Huduma mbaya Tanzania: Ni Ukoloni wa akili, si uzembe wa mfanyakazi

Huduma mbaya Tanzania: Ni Ukoloni wa akili, si uzembe wa mfanyakazi

Joined
Jul 8, 2024
Posts
5
Reaction score
4
Utangulizi: Tulipoishia mwezi uliopita,

Mwezi uliopita, kama mtaalamu na mzoefu wa utoaji huduma (Customer Experience/CX), niliorodhesha dalili za huduma mbaya Tanzania: vitu kama"chenji na pipi," simu zisizopokelewa, majibu kama"Boss/mkubwa hayupo," na hadithi ya mgeni aliyeambiwa aende akalale ndiyo ajue kama kuna mbu. Hayo yote yalikuwa ni dalili tu/symptoms. Leo nataka kuchoma kidonda kwenye kiini chenyewe: CX Tanzania haijawahi kuwa mbaya kwa bahati mbaya. Hii Imetengenezwa kwa makusudi kabisa kuwa mbaya na sisi wenyewe ,kuanzia viongozi,wataalamu/wasomi, wafanyabiashara na hata wateja tena wenyewe ndio wahandisi wa ubovu huu hata kama hatuko tayari kukiri.

Nataka niseme jambo litakalowakera wengi wenu: kila "Customer Journey Map" tunayoichora kwenye ubao mzuri kwenye ofisi zetu, na kila "Net Promoter Score/kipimo cha Huduma kwa ujumla" tunayojivunia kwenye ripoti ni uongo mtupu ikiwa hatujakiri kwamba muundo mzima wa jinsi tunavyomhudumia mteja Tanzania bado umejengwa juu ya msingi wa kikoloni. Tunaiishi CX kwa maneno ya Kiingereza tu huku roho na akili zetu bado ni zile zile za "bwana na mtumishi."

ifuatayo ni mifano halisi na hoja za msingi za kwanini huduma zetu(CX) zimejengwa kwenye misingi na mawazo ya kizamani/kikoloni;​

1. Tunamthamini Mteja Kwa Rangi ya Ngozi na Lafudhi, Si Kwa Thamani Yake

Kwa uzoefu wangu katika taaluma ya CX, wateja hutofautishwa kwa mahitaji na thamani ya kibiashara yani CLV(Customer Lifetime Value) kamwe si kwa sura,rangi,jinsia,umri ,elimu n.k. Lakini nenda mwenyewe ukajionee: ingia hoteli ya kitalii au mgahawa wa kifahari ukiwa umevaa kawaida na kuzungumza Kiswahili, kisha rudi saa moja baadaye ukiwa na rafiki wa kigeni/a foreigner. Utaona tofauti kubwa sana, yaani sauti nyororo zaidi kwa mgeni, tabasamu pana zaidi, uvumilivu wa hali ya juu na maneno mazuri kama “ngoja niangalie namna nyingine ya kukusaidia” Njoo kwa mzawa sasa ,kuna kaukavu flani, dharau na maneno kama"hatuna" ya moja kwa moja,ki ukweli ni hali ya kutisha sana kwenye huduma zetu na kibaya zaidi watu wengi wanaona hali hii kama kawaida tu.

Watanzania hebu tuwe wakweli: hii si CX kabisaa, huu ni ubaguzi wa rangi uliovishwa koti la "huduma bora kwa wateja." Tunawahudumia wageni kama walivyokuwa wakihudumiwa mabwana wa kikoloni na tunawahudumia wenzetu kama walivyokuwa wakihudumiwa "wenyeji" enzi hizo kwa dharau, ukavu na hisia ya "wewe si muhimu sana." Kama mtaalamu wa CX, hii inaniumiza zaidi ya jambo lolote lile, kwa sababu inamaanisha tunapoteza mabilioni ya thamani ya wateja wa ndani kwa sababu tu ya sumu ya kiakili tuliyoirithi bila kuiuliza.
2. Lugha Yetu Wenyewe Imekuwa Alama ya Udhalilishaji Mbele ya Kaunta za watoa huduma

Kipimo mojawapo cha CX ni tone of voice yani jinsi biashara inavyozungumza na mteja. Nenda benki, ofisi ya serikali au kampuni kubwa za mawasiliano: mteja anayeongea Kiingereza chenye lafudhi "sahihi" hupata heshima ya papo hapo anaitwa "Sir/Madam," anasaidiwa haraka, makosa yake yanasameheka kirahisi. Yule anayeongea Kiswahili safi cha mtaani, hata akiwa na tatizo lile lile, anaonekana "mtu wa kawaida tu".

Kwa uzoefu hili si tatizo dogo la mawasiliano ni ushahidi kwamba bado, miaka zaidi ya sitini baada ya uhuru, tunaamini kimya kimya kuwa lugha ya mkoloni inatoa heshima na lugha yetu wenyewe ni alama ya udhaifu. Kampuni yoyote inayodai "tunaweka mteja kwanza" lakini bado inambagua mteja kwa lugha anayozungumza, inadanganya na ninakataa kabisa kuita hio "huduma bora."​

3. "Boss/Meneja/Mkubwa Hayupo" Ni Utumwa Uliovishwa Suti

Nguzo kuu ya CX duniani kote ni kumjengea uwezo na kumpa mamlaka mfanyakazi wako anayepokea/kukutana na wateja mara kwa mara(frontline empowerment) ili kutatua tatizo la mteja papo hapo. Tanzania, bado tumejenga mifumo inayomfanya kila mfanyakazi kuwa "mtumwa wa maagizo" yani mfanyakazi hawezi kuamua, hawezi hata kuhurumia lakini pia hawezi kutenda bila kibali/ruhusa ya "mkuu/mkubwa/boss." Nafikiri mnapata picha kamili ya muundo wa kiutawala wa kikoloni ambao kwa kipindi kile Bwana Shauri au Mkuu wa Kitengo ndiye pekee mwenye sauti na wengine wote ni watekelezaji tu wasio na akili ya kuamua.

