Halikuwa suala la dini au udini. Ilikuwa ni "damu." Damu yao iliwaunganisha. Walikuwa ni Waislamu na Wakristo, pia kutoka pande zote mbili za Muungano. Huo ndiyo ukweli na inatubidi tuseme ukweli. Mimi ni Mkristo mweusi mwenye asili ya Kiafrika kutoka moja ya makabila ya hapa nchini Tanzania.
Kwa wale waliompinga na kumchafua, Salim Ahmed Salim hakuwa "damu" yao ingawa ana damu hiyo kutoka upande wa mama yake. Lakini waliona damu hiyo haitoshi, ni kidogo sana, kutoka upande wa mama yake. Pamoja na damu ya kigeni kabisa kutoka upande wa baba yake, waliona hakuwa "mmoja wetu." Kwa mfano, wazazi wa Salim Ahmed Salim wengekuwa Wamanyema au Wanyamwezi au wa kabila lingine lolote, au kutokana na mchanganyiko wa makabila, asingekuwa na tatizo kuchaguliwa kuwa mgombea wa uraisi kutoka Chama Cha Mapinduzi na angeshinda uchaguzi kuwa raisi wa Tanzania.
Miongoni mwa waliompinga walikuwa viongozi kadhaa. Lakini kulikuwa na viongozi wa taifa, hasa kutoka upande wetu wa bara, waliomuunga mkono. Kwa wale waliompinga, walimpinga kwa sababu hakuwa na "damu yetu."
Bila shaka bado kuna ambao wana msimamo huo. Akija mwingine kama Salim kugombea uraisi, au mwingine kama Amir Jamal (ambaye hakuwahi kugombea uraisi lakini alikuwa karibu sana na Mwalimu Nyerere kuliko mawaziri wote tangu tupate uhuru), atakumbana na tatizo hilo.
Kuna Watanzania ambao bado hawajajifunza chochote kutokana na athari za ukabila au ubaguzi wa aina yoyote ingawa wanajua matokeo na madhara yake katika nchi jirani: Rwanda, Burundi na Kenya. Matokeo ya siasa na sera za ukabila na ukanda nchini Nigeria, na katika nchi zingine katika bara letu, siyo ya kujivunia. Siyo msingi wa amani na umoja wa nchi yoyote.
Enzi ya Mwalimu Nyerere, msingi wa umoja wetu nchini Tanzania na katika bara letu ulikuwa ni: "Afrika ni moja. Binadamu wote ni ndugu zangu." Halafu sasa tunaulizana makabila, na kadhalika, na asili yetu "kuhakikisha" ni raia au "ni ndugu yangu kwa sababu anatakoka kwetu." Kwenu wapi? Kwenu si Tanzania yote?
Kuna hata wenzetu ambao ni raia wanaoambiwa, "rudi kwenu," "mkimbizi we," "Mnyasa huyo," "Karundi hako," na kadhalika, kwa sababu mbalimbali (pamoja na kutofautiana kimawazo na viongozi) hata kama wana uthibitisho kwamba ni raia.
Tukianza kufukuzana, na kuambiana wewe siyo Mtanzania, nani atabaki hapa? Wagogo tu? Na Watindiga, Wanyaturu na wengineo wenye "asili" ya mikoa ya kati? Wao pia walitoka mahali pengine, katika bara letu, nje ya eneo ambalo sasa linaitwa Tanzania.
Ni dhambi ukitoka sehemu za mpakani na nchi jirani? Ni kosa gani hata ukiwa na asili nje ya bara letu lakini ni raia wa Tanzania?
Kuna hata ambao walisema Nyerere ni Mtusi (kwahiyo siyo Mtanzania na haipendi nchi yetu kwa sababu ya Utusi wake kama Christopher Mtikila alivyosema) ingawa pia inasemekana alikuwa na asili ya Kijaluo kutoka Kenya au visiwa vya Ssese ziwani Nyanza.
Lakini hata kama ni kweli alikuwa na asili ya Kitusi pia, labda upande wa mama yake (ni mfano tu), kuna kosa gani? Hakuna watu wa asili ya Kitusi ambao ni raia wa Tanzania? Hakuna Watusi wanaoweza, na wanaostahili, kuwa raia wa Tanzania? Kwa nini yawe makabila fulani tu? Na kwa sababu gani?
Hata kama ulizaliwa nchi nyingine, unaweza kuwa raia wa Tanzania ukitaka kuwa raia wa nchi yetu; kwa mfano, Derek Bryceson, Shirley Graham Du Bois, na wengineo waliozaliwa nje ya nchi yetu, na nje ya bara letu, bila kujali "sina kundi langu au la watu wa asili yangu watakao nitetea kupata haki zangu au watakaopigania haki zetu" kama Wazungu, Afro-Americans, Waha, Wagogo, Wahindi, Wasafwa, Wakurya, Wasomali, Wazanaki, Waarabu, Wapogoro, Wafipa, Wameru, Wamatumbi na kadhalika. "Haki zangu na haki zetu" ni haki ambazo ni haki za wananchi wote kama watu binafsi na siyo kwa sababu ni watu au wananchi wa makundi fulani.
Raia wote wa nchi yetu, waliozaliwa nchini na waliozaliwa nje ya nchi yetu, wote ni sawa. Hakuna ambaye ana haki zaidi kuliko mwingine, hakuna ambaye ni bora kuliko raia mwenzake. Ni uraia wa mtu binafsi bila kujali alikotoka. Huo ndiyo msingi wa haki na umoja wa nchi yetu.
Ndiyo maana Nyerere alipoanza rasmi kudai uhuru kutoka kwa wakoloni miaka ya hamsini, alisema tutajenga nchi yetu ya Tanganyika, na taifa letