The Palm Beach
JF-Expert Member
- Dec 30, 2015
- 1,967
- 4,267
View: https://youtu.be/5Y7PcWedUNE?si=nXAlvjXG1G6V-4Mu
KWANINI NO REFORMS, NO ELECTION?
Ni kwa sababu:
1. Kwa utaratibu wa kisheria, kikanuni, kikatiba na wa kiserikali, uchaguzi salama usioambatana na mauaji, huru, wa wazi na haki hauwezekani tena kufanyika ktk nchi hii..
2. NO REFORMS, NO ELECTION, maana yake ni kuwa, bila kufanyika kwa mabadiliko ya kisheria, kikanuni na kikatiba, basi hizi chaguzi za kiinimacho Tanzania hazitafanyika tena maana tutazuia zisifanyike kwa kujenga hoja kwa wananchi, wanachama wetu, taasisi za kiraia na za kidini, viongozi wa dini, nchi wahisani wa Tanzania, taasisi za haki za kibinadamu za kitaifa na kimataifa hadi waelewe na kutuunga mkono..."
TAKWIMU ZA KIUCHAGUZI KUONESHA KUWA UCHAGUZI SALAMA, HURU, WA HAKI NA WAZI HAUWEZEKANI TENA TANZANIA:
A: UCHAGUZI WA MITAA NA VIJIJI WA 2014
√ Jumla ya vijiji vilikuwa 11,748.
• CCM ilishinda vijiji 9378 (80%)
• CHADEMA vijiji 1,754 (15%)
√ Jumla ya mitaa yote ilikuwa 3,875
• CCM ilishinda mitaa 2,583 (67%)
• CHADEMA ilishinda mitaa 980 (25.29%)
B: UCHAGUZI WA VIJIJI NA MITAA 2019
√ Jumla ya vijiji ilikuwa 12,262
• CCM ikashinda 12,260 (99.99%)
• CHADEMA (haikutajwa kabisa)
√ Jumla ya mitaa nchini 4,263
•CCM ikashinda mitaa 4,263 (100%)
• CHADEMA (haikutajwa kabisa)
C: UCHAGUZI WA VIJIJI NA MITAA MWAKA 2024
√ Jumla ya vijiji ni 12,271
• CCM ikashinda vijiji 12,150 (99%)
• CHADEMA ikashinda vijiji 97 (0.79%)
√ Jumla ya mitaa ni 4,264
• CCM ikashinda mitaa 4,213 (99%)
• CHADEMA ikashinda mitaa 36 (0.84%)
✔️ Katika kujenga hoja yake amesema, chaguzi za mwaka 2019 na 2020 zimeweka rekodi za kuengua karibu wagombea wote wa vyama vingine huku wa CCM wakibaki wote kwa vigezo visivyo vya kikatiba mfano kukosea jina, kukosea kuandika jina la chama nk
✔️Ametolea mfano wa jimboni kwake Singida Mashariki lililokuwa na vijiji 50 mwaka 2014, kuwa CHADEMA ilishinda vijiji 47 na CCM kuambulia vijiji 3 pekee. Lakini eti ktk chaguzi za mwaka 2019 na 2024, CHADEMA ikakosa Kijiji hata kimoja kwa kuwa wagombea wake hawakuwa na sifa na waliofanikiwa kupenya na kugombea, kura zao ziliibwa zote na kupewa wagombea wa CCM kwa kutangazwa washindi kwa nguvu ya Polisi wakiwa na bunduki..!
UKWELI WA SASA NI KWAMBA:
1. CHADEMA Ina watu werevu zaidi sasa kuliko ilivyokuwa mwaka 2014 na kama uchaguzi ni huru, wa wazi na wa haki CCM haiwezi kushinda popote..!
