Analogia Malenga
JF-Expert Member
- Feb 24, 2012
- 5,108
- 10,191
Abu Ibrahim al-Qurayshi alikuwa mwanajihadi mkongwe wa Iraq ambaye jina lake halisi lilikuwa Amir Mohammed al-Mawla.Image caption: Abu Ibrahim al-Qurayshi alikuwa mwanajihadi mkongwe wa Iraq ambaye jina lake halisi lilikuwa Amir Mohammed al-Mawla.
Kundi la Islamic State (IS) limemtaja kiongozi mpya baada ya kuthibitisha kifo cha Abu Ibrahim al-Qurayshi.
Ujumbe wa sauti uliotumwa mtandaoni ulisema Abu al-Hassan al-Hashemi al-Qurayshi sasa ni "khalifa", bila kutoa maelezo zaidi kuhusu utambulisho wake.
Ujumbe huo haukutaja jinsi, wapi au lini Abu Ibrahim al-Qurayshi alikufa.
Marekani imesema mwanajihadi huyo wa Iraq alijilipua na kuua familia yake wakati wa shambulio la kikosi maalum kwenye maficho yake kaskazini-magharibi mwa Syria tarehe 3 Februari.
Rais Joe Biden alisema kifo chake "kiliondoa tishio kubwa la kigaidi kwa ulimwengu", akimtuhumu kwa kusimamia kuenea kwa washirika wa IS duniani kote na kuwa "kikosi kinachoendesha" mauaji ya kimbari ya watu wa Yazidi.
Ujumbe wa sauti wa Alhamisi uliwasilishwa na msemaji mpya wa IS, Abu Umar al-Muhajir, ambaye alifichua kuwa mtangulizi wake Abu Hamza al-Qurayshi pia alifariki hivi karibuni.
Muhjair alisema hawezi kufichua jina halisi la kiongozi huyo mpya, lakini aliwataka wafuasi wake kuapa utii kwake.
Kumekuwa na uvumi kwamba mgombea anayewezekana zaidi alikuwa mtu wa Iraqi anayeitwa Bashar Khattab Ghazal al-Sumaidai, anayejulikana pia kama Abu Khattab al-Iraqi, Hajji Zaid na Ustath Zaid.
IS wakati fulani ilishikilia kilomita za mraba 88,000 (maili za mraba 34,000) kutoka mashariki mwa Iraq hadi magharibi mwa Syria na kuweka utawala wake wa kikatili kwa karibu watu milioni nane.
Kundi hilo lilifurushwa kutoka eneo lake la mwisho mwaka 2019, lakini Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa bado lina wapiganaji kati ya 6,000 na 10,000 nchini Syria na Iraq ambao wanaendelea kufanya mashambulizi ya kugonga na kukimbia, kuvizia na milipuko ya mabomu kando ya barabara.
Kifo cha Abu Ibrahim al-Qurayshi katika jimbo la Syria linaloshikiliwa na upinzani la Idlib kimekuja siku chache baada ya shambulio kubwa la IS kwenye jela inayodhibitiwa na Wakurdi katika mji wa kaskazini-mashariki wa Syria wa Hassakeh - operesheni muhimu zaidi ya kundi hilo kuwahi kutokea kwa miaka mingi.
Takriban walinzi 121, wapiganaji wa wanamgambo wanaoongozwa na Wakurdi na raia waliuawa katika wiki moja ya makabiliano makali, pamoja na wafungwa 374 na washambuliaji wa IS, maafisa walisema.
Mapema wiki hii, kundi la waangalizi lilisema kuwa IS ndiyo iliyohusika na shambulio dhidi ya basi la kijeshi katika jangwa la kati la Syria na kusababisha vifo vya wanajeshi 15 wa serikali.
BBC Swahili