Tunapiga kelele kuhusu utatuzi wa papo hapo na waharaka "First Contact Resolution" kwenye semina za CX, huku tukijua wazi kuwa wafanyakazi wetu hawana hata ruhusa ya kumwambia mteja "pole, nitakusaidia sasa hivi" bila kupiga simu kwa mtu mwingine kwanza. Tunamfunga mfanyakazi minyororo ya kiutawala kisha tunashangaa kwa nini mteja anaondoka akiwa amekasirika.​

4. Tunamdharau Mteja kwa Sababu Tunajua "Hana Pa Kwenda"

Msingi mwingine muhimu wa CX duniani kote ni ushindani/competition, yani biashara inapambana kumridhisha mteja kwa sababu inajua ana chaguo la kuondoka na kwenda sehemu nyingine. Lakini njoo kwa wafanyabiashara wengi wa Tanzania,wao wanaendesha huduma kwa mantiki ya kikoloni: "atarudi tu, ana wapi pa kwenda?"ndo yale ya “we build they will come” Hii ni fikra ile ile aliyokuwa nayo mkoloni kuhusu mtawaliwa kwamba hana namna nyingine ila kunyenyekea, hivyo hakuna sababu ya kumheshimu.

Ndiyo maana biashara nyingi Tanzania hazioni CX kama uwekezaji wa kimkakati bali kama "gharama isiyo ya lazima" kwa sababu bado tunaamini kimya kimya kuwa mteja wetu ni "raia" asiye na uwezo wa kuasi, si "mfalme" mwenye uwezo wa kuhama.
5. Elimu Yetu Inatuzalishia Wafanyakazi wa CX Waliolelewa Kunyamaza

Sitaki kuligusa hili kwa upana, lakini kitaaluma ni lazima nikiri: mfumo wetu wa elimu na malezi hutufundisha "kunyamaza mbele ya mamlaka" kabla hata hatujaanza kazi. Mfanyakazi aliyefunzwa tangu shuleni kutohoji mwalimu, hawezi ghafla kuwa na ujasiri wa "kumhoji" mteja kwa lengo la kumtatulia tatizo au kumpinga msimamizi wake pale anapoona kosa. Tunatengeneza wafanyakazi wa CX walio na akili ya kutii, si akili ya kutatua. Hili si mjadala wa jumla wa elimu ni tatizo la moja kwa moja la CX training design linalohitaji ufumbuzi wa kitaaluma, si wa kimaadili tu.​

Hitimisho La Muda: Tunaendelea Kuabudu Mkoloni Kwenye biashara zetu

Tuwe wakweli: Customer Journey Mapping, customer satisfaction, Net Promoter Score, Voice of Customer na zana nyignine zote za kisasa za CX zitabaki ni mapambo tu kwenye karatasi ikiwa hatutakiri kwamba tunachohitaji si zana mpya, bali ukombozi wa kiakili. Hatuwezi kudai tunajenga CX ya kisasa huku roho na akili zetu za kuhudumia wateja bado zimefungwa minyororo ya enzi za ukoloni na hatuwezi kudai tunajenga "uchumi wa dola trilioni moja" ifikapo 2050 huku CX ikiwa bado ni jambo la pembeni kwenye mipango yetu ya kitaifa.

Wiki ijayo, Sehemu ya Tatu, nitakuja na CX Training model&road map inayolenga kuvunja mzunguko huu wa kiakili kuanzia jinsi tunavyoajiri, jinsi tunavyofundisha, hadi jinsi tunavyowapa mamlaka wafanyakazi wetu wa mstari wa mbele. Lakini leo, nataka jibu gumu kutoka kwenu:

Je, unakubali kwamba wewe binafsi kama mfanyakazi, meneja au hata mmiliki wa biashara umewahi kumhudumia mzungu au mgenii yeyote vizuri zaidi ya mzawa bila hata kujitambua? Na kama jibu ni "ndiyo," tunaendeleaje kuita hilo "utamaduni wetu wa ukarimu" wakati kwa uhalisia ni mabaki ya akili tuliyoachiwa na mkoloni? Na muhimu zaidi: kwa nini nchi yetu haijawahi kuiweka CX kwenye meza ya mipango ya kitaifa kama Mauritius, Morocco na Singapore walivyofanya ,je, ni kwa sababu hatujaiona thamani yake ya kiuchumi au ni kwa sababu bado hatuamini mteja wetu wa ndani anastahili hilo?

Nakaribisha maoni yenu hasa kwa wale wafanyabiashara au wafanyakazi wanaosimamia huduma za wateja moja kwa moja.

(Itaendelea wiki ijayo — Sehemu ya Tatu: Kujenga CX Training Model&roadmap ya Kitanzania Inayovunja Fikra za Kikoloni).
Cheers​
 
Back
Top Bottom