2. Sababu kubwa ya kushinda CCM ni kwa kuwa sasa wanatumia bunduki, jeshi kuiba/kupora uchaguzi wote kabisa..
3. Hakuna sehemu yenye unafuu kuanzia vitongojini, Kijiji, kata, jimboni, wilaya, mkoa na taifa. Kote ni uozo na uchafu mtupu, hakuna uchaguzi bali ni vita na mapambano na Polisi na TISS na mahali pengine wameingiza na kuitumia Jeshi la wananchi (JWTZ)...!
4. Ukiona mazingira ya uchaguzi nchi nzima yako hivi, tambueni kuwa uamuzi wa namna hii umefanyikia Ikulu...!!
KWANI KUNA SHIDA GANI KTK MFUMO WETU WA UCHAGUZI WA SASA?
Una shida kwa sababu;
1. Ni mfumo wa ki - CCM, ulitengenezwa na CCM, kwa ajili ya CCM, unaifaidisha CCM na kwa sababu hiyo si mfumo wa kidemokrasia na unawaumiza wananchi na nchi yote..!
2. Ni wa CCM kwa kuwa, uchaguzi mkuu unasimamiwa na Tume ya Uchaguzi ambayo ni ya CCM ambayo huteuliwa na kupewa maelekezo na Mwenyekiti wa CCM ambaye mara zote huwa ndiye Rais wa nchi..
3. Aidha, Mwenyekiti wa CCM ambaye naye mara zote huwa ni mshiriki na mshindani ktk uchaguzi ndiye anayeteua Mwenyekiti wa Tume, wajumbe wote wa Tume na mkurugenzi wa uchaguzi wa Tume. Ndiye mwajiri na mteuzi wa wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo (wakurugenzi wa halmashauri za miji, wilaya, manispaa na majiji), watendaji wa kata na wa vijiji. Katika mazingira haya, hawa kamwe hawawezi kutenda haki Bpbali watampendelea aliyewateua....!
4. Mfumo wa ugawaji majimbo ya uchaguzi ni wa hovyo na umejaa uchafu mtupu kwa kuwa hauzingatii idadi ya watu (wakaazi). Maeneo ambayo CCM Ina uhakika wa kushinda imeyagawa ktk vijimbo vingivingi Ili mradi iingize Wabunge wengi bungeni. Mfano DSM yenye wapiga kura wengi 3,427,000 (takwimu za Tume ya Uchaguzi za mwaka 2020) iko sawa na wapiga kura wa mikoa ya Rukwa, Pwani, Songwe, Iringa, Katavi na Njombe kwa pamoja. Lakini DSM ina majimbo 10 tu (sawa na na wastani wa wapiga kura 327,000 kila Jimbo huku Mikoa hiyo 6 kwa ujumla ikiwa na majimbo 37 sawa na wastani wa wapiga kura 91,000 kila Jimbo. Usawa uko wapi hapo?
5. Hii ni huku Tanganyika. Ukienda Zanzibar, majimbo ya uchaguzi huko yana wastani wa wapiga kura 10,000 kwa maana kuwa mbunge toka Zanzibar anaweza kuchaguliwa na watu wasiozidi 2,500 akaja Dodoma na akawa na haki sawa na mbunge anayehudumia wapiga kura 327,000..! Usawa uko wapi hapa..?
MAPENDEKEZO YA MSINGI YA MABADILIKO YANAYOTAKIWA KUFANYIKA SASA:
• Mapendekezo ya mabadiliko ya kimfumo tunayoyatoa hapa, yapo pia kwenye taarifa za tume mbalimbali zilizoundwa na serikali hiihii chini ya CCM tangu mwaka 1991 kabla hata CHADEMA haijazaliwa. Tume hizo ni;
1. Tume ya Jaji Francis Nyalali ya mwaka 1991 (Rais Hayati Ally Hassan Mwinyi)
2. Tume ya Jaji Robert Kissanga ya mwaka 1998 (Rais Hayati Benjamin Mkapa)
3. Tume ya Jaji Mark Bomani ya mwaka 2003 (Rais Hayati Benjamin Mkapa)
4. Tume ya mabadiliko ya Katiba ya Jaji Joseph Sinde Warioba ya mwaka 2014/2015 (Rais Jakaya Mrisho Kikwete)
Tume hizi zote zilipendekeza mabadiliko yafuatayo na sisi CHADEMA ndimo tunamopita:
PENDEKEZO #1: Lazima tuwe na Tume Huru kwelikweli ya uchaguzi ambayo; Hiyo Tume iweje Ili tuite kuwa ni Tume uchaguzi Huru kwelikweli...?
