The Sheriff
JF-Expert Member
- Oct 10, 2019
- 747
- 2,112
Aliyekuwa mbunge na mwanaharakati wa demokrasia Nathan Law ni miongoni mwa watu sita ambao pasipoti zao za Hong Kong zimefutwa na serikali.
Serikali ya Hong Kong leo Jumatano, Juni 12, 2024 imesema kwamba imefuta hati za kusafiria za wanaharakati sita wa kidemokrasia walioikimbilia Uingereza, na kuwaita "wahalifu wanaotafutwa".
Hong Kong mwaka jana ilitoa zawadi ya HK$1 milioni (takribani Dola za Kimarekani 128,000) kwa atakayewakamata wanaharakati 13 walioko nje ya nchi ambao mamlaka zinawatuhumu kwa kutenda makosa ya usalama wa taifa.
Wanaharakati hao sita waliotajwa, wote wakiwa kwenye orodha ya zawadi, wanachukuliwa kuwa “wahalifu wanaojificha Uingereza,”
"Wanaendelea kushiriki waziwazi katika shughuli zinazohatarisha usalama wa taifa... Kwa hivyo tumechukua hatua hii kuwapa pigo kubwa," msemaji wa serikali alisema katika taarifa, akiorodhesha "kufuta pasipoti za HKSAR" kama mojawapo ya hatua.
Watu hao sita ni Nathan Law, Mung Siu-tat, Simon Cheng, Finn Lau, Fok Ka-chi na Choi Ming-da.
Maafisa wa Hong Kong wametaja sheria ya usalama wa taifa iliyopitishwa Machi kama msingi wa kisheria wa kufuta pasipoti zao.
Polisi wameongeza kwamba yeyote atakayetoa fedha, kukodisha mali au kuendesha biashara na waliotajwa anaweza kukabiliwa na kifungo cha hadi miaka saba gerezani.
Hatua hiyo imekuja katika kumbukumbu ya mwaka wa tano ya mapigano ya vurugu kati ya waandamanaji na polisi ambayo yalionesha kuongezeka kwa vurugu katika maandamano ya kutetea demokrasia ya Hong Kong mwaka 2019.
Hatua hizi zimelaaniwa kwa kuwa “tishio kwa demokrasia na haki za msingi za binadamu”.
Kiongozi wa jiji John Lee, ambaye ameadhibiwa na Marekani kwa jukumu lake kama mkuu wa usalama mwaka 2019, amesema wanaharakati wanaotafutwa watafuatiliwa maisha yao yote hivyo kuwataka wajisalimishe.
Beijing iliweka sheria ya usalama wa taifa iliyopanuliwa Hong Kong mwaka 2020 kufuatia maandamano makubwa na wakati mwingine ya vurugu.
Sheria hiyo ambayo imebadilisha jamii ya Hong Kong na kubomoa ukuta wa kisheria uliokuwepo kati ya jiji na China bara inadai ina uwezo wa kuwawajibisha watu wanaotuhumiwa kote duniani.
Watu hao sita waliotajwa Jumatano wametuhumiwa kwa makosa ya usalama wa taifa ikiwa ni pamoja na uchochezi wa kujitenga, uchochezi wa uasi na ushirikiano na nchi za nje, makosa ambayo yanaweza kuwafikisha gerezani maisha.
Sheria mpya ya usalama wa taifa iliyopitishwa Machi imewapa mamlaka za Hong Kong nguvu zaidi za utekelezaji, ikiwemo kufuta pasipoti.
AFP