KILIO CHA MIFEREJI YA DAMU IENDAYO ETHIOPIA
SEHEMU YA TISA
Kwenye sehemu iliyopita nilieleza namna ambavyo Kagame aliwaongoza RPF kufanya mashambulizi ya akili dhidi ya vikosi vya serikali ya Rais Habyarimana.
Pia nilieleza namna ambavyo baada ya mashambulizi hayo yenye mafanikio ya RPF kuliibuka tena upya kwa kasi kubwa mauaji dhidi ya Watusi walioko ndani ya Rwanda. Baadae Wahutu wenye mamlaka na ushawishi wakaanzisha kampeni ya kuhamamisha uuaji wa watusi, kampeni ambayo iliendeshwa kwa propaganda kwenye radio na machapisho ya majarida, magazeti na vipeperushi.
Tuendelee….
MAJADILIANO YA AMANI JIJINI ARUSHA
Licha ya serikali ya Rais Habyarimana kuratibu propaganda hizi dhidi ya watusi lakini jumuiya ya kimataifa hasa, nchi ya Ufaransa ambayo wana maslahi ya moja kwa moja kwenye nchi ya Rwanda, kwamba jamii ya kimataifa walihitaji amani irejee tena ndani ya Rwanda.
Baada ya presha hii kuwa kubwa sana ilimbidi Rais Habyarimana kutangaza kwamba anaruhusu kurejea tena kwa mfumo wa vyama vingi.
Ufaransa waliamini kwamba kama demokrasia ingeruhusiwa tena na watu kupata majukwaa ya kusemea kero na madukuduku yao na kuwania uongozi wa nchi, basi labda mapambano ya silaha yangekoma.
Ni katika kipindi hiki Rwanda ilishuhudia kuanza kuundwa tena kwa vyama bya siasa kama vile Republican Democratic Movement (MDR), Social Democratic Party (PSD) na Liberal Party (PL).
Licha ya hatua hii muhimu iliyopigwa na nchi ya Rwanda kuruhusu demokrasia lakini ubaya ni kwamba Rais Juvenile Habyariamana rohoni mwake bado alikiwa na nia ovu. Moyoni mwake alikiwa amejawa na woga wa kupoteza madaraka yake. Kwa hiyo alichokuwa anakifanya ni kuweka mkono wake kwenye uanzishwaji wa vyama vyote hivi vya kisiasa. Yaani kwa maneno mengine vyama hivi vya siasa vilikiwa ni geresha tu ili kuridhisha jumuiya ya kimataifa.
Hii inathibitishwa na hata misimamo ya vyama hivi ambavyo vyote vilikuwa vinapinga vikali RPF na Kagame. Au ushahidi mwingine ni kuanzishwa kwa chama cha Coalition for the Defense of the Republic (CDR) ambacho kilianzishwa katikati ya miaka ya 1991. Chama hiki kilikuwa na msimo mkali wa kihutu na kukandamiza watusi kuzidi hata chama tawala cha Habyarimana mwenyewe, MRND. Na pia chama hiki kilikuwa na mafungamano makubwa na 'akazu'.
Rais Habyarimana ili kuwafurahisha jamii ya kimataifa kwa viini macho vyake, mwezi October 1991 aliunda upya baraza lake la mawaziri. Lakini baraza hilo ajabu halikujumuisha wanasiasa kutoka chama kingine chochote zaidi ya chama chake cha MNRD.
Hata wale ambao walikuwa wanajitahidi kuunda vyama vya kweli vya upinzani ambavyo havifungamani na Rais Habyarimana na genge lake, walikuwa wanapotezwa haraka na wengine kutupwa gerezani huku Rais Habyarimana akijitetea kwa kisingizio kwamba watu hao ni mapandikizi ya RPF.
Baadae jumuiya ya kimataifa ikiongozwa na ufaransa ilimjia juu Rais Habyarimana kwamba aache kuwachezea akili na badala yake aruhusu demokrasia ya kweli na baraza lake la mawaziri liakisi makundi yote ndani ya nchi ya Rwanda.
Ndipo hapa mwezi April, 1992 ilimbidi Habyarimana kuunda tena upya baraza la Mawaziri na kujumuisha wanasiasa wengine kutoka upinzani japokuwa bado ilikuwa ni kwa uchache sana.
Viongozi hawa wa vyama vya upinzani ndio ambao walifanikisha kufanya mazungumzo na Kagame mwezi July mwaka huo huo 1992 na kukubaliana kusitisha kwa muda mapigano na vikosi vya serikali.
Arusha International Conference Center
Hapa ndio mwanzo wa mzungumzo ya amani Arusha, hapa Tanzania.
Tanzania tulibebeshwa zigo la kuongoza mazungumzo haya ya amani na jumuiya ya kimataifa kutokana na nchi yetu kuwa chimbuko la mambo mengi hapa Afika Mashariki na ukanda huu wa maziwa makuu. Hii pia ilitokana na turufu ya Tanzania kuwa nchi ya kimkakati kidiplomasia na kuwa ndiyo nchi pekee iliyo karibu na Rwanda ambayo walau tulikuwa tunaonekana tuko 'neutral' kwenye mzozo huo tofauti na nchi kama Uganda, Zaire na Burundi.