• Tume Huru ya Uchaguzi isiwe ya Rais ambaye yeye ndiye atateua Mwenyekiti na wajumbe wake
• Tume Huru ya Uchaguzi iwe na bajeti inayojitegemea na kupitishwa na Bunge kuendesha shughuli zake. Itoke kwenye utaratibu wa Sasa wa mpaka kupiga magoti kuomba pesa toka kwenye bajeti ya wizara au ofisi ya waziri mkuu au Rais..
• Rais asiteue mtu yeyote kusimamia uchaguzi na badala yake, Tume iwe na wafanyakazi wake wa kudumu na wa mikataba ya muda mfupi/maalumu inayowajiri yenyewe na watawajibika kwa Tume pekee..
• Rais asiwe na mamlaka na mtu yeyote kuanzia msimamizi wa kituo cha kupigia kura hadi kwa Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na wakurugenzi wa Tume wote..
PENDEKEZO #2: Ugawaji wa majimbo lazima ufanyike upya kwa kuzingatia kigezo cha idadi ya watu kama ilivyokuwa katika sheria za uchaguzi na katiba kuanzia mwaka 1961 hadi 1991. Kigezo cha miumdombinu na jiografia ya eneo hakifai na ni cha hovyo...
PENDEKEZO #3: Daftari la wapiga kura litengenezwe upya kwa kuandikisha wapiga kura wote upya kwa kuondoa wapiga kura hewa wote. Aidha, Daftari la wapiga kura sio Siri Bali lazima liwe wazi (accessible) kwa yeyote anayetaka kuliangalia Ili mradi kuweka utaratibu rahisi na wa wazi kufanya hivyo...
PENDEKEZO #4: Utaratibu wa kuengua wagombea wote iwe wa CCM, CHADEMA au chama chochote kwa sababu ambazo si za kikatiba ukomeshe na kupigwa marufuku mmoja na sheria tutakazotunga...
PENDEKEZO #5: Utaratibu wa vyombo vya mabavu police na TISS kuwafanyia vurugu wagombea wa vyama pinzani na CCM upigwe na marufuku na sheria na sheria iweke utaratibu wa kuwashitaki, kuwalipisha fidia na kufukuzwa kazi mwenye mamlaka yeyote atakayetumia mamlaka yake vibaya kwenye eneo hili....
PENDEKEZO #6: Utaratibu wa Sasa wa mawakala wa wagombea wa vyama vya siasa kuapishwa kiapo cha kutunza siri ni batili na hauna sababu na unaleta urasimu usio na maana yoyote kwa sababu kwenye kituo cha kupigia kura hakuna Siri ya kutunzwa hapo kwa sbb kila kitu kinatakiwa kufanyika kwa uwazi huku kila mtu akiona. Barua rasmi tu ya chama cha siasa ambacho wakala anatoka Ili kusimamia kura za mgombea wake inatosha kumfanya atambuliwe na msimamizi wa kituo cha uchaguzi...
PENDEKEZO #7: Utangazaji wa matokeo ya uchaguzi kuanzia kwenye kituo cha kupigia kura ufanyike tu pale ambapo mawakala wa wagombea wote wameridhika na kusaini fomu za matokeo. Kwenye kituo cha majumuisho iwe ni kwenye nafasi ya uenyekiti wa kitongoji, mtaa, Kijiji, udiwani, ubunge au u - Rais, matokeo yatangazwe pale tu ambapo wagombea wote wameridhika na kusaini fomu ya matokeo. Kama mgombea au wakala wa mgombea hajaridhika kwa sababu hii au ile sheria iseme ni marufuku kwa msimamizi wa kituo kutangaza matokeo hayo. Na ikitokea hivyo, basi mgogoro wa namna hiyo uende mahakamani kuamuliwa....
