Kwanini vizazi vya ukoo wa Yesu vinajipinga katika Mathayo na Luka.
Kwamfano tukisoma katika injili ya Mathayo, tunaona, mwandishi anaanza kueleza ukoo wa Yesu tangu Ibrahimu Mpaka Yusufu, lakini alipofika kwa Daudi, aliendelea na kusema Daudi akamzaa Sulemani, (Mathayo 1:6)..Lakini tukirudi tena kwenye Luka hapo hapo tunaona Daudi alimzaa Nadhani (Luka 3:31), Hiyo ni kuonyesha kuwa Yesu alipitia uzao wa Nathani na sio wa Sulemani, kulingana na Luka. Lakini Mathayo anasema alipitia kwenye uzao wa Sulemani, kwanini iwe hivyo?
Pia ukisoma tena mwishoni utaona kulingana na Injili ya Mathayo, baba yake Yusufu alikuwa ni Yakobo, lakini Luka anatuambia baba yake Yusufu alikuwa ni Eli (Luka 3:23).. Naomba ufafanuzi juu ya hili.
JIBU: Ni wazi kuwa ukisoma kitabu cha Mathayo na kile cha Luka utaona kuna tofauti kubwa kwenye vizazi vya ukoo wa Yesu. Luka anatuambia baba wa Yusufu alikuwa ni Eli, na Mathayo inasema babaye alikuwa ni Yakobo. Lakini je! Hilo linamaanisha biblia inajipinga?
Jibu ni la! Ikumbukwe kuwa zamani katika taifa la Israeli walikuwa na desturi ya mtu kumnyanyulia ndugu yake uzao, na mtoto huyo kuitwa kwa jina la marehemu ikiwa mtu huyo atakufa kabla hajapata mtoto.. Soma. Kumbukumbu 25:5-6,
Kwamfano, kama wewe ni mwanaume umezaliwa katika familia, na ukaoa, lakini kwa bahati mbaya ukafa bila kupata mtoto, basi anatafutwa ndugu yako wa karibu aidha katika familia au katika ukoo, Yule aliye karibu zaidi na wewe, kisha anakwenda kumuoa huyo mke wako uliyemwacha, kisha anamzalia mtoto, lakini huyo mtoto hataitwa kwa jina lake, bali ataitwa kwa jina lako wewe marehemu, haijalishi kuwa watoto huyo watakuwa wametoka katika viungo vya mtu mwingine. Na Wanafanya hivyo ili kulitunza jina lako lisipotee.
Na ndicho walichokifanya Israeli wakati ule, ndicho alichokifanya Boazi kwa Ruthu, (ukisoma Ruthu 4:6-9)
Sasa tukirudi katika Injili. Mathayo aliandika Uzao wa Yusufu (Babaye Yesu), akifuata ubaba wa kibaolojia, na Luka aliandika uzao wa Yusufu akifuata ubaba wa kijina.
Ikiwa na maana kuwa Eli pengine alikufa kabla ya kupata mtoto, hivyo Yakobo akamchukua mke wake, na kuzaa naye ili kumtunzia jina, ndipo akamzaa Yusufu. Hivyo kibaolojia Yusufu alikuwa ni mtoto wa Yakobo lakini kisheria alikuwa ni mtoto wa Eli.
Na ndio maana Yakobo hatajwi katika injili ya Luka, bali ni Eli.. Lakini Mathayo anamtaja Yakobo Kama baba wa Yusufu lakini kibaolojia. Hivyo maandiko yapo sawa.