SoC02 Hospitali za Rufaa kuwaachia majukumu yote ya kitabibu wanafunzi wa udaktari pasipo usimamizi wa kutosha - chanzo cha vifo vingi

Stories of Change - 2022 Competition

cupvich

JF-Expert Member
Joined
Aug 2, 2022
Posts
408
Reaction score
247
UTANGULIZI
Nikiwa wodini nauguza mgonjwa wangu katika moja ya hospitali kubwa ya Rufaa nchini, Nilimsikia daktari mmoja akitumia lugha ya kiingereza kuwaambia wanafunzi wanao somea udaktari ambao walikuwa wakitoa huduma kwa mgonjwa aliyekuwa kitanda cha pembeni na alicho mgonjwa wangu maneno haya nanukuu "MMEKOSEA, HAMKUTAKIWA KUMCHOMA SINDANO HIYO". Hakika nafsi yangu iliogopa sana, Nilihisi kana kwamba amefanyiwa mgonjwa wangu, hivyo niliwaza iwapo angekuwa ni mgonjwa wangu na nimesikia maneno yale ya daktari ningechukua hatua gani. Ilinifanya kufuatilia kwa ukaribu maendeleo ya Mgonjwa yule tokea siku ile kwasababu nilikuwa pale kwa wiki moja nikimuuguza mgonjwa wangu, Baada ya siku moja nilipewa taarifa kuwa Mgonjwa yule alifariki Dunia.

Hospitali zetu za rufaa zimekuwa kimbilio kwa walio wengi katika suala zima la matibabu, hii ni kutokana na kuaminika kwamba zina wataalamu wa kutosha. Lakini pia zinaweza kutoa huduma za kibingwa. Kwa hapa kwetu Tanzania tumebarikiwa kuwa na Hospitali za rufaa za mikoa lakini pia tuna hospitali za rufaa za kanda kama vile HOSPITALI YA RUFAA YA KANDA MBEYA, HOSPITALI YA RUFAA YA KANDA KCMC, HOSPITALI YA RUFAA YA KANDA BUGANDO pamoja na hospitali kubwa ya taifa MUHIMBILI. Hospitali hizi za rufaa za kanda zina Vyuo ambavyo hutoa mafunzo kwa wataalamu wa Afya kama vile madaktari, manesi na wafamasia. Vyuo hivyo ni MUHAS,BUGANDO, MCHAS, na KCMCo pamoja na vyuo vingine vinavyopatikana katika hospitali za mikoa na Hospitali zingine za Binafsi na mashirika ya dini.

Wanafunzi hawa wa udaktari walioko wafunzoni wamekuwa wakitumia muda mwingi kufanya mazoezi kwa vitendo katika hospitali zetu jambo ambalo ni Zuri kwani linawajenga na kuwaimarisha vyema katika Sekta hiyo muhimu ya afya. Lakini pia wamekuwa wakirahisisha utoaji wa huduma za afya kwa kuongeza wahudumu wa afya katika hospitali zetu ukizingatia kwamba vituo vingi vya afya pamoja na hospitali zetu Bado zina changamoto kubwa ya upungufu wa wataalamu wa Afya. Kwa ujumla wanataalamu hawa walioko mafunzoni hususani madaktari wanafanya kazi kubwa.

TATIZO LINAANZIA HAPA.
Kwa Bahati mbaya, hospitali zetu zimewaamini Wanafunzi hawa walioko vyuoni kupitiliza kiasi cha Kuwapangia Zamu za kuwaona wagonjwa pasipo usimamizi wa daktari mzoefu na kufanya matibabu kwa mgonjwa hata kwa wagonjwa ambao wako katika hali mbaya. Jambo ambalo ni Hatarishi kwa afya ya mgonjwa. Hii imesababisha kutokea kwa vifo vingi kutokana na kwamba wanafunzi hawa wa afya hawajawa bado na Utaalamu wa kutosha katika kutoa huduma za afya kwa kiwango kinachostahili ukilinganisha na madaktari wazoefu.

