Ozark,
Nilifanya mhadhara University of Iowa, Iowa City mwaka wa 2011 na nilipewa takwimu za CIA kuhusu ''Tanzania Religious Distribution.''
Takwimu hizi zinaonyesha kuwa Waislam ni ''minority'' Tanzania.
Jibu langu nililotoa mfano wake ni kama huo hapo chini:
"Mtu akikuwekea mbele ya macho yako fimbo iliyopinda na akaitangaza kote kuwa fimbo hiyo imenyooka jibu lake ili lieleweke vyema ni kuweka fimbo iliyonyooka pembeni ya fimbo iliyopinda.
Macho hayadanganyiki.
Clip imeonyesha kuwa Tanganyika ni nchi ya Kikristo.
Zanzibar haina ubishi kuwa ni nchi ya Kiislam lakini ili kunogesha kilichokusudiwa imewekwa picha ya kanisa.
Wamishionari wamefika Tanganyika miaka ya 1800 na kufuatiwa na wakoloni na wamewakuta Waislam na Uislam uko zaidi ya miaka 1000.
Hapa tunacheza na picha na sauti ya fimbo iliyonyooka dhidi ya fimbo iliyopinda.
Mmishionari Johann Krapf kafika Vuga kwa Chief Kimweri mwaka wa 1848 kamkuta anatawala raia Waislam na wanajua kuandika, kusoma na kuhesabu.
Tunaweka picha ya Kimweri kavaa kanzu, juba na kapiga kilemba yuko katika baraza lake anaamua kesi akiandika kwa herufi za Kiarabu.
Krapf kaukuta Uislam Zanzibar na kaukuta Uislam Milima ya Usambaa.
Wajerumani wamefika Kilwa wamewakuta wenyeji wake wote Waislam na kukutana na upinzani mkali kutoka kwa Waislam wakiongozwa na Hassan Omari Makunganya.
Tunaweka picha ya Msikiti Mkuu wa Kilwa na picha ya Makunganya aliyenyongwa na Wajerumani mwaka wa 1895.
Tunaweka pia picha ya mnara wa kumbukumbu ya Waislam wa Kilwa walionyongwa na Wajerumani kwa kunyanyua silaha kuipigania nchi yao.
Vita vya Abushiri na Wajerumani viliitikisa utawala wa Wajerumani.
Abushiri alinyongwa Pangani mwaka wa 1889.
Abushiri kabla ya kifo chake alifika Kalenga kwa Mtwa Mkwawa na kumsilimisha Mkwawa.
Mkwawa akachagua jina la Abdallah na akamfunza kusoma na kuandika.
Viongozi hawa wawili walikuwa maadui wakubwa wa Wajerumani.
Barua alizoandika Mtwa Mkwawa kwa herufi za Kiarabu zipo Mkwawa Museum, Kalenga.
Leo Manispaa ya Iringa ina misikiti 25 yote inasaliwa Ijumaa na Mkoa mzima una misikiti 80.
Zinawekwa picha ya Mtwa Mkwawa na kizazi chake katika utawala wa Wahehe hadi leo pamoja na picha za misikiti iliyoko Iringa.
Huu ndiyo urithi alioacha Mtwa Mkwawa aliyesilimishwa na Abushiri bin Salim.
Mwaka wa 1905 Vita Vya Maji Maji vikaanza dhidi ya Wajerumani hadi mwaka 1907.
Hapa kuna historia kubwa ya majemadari 67 wa vita hivi walionyongwa na kuzikwa katika kaburi moja la halaiki isipokuwa Nduna Abdulrauf Songea Mbano.
Inawekwa picha yake Nduna Abdulrauf Songea Mbano.
Historia yake inaelezwa kuwa huyu ndiye Songea Mbano ambae waandishi wa historia ya Tanganyika wanakwepa kuandika jina lake la Kiislam "Abdulrauf," kwa hofu ya kuidumisha historia ya Uislam Tanganyika.
Halikadhalika wanakwepa kuandika jina la mwanamke pekee aliyenyongwa na Wajerumani kwa kuwa mmoja kati ya majemadari wa vita ile Bi. Khadija bint Mkomanile.
Waandishi wa historia ya Tanganyika wanamtaja kwa jina moja tu "Mkomanile."
Wanataka kufifilisha historia ya vita hivi na Waislam.
Ikiwa tutakaa kimya bila kujibu clip kama hizi hakika dunia itaamini kuwa Tanzania ni nchi ya Kikristo.
Historia ya uhuru wa Tanganyika iligeuzwa ikawa historia ya Julius Kambarage Nyerere.
Historia ya TANU ikawa historia ya mtu mmoja.
Hili lilifanikiwa kwa kuwa tulikaa kimya lau kama walikuwapo wazalendo wenyewe walioupigania uhuru kwa hali na mali zao.
Sasa tueleze harakati za uhuru wapi zilianzia.
Tunaweka picha ya Dictionary of African Biography (DAB).
Kinawekwa kipande kifupi kinachomweleza Dr. Kwegyir Aggrey (1875 - 1927) kisha ndani ya Kamusi hilo hilo tunatoa na kumwekea mtazamaji wa clip yetu kipande kifupi cha Kleist Abdallah Sykes (1894 - 1949).
Wazalendo hawa waliotajwa ndani ya Kamusi hilo tunaeleza hawamo katika historia rasmi ya Tanganyika.
Mazungumzo kati ya Waafrika hawa wawili Dar-es-Salaam mwaka wa 1924 ndiyo yalisababisha Kleist kuunda African Association mwaka wa 1929 kisha kuunda Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika (Umoja wa Waislam wa Tanganyika) mwaka wa 1933.
Vyama vyote hivi viwili vilitawaliwa na Waislam.
Kwa nini ilikuwa hivi?
Swali hili atajibu mtazamaji.
Vyama hivi viwili ndivyo vilivyowasha moto wa utaifa kwa kuunda TANU mwaka wa 1954 kupigania uhuru wa Tanganyika Waislam wakiwa mstari wa mbele.
Tunaweka picha ya wanawake Waislam katika kupigania uhuru wa Tanganyika.
Tunaweka picha za masheikh walioongoza kupigania uhuru umoja Watanganyika.
Hawa wakaja na kauli mbiu: "Uhuru na Amani."
Kwa kuhitimisha tutauliza.
Huu wingi wa Wakristo Tanganyika umeanza lini?
Kwa nini madai haya hayakuwapo miaka yote na katika historia ya nchi hii wakati wa kupigania uhuru wa Tanganyika?
Iweje wingi huu uzuke ghafla miaka hii tena bila kufanya sensa na kuweka kipengele cha dini?
Huu Ukristo unaopigiwa chapuo leo nini sababu yake?
Hakuna nchi duniani iliyokombolewa kwa amani au kwa kupigana vita ikawa wapigania uhuru wake ni kutoka jamii ndogo yenye watu wachache.
Halikadhalika hakuna nchi iliyoingia katika kudai uhuru wake ikawa waliokuwa mstari wa mbele kudai uhuru ni watu kutoka jamii iliyokuwa haina uongozi katika wingi wa wananchi ndani ya harakati hizo.
Tafuta dunia nzima hili hutolipata."
Nilipomaliza kujibu ukumbi mzima ulikuwa kimya kabisa.
Mkuu wa African History Northwestern University, Jonathon Glassman alinifata na kuniomba hapo hapo twende chuoni kwake tukafanye mjadala kama huu.
Nilikubali mwaliko na nikazungumza Northwestern University katika Ukumbi wa Eduardo Mondlane.