Kwa mujibu wa Ratiba iliyotolewa na Tume, Wajumbe wa Tume wamegawanywa katika makundi saba na kila kundi litakusanya maoni ya wananchi katika mkoa mmoja kwa siku ishirini na nane. Kwa mujibu wa Ratiba hiyo, kila kundi litatembelea
kila wilaya iliyopo katika mkoa husika ambapo kitafanya mikutano miwili kila siku.
Kwa kuzingatia utaratibu ambao Tume imeuweka, Wajumbe wa Tume wakifika katika vituo vya mikutano hutoa maelezo ya utangulizi kuhusu madhumuni na kazi za Tume. Baada ya maelezo hayo,
kila mwananchi hupewa fursa ya kutoa maoni yake kwa mdomo kwa muda usiopungua dakika tano.
Wale wanaotoa maoni kwa njia ya maandishi, hupewa muda wa kutosha kufanya hivyo. Kwa mujibu wa Ratiba hiyo, kila kundi linapaswa kufanya mikutano miwili kwa siku ambayo hudumu kwa saa tatu kila mmoja.
Tume inatambua kuwa wananchi wana shauku kubwa ya kutoa maoni yao kuhusu Katiba Mpya na ingependa kumfikia kila mmoja mahali alipo. Hata hivyo, kwa kuzingatia jiografia ya nchi na muda ambao Tume imepewa, Tume imepanga ratiba ambayo itawezesha wananchi kutoa maoni kwa kuzingatia jiografia ya eneo husika.
Hivyo basi, Tume inatoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika maeneo ambayo itafanya mikutano na kutoa maoni yao.
Tume inachukua fursa hii kuwafahamisha wananchi kuwa Ratiba ya mikutano ya kukusanya maoni haikupangwa kwa kuzingatia Kata bali imepangwa kwa kuzingatia eneo ambalo linaweza kujumuisha wananchi kutoka zaidi ya Kata moja.
Tume pia inapenda kuwafahamisha wananchi kuwa wanaweza kuwasilisha maoni kupitia tovuti ya Tume (
www.katiba.go.tz); barua pepe (
maoni@katiba.go.tz) au kwa njia ya posta kupitia anuani zifuatazo:
a) Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Makao Makuu, Mtaa wa Ohio, S.L.P 1681,
DAR ES SALAAM Au
b) Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jengo la Ofisi ya Mfuko wa Barabara, Mtaa wa Kikwajuni/Gofu, S.L.P. 2775,
ZANZIBAR