupinga usajili wake.
Bi Zainabu, mke wa Ally Sykes anakumbuka siku moja adhuhuri, jua lilikuwa kali, wakati Nyerere alipokwenda nyumbani kwao Mtaa wa Kipata (Siku hizi Mtaa wa Kleist) ambako Ally na kaka yake Abdulwahid walikuwa wakimsubiri atoke mjini alikokwenda kushughulikia tasjila ya TANU.
Alipofika Nyerere alionekana amechoka taabani na mwenye wasiwasi.
Alizama ndani ya sofa akaufunika uso wake kwa mikono yake na akakaa kimya kwa muda.
Abdulwahid na Ally walikuwa wakimsubiri azungumze.
Nyerere alikuwa na habari mbaya.
Serikali ilikuwa imekataa kuisajili TANU.
Nyerere aliwaambia kuwa serikali ilikataa kutoa usajili kwa sababu za kiufundi.
Serikali ilidai kuwa TANU haikuwa na wanachama.
Baada ya kufahamu kuwa serikali imekataa maombi ya TANU kwa kuwa ati haikuwa na wanachama wa kutosha, mithili ya onyesho la mchezo wa kuigiza unaokwenda haraka, Abdulwahid alitumia hekima na mara moja akamuomba Said Chamwenyewe aende nyumbani kwao Rufiji kusajili wanachama kwa ajili ya TANU.
Rufiji ni sehemu ya Waislam watupu.
Kwa ajili hii TANU haikuwa na tatizo la kuwapata wanachama.
Kwa hakika wanachama wa mwanzo wa TANU walikuwa kutoka Gerezani na Rufiji.
Illife ameandika kuwa:
"Mwelekeo wa kuungwa mkono kwa TANU mjini Dar es Salaam unahitaji uchunguzi, lakini mapato ya fedha kwa mwaka 1958 yanaonyesha sehemu iliyo kubwa ya kuungwa mkono chama ilikuwa kutoka makazi ya Waafrika - Kariakoo, Ilala, Gerezani... kufikia Septemba, 1955 Dar es Salaam ikiwa na watu kama 110,000 - ilichukua kiasi cha 25,000 kati ya 40,000 za kadi za uanachama wa TANU zilitolewa kote nchini.
Huu ulikuwa ndiyo msingi ambao TANU iliteka Tanganyika.''
Abdulwahid sasa akiwa na umri wa miaka 30, alikuwa amekamilisha lile lengo lake kubwa katika maisha yake, lengo ambalo lilianza kwa marehemu baba yake ambaye miaka ishirini na moja iliyopita alitabiri kuendelea kwa mapambano kati ya Waafrika wa Tanganyika na serikali ya kikoloni.
Kleist Sykes alikuwa halikadhalika ametabiri jukumu la kizazi kijacho.
Katika barua aliyomwandikia Mzee bin Sudi, Rais wa African Association, mwaka wa1933, Kleist katika umri mdogo wa miaka ishirini na tisa, akiwa kijana mdogo sana aliandika maneno haya:
"Tupambane kwa nguvu zetu zote kuelekea njia ya ustaarabu kama vile watu wa makabila mengine wanavyofanya.
Haidhuru kitu ikiwa hatukamilishi kila kitu.
Wale watakaokuja baada yetu watakamilisha yatakayobakia."
Kwa hakika Kleist alikuwa mtu wa fikra.
Alizungumzia kuhusu ''ustaarabu'' ambao hivi leo ungemaanisha ''kujitawala'' na kuhusu makabila ambayo TANU imeyageuza kuwa ''taifa.''
Katika mwaka wa 1954 robo karne baadaye katika jengo lilo hilo, 25 New Street ambalo Kleist alisaidia kulijenga kwa njia ya kujitolea, kizazi kipya nchini Tanganyika kilikuwa kikiigeuza African Association aliyoiunda katika mwaka 1929 kuwa chama cha siasa.
Lengo lake lilikuwa kuwatayarisha Watanganyika kujitawala.
Miongoni mwa waliokuwa wakiongoza harakati za kudai uhuru zilizokuwa zikiibuka walikuwa watoto wake watatu, Abdulwahid, Ally na Abbas."
Bahati mbaya sana nyumba yenyewe haipo hivi sasa badala yake wamejenga ghorofa hiyo hapo chini katika kiwanja kile ilipokuwapo nyumba hii.
Hii nyumba ndipo Ally Sykes alipoficha mashine ya aliyokuwa akichapa makaratasi ya uchochezi dhidi ya Waingereza na kuyasambaza nchi nzima.