##Haya👆👆ndiyo Mapendekezo ya msingi ambayo ndio shida za mfumo wote wa chaguzi za Tanzania zimelala hapo. Haya yakirekebishwa, tutaingia kwenye uchaguzi bila shida...
JE, WATASIKILIZA NA KUKUBALI KIRAHISI TU?
1. Anasema Tundu Lissu kuwa, tunajua hawatakubali kusikiliza na kuyatendea kazi haya kirahisi rahisi tu na ndio maana tupo hapa tunaelekezana na kufundishana Ili tuende huko nje kuineza movement hii na kutengeneza mazingira ya kuwalazimisha watende yawapasayo kutenda sasa...
2. Ni lazima tuingie kazini kupambana kwelikweli. Tuwashirikishe watu wote. Tuwaulize na kuwaambia wenzetu nyie mnajiandaa na uchaguzi ili iweje iwapo mnajua kabisa kuwa mnakwenda kuchinjwa kama makondoo chini ya utaratibu, kanuni, sheria na katiba hii? Ili iweje iwapo mnajiandaa kwenda kuenguliwa? Ili iweje iwapo iwapo tunajua fika kuwa unakwenda kupiga kura yako ambayo haina thamani yeyote maana haitahesabiwa? Unagombea ili iweje iwapo unaenda kunyang'anywa ushindi wako kwa bunduki? Ili iweje iwapo kama wewe ni mgombea basi Kuna uwezekano wa kutekwa unaporudisha fomu ya uteuzi, kuteswa na kuuwawa kama ilivyokuwa kwa wagombea wengi mwaka 2019, 2020 na 2024...?
3. Tuwaambie na kuwashirikisha kwa njia zozote watu wote (wananchi), wanachama wetu, viongozi wa dini, taasisi za kidini, taasisi za kiraia, mashirika na taasisi za kutetea na kupigania haki za kibinadamu za ndani na nje ya nchi yetu, nchi wahisani zinazoisadia Tanzania, taasisi za kimataifa kama UN, AU, Jumuiya ya Ulaya nk...
Tukifanya kazi yetu vizuri, sekeseke na pressure ya ndani na nje ya nchi itakuwa sio ya kawaida na mwisho wa siku tutaheshimiana na kama taifa tutakaa chini Ili kupata mwafaka wa kitaifa kwa pamoja na hivyo nchi kupata mabadiliko tuyatakayo...
JE, ITACHUKUA MUDA GANI KUFANYIKA KWA MABADILIKO HAYA?
√ Haijalishi itachukua muda gani. Lakini kwa uzoefu wa nchi jirani kama vile Kenya, yaweza kuwa kati ya miaka 2 hadi 3 ndiyo kila kitu kinaweza kuwa sawa kuanzia mabadiliko ya kikatiba, sheria mbalimbali na taratibu, kanuni na kutengeneza taasisi mpya za kiuchaguzi...
√ Anasema, kama itakuwa kuna nia dhabiti na ya kweli ya kuleta mabadiliko hatuna shida tutasubiri maana tumevumilia kwa miaka zaidi ya 30, hivyo kusubiri miaka 2 au 3 sio shida iwapo tu tutapata mabadiliko ya kweli na ya haki...
Kazi kwako Rais Samia Suluhu Hassan na CCM yako. Ni uchaguzi wako, utenfe jema wakati wa amani au unasubiri wakati wa shari...
Mtazame na msikilize mwenyewe Tundu Lissu hadi mwisho kwenye video hiyo👆👆
Lucas Mwashambwa, Tlaatlaah, Pascal Mayalla, Retired mnaonaje Mapendekezo haya?