Historia ya Omari Suleiman Nyumba Yake Ndiyo Akifikia na Kulala Julius Nyerere Wakati wa Kupigania Uhuru

Historia ya Omari Suleiman Nyumba Yake Ndiyo Akifikia na Kulala Julius Nyerere Wakati wa Kupigania Uhuru

Mohamed Said

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2008
Posts
21,967
Reaction score
32,074
HISTORIA YA FUNDI CHEREHANI OMARI SULEIMAN RAFIKI KIPENZI WA JULIUS NYERERE WAKATI WA KUPIGANIA UHURU WA TANGANYIKA

Mwaka 1955 wakati wimbi la utaifa wa Tanganyika lilipokuwa limepanda sana nchini Tanganyika Omari Suleiman alikuwa na umri wa miaka 43.

Omari Suleiman alikuwa fundi cherahani akifanya shughuli zake katika nyumba moja katikati ya mji wa Dodoma.

Mkabala na nyumba ambamo Omari Suleiman alikuwa amepanga chumba kimoja ilikuwa nyumba aliyopanga Taratibu.

Mara baada ya kupewa uhamisho kutoka Singida, Taratibu alimuuliza jirani yake, Omari Suleiman, kama kuliwepo na tawi la TANU pale mjini.

Omari Suleiman alimwambia Haruna Taratibu kuwa hapakuwepo na tawi la TANU mjini Dodoma na alimjulisha habari kuwa kulikuwa na tetesi mjini kuwa Hassan Suleiman amemuahidi na kumhakikishia DC kuwa yeye, akiwa katibu wa Jimbo wa TAA, hatairuhusu TANU kusajiliwa katika Jimbo la Kati bila ya idhini yake.

Lakini ukweli ulikuwa Hassan Taufik Suleiman alikuwa tayari ameisajili TANU lakini hakumfahamisha mtu yoyote wala kufanya juhudi yoyote kuitisha uchaguzi au kufanya mkutano.

Hassan Suleiman kama, Omari Suleiman alikuwa na umri wa miaka 43 mwaka 1955.

Tofauti na Omari Suleiman, Hassan Suleimani alikuwa ameelimika na alikuwa mwanasiasa mwenye uzoefu akiwa amekiongoza chama cha African Association.

Haruna Taratibu, Omari Suleimani na marafiki zake wachache waliunda kamati ndogo ili wapate ruhusa ya kufungua tawi la TANU.

Katibu mwenezi wa TANU, wakati ule Oscar Kambona, aliwaandikia kuwaeleza kuwa Hassan Suleiman tayari alikuwa ameshaisajili TANU na ikiwa uchaguzi wa viongozi haujafanyika basi waonanena na yeye pamoja na Ali Juma Ponda.

Omari Suleiman na Haruna Taratibu hawakuridhika na majibu kutoka makao makuu ya TANU kwa hiyo walikwenda kutafuta ushauri kwa Edward Mwangosi, aliyekuwa mwanachama mkongwe wa African Association.

Mwangosi aliishauri kamati ile iitishe mkutano Community Centre ili kujadili kufungua tawi la TANU, na Hassan Suleiman na Ali Juma Ponda waalikwe kuhudhuria.

Kadhalika Mwangosi aliishauri kamati ile kuwaalika walimu waliokuwa wakifundisha Kikuyu Secondary School, wengi wao wasomi kutoka Makerere kuhudhuria mkutano huo.

Mwangosi aliwaambia wajumbe wa kamati ile ndogo kuwa wasomi wa Makerere walikuwa ni muhimu sana kwenye chama kwa kuwa wangetoa uongozi uliokuwa unatakiwa.

Karibu ya watu 40 pamoja na wale wasomi wa Makerere, miongoni mwao Job Lusinde walihudhuria mkutano ule.

Lusinde alikuja kuwa waziri, na Amon Nsekela, alikuja kushika nyadhifa muhimu katika serikali na vilevile kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza.

Hassan Suleiman na Ali Ponda hawakutokea mkutanoni.

Wakati wanakusanyika kwa ajili ya mkutano, afisa wa Community Centre aliwaambia kuwa alikuwa amepokea amri kutoka kwa DC kuwa mkutano huo usifanyike.

Kufuatia amri ile watu walitawanyika mara moja.

Alexander Kanyamara aliyekuwa Mwafrika tajiri mjini Dodoma na rafiki wa John Rupia, wakati ule makamu wa rais wa TANU, aliwataka kuahirisha mkutano huo kwa sababu ya kutokuwepo kwa viongozi wa juu wa TAA, Hassan Suleiman na Ali Ponda.

Kutokana na sababu hii na vile vitisho vya DC, mkutano uliahirishwa bila kupanga tarehe ya mkutano mwingine.

Asubuhi iliyofuata Taratibu alikamatwa na polisi na kupelekwa kwenye ofisi ya DC, (hivi sasa ofisi hiyo ni ofisi ya Waziri Mkuu).

Taratibu alimkuta Hassan Suleiman pale ofisini akizungumza na DC, Bwana Smith.
DC alianza kumsaili Taratibu kwa kumuuliza kama alikuwa akijua kuzungumza Kiingereza.

Taratibu alijibu kuwa yeye hakusoma.

Akizungumza Kiingereza Hassan Suleiman alimwambia DC kuwa yeye ndiye katibu wa TANU mjini Dodoma.

DC, Bwana Smith, alimshutumu Taratibu kwa kuunda chama haramu na kwa kuitisha mkutano usio na idhini ya serikali katika Community Centre jana yake ambao ulielekea kuvuruga amani.

Bila woga Taratibu alijibu kwamba yeye alikuwa na mamlaka ya kuitisha mkutano kwa sababu alikuwa mwanachama wa chama cha siasa kilichosajiliwa kihalali.

Wasomi wa Makerere, ambao Mwangosi aliwaamini sana katika kuunda TANU, walipopata habari kuhusu mkasa wa Taratibu na DC, Bwana Smith, waliogopa.

Waliamua kujiweka mbali kabisa na mambo ya siasa na kuendelea na kazi yao ya kufundisha.

Haruna Taratibu na Omari Suleiman sasa waliamua kugeuza mbinu, waliitisha mkutano wa siri usiku nyumbani kwa Swedi bin Athumani.

Mkutano huu uliamua kuwa Taratibu lazima aende makao makuu ya TANU Dar es Salaam akazungumze na Nyerere ana kwa ana kuhusu matatizo yaliyokuwa yakiikabili TANU Dodoma.

Mahdi Mwinchumu aliyekuwa mwanachama wa TANU Dar es Salaam alijitolea kufuatana na Taratibu hadi makao makuu ya chama Dar es Salaam kwa kuwa alikuwa akijuana na viongozi wa TANU.

Said Mussa mjumbe mwingine wa ile kamati ya siri alijitolea vilevile kufuatana na Taratibu na Mwinchumu hadi Dar es Salaam.

Siku ya kuondoka Job Lusinde alikwenda stesheni ya gari moshi kuagana na ule ujumbe uliokuwa ukielekea Dar es Salaam, makao makuu ya TANU.

Lusinde aliuambia ule ujumbe kuwa jamaa wa Makerere wanaunga mkono maamuzi yote yatakayoamuliwa na ile kamati ya siri.

(Kutoka kitabu cha Abdul Sykes).

1735033100853.jpeg

1735033144940.jpeg

Nyumba ya Omari Suleiman, Dodoma
1735033266602.jpeg
 
Back
Top Bottom