CHANZO CHA TATIZO.
Ni kweli kwamba siku hizi Teknolojia imerahisisha ufanyaji wa kazi katika hospitali zetu.Teknolojia imechukua nafasi kubwa sana katika utoaji wa huduma katika vituo vya afya na Hospitali, na ndio maana utakuta Daktari anayeingia katika zamu ya usiku anaweza kumfahamu vizuri mgonjwa aliyelazwa wodini, matibabu aliyoyapata na matibabu anayotakiwa kuyapata hivyo kumrahisishia kuendeleza matibabu kwa mgonjwa. Lakini ukuaji huu wa Teknolojia usiwe Sababu ya kuwaachia majukumu yote wanafunzi wa udaktari walioko Vyuoni kwani waliowengi bado hawajapata maarifa ya kutosha katika kutoa huduma za kitabibu. Lakini pia wingi wa hawa wanafunzi katika hospitali zetu kisiwe kigezo cha madaktari wazoefu na wenye majukumu ya kutoa huduma za afya kusahau wajibu wao wa kuwahudumia wagonjwa. Wengi wa hawa wanafunzi wa udaktari wamekuwa wakitoa huduma kwa hisia ili tu kukamilisha matakwa ya kozi wanazosomea ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi kwa vitendo. na hivyo kuhatarisha maisha ya mgonjwa.

ATHARI ZITOKANAZO NA TATIZO HILI.
Utakubaliana nami kuwa Siku zote Mwanafunzi atabaki kuwa mwanafunzi, hata kama ni mwanafunzi wa udaktari mwaka wa nne au wa tano. Na sifa mojawapo aliyonayo mwanafunzi ni kutokujiamini kwa asilimia mia moja, hivyo kupelekea kufanya jambo kwa Jazba na Mihemko ilimradi tu kukamilisha takwa fulani. Hivyo nilazima uongozi wa hospitali zetu uwachukulie wataalamu hawa wa afya kama wanafunzi na kuwasimamia katika huduma zote za kitabibu katika hospitali zetu kwa manufaa mapana ya mgonjwa na mtoa huduma.

Kutokana na kuwatumia madaktari mafunzoni katika hospitali zetu hizi za rufaa, Huduma katika hospitali hizi zimekuwa zikishuka kadiri siku zinavyokwenda licha ya serikali Kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha katika kuboresha mazingira ya utoaji huduma katika hospitali hizi, ikiwa ni pamoja na Ununuzi wa vifaa vya kutolea huduma za afya, Uongezaji wa majengo ya kutolea huduma za afya na kuongeza watumishi wa afya. Jambo hili si zuri kwasababu linapunguza imani kwa wananchi hivyo kutumia gharama kubwa kupata matibabu katika hospitali za binafsi.

Usalama wa mgonjwa awapo hospitalini ni muhimu sana. Muda mwingi mgonjwa hubaki na wataalamu wa afya kwa ajili ya matibabu. Hivyo ndugu jamaa na marafiki huamini kuwa Daktari au mtaalamu yeyote wa afya ana nafasi kubwa katika kuokoa maisha ya Mgonjwa. Wote tunaamini kwamba mtaalamu yeyote wa afya anatakiwa awe na ujuzi wa kutosha katika kumhudumia mgonjwa ili kuokoa maisha yake. Iwapo mtaalamu huyo wa afya atakosa ujuzi na maarifa ya kutosha maisha ya mgonjwa yatakuwa hatarini, na hata kuwa ametekeleza majukumu yake ipasavyo. Lakini pia kukosekana kwa maarifa ya kutosha kutamfanya mtaalamu huyo kushindwa kujiamini katika kazi yake.

