KUTOKA KWA : MSANII, JOTO LA MOTO.
Nimekaa na kuwaza, kuhusu huyu jabali.
Ni mengi ametufunza, kwa tungo zenye akili.
Inabidi kuitunza,heshima ya huyu nguli.
Tumuenzi Marijani,ni jabali la muziki.
Hebu tuje na mpango,kazi zake tuzienzi.
Tusambaze na mabango,tuwajuze wanafunzi.
Kwamba aliishi bongo, gwiji fundi wa utunzi.
Tumuenzi Marijani,ni jabali la muziki.
Kongole kwa Waandishi,mfanyao kumbukizi.
Kwa picha na maandishi,dumisheni hiyo kazi.
Sifa zake zinaishi,zisomwapo zake nyuzi.
Tumuenzi Marijani,ni jabali la muziki.
Wasanii wa kisasa,yawapasa kukumbuka.
Maneno kama msasa, ujumbe aliusuka.
Alionya na kuasa, kwa tungo zisizochoka.
Tumuenzi Marijani,ni jabali la muziki.
Aliimba ya siasa, furaha mapenzi pia.
Tungo tamu kama pesa, thamani kama rupia.
Kisa baada ya kisa,jabali alitupia.
Tumuenzi Marijani,ni jabali la muziki.
Nitazitaja baadhi,vijana mzikumbuke.
Nyimbo kali zenye hadhi,aliimba na wenzake.
Zenye ya kwetu mahadhi,hakumuiga Maneke.
Marijani wa Rajabu, heshima yake apewe.
Naanza na Mwanameka,wimbo tuliusikia.
Dada mwingi wa vibweka,Musa kamchepukia.
Kidume kaweweseka,ndoa haikubakia.
Marijani wa Rajabu, heshima yake apewe.
Akaja kwa Matilida, wimbo ulijieleza.
Ulezi ulimshinda, binti aliyeteleza.
Starehe alipenda, mwana akatelekeza.
Marijani wa Rajabu, heshima yake apewe.
Alimuita Mayasa,ushauri akapewa.
Aache mwili kutesa, ngozi yake kuchubuwa.
Asichome bure pesa,uzuri ni kuzaliwa.
Marijani wa Rajabu, heshima yake apewe.
Nguli pia aliimba, kuhusu Masudi nunda.
Mwizi fundi wa kukomba,kijana aliyepinda.
Jabali alimuimba, mpaka Sudi akasanda.
Marijani wa Rajabu, heshima yake apewe.
Alikumbusha wanywaji, pombe sio chai ile.
Wasiinywe kama maji, walewe kama Masele.
Wanywe wanachohitaji,sio bilauri tele.
Tuziite Marijani, tuzo zetu za muziki.
Na Wasanii wa leo,yawafaa mfahamu.
Muziki sio wa leo, zilikuwepo awamu.
Kabla kuwepo video, tulifaidi utamu.
Tuziite Marijani, tuzo zetu za muziki.
Kiba Fidi Dayamondi,Mpoto na Jide dada.
Simtafuti mshindi, nawaita kwenye mada.
Hiki ni chenu kipindi,semeni bila husuda.
Tuziite Marijani, tuzo zetu za muziki.
Wasanii wa miaka, mlikuwa enzi zile.
Makassy Zoro Bitchuka, Kitime na Jumbe yule.
Maoni yenu twataka,Mumtaje mteule.
Tuziite Marijani, tuzo zetu za muziki.
Nimefika ukingoni, ila ujumbe ubaki.
Baraza na wizarani,ushauri muucheki.
Hebu mje hadharani,mawazo muyaafiki.
Tuziite Marijani, tuzo zetu za muziki.