STORY: INNOCENT KILLER (THE REVENGE)
STORY WRITER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP : 0621567672
EMAIL:
thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+
SEHEMU YA 34
SONGA NAYO............
“Huko mbweni ni baridi sana hauhitaji hata feni”, ni moja ya mistari maarufu sana ambayo watu wengi hupenda kuitaja pale wanapokuwa wanaitaja Mbweni, huko ndiko kulikuwa nyumbani kwa Lusubilo Mtindiga, familia yake yote ilikuwa ikiishi huko na huko ndiko kulikuwa nyumbani kwake ambako mara nyingi asipokuwa na majukumu ya kazi alikuwa akipatikana, Jaiwelo Mkupi Makubilo alihitaji Kwenda huko baada ya kutoka Ikulu ili akakutane na rafiki yake ambaye walikuwa wanaitana ndugu wa damu ili akamueleze ni mambo yapi ambapo alionekana kuyajua na akaamua kuyakumbatia kwenye kifua chake bila kuweza kumshirikisha mwenzake huyo, hilo jambo lilimfanya aghafilike sana kwenye moyo wake alihisi mwenzake huyo huenda kuna mambo mengi sana ambayo huwa anamficha na hataki yeye aweze kuyajua kabisa kwenye maisha yake. Baada ya kutoka nje ya Ikulu alipanda kwenye gari na kumtaka dereva wake huyo aondoke haraka sana maeneo hayo, cha ajabu baada ya kufika nje tu alimwambia dereva huyo ashuke kwenye gari na aende kwake siku hiyo alitaka kuendesha mwenyewe lilikuwa ni jambo la hatari sana kumuacha kiongozi wa ngazi ya juu kabisa ya jeshi kufanya jambo la hatari kama hilo kwenye maisha yake lakini hakuwa na namna baada ya kuambiwa kwa ukali sana ikamlazimu kushuka akiwa anasikitika huku akiwa anamuaga bosi wake huyo kwa macho na kwa aina ya spidi ambayo aliondoka nayo pale.
Lusubilo Mtindiga alikuwa kwenye chumba chake cha mazoezi ndani ya chumba chake ambacho kilijengwa kwa vioo tu na kumfanya mtu ambaye angekuwa nje kama kusingefunikwa kitu chochote basi angeshuhudia kila ambacho mtu wa ndani ya chumba hicho angekuwa anakifanya na alikuwa akifanya hivyo makusudi kwa miaka mingi sana, chumba hicho kilikuwa ndani ya uzio mkubwa wa fensi ndefu ambayo pia ilikuwa na ulinzi mkali sana. Akiwa ndani ya chumba hicho alikuwa ameshika Upanga kwenye mkono wake na nguo nyepesi zikiwa kwenye mwili wake, alipenda sana kufanya mazoezi na upanga tangu akiwa kijana mpaka uzee ulikuwa unamnyemelea na kwa mbali kabisa juu ya ghorofa ya pili alikuwa amesimama mwanamama ambaye umri wake ulikuwa umemtupa mkono kiasi uzee ulikuwa unamuita kwa kasi sana, alikuwa kwenye tabasamu pana sana kumuona mwanaume huyo akiwa anafanya mazoezi hapo ni zoezi ambalo amelishuhudia kwa idadi ya miaka mingi sana mpaka leo kila mwanaume huyo alipokuwan anaenda kufanya mazoezi basi ilikuwa ni lazima aache chumba hicho wazi bila kufunika mapazia makubwa ambayo yalikuwa yamewekwa kwa ndani ili kumuwezesha mwanamke huyo kuweza kuona kila kilichokuwa kinaendelea humo ndani.
Akiwa anaendelea kufanya hayo mazoezi ambayo alikuwa anaishia kujisonya mwenyewe kwa sababu kuna vitu alikuwa anatamani kuvifanya ila mwili ulikuwa unakataa kutokana na mifupa kukomaa kupitiliza kulingana na umri Kwenda sana hivyo kuna vitu vilikuwa vinamkera hali hiyo inapo mtokea ila hakuwa na namna, alisikia mlio wa honi ambao ulikuwa unapigwa kwa fujo sana, alisikitika wala hakuhangaika kugeuka kuangalia getini. Geti lilifunguliwa na mtu huyo akaingiza gari lake ndani hata hakukumbuka kulizima alishuka kwa haraka mno akiwa mwingi wa hasira kwenye uso wake, walinzi waliokuwa hapo walikuwa wanampa heshima yake kwa sababu alikuwa ni kiongozi mkubwa mno ndani ya nchi hata hivyo hakujibu salamu ya mtu yeyote yule safari yake ilienda kuishia ndani ya chumba ambacho alikuwa anafanya mazoezi ndugu yake.
“Sijui lini utaacha kuwa kwenye hali kama hiyo kiongozi mkubwa kama wewe haupaswi kuwa namna hiyo utajikuta umefanya maamuzi ya hovyo sana ambayo yanaweza kuleta maafa makubwa kwa vijana wako na kwa taifa pia” IGP aliongea baada ya kumuona mwenzake kaingia kwa hasira sana huku akimrushia upanga ambao ulikuwa umewekwa kwenye ala yake ukutani na mwanaume huyo aliudaka akiwa kwenye suti yake safi.
“Ungekuwa unajali kuhusu hilo usingekuwa mtu wa kuanza kunizunguka mimi” aliongea kwa hasira akiwa anamfuata rafiki yake huyo kwa kasi, mkewe na IGP baada ya kuona shemeji yake kaja hakuendelea kukaa pale alitoka na kuwaacha wanaume hao wapigane, ni mara nyingi huwa inakuwa hivyo pale wanapokutana kwenye mazingira kama yale na yeye huwa hapendi kabisa kushuhudia watu hao wakiwa wanacheza na maisha yao kimasiara sana namna hiyo wakiwa na mapanga ya kweli kwenye mikono yao. IGP alikwepa upanga kwa kujigeuza haraka na kutua nyuma alisogea kwa kasi sana na kumfikia mkuu wa majeshi ambaye aliinama kidogo upanga ukapita juu kidogo ya kichwa chake na kupukutisha nywele kadhaa kichwani.
“Kipi hicho ambacho unasema nakuzunguka ndugu yangu? mbona mimi nawewe hatujawahi kuzungukana kwa lolote” IGP alijibu huku akiuingiza upanga wake kwenye ala yake kwani mwenzake huyo aliutupa chini kwa hasira alizokuwa nazo hakuhitaji waendelee kupigana tena kwa sababu sicho kilichokuwa kimemleta siku hiyo na nje kulikuwa kumepambazuka kabisa na wasakatonge walikuwa wanaendelea na mambo yao kama ilivyokuwa kawaida ya siku zote.
“Nina swali ambalo ni dogo na ni fupi sana ila ni la mhimu sana tena sana nadhani huwa unanielewa ninapokuwa ninaweka msisitizo kwenye mambo yangu”
“Ok uliza unachotaka kukisema”
“Naomba uniambie mkurugenzi wa usalama wa taifa ni nani na kwanini mmeamua kunificha kuhusu hili swala?” baada ya kuongea IGP alimtazama mwenzake huyo bila wasiwasi
“Unamaanisha nini kusema hivyo?”
“MD usitake kupoteza muda kwa jambo ambalo linaeleweka hivi ninavyo ongea nawewe nimetoka kwa mkuu wa nchi nimembana sana aniambie kwanini mtu wa mhimu kama mimi kwenye taifa nafichwa mambo nyeti kama haya halafu rafiki zangu wamekufa? Mimi natakiwa kushirikiana na hao usalama wa taifa kuhakikisha mhusika anakamatwa halafu nafichwa nawewe hapo unajua kila kitu na bado unanikalia kimya kabisa kana kwamba hujui lolote hebu nambie ni hilo tu mimi nitaondoka” kwa maelezo ambayo aliyatoa IGP hakuona sehemu ya kukwepea, alimuongoza mtu huyo wakatoka hapo na Kwenda nje kwenye bustani sehemu ambayo ilikuwa imejengwa kwa ajili ya kupumzika, kulikuwa na meza ndogo ambayo juu yake kulikuwa na vitabu walikaa hapo haukupita muda mke wa IGP aliwaletea kahawa na kumsalimia shemeji yake huyo kisha akawapisha wanaume wayajenge huku wakiendelea kushushia kahawa kuyapasha matumbo yao.
“Ndiyo hicho tu basi unachotaka kukijua?”
“Yes, ni hicho ila ndani yake kina mambo mawili kwanza nahitaji kujua hizi taarifa unazo tangu lini lakini pia nahitaji kujua kwamba kwanini hizi taarifa zinalindwa kwa siri sana namna hii?” aliongea huku akiwa anaiweka suti yake vizuri na kunyanyua kikombe cha kahawa, alipiga mafunda matatu na kutulia ulikuwa ni muda mwafaka wa kumjua mkuu wa idara ya usalama wa taifa
“Jason Markvelous Japhary” IGP alitamka kwa msisitizo sana macho yake yakiwa makavu lakini mwenzake ni kama aliona mwenzake anafanya mzaha kwenye mambo ambayo yalikuwa yanahitaji taarifa zinazo eleweka
“Hahahahahah hahahah hahah, sasa ndugu yangu naona nawewe umeanza kuwa na ugonjwa wa akili, mimi nimekuuliza kuhusu mkurugenzi wa idara ya usalama wa taifa sijakuuliza mdogo wa ndugu yetu Mark hahahhah sasa huyu mtoto anaingiaje kwenye hizi maada za kikubwa? Ebu nijibu nilicho kuuliza niwahi mahali leo binti yangu anafika nataka niwepo nyumbani atakapokuwa anafika atajisikia vibaya sana kama asipo nikuta au nikichelewa kukutana naye kwa muda ambao atakuwepo hapa Tanzania” mheshimiwa alicheka sana huku akikinyanyua kikombe chake cha kahawa tena akiwa ameweka miguu nne kabisa hakuwa na shaka leo alikuwa analipata jibu lake ambalo lilikuwa linamchanganya sana akili.
“Huyo ndiye mkurugenzi wa usalama wa tai………” IGP hakumalizia kauli yake CDF mkono wake ulikuwa ukitetemeka sana baada ya kuisikia hiyo kauli kutoka kwenye mdomo wa ndugu yake kabla hata hajamaliza kikombe hicho kilimponyoka kwenye mkono wake na kahawa hiyo yote iliishia kwenye mapaja yake, hata hakushtuka alibaki ameganda mdomo ukiwa wazi licha ya kahawa hiyo kuwa ya moto sana, kikombe kilijipigiza chini na kupasuka hiyo hali ilimshtua mpaka mke wa IGP alitaka kuja lile eneo kufanya usafi lakini IGP alimzuai kwa mbali kwa mkono hayo mazungumzo walitakiwa kuyamaliza wenyewe hawa ndugu wawili, usoni kwake IGP alikuwa yupo siriasi sana kuliko anavyokuwa siku zote mdomo wa CDF ulikuwa ukitetemeka na kucheza cheza akiwa kama vile anasimuliwa hadithi za nchi zinazo dhaniwa kwamba zitatokea lakini hazitokei.
“You must be kidding MD! (utakuwa unatania MD)” aliongea kwa shida mdomo wake ukiwa unatetemeka sana
“Hilo ndilo jibu sahihi la swali ambalo wewe umeniuliza” IGP uso wake haukuwa na masihara hata kidogo wakati anamjibu rafiki yake
“Hapana yule mtoto aaaaaagr Hapana Hapana, yule amekua mimi namuona mpaka anapelekwa huko nje kusoma, kwanza ni mdogo yule hiyo nafasi kaipataje pataje na kaipatia wapi? Hapana Hapana naomba uniambie kwamba ulikuwa unanitani” mheshimiwa huyo bado nafsi yake ilikuwa inagoma kabisa kuamini kile ambacho mwenzake alikuwa akimwelekeza hapo hakuhitaji kuziamini hizo habari kwamba eti zilikuwa ni za kweli kivipi yani? Nafsi iligoma kabisa.
“Nakujibu swali la pili na la tatu, ni kwamba hizo taarifa namimi nimezipata usiku huu lakini pia sijui kwanini hizi taarifa zilikuwa zinafichwa sana namna hii nadhani mhusika mwenyewe anaweza kuwa na majibu sahihi zaidi” IGP alikuwa anaongea kiwepesi mno kiasi kwamba mpaka mwenzake huyo alibaki anamshangaa tu, CDF aliingiza mkono kwenye mfuko wa mbele koti lake la suti alitoa tablet ndogo na kuingia kwenye mtandao. Aliandika jina la Jason zilikuja taarifa zile zile ambazo yeye alisimuliwa na mwana historia wa Ikulu alitabasamu lakini kwa hasira mno.
“MD who is this kid? Na imekuwaje mpaka akapewa nafasi kama hiyo mtoto laini sana namna hii? Hakuna watu kwenye nchi yetu mpaka mtoto kama yule ndiye anapewa nafasi kubwa sana namna hii? How mbona mnataka kuichanganya sana akili yangu namna hii” aliongea kwa jazba sana huku akili yake ikiwa inapingana yenyewe kuna sehemu ya akili yake ilikuwa kama inataka kukubali hilo jambo lakini sehemu nyingine ilikuwa inagoma.
