- Source #1
- View Source #1
Salaaam wakuu, tafadhali naomba kujua uhalisia wa hii taarifa iliyowekwa kwenye gazeti hili la Mwananchi khusu Mzee warioba kuwa ametoa pongezi, haki na uhuru umefanikisha uchaguzi.
- Tunachokijua
- Jaji Joseph Sinde Warioba alikuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia Novemba 5, 1985 hadi Novemba 9, 1990. Pia ni Mwanasheria, Mwanasiasa na Jaji maarufu anayeheshimika Kitaifa na Kimataifa kwa mchango wake mkubwa katika masuala ya Sheria na Utawala Bora.
Kadhalika aliwahi kuwa Jaji katika Mahakama ya Kimataifa ya Sheria ya Bahari ya Hamburg, Ujerumani yenye makao yake makuu nchini Ujerumani kuanzia 1996 hadi 1999. Warioba aliongoza Kundi la Waangalizi wa Jumuiya ya Madola katika uchaguzi wa Aprili 2007 Nigeria. Alitoa tathmini chanya ya uchaguzi huo, akiuona kuwa ulikuwa wa maendeleo huku pia akisema kulikuwa na dosari. Kadhalika amekuwa ni moja kati ya viongozi wastaafu ambao hawakubali kukaa kimya dhidi ya ukiukwaji wa taratibu za kidemokrasia na utawala bora, tazama hapa akitoa maoni yake juu ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Mnamo Disemba 04, 2024 Warioba alifanya mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mabo mengine alizungumzia mchakato mzima wa uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 27, 2024. Kumeibuka picha ya Gazeti linaloonekana kuwa la Mwananchi ambalo katika ukurasa wake wa mbele lina kichwa cha habari kinachosomeka “Haki na uhuru umefanikisha uchaguzi… Warioba atoa pongezi tena”
Je ni upi uhalisia wa taarifa hiyo?
Ufuatiliaji wa kimtandao uliofanywa na JamiiCheck umebaini kuwa taarifa hiyo imepotoshwa kutoka kwenye uhalisia wake kutoka kwenye nakala rasmi ya gazeti la Mwananchi lililotolewa tarehe 05/12/2024.
Nakala rasmi ya gazeti la Mwananchi ukurasa wa mbele ina kichwa cha habari kinachosomeka “MIZENGWE, VURUGU KWENYE UCHAGUZI… Warioba atoa angalizo tena” ambapo nakala nyingine imepotoshwa kwa kuwekewa kichwa cha habari tofauti kinachosomeka “Haki na uhuru umefanikisha uchaguzi… Warioba atoa pongezi tena”
Aidha nakala halisi inaonesha taarifa kamili inapatikana ukurasa wa 4 tofauti na nakala iliyopotoshwa ambayo inaonesha ukurasa wa pili ambao hauna taarifa hiyo.
Taarifa kamili inayopatikana ukurasa wa nne wa gazeti hilo inaweka bayana maoni ya Warioba dhidi ya uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 ambapo alibainisha kasoro zilizojitokeza na kumtaka Rais Samia Suluhu Hassan na Chama cha Mapinduzi CCM kuchukua hatua kwa kuweka maslahi pembeni pamoja na vyama vya upinzani kujadili changamoto zilizojitokeza kuepuka machafuko ya kisiasa kama yaliyotokea mwaka 2000 Zanzibar.
Vilevile gazeti hilo limeambatanisha nukuu mbalimbali za jaji Warioba, moja ya nukuu hizo inasema “Nimeona serikali inasema uchaguzi umefanikiwa kwa asilimia 100, unawezaje kusema hivi wakati watu wanakufa? ilinishtua.”
Unaweza kurejea hapa kutazama mkutano wa Jaji Warioba na waandishi wa habari.
View: https://www.youtube.com/live/-8uUaq_g1N4?si=ujv5Sg1u5dedHj3O