Mazungumzo haya ya kurejesha amani nchini Rwanda yaliyokuwa yanaendelea pale Arusha yalikuwa yanahusisha pande nne.
Upande wa Kwanza ulikuwa unaundwa na wahutu wenye msimamo mkali ambao walikuwa wanaongozwa na familia ya mke wa Rais Habyarimana, Bi. Agathe Habyarimana. Hawa waliwakilishwa na chama cha CDR (Coalition for the Defence of the Republic) pamoja na watu wenye msimamo mkali ndani ya chama tawala cha MRND.
Kundi hili japokuwa walikuwepo kwenye mazungumzo haya ya amani Arusha lakini walikuwa wanaupinga mchakato mzima. Walikuwa hawataki kuacha upenyo wowote wa RPF au watusi kumegewa madaraka ya nchi na walikuwa wanawaona watusi wote ndani ya Rwanda ni maadui zao na suluhisho bora zaidi labda wahamishwe wote kutoka Rwanda la sivyo 'watawahamisha' kwa lazima.
Hili lilikuwa ni kundi la kwanza.
Kundi la pili walikuwa ni vyama vya upinzani (ukiindoa CDR japokuwa navyo vilikuwa vinaendeshwa na wahutu). Hawa walikuwa na msimamo wa kati. Walikuwa wako tayari kwa mazungumzo na kumaliza mgogoro huo mezani. Lakini pia walikuwa hawana imani na RPF wakiwaona kama vile ni watu wanaojaribu kuharibu itikadi ya Mapinduzi ya mwaka 1959 ambayo yalianzisha utawala wa Kihutu ndani ya Rwanda.
Kundi la tatu lilikuwa ni RPF. Hapa naomba watu tufahamu kitu kimoja muhimu sana. Kagame alihudhuria mazungumzo haya ya amani kinyume kabisa na matakwa ya wenzake, washauri wake wakuu na makamanda wa ngazi za juu wa RPF. Washauri wake na makamanda wenzake na viongozi wote wa RPF walikuwa kinyume kabisa na mazungumzo hayo ya Arusha na walikuwa na sababu ya msingi kabisa. Hawakuona kundi lolote kwenye hayo mazungumzo ambalo walikuwa tayari kukubali watusi kujumuishwa kwenye uongozi wa nchi na kuishi kama raia halali ndani ya Rwanda. Kwa hiyo hawakuona sababu ya wao kushiriki mazungumzo hayo na waliyaona kama ni njia ya kuwarudisha nyuma kwenye harakati yao ya kuichukua Rwanda kijeshi.
Lakini Kagame aliona kiti cha tofauti kabisa… alikuwa anajua fika kabisa kwamba wenzake kwenye mazungumzo yale hakuna upande wowote ambao ulikuwa na nia njema na RPF na watusi. Lakini Kagame ikumbukwe kwamba alikuwa amefanikiwa sana kujenga taswira chanya ya RPF ulimwenguni (kumbuka ambavyo nilieleza nidhamu ambayo aliwawekea wanajeshi wake). Hakutaka kabisa kupoteza karata hii muhimu ya taswira chanya ya RPF kwenye jumuiya ya kimataifa. Kwa hiyo alishiriki mazungumzo hayo ili kuonyesha jumuiya ya kimataifa kwamba yeye na RPF yake wanataka suluhu ndani ya Rwanda na nia yao ni njema na safi kabisa, japokuwa uhalisia wa moyoni mwake na lengo lake kuu lilikuwa ni kuiweka Rwanda mikononi mwake.
Hili lilikuwa ni kundi la tatu.
Kundi la nne lilikuwa ni wa wawakilisbi wa Rais Habyarimana mwenyewe. Huyu yeye alitawaliwa na woga wa kupoteza madaraka. Kwa hiyo hadharani aliongea kama mtu ambaye yuko tayari kufanya suluhu na kushirikisha makundi mengine kwenye uongozi wa nchi lakini nyuma ya pazia alikuwa anafanya kila awezalo kukwamisha mazungumzo hayo.
Mazungumzo Arusha yalichanja mbuga huku kila upande ukiwa na nia yake moyoni.
Katika mzungumzo yale ndipo hasa rangi halisi za Rais Habyarimana zilionekana. Habyarimana alijidhihirisha kabisa kwamba lengo yake kuu lilikuwa ni madaraka haijalishi ni nini anatakiwa kufanya. Kama ni kuua watusi ili abaki madarakani basi ataua. Kama ni kusaliti wahutu wenzake ili abaki madarakani basi atafanya. Mazungumzo ya Arusha yalidhihirisha wazi kabisa kwamba Habyarimana hakuwa na nia yoyote moyoni 'kutetea' wahutu wenzake bali kitu pakee ambacho kilikuwa muhimi kwake ni madaraka.
Kutokana na mzungumzo kwenda kwenye muelekeo ambao ulikuwa unatoa picha kwamba suluhu inaweza kupatikana, wahutu wenye msimamo mkali wakiwakilishwa na chama cha CDR walijitoa kwenye mzungumzo hayo. Lakini hii haikuzuia mazungumzo kuendelea.
