Mtoa Taarifa
JF-Expert Member
- Sep 21, 2024
- 213
- 671
Watuhumiwa watano akiwamo katibu wa Mbunge wa jimbo la Kilolo Kefa Walles, Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi kupitia CCM wilaya ya Kilolo Hedikosi Kimwaga, Diwani kata ya Nyanzwa Boniface Ugwale maarufu kama 'Katili', Wille Chikweo na Silla Kimwaga wamefikishwa mbele ya Mahakama ya wilaya ya Iringa kwa tuhuma za kumuua aliyekuwa katibu wa CCM Wilaya ya Kilolo Bi. Christina Kibiki.
Kesi hii ya Jinai namba 34404 ya Mwaka 2024 iliyowahusisha baadhi ya viongozi wa CCM imesomwa mbele ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Iringa Rehema Mayagilo na kusimamiwa na mwendesha mashtaka upande wa Jamhuri Sauli Makori.
Imeelezwa mahakamani hapo kuwa watuhumiwa hao walitenda kosa hilo Novemba 12, 2024 eneo Banawanu lililopo kata ya Mseke majira ya usiku nyumbani alipokuwa akiishi Marehemu Bi. Christina Kibiki.
Hata hivyo watuhumiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwani upelekezi wa kesi hii bado unaendelea hivyo kesi imeahirishwa hadi Januari 7, 2025 ambapo itakuja tena kwa ajili ya kutajwa.
Ikumbukwe Bi Christina Kibiki aliuawa kikatili kwa kuchomwa na vitu vyenye Ncha kali eneo la tumboni kisha kupigwa risasi na watu wasiojulikana usiku wa novemba 12, 2024 akiwa nyumbani kwake.
Watuhumiwa wote wamerudishwa rumande wakisubili tarehe tajwa kwaajili kujibu kesi inayowakabili baada ya upelekezi wote kukamilika.
**************
WATU watano wamefikishwa mahakamani wilayani Iringa kwa mashtaka ya mauaji ya aliyekuwa Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kilolo, Christina Kibiki.
Miongoni mwa washtakiwa hao, wamo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Wilaya ya Kilolo, Hedikosi Kimwaga na Diwani wa Nyanzwa, wilayani Kilolo, Boniphace Katili.
Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani jana saa nane mchana mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Iringa, Rehema Mayagilo huku ulinzi ukiwa umeimarishwa katika viwanja vya mahakama hiyo.
Akisoma hati ya mashtaka katika kesi hiyo ya jinai namba 34404 ya mwaka 2024 ya mashtaka ya mauaji, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Sauli Makori alidai mahakamani huko kuwa washtakiwa hao; Kefa Wales, Silla Kimwaga, Boniphace Katili, Willy Chikweo na Hedikosi Kimwaga, kwa pamoja wanashtakiwa kumuua Christina Kibiki.
Alidai kuwa watuhumiwa hao walitenda kosa hilo la mauaji Novemba 12, 2024 katika kijiji cha Ugwachanya, wilayani Iringa.
Hata hivyo, Makori alidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika. Mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi Januari 7 mwaka huu, kesi hiyo itakapotajwa tena.
WASAFI MEDIA/ NIPASHE