Halisi
JF-Expert Member
- Jan 16, 2007
- 2,802
- 614
Ubia upo, tuwajue wabia
Jenerali Ulimwengu
Julai 15, 2009
(Baada ya kuomboleza hasara kubwa iliyotupata kutokana na kifo cha ghafla cha Haroub Othman, sasa tuendelee na hoja yetu).
Katika makala ya mwisho nilijadili jinsi ambavyo watawala wetu wamekumbwa na kile nilichokiita mbano wa zama (time warp) unaowafanya waamini kwamba wanaweza kutenda kama Mwalimu Nyerere katika utawala wake, bila hata hivyo kufuata nyayo za Nyerere katika masuala makuu aliyoyasimamia.
Dalili mojawapo ya kile nilichokiita u-Nyerere-nusu ni yale matamshi niliyowahi kuyasikia mara tatu kutoka kwa watawala wetu wakuu. Mara ya kwanza niliyasikia kutoka kwa Rais Benjamin Mkapa, na mara ya pili nimeyasikia kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete: Urais Wangu Hauna Ubia.
Ukitazamwa kwa haraka msemo huu hauna tatizo. Ni kweli kwamba raia wa Tanzania wanapomchagua mtu kuwa rais wao hawataraji kwamba ataingia ubia na mtu mwingine ambaye kwa hakika watakuwa hawamjui. Katika mpangilio wa kikatiba, labda ni makamu wa rais ndiye anaweza kuonekana kama mbia kwa maana alikuwa mgombea mwenza, na mwenza ni aina ya mbia.
Isitoshe, kama ambavyo nilikwisha kuonyesha huko nyuma, Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania inamfanya Rais wa Jamhuri kuwa na madaraka makubwa kiasi kwamba mawaziri ni kama watumishi wake, washauri wasiokuwa na uwezo wa kuamua jambo lo lote isipokuwa kwa kuelekezwa na Rais. Anaweza kufanya lo lote: kumfukuza ye yote kati ya mawaziri wake (Rais Mwinyi alifukuza baraza zima mwaka 1990); kubadilisha majina na miundo ya wizara; kuamua wizara gani ifanye nini na nini isifanye na kadhalika.
Mbali na baraza la mawaziri, Rais anaweza kukataa kutia saini muswada wa sheria, na akikataa unabaki kuwa muswada tu, na anaweza kuvunja Bunge katika mazingira fulani. (Kwa njia fulani ambayo si rahisi kuielewa Rais pia ni sehemu, nusu, ya Bunge!)
Pia ndiye anayeteua msururu mrefu wa watendaji na wakuu wa watawala kutoka ngazi ya Taifa hadi wilayani, hata kama mara nyingi jina lake linatumiwa na wajanja kujipachikia watu wao halafu wananchi wanaambiwa, Rais kamteua fulani.
Yote haya, na mengine mengi sana, yanadhihirisha ukweli ule, kwamba rais wetu hana mbia; yeye ndiye Bwana Mkubwa, Alfa na Omega nchini. Huo ndio ukweli.
Lakini si ukweli wa kusherehekea, wala si jambo la kujivunia. Ni jambo la kutafakari kama tatizo na kulitafutia ufumbuzi, baada ya kutambua madhara yake. Nilikwisha kueleza katika makala zilizotangulia kwamba mpangilio tulo nao ni ule tulioachiwa wakati tunapata Uhuru wa Tanganyika, na kwa kiasi kikubwa ni utaratibu uliowekwa na Waingereza.
Leo hii hautufai tena. Wala tusijidanganye kwa kusema kwamba tumekuwa tukifanya marekebisho ya Katiba ya mara kwa mara na kuweka sawa yote yaliyotakiwa kuwekwa sawa (viraka vinavyozungumziwa). Hili si kweli kwa sababu masuala ya kimsingi ya falsafa na nadharia ya utawala bora hayajaguswa, na mojawapo linalojitokeza ni hili linalosikika kama Urais Wangu Hauna Ubia.
Haiwezekani kuendesha nchi kubwa kama Tanzania, kubwa kwa eneo, kubwa kwa wingi wa watu na kubwa kwa wingi na ugumu na uzito wa matatizo, bila ubia. Haiwezekani kumrundikia mtu mmoja madaraka ya kila aina na katika ngazi zote nchini halafu ukamwacha afanye kazi zake bila ubia.