Mwezi August 1992 pande zote zilizopo pale Arusha walifikia makubaliano ya kuridhisha kabisa. Walikubaliana kwamba inapaswa iundwe serikali ya umoja wa kitaifa ambayo itajumuisha pande zote ndani ya Rwanda yaani chama tawala MRND, wapinzani na RPF.
CDR na wahutu wenye msimamo mkali ndani ya MRND walikataa vikali makubaliano hayo japokuwa tayari walikuwa wamejitoa kwenye mchakato wa majadiliano. Kuonyesha hasira zao wakaanza tena chokochoko za kuua watusi ili kuwakatisha tamaa RPF kwenye mzungumzo.
Katika usiku mmoja eneo la linaloitwa Kibuye, nyumba mia tano za watusi zilichomwa moto na watu 85 kuuwawa kwa kukatwa mapanga.
Kagame na RPF wakafumbia macho chokochoko hizi na kuendelea kuwepo kwenye majadiliano Arusha.
Mwanzoni mwa mwaka 1993 majadiliano yalifikia hatua nzuri zaidi na pande zote kutia saini mkataba maalumu wa makubaliano. Walikubaliana kwamba iwepo serikali ya umoja wa kitaifa ambayo itajumuisha pande zote isipokuwa chama cha CDR na wahutu wenye msimamo mkali. Serikali hii itakuwa ya mpito na kusimamia mchakato wa kuhakikisha kuwa kunafanyika uchaguzi huru na wa haki na ili kupata serikali ya kudumu.
CDR na wahutu wenye msimamo mkali pamoja na 'zero metwork' (akazu) waliona hili kama ni tusi kubwa sana kwao. Kwanza walijiona wao kuwa ndio wenye haki ya kutawala Rwanda alafu wameachwa nje ya mpango huo wa kuunda serikali ya Kitaifa. Pili waliona ni tusi kubwa kwao na dhidi ya Mapinduzi ya mwaka 1959 kuwajumuisha Watusi kwenye uongozi wa nchi.
Ilifikia hatua mpaka katibu mkuu wa chama tawala cha MRND Bw. Mathieu Ngirumpatse alitoa tamko kudai kwamba chama chake hakitambui makubaliano hayo na wala hawawezi kuyaheshimu. Tamko hili lilikuwa kinyume kabisa na Rais Habyarimana na wawakilishi wa MRND kwenye mazungumzo kule Arusha.
Ndipo hapa walifikia uamuzi kwamba adui yao wa kwanza ni Rais Juvenile Habyarimana. Wanapaswa kumshughulikia yeye kabla ya kuwashughulikia 'adui' yao mkuu wa siku zote, Watusi.
Rais Habyarimana pia alijua hila hizi ambazo zilikuwa zinapangwa na Wahutu wenzake dhidi yake. Akamua kuchukua hatua ya kufifisha ushawishi wa Akazu kwenye serikali yake. Akaanza kuwaondoa kwenye nafasi zote nyeti ambazo aliwaweka awali. Zoezi hili halikuwa si rahisi kwani alipata upinzani mkubwa kutoka kwa Wahutu wenzake hadi kufikia hatua ya kutishiwa kufanyiwa mapinduzi ya kijeshi. Kwa hiyo licha ya kuondoa akazu kwenye sekta na idara muhimu ilimlazimu kuwaacha baadhi.
Kati ya akazu ambao aliwaacha na alikuja kujutia baadae walikuwa ni Augistin Ndindiliyimana ambaye alikuwa ni Mkuu wa Jeshi la Polisi pamoja na Théoneste Bagosora ambaye alikuwa mnadhimu mkuu wa jeshi.
Kutokana na makubaliano ambayo Habyarimana aliyafanya na RPF na mkakati wake wa kuwaondoa akazu kwenye nafasi muhimu, ndipo hapa ambapo wahutu wenye msimamo mkali kwenye kila idara na taasisi waliyopo walianza kutengeneza 'idara' mahususi za pembeni zenye kujumuisha wahutu wenye msimamo mkali. Yaani kila idara au taasisi walikuwa wanaunda idara pacha pembeni yake ambayo wanachama wake ni wahutu wenye msimamo mkali tu. Yaani tuseme kwa mfano Idara ya Usalama wa Taifa, akazu wanaunda 'idara' ndogo ya pembeni ya wahutu wenye msimamo mkali pekee.
Na ni hapa na katika kipindi hiki ndipo ambapo wazo la 'mauaji ya kimbari' lilizaliwa. Kwamba wanapaswa kufanya kile ambacho jina lao linaakisi, 'Zero Network'.
Wanapaswa 'kuisafisha' Rwanda. Wanapaswa kuhakikisha hakuna mtusi anayetembea juu ya ardhi ya Rwanda. Wanapswa kufanya 'suluhisho' la kudumu juu ya tatizo lao hili la Watusi.
Sehemu ya 10 itaendelea leo jioni…
Habibu B. Anga alias 'The Bold'- 0718 096 811
To Infinity and Beyond
Follow, Subscribe and WhatsApp