“Wewe hapo ndo unamuita yule bwana mdogo ni laini laini?” IGP aliuliza kistaarabu huku akipata kahawa yake na kutulia
“Sio mara ya kwanza unaonyesha viashiria vya kumuogopa huyo bwana mdogo ebu naomba nijibu maswali yangu niliyo kuuliza hapo juu kabla hujatoa hilo neno” aliongea akiwa anajifuta futa ile kahawa ambayo ilimdondokea kwenye mapaja yake.
“Ulitakiwa kwanza kujiuliza kwanini kijana mdogo kama yule alikuwa anajiamini sana kuja mpaka nyumbani kwako muda kama ule na kuongea na wewe kijasiri sana namna ile, huyo ambaye wewe unamuita mlaini sana sidhani kama umewahi hata kuona namna anavyofanya mauaji nafikiri ungekuwa haumtaji taji kiwepesi sana namna hii, yule ndiye mkurugenzi mkuu wa usalama wa taifa ila hata hao majasusi wenyewe na vijana wote ndani ya idara hawamjui na kuna sababu za msingi za yeye kuto julikana. Yule ni mtu wa kutisha kuliko hata neno lenyewe linavyo tamkwa na ni mtu ambaye huwa haongei mara mbili kwenye maisha yake anapokuwa huko kwenye ulimwengu wake ndiyo maana huwa unamuona hapendi kubishana kabisa huwa anaamua kukaa kimya kwenye mambo mengi sana na hiyo ndiyo silaha yake kubwa anayo itumiaa kuuhadaa ulimwengu wa watu wasio mjua na kuwaaminisha kwamba yeye ni dhaifu na ni laini sana”
“Uhatari wake ni upi huo ambao wewe unauzungumzia?”
“Mbali na kuwa mkurugenzi wa usalama wa taifa yule ni kiongozi wa kundi moja la hatari sana linalo itwa “Five poisoned serial killers (Wauaji watano waliotiwa sumu mfululizo)” wote ni vijana wadogo sana na inasemekana hili ndilo kundi la hatari zaidi kuwahi kutokea kwenye historia nzima ya taifa hili, wanapopewa amri na kiongozi wao kwamba lifanyike jambo fulani hata wakiwa wawili tu basi hiyo sehemu inageuka kuwa kama uwanja wa mauaji kwa jinsi walivyo, ubaya wa hawa vijana hawajulikani na mtu yeyote yule zaidi yake yeye mwenyewe Jason na hata ambao wanajua siri zake baadhi hawawajui vijana hawa hata mmoja ila kwa mimi namjua mmoja tu pekee kati yao. Kumjua ninako maanisha mimi sio kwamba nimewahi kumuona au nalijua hata jina lake la kuzaliwa hapana ila nimewahi kusikia kwamba anafanyia kazi kwenye moja ya vyuo bora sana kwenye nchi hii, kinatumia maandishi matatu tu NIT kikiwa ni kifupisho cha National Institute of Transpot, hiki ndicho chuo pekee cha usafirishaji kinachotegemewa Afrika ya mashariki na kati lakini pia kwa Afrika inasemekana vipo viwili tu basi, ni chuo kidogo kwa mwonekano ila kina sifa kubwa sana ndani yake na kinatajwa kuwa miongoni mwa vyuo bora zaidi ambavyo vinaenda kuokoa tatizo la elimu na usafirishaji kwenye bara ya Afrika kwa miaka kumi ijayo. Sasa ndani ya hicho chuo ndiko aliko mmoja wa hawa vijana watano tena nasikia ni mlinzi wa kawaida sana unaweza kumuita mgambo tu ambaye kaajiriwa na mshahara wake wa laki mbili kwa mwezi una…….” IGP alitaka kuendelea lakini alikatishwa na ndugu yake huyo.
“Haya mambo unayo niambia hapa ni mambo ambayo yapo kwenye hii nchi au umetunga hadithi zako za kwenye movie ili ionekane kwamba umenijibu nilicho kuuliza?” CDF alikuwa anapewa mambo ya ajabu ambayo hata yeye kama mkuu wa majeshi hakuwahi kuyafikiria wala kukutana nayo sasa alishangaa mwenzake huyo alikuwa anayatoa wapi mambo ya kutisha sana namna hiyo alibaki ameduwaa.
Huo ndio ulimwengu wa watu wenye mabavu, unadhani eti inawezekana kweli huyu huyu Jason ambaye tumemsoma ndiye mkurugenzi wa usalama wa taifa? Eti ndiye mtu wa kutisha sana tena anamiliki kundi la hatari sana namna hii na hilo kundi ni la nini? Mimi bado siamini kama kuna ukweli kutoka kwenye mdomo wa IGP niseme tu sehemu ijayo huenda ikatufungua kidogo.
Wasalaam
Bux the storyteller.