Urais kwa wagombea wa TLP moto
Send to a friend Monday, 12 July 2010 08:56
James Magai
WAKATI wajumbe wa mkutano mkuu wa Taifa wa Chama cha Tanzania Labour (TLP) wakitarajiwa kumpitisha mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, kuna taarifa za kuwepo mvutano baina ya pande mbili zinazovutana, mmoja ukidai kuwapo kwa njama za kumuengua mmoja wa wanachama walioomba kuteuliwa katika nafasi hiyo, huku mwingine ukipinga.
Habari zilizolifikia Mwananchi kutoka katika vyanzo vya kuaminika ndani na nje ya chama hicho zinasema kuwa uongozi wa juu wa chama hicho umepanga kumwengua mmoja wa wanachama waliochukua fomu za kuomba kuteuliwa, Macmillan Lyimo.
Habari kutoka katika vyanzo hivyo zinadai kuwa uongozi huo wa juu wa chama hicho unapanga kumwengua Lyimo na kumwacha Mutamwega Mgahywa apite moja kwa moja.
Habari kutoka ndani ya chama hicho zinadai kuwa kuna baadhi ya wanachama ambao wanapinga mpango huo kwa madai kuwa Mgahywa ambaye amewahi kuwa mbunge wa Jimbo la Mwibara wilayani Bunda mkoani Mara kwa muda wa miaka 10 hana sifa za kugombea nafasi hiyo.
Hata hivyo akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu kuhusu madai hayo ya kutokuwa na sifa ya kielimu kugombea nafasi hiyo na vyeti alivyoviwasilisha kwa katibu mkuu, Mgahywa alisema madai hayo hayana msingi wowote.
Kuhusu kiwango chake cha elimu Mgahywa ambaye alilieleza Mwananchi kuwa ataweza kulitolea ufafanuzi wa kina na kwa vielelezo leo ikiwa ni pamoja na kutangaza msimamo wake, alisisitiza kuwa yeye ni msomi wa kutosha na kwamba hana wasiwasi na madai hayo.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa TLP Hamad Tao alikanusha madai ya Mgahywa kuwasilisha vyeti vya sekondari wakati akirejesha fomu huku akisisitiza kuwa ni msomi mwenye shahada ya udaktari.
Alisema hata hivyo katika katiba ya chama chao hakuna kipengele cha kiwango cha elimu kwa mgombea wa nafasi hiyo wala kwenye katiba ya nchi bali hiyo iko kwa CCM tu.
Kuhusu mpango wa kumuengua Lyimo Tao alisema hakuna mpango huo na kwamba waombaji wote watapigiwa kura na kwamba taarifa hizo ni woga wa aliyezitoa akidhani kuwa kuna mmoja atapendelewa.
Habari zaidi kutoka ndani ya chama hicho zilidai kuwa uongozi wa juu wa chama hicho umeapa kufanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa hapitishwi na kwamba mpango huo una maslahi binafsi.
Wakimweleza Lyimo, baadhi ya wanaTLP hao ambao hawakutaka majina yao kutajwa walidai kuwa ingawa hajulikani sana katika anga za siasa, lakini ndio mgombea anayeweza kutoa upinzani mkubwa kwa CCM
Mimi namfahamu Lyimo, nimekuwa nikifuatilia vitabu vyake anavyoviandika, ana mawazo na mtizamo mzuri ambao unaweza kuleta mabadiliko katika nchi, alisema mmoja wa wana TLP hao na kuongeza;
Ndiye mgombea ambaye akisimama kuelezea sera zake atatoa upinzani mkubwa kwa wagombea wengine na nina imani wananchi wengi wanaweza kumuunga hata mkono maana watu wameshachoka na CCM.
Kwa upande wake Lyimo alipoulizwa kuhusu madai hayo ya mpango wa kumuengua, alisema yuko kwenye mkutano lakini alijibu kwa ufupi tu kuwa hawezi kuzungumza zaidi kwa sasa bali anasubiri kuona kitakachotokea leo.
Hata hivyo habari zilizolifikia Mwananchi jana kutoka katika chanzo kingine cha habari cha kuaminika ndani ya chama hicho muda mfupi kabla ya kwenda mitamboni zilisema kuwa uongozi wa chama hicho umesalimu amri katika mpango huo.
Chanzo hicho kililidokeza Mwananchi kuwa uongozi wa chama hicho umeamua kusitisha mpango huo wa kumwengua Lyimo, kwa hofu ya kusababisha mtafaruku ndani ya chama, baada ya kuona kuwa kuna nguvu kubwa iliyo nyuma yake ndani na nje ya chama hicho
Mwenyekiti-Augustino Lyatonga Mrema
Katibu Mkuu-Hamad Rajab Tao
Wote choka mbaya, kuna chama hapo kweli?