Pascal,
Hili la ufadhili mkuu si rahisi kulieleza kwa uhakika na kusema kuwa fulani alimzidi mwenzake katika kuchangia.
Wafadhili wa TANU pale New New Street walikuwa John Rupia, Dossa Aziz Abdul na Ally Sykes na kila mtu alitoa kwa nafasi yake na kwa njia nyingi tofauti.
Kutajwa katika ufadhili kunategemea na kile kilichotolewa kwa wakati gani na kilikuwaje cha kuonekana au cha faragha.
Dossa Aziz alitoa gari nzima kuipa TANU kwa matumizi ya Mwalimu Nyerere.
Abdul Sykes nyumba yake ndiyo ilikuwa kama ofisi ya pili ya TANU kwa shughuli nyingi za chama na kwa ajili hii saa 24 watu wakiingia na wageni wakifikia kwake kutoka sehemu tofauti za Tanganyika kuanzia machifu hadi watu wa kawaida na wengine ilibidi wakae kwake.
Nyumbani kwa Abdul Sykes, Mzee Abdallah aliyekuwa mhudumu wa ofisi ya Abdul Kariakoo Market anasema kuna nyakati alikuwa anachinja hadi kuku 20 kwa siku kupeleka nyumbani kwa Abdul kwa ajili ya kitoweo.
Dossa Aziz yeye alikuwa akitoa matumizi ya siku kwa siku ya ofisi ya TANU na yeye na Mzee Rupia, Abdul na Ally ndiye pia wakilipa bili zote za chakula na vinywaji katika kila shughuli ya TANU kwa siku za mwanzo hadi walipokuja kusaidiwa na Baraza la Wazee wa TANU mfadhili mkubwa akiwa Mshume Kiyate.
Si rahisi kusema fulani yeye alitoa zaidi ya fulani kwa kuwa wafadhili wa TANU wote walisaidiana.
Iko siku In Shaa Allah nitaeleza kisa cha ''sanduku la fedha la Bwana Abdul'' kama nilivyoelezwa na mkewe mama yetu Bi. Mwamvua.
Historia ya TANU ina mengi sana.