Mimi siwezi kufurahia kifo cha mtu yeyote, lakini nilikuwa naomba sana tumpate kiongozi mkuu mwingine wa nchi. Kiongozi mwenye hekima, mwenye utu, anayetambua kuwa yeye ni hinadamu kama walivyo binadamu wengine, kiongozi anayejua kuwa hana mamlaka ya kuondoa uhai wa mtu, kuteka au kuwapoteza watu kwa vile tu wamekosoa. Tumpate kiongozi mwenye kupenda haki, anayeheshimu katiba na sheria, asiye mnafiki wala laghai. Asiyeweza kufanya ulaghai kwenye mifumo yetu ya uchaguzi.
Rais Magufuli ameondoka, imebakia historia. Aliyoyatenda, ni yeye ma aliye mkuu kuzidi sisi sote. Lakini tuendelee kuomba maana mifumo na sheria mbaya bado zimebakia vile vile. Waliochukua madaraka, wanaweza, kwa dhamira njema, kubadili ili watu waongozwe kwa haki:
Katiba ya wananchi
Tume huru ya uchaguzi
Sheria gandamizi
Tusiache kuomba kwaajili ya haki ya Watanzania. Mh. Samia, hayo mambo matatu ayafanyie kazi. Kutoyafanyia kazi, hasira ya Mungu haitakoma kwa wanaodhulumu haki za wananchi.
Marehemu ana utu na roho sawa kama Ben Saanane, kama Azory Gwanda, kama yule diwani kupitia CHADEMA wa Dar na Kilombero, sawa na Mdude na TL walioponea kwenye tundu la sindano. Kama tumeumizwa na kifo cha Rais Magufuli, tuumizwe sawa na vifo/kupotea kwa Saanane, Azory, Mawazo, na wale wote waliouawa kwa kuchinjwa kama kuku, huku baadhi ya wanaCCM shetani wakishangilia.
Utu wetu na uhai wetu vivuke hisia na ushabiki wetu wa kisiasa. Uhai na utu wa Mtanzania yeyote, bila ya kujali cheo chake, chama chake, dini yake, umri wake na hali yake, vina thamani sawa mbele za Mungu. Tunaweza kumpamba sana marehemu, kaburi lake, jeneza lake, na bendera nusu mlingoti, na nyimbo nyingi nzuri, lakini kama alikuwa na mkono katika vifo vya wasio na hatia, ni kazi bure - waliodhulumiwa watakuwa mbele yake wakimsuta kwa uovu mbele ya mahakama isiyo na upendeleo, ya Baba Mungu wetu.
Niliomba sana, tumpate kiongozi mwingine atakayerudisha amani ya mioyo kwa Watanzania wote. Kiongozi mwenye kutambua kuwa kwa yeye kuwa kiongozi haimaanishi anafahamu kila kitu kuwazidi Watanzania wote kwa umoja wetu. Kama Mwenyezi Mungu ameamua kujibu maombi yetu kwa namna hii, basi hatuna uwezo wa kuhoji hekima yake.
Mungu wetu atusaidie, tunyanyukapo na kupanda, iwe kwa vyeo, mali au namna nyingine yoyote, tusipungukiwe hekima, tukajisahau na kuamini kuwa ubinadamu wetu nao umepanda dhidi ya ubinadamu wa watu wengine.