Hivi, hata chama chake kilichomweka madarakani hana ubia nacho? Ni kweli, najua, na nimekwisha kulijadili, dhana ya chama katika nchi zetu haina maana kubwa, na chama kimebakia ni chombo cha kuvukia (aina ya pantoni) kwenda kwenye madaraka ya dola, basi. Lakini si ungelidhani kwamba hilo ni tatizo la kutatuliwa na si jambo la kujigamba nalo?
Kila mtu anayetaraji kufanya kazi kubwa, kwa mfano ya kuendesha nchi kama hii, atahitaji kuwa na wabia wengi, tena wabia makini, kama anataka kufanikisha kazi yake. Aidha ni bora ubia huo na wabia hao wakajulikana wazi, na ikajulikana ubia huo umeundwa ili ufanikishe shughuli gani.
Hili lisipofanyika kwa uwazi, na kama kauli itaendelea kuwa ile ile ya Sina Ubia na Mtu tutakuwa tunapigwa changa la macho ili tusijue ni nini kinaendelea, kwa sababu ubia utakuwapo tu, tutake tusitake. Ni kwamba utakuwa ni ubia uliojengeka kizani na unaoendelezwa kwa kificho, lakini ubia utakuwapo.
Wananchi hawataweza kujua kwa uhakika ubia huo ni wa mtawala wao na watu gani, na mara nyingi watakuwa wakipashana habari hizo kwa minongono, uvumi, tetesi na umbeya.
Kwa mfano Rais atafanya jambo linaloonekana jipya na la kushangaza kidogo, labda likiwa linatoa maslahi na faida kwa kundi fulani la raia. Ili kueleza ni kwa nini Rais wao kafanya hivyo, raia wanaweza kuanza kuunganisha kitendo cha mtawala wao na uhusiano wa ki-ukwe uliopo kati yake na familia fulani, au urafiki wa utotoni na mtu fulani, au kitu cho chote kingine wanachoweza kukikisia na kukifanyia hesabu za mbili ongeza mbili.
Haya ninayoyasema hapa si mambo ya kudhania tu, wala sikuyaota; yametokea hapa hapa nchini, na mfuatiliaji wa masuala haya atayatambua. Wakati Mwalimu Nyerere anasema, katika miaka ya 1990, kwamba kiongozi asiwe mtu wa kulala kitandani na mkewe, na mkewe akamnongoneza neno, na kesho yake neno hilo likawa ni sera ya serikali, alikuwa analizungumzia hili ninalolisema.
Najua wako watu waliodhani kwamba Mwalimu alikuwa akimsema mrithi wake aliyekuwa madarakani wakati huo, Mzee Ali Hassan Mwinyi, lakini binafsi naamini alikuwa anajaribu kueleza maamuzi yanayofanyika kutokana na mchakato usiokuwa rasmi, uwe ni kati ya mume na mke, ndugu na ndugu, rafiki na rafiki, shemeji na shemeji, mkwe na mkwe, au mshikaji na mshikaji.
Muhimu kutambua hapa ni kwamba katika mzingira yetu, mtawala amelimbikiziwa majukumu mengi ambayo yeye peke yake hawezi kuyamudu. Aidha, kwa jinsi mambo yalivyo, ni kwamba yeye ndiye Qasim, mgawaji wa riziki kwa kugawa nafasi za ajira nono, na wakati mwingine kuamua nani apate kandarasi nono na nani aruhusiwe kufanya biashara kubwa.
Tunalo kabila kubwa sana la watu ambao maisha yao yote yamekuwa ni ya kutegemea kuajiriwa katika nafasi za serikali, mashirika yake au ndani ya chama-tawala. Hawa wote wanalazimika kujiwekea mazingira ya kukubalika na kupendeka kwa Bwana Mkubwa siku zote, na ikiwa wanaweza kuunga urafiki na watu wanaodhaniwa kwamba ndio washikaji wa Mkubwa, watafanya hivyo.
