Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) limesema tukio lililotokea katika ndege yake aina ya Airbus A220-300 iliyokuwa ikitoka Dar es Salaam kwenda jijini Mbeya kupata hitilafu kwenye moja ya injini zake kuwa ni dogo na la kawaida.
Ndege ya shirika hilo namba 106 iliyoanza safari saa 12 jioni Jumamosi Februari 24, mwaka huu, ililazimika kukatisha safari na kurejea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam baada ya injini yake moja kupata hitilafu na kusababisha moshi ndani ya ndege.
“Kuna injini moja ilipata joto sana na ikawa na mafuta mengi ndiyo yaliyosababisha moshi ambao, uliingia kwenye mifumo ya hewa (AC) na ndiyo sababu moshi huo ukawafikia abiria sio ndege kuungua moto kama ilivyoelezwa,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Mhandisi Ladslaus Matindi alipozungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi, Februari 29, 2024 jijini Dar es Salaam.
Kauli hiyo ya Mhandisi Matindi inakuja baada ya Mwananchi kuripoti tukio la injini ya ndege hiyo kupata hitilafu na kusababisha taharuki kwa abiria waliokuwemo ndani ya ndege hiyo.
Baadhi ya abiria waliozungumza na Mwananchi, walieleza kuwa moshi huo ulisababisha taharuki, lakini baadaye marubani na wahudumu wa ndege walifanikiwa kudhibiti na hali kurejea kawaida.
Hata hivyo, ndege hiyo ililazimika kurejea Dar es Salaam na baada ya saa chache baadhi ya abiria waliendelea na safari huku wengine wakibadili tarehe ya safari.