Analogia Malenga
JF-Expert Member
- Feb 24, 2012
- 5,108
- 10,191
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo amewaagiza wamiliki wa kumbi za starehe na burudani kuhakikisha sauti zitokanazo na shughuli zao hazizidi viwango vinavyokubalika kwa mujibu wa sheria.
Waziri Jafo amesema hayo hii leo Jijini Dodoma wakati wa kutoa Tamko kwa umma juu ya udhibiti wa uchafuzi wa mazingira utokanao na kelele na mitetemo na kuwaagiza wamiliki wa maeneo ya burudani na starehe kuzingatia matumizi ya vipima kelele na vizuia sauti kama ilivyoelekezwa kwenye masharti yote ya leseni zao.
Kwa upande mwingine Waziri Jafo ametoa rai kwa viongozi wa Dini kupitia Kamati za Amani, kulijadili suala hili la Kelele na Mitetemo iliyopitiliza kutoka kwa baadhi ya nyumba za ibada ili kupata namna bora ya kuendesha ibada kwa maslahi mapana ya afya ya jamii.
Aidha, Waziri huyo ameutaka umma wa Watanzania kuhakikisha agenda ya kelele na mitetemo inakuwepo kwenye mikutano ya wakazi na kuwaomba wananchi kutoa taarifa kuhusu kero na mitetemo kwa Ofisi za Serikali za Mitaa au NEMC kwa namba za bure (0800110115 au 0800110117 au 0800110116).
Amesema yeyote atakayesababisha kero zitokanazo na kelele na mitetemo kinyume na Kanuni za Usimamizi wa Mazingira (Udhibiti wa kelele na mitetemo) za mwaka 2015 atakuwa amevunja sheria na adhabu yake ni faini isiyopungua shilingi milioni moja au kifungo kisichozidi miezi sita, sambamba na kufungiwa kwa biashara husika.
Nae Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dorothy Gwajima amesema wataendelea kuelemisha jamii juu ya athari za kiafya zitokanazo na kelele na mitetemo iliyopitiliza ili kuwa na jamii yenye afya bora.
ITV