HITIMISHO
Madaktari walioko mafunzo pamoja na wataalamu wengine wa afya wanafanya kazi kubwa na nzuri katika kurahisisha utoaji wa huduma katika hospitali zetu, Lakini Uongozi wa hospitali zetu kwa kushirikiana na vyuo vinavyotoa wataalamu hawa wa afya hauna budi Kuwasimamia ipasavyo wakati wote wanapotoa huduma kwa wagonjwa ikiwa ni pamoja na kuwapanga pamoja na Madaktari wazoefu ili kuifanya huduma yao ya matibabu iwe salama na yenye kuleta matumaini kwa mgonjwa na Kuepukana na Vifo vinavyotokana na UZEMBE wa watoa huduma za afya.

Wenu
Mwita Ngutunyi Mohono
S.l.p 237 Mbarali- MBEYA
0762185894
mwitangutunyimohono@gmail.com
 
Upvote 49
Asante sana kwa andiko hili zuri. Ni kweli siku hizi katika hospitali zetu hizi wanafunzi wa udaktari wamekuwa wakiachiwa majukumu yote ya kitabibu. Ipo haja ya serikali kuliona hili inakatisha tamaa wananchi kupeleka wagonjwa katika hospitali hizi. Yaani unakuta madaktari wanafunzi wakitibu wagonjwa inapotokea shida ndipo daktari mzoefu anaitwa.
 
Sio kweli kiongozi. Tembelea hospitali zetu hizi
 
Ili ujue kuendesha baiskeli ni lazima uachwe kusukumwa then uende mwenyewe hata kama utaanguka.

Katika hospital policy hakuna anayeachiwa wodi ambaye hajaiva hii nakataa Fanya tafiti zako vizuri. Mpaka mwanafunzi anaachiwa wodi means yupo vizuri, mistake huwa zipo hata kwa hao specialist unaowasemea na ndiyo maana kila toxicity drug ina antidote yake kwa emergency management.

Napinga kabisa hoja ya kusema wanaoachiwa wodi hawajaiva lahasha sio kweli kabisa.
Sheria haimruhusu mwanafunzi wa diploma mwaka wa1 na wa2 kuingia night shift wala kuachiwa wodi kwa wale wa diploma na hata ufanyaji wa practice wanakuwa more under supervision ndivyo inavyofanyika kwenye hospital zote.
Ukirudi kwenye bachelor degree pia in hivyo hivyo wanafunzi wanaruhusiwa kujifunza kwa vitendo rasmi kuanzia mwaka wa3 na wa4 wanaruhusiwa kufanya kwa vitendo, na ule mwaka wa internship ndiyo wapo radhi kuachiwa wodi. Na hii ndiyo inafanyika katika hospital unazosema.
Usiandike maoni bila ya tafiti zenye kujitosheleza au sio muhusika wa kada husika ya afya maana hufahama principles zake kiundani zaidi.

Hoja nzuri ila haina tafiti na napinga msemo wako wa kusema wanaachiwa kazi zote wao wale ambao wanafunzi hawajaiva vizuri. SIOKWELI.
Tutabishana mpaka kesho kama sio muhusika kada ya afya.
Futa uzi huu
 
Usiandike makala kwa hisia zako binafsi au kwa jambo binafsi lililokusibu, hapa ndipo wabongo tunafeli.
Fanya tafiti vizuri then ndiyo uje na maoni yenye kujitosheleza. Ndiyo utekelezaji wa Sera unawajibika kuchukua hayo maoni
 
Nadhani hujasoma andiko langu lote.. hapo ndipo shida inaanzia.
Lengo kuu la andiko langu ni kukemea tabia ya Kuwaamini kupitiliza madaktari hawa wanaokuwa mafunzoni kwasababu.. Wengi wanalalamika wao kuachiwa wagonjwa wao. Wakati mwingine huduma zinakuwa duni. Na sio kwamba sijawahi kushuhudia au cfahamu.

Sina nia mbaya hata kidogo na wanafunzi hawa wa udaktari mafunzoni kwasababu nami nahusika. Napongeza kazi yao ni muhimu sana wawepo ila WANAPOTOA HUDUMA WAWEKATIKA UANGALIZI MAALUM.
 
