Picha: Ubungo Manispaa
Mwaka 2021, Mwenge wa Uhuru ulizindua Hospitali hii ya Ubungo ili kusaidia Wakazi wa maeneo hayo kuwa na Hospitali ya Wilaya.
Hospitali hii inatoa huduma nyingi na za msingi kuanzia huduma ya mama na mtoto, kujifungua, hadi upasuaji.
Licha ya kuwa hospitali hii yenye majengo mazuri na masafi kusaidia wakazi wa maeneo ya karibu, kumekuwa na tabia ambayo si ya kawaida kwa baadhi ya madaktari nyakati za usiku.
MALIPO KINYEMELA
Utaratibu wa kupata matibabu hufuatwa kama kawaida mara tu mgonjwa anapofika hospitalini hapo ambapo hufungua ‘file’ kwa shilingi 3,000.
Baada ya hapo mgonjwa huelekea kwa daktari ambapo baada ya kusikilizwa tu daktari humuandikia mgonjwa vipimo vya kufanya na kumtajia bei hapo hapo.
Daktari huandika vipimo ambavyo katika hospitali hiyo vipimo kama mkojo, choo hupimwa kwa Sh 5,000 na full bloodpicture ni Sh 15,000.
“Mimi nilienda usiku kumpeleka mtoto alikuwa anaumwa, daktari aliniandikia vipimo vinne kwa bei ambayo nilimwambia kwa wakati huu sina pesa hiyo naomba nifanye vipimo vichache” – anasimulia mmoja wa wagonjwa.
Mgonjwa huyu anasema aliandikiwa vipimo vya choo, mkojo na fullbloodpicture kwa Shilingi 25,000 vyote.
“Aliniambia kama sina nisijali kwani nina kiasi gani?, nikamtajia na akaniambia sasa nenda moja kwa moja Maabara ukampe hela mtu wa maabara atakupima, mwambie tu doktari kaniambia nije nilipe hapa”.
Hivyo, inapotokea mteja hana kiasi hiko cha pesa, humpunguzia hapohapo na kumuelekeza moja kwa moja Maabara akalipie huko bila kupata risiti.
KWANINI ULIPAJI WA KINYEMELA?
Wananchi wengi wa maeneo ya karibu na hospitali hii kama Ubungo, Kilungule, Docha na maeneo mengine ya karibu wanasema bei za vipimo na dawa haiendani na vipato vya Wananchi wa kawaida wanaotumia Hospitali za Serikali bila bima.
Hivyo, hiyo inafanya kuwa rahisi kwa Mwananchi wa kawaida kukubali kulipa pesa pungufu Maabara bila kupewa risiti ili aweze kupata vipimo na matibabu.
Jengo la maabara
MALIPO BILA RISITI YANAENDA WAPI?
Malipo haya hayaingii katika mfumo wa malipo hospitalini hapo na moja kwa moja hupokelewa na mtu wa Maabara ambaye huwa na mawasiliano ya moja kwa moja na daktari.
NI KWELI GHARAMA NI KUBWA?
Mmoja wa daktari katika hospitali hii anasema Wananchi wengi wanalinganisha bei za hospitali hiyo na Vituo vya Afya vilivyopo katika maeneo hayo, akidai kuwa ni Hospitali ya Wilaya, hivyo hata bei lazima itofautiane.
Kingine anadai kuwa hospitali ni mpya na bado inapaswa kujiendesha yenyewe kwani haijaanza kupata wagonjwa wengi kama ilivyo kwa hospitali kama ya Kimara na maeneo mengine.
Swali la kujiuliza ni kuwa kama hospitali hii inatafuta pesa za kujiendesha na bado kuna pesa zinazolipwa bila stakabadhi na hazijulikani zinakwenda wapi, je itafika safari yake ya kujiendesha?