Sasa hamtaki kukubali kuwa nchi yenu ni maskini? Waziri Mkuu kasema sisi ni "maskini sana" halafu mnakataa; mnataka Rais atumie usafiri gani kuendana na hadhi yake kama Amiri Jeshi Mkuu, na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi. Hawezi kusafiria Corolla!
Lengo la viongozi wengi wa Afrika kumng`oa mkoloni halikuwa kwa sababu walikuwa na uchungu wa kuboresha maisha ya wananchi wao bali walikuwa wamejaa hamu ya kuishi maisha ya mkoloni aliyokuwa akiishi Ikulu.
Hivyo waliwatimua magavana wa kikoloni ili wao wakalie zile ikulu walizokalia wakoloni,watembelee magari yenye hadhi na heshima waliyotembelea magavana hao na waishi maisha yaleyale ya kifahari kama mtawala wa kikoloni alivyoishi bila kujali wananchi walalahoi kama vile gavana mkoloni alivyokuwa hajali walalahoi.
Tofauti ya utawala wa kikoloni na wa kiafrika tofauti yake ni ngozi tu.Ikulu ya zamani alikuwepo mzungu mwenye nywele nyeupe wakati ikulu ya sasa yuko ngozi nyeusi.Lakini huwezi kuwatofautisha yupi mkoloni na yupi si mkoloni kwa kuangalia maisha yao,magari wanayotembelea,misafara inayowasindikiza na wanavyoshindwa kuwajali wananchi. Karibu wote wanafanana tu.
Labda Waziri mkuu Pinda ndiye yuko tofauti kidogo labda kwa kuwa anatoka kabila maskini dogo la wakonongo ndiyo maana hana makuu na anapenda kuwa karibu na watu wa hali ya chini na kujitambulisha nao na kusikiliza na kujali kero zao, tofauti na wenzie wengi ambao hupenda kujitambulisha kama sehemu ya matabaka ya watu wa juu waendesheo maisha KI-BMW na KI-BENZI kama alivyofanya gavana mkoloni waliyemtimua walipodai uhuru ili wakalie wao nao wafaidi kama yeye alivyofaidi.
Nchi nyingi za kiafrika haziendelei kwa sababu kilichobadilishwa ni rangi ya mtawala. Badala ya mtawala mkoloni mzungu sasa nchi za kiafrika zina watawala wakoloni weusi.Lakini vitendo vyao,staili za maisha yao ni zile zile hazina tofauti na za watawala wakoloni.Kodi zinazokusanywa lengo kuu kama ilivyokuwa wakati wa mkoloni ni kwa ajili ya kugharimia utawala ikiwemo mishahara,posho nono na magari ya kifahari ya watawala.Pia kazi ingine ni kujenga barabara nzuri ili magari yao ya kifahari yasiumie yakisafiri na kumrusha rusha mheshimiwa mtawala akajisikia vibaya.Masuala mengine ya maendeleo hilo si jukumu la serikali ni la mwananchi mwenyewe ajiletee maendeleo yake.Wakati wa mkoloni jukumu la kujiletea maendeleo lilikuwa ni la mwananchi mwenyewe na baada ya uhuru jukumu la kujiletea maendeleo ni la mwananchi mwenyewe.Hivyo hakuna tofauti ya mtawala kiutendaji kati ya mkoloni wa zamani na sasa.
Kazi ya mtawala iwe ni wa kikoloni au wa sasa kazi yake kubwa ni kuzunguka kwenye BMW na BENZ zake akiwapungia mikono wananchi waliochoka kwa umaskini na kukata tamaa waliojipanga barabarani kwa kulazimishwa na watawala wa maeneo kujipanga barabarani kwa masaa mengi kusubiri kushangilia misafara ya mtawala ya Mi- BMW na Mi-BENZ inayopita kwa kasi na mbwembwe nyingi za ving`ora,mikao ya kininja kama ya sinema ya wanausalama,ma-mabaunza n.k inapopita mbele yao ili mheshimiwa mtawala na waandishi wake wa propaganda waandike kuwa alishangiliwa kila alikoenda na misafara mirefu ya wananchi wanaompenda ambao walimgojea kwa hamu kwa masaa mengi ili wamshangilie mtawala wao mpendwa aliyekuwa kafichwa kwenye gari lenye usalama wa hali juu lililonunuliwa kwa mamilioni ili kuwazuia wenye wivu wanaomwonea gere mtawala anavyofaidi raha kuliko wao wasimshambulie kwa hasira za njaa yao na gere yao.
Nchi zetu bado ziko chini ya wakoloni.Kabla ya uhuru ilikuwa ni ukoloni PART ONE sasa hivi baada ya uhuru ni Ukoloni PART TWO. Ndiyo maana kiongozi bila kutembelea BMW,BENZ uongozi wake unakuwa haujakolea au kukamilika sawasawa.