Hakuna biashara yenye pesa kama healthcare, big number ya watu bongo wana pesa za kulipa matibabu yao ila wanataka huduma nzuri tuu za uhakika na wala hawataki kwenda India wala Europe kutibiwa, i hope mtu mmoja ataamka aanzishe hospitali ya maana na kuweka gold standard bila longolongo au kazi za mikato mikato ajichotee hayo mabilioni ambayo yanaenda nje....FURSA!!
 
Mwandishi haelewi kbs system ya hosp inavyofanya kaz, pia hajui matibabu ni nn, .
.
Hawa wanafunz/interns ni maDaktari wa kupita kila mwaka, hospital hua ina staff wake ambao wako kweny roaster/ratiba ya kila sku na interns wana roaster zao, so haiwezekan intern apangiwe zamu peke ake.
.
Kila asubuhi hua kuna morning report ambapo intern pamoja na supervisor wake (permanent employee either specialist au experienced dr) watarepot taarifa za 24hrs.
.
, Then watapita kwny morning rounds kuangalia wagonjwa na kufanya maamuzi na kuandika dawa za 24hrs, na hapo matibabu yanakua yamekamilika,
.
Sasa kinachofuata ni kwenda kunywa chai then wanaoenda clinic wataenda, wanaoingia theatre wataenda, wanaorud hom wanarudi, wodini anabaki intern na nurse wa zamu, kutimiza yaliyoamriwa asubuhi,
.
Km kuna tatizo, intern atawasiliana na Supervisor/Muajiriwa permanent wa hospital alie kwny zamu, na ataelekezwa afanye nn, na tatizo likiwa kubwa itaenda kwa hatua hadi kwa super specialist,
.
Ndugu sio lazima specialist aje amchome sindano mgonjwa wako ndo ujue ametibiwa na Daktar mzoefu,
Hyo ni Common misconception ambayo ndugu wa wagonjwa hua mnayo, mkimuona intern muda wote mnajua ndo Daktar pekee anaefanya matibabu,
MKO WRONG SANA,.
.
P.S
ni rare sana mgonjwa kupewa dawa ambayo sio sahihi, na hta ikitokea hawezi kabisa kufa, maana ile sio sumu, ni dawa, one injection haiwez kua lethal,.

Pia sio jambo la kushangaza Daktar mmoja kubadili dawa alizoandika Daktar mwngne, ni swala la Kuzidiana elimu na uzoefu, na haimanishi zilizofutwa ni mbaya, ila zilizoandikwa yawezekana ni bira zaid kulingana na uzoefu.

Kingne fanya utafiti kuhus kero za wahudum wa afya na maslahi yao, sio kuwakandia tu afu baadae kuwatext kuwaomba dawa za UTI.
 
Asante sana rafiki kwa kusoma andiko langu.

Binafsi naheshimu kazi kubwa inayofanywa na Watu hawa wa kada ya Afya wakiwemo madaktari. Hakika wanafanya kazi nzuri na serikali haina budi kupitia upya maslahi yao.

Lakini pia NATAMBUA mchango mkubwa walionao Madaktari mafunzoni katika hospitali zetu hususani hizi za Rufaa. Na hata wakati mwingine nilipendekeza wawe wanapata posho kuanzia mwaka wa tatu ilimradi tu wafanye kazi kwa moyo hata kama bado ni wanafunzi.

KIINI KIKUBWA CHA ANDIKO LANGU NI KUONYESHA KUWA PAMOJA NA KAZI KUBWA WANAYOFANYA WANAFUNZI HAWA WA UDAKTARI. NI SHARTI WASIACHIWE KWA ASILIMIA ZOTE kutoa matibabu katika Hospitali zetu hizi kubwa.

Hizi hospitali za RUFAA Zinatakiwa kuwa kioo katika utoaji bora wa Huduma za afya kwasababu Serikali imewekeza Pesa nyingi katika hospitali hizi ili kuweka mazingira mazuri ya utoaji huduma. Kama vile Kuongeza vifaa muhimu hospitali, Majengo ya kutolea huduma na kuajiri watumishi wapya.
 
Asante kwa kuliona hili mwanajukwaa. Ni kweli kabisa kwamba wananchi wanapenda kuona huduma za afya zikiborewa bila longolongo. Yote hii itawezekana katika hospitali zetu kwa kuweka usimamizi bora wa kutoa huduma ikiwa ni pamoja na kuwasimamia vyema madaktari walioko mafunzoni katika masomo yao kwa vitendo.
 
Juzi hapo kidogo tumpoteze ndugu yetu alifanyiwa operation ya kujifungua na wanafunzi huko Arusha hospital inaitwa Seriani
 
Juzi hapo kidogo tumpoteze ndugu yetu alifanyiwa operation ya kujifungua na wanafunzi huko Arusha hospital inaitwa Seriani
Pole sana ndugu yangu. Pamoja na kazi kubwa wanayoifanya wataalamu hawa wa afya. Ipo haja ya kuwepo usimamizi wa kutosha katika hospitali zetu hizi ili HUDUMA za AFYA ziwe bora na kujenga imani kwa wananchi.
 
Hujui wewe
Ni kweli. Jambo usilolijua huwezi kuwa na ushuhuda nalo. Wananchi wengi wa kipato cha kati na chini wanaweza kuwa na ushuhuda wa kutosha. Serikali kupitia kwa Rais wetu mh. Samia suluhu hassan imekeza kiasi kikubwa cha fedha katika hospitali hizi. NI SHARTI ZIWE ZA VIWANGO VIKUBWA.
 

Hajasema wasifanye mazoezi kwa vitendo,mleta mada anachopinga ni kuwaachia majukumu peke yao bila uangalizi wa daktari mzoefu/aliyeko kazini
Hakuna mwanafunzi anaye achiwa mgonjwa hospital za serikali nikushauri
Mbona jamaa kakueleza hapo ratiba ilivyo kwani kunasehemu kasema kwamba mwananfunzi anaachiwa mgonjwa au kakwambia anapewa maelekezo na mwalimu wake ?
 
Tufanye wewe unajua sasa
 

Hospitali ya Rufaa ya KCMC inaongoza kwa kuwaachia majukumu yote ya kitabibu wanafunzi wa udaktari pasipo usimamizi wa kutosha na imesababisha chanzo cha vifo vingi Katika Hospital hiyo Kila siku Kila saa.​

 
Hakuna mwanafunzi anaye achiwa mgonjwa hospital za serikali nikushauri

Mbona jamaa kakueleza hapo ratiba ilivyo kwani kunasehemu kasema kwamba mwananfunzi anaachiwa mgonjwa au kakwambia anapewa maelekezo na mwalimu

Hakuna mwanafunzi anaye achiwa mgonjwa hospital za serikali nikushauri

Mbona jamaa kakueleza hapo ratiba ilivyo kwani kunasehemu kasema kwamba mwananfunzi anaachiwa mgonjwa au kakwambia anapewa maelekezo na mwalimu wake ?
Nakuelewa fika rafiki. Lakini nadhani changamoto ipo katika kulielewa andiko langu. Nashukuru nimepata wasaa wa kuwasiliana na waatalumu wabobezi katika kada hii. Pamoja na mazuri wanayoyafanya. Lakini wanakubaliana nami kuwa changamoto hazikosekani. Ni sharti sasa hospitali zetu hizi kubwa Ziongeze usimamizi kwa wanafunzi wanao somea udaktari ili kujenga imani ya kutosha kwa wananchi.
 
Unaandika tu kaka, alafu huna hoja tufanye nimekubali Mimi sijui
Hutakiwi kukubali mwanajukwaa bila kuelewa unakubali nini. Mimi na wewe tuna wajibu mkubwa katika maendeleo ya hospitali zetu.

Hatuko kushindana bali kuwekana sawa. Kwasababu uwekezaji mkubwa sana unefanywa katika sekta hii ya afya nchini. Nichukue fursa hii kumshukuru mheahimiwa Rais na wizara ya afya kwa ujumla kwa kufanya makubwa katika kuboresha huduma za afya nchini.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…