Kati ya wasaka vyeo na wasaka kandarasi na wale wanaodhaniwa kwamba wako karibu na kiti cha enzi, kimezuka kiwanda cha mahusiano ya kifisadi ambacho ndicho kinachukua nafasi ya asasi za uongozi wa nchi.
Hali hii inakuwa haiepukiki katika mazingira ambamo asasi kama chama cha siasa kinachojiita chama tawala hakina nguvu za kifalsafa, kiitikadi wala kisiasa kuweza kuisimamia serikali au kumwelekeza Bwana Mkubwa katika kazi yake.
Unapowadia wakati wa uchaguzi, kiwanda hiki kinaingia katika gia kubwa kuhakikisha kwamba Bwana Mkubwa, chama chake na watu wake wanabakia, au wanaingia, madarakani. Zinakusanywa fedha kutoka kila mahali isipokuwa kule kunakokubalika kihalali.
Kwa kuwa hakuna ubia unaokubalika kwamba upo, na ubia uliopo ni wa kificho, ukusanyaji wa fedha za kampeni unafanyika, kama mambo mengine, katika kificho, na wananchi hawelewi vyema ni wapi fedha hizo zimetoka, ni akina nani waliochanga na maslahi yao ni yapi katika uchangaji huo.
Haya nayo sikuyazua, ni mambo yanayojulikana na ambayo yatatuathiri kwa muda mrefu ujao. Neno la Kiingereza 'opacitylinaeleza dhana yangu ya msingi, kwamba kila kitu ni opaquemambo mengi yanaendeshwa katika kiza, na ni machache mno yanayoonekana kwa uwazi.
Msomaji akirudi nyuma kidogo atakumbuka nilivyoelezea watu wanaoingia katika serikali, tuseme Baraza la Mawaziri, kwa sababu wanatakiwa wamsaidie Rais katika kuendesha nchi. Itakumbukwa vile vile nilivyoeleza jinsi wanavyojitahidi sana kutokuwa na fikra zao, na badala yake wanasubiri busara za Bwana Mkubwa, na wao wanakuwa watekelezaji - aina fulani ya matarishi.
Haya ndiyo matunda ya Urais Wangu Hauna Ubia, na matokeao yake ni serikali kukosa mwelekeo, kuhaha kila siku toka jambo moja hadi jingine, na hatimaye kumfanya mtawala anayeondoka madarakani kuondoka na kila kitu alichokuwa akikisimamia (kama alikuwa nacho) wakati akiwa madarakani. Ndiyo yaliyotokea kwa Nyerere (yeye alikuwa nacho), na ndivyo yatakavyotokea kwa wengine waliomfuata.
Wakati tukisubiri hayo kujidhihirisha, wale wanaopewa angalau vijinafasi vya uongozi watakuwa wanahangaika kwa nguvu zao zote kutengeneza viota vyao, kukusanya fedha za kampeni zijazo, kujenga majumba, kununua magari, mashamba na hisa za makampuni na kupokea rushwa kushoto, kulia na kati, yote hayo wakitumia nafasi walizopewa katika utawala. Hapo hakuna tumaini la kujenga uongozi wa aina yo yote; tunachojenga ni kundi la watu, kabila zima, watu wanaoishi kwa ajili ya leo.
Haishangazi, basi, kwamba hakuna jambo linaloashiria uendelevu. Sana sana watawala wetu wakitaka kuangalia mbali, hawaendi zaidi ya miaka iliyosalia kabla ya uchaguzi ujao. Januari 2006 ilibaki miaka mitano; leo imebaki miezi 18. Huo ndio upeo.
Wala haishangazi kwamba tunazidi kushuhudia jinsi umasikini unavyozidi kuwatesa watu wetu. Pasipokuwa na ubia wa wazi, hakuna njama inayodumu ya kuleta maendeleo, na badala yake kila mmoja anatafuta maslahi yake ya muda mfupi. Pale panapokuwa na dalili ya ubia, unakuwa ni ubia wa kiushikaji, na huu hauendi masafa marefu, kwani kinachofanyika ni kunyakua, kukwapua, kunyofoa kila kinachoonekana kuwa na maslahi ya sasa hivi.
Hivyo sivyo mataifa yanavyoendelea.
Itaendelea
jenerali@gmail.com
Source: Ubia upo, tuwajue wabia
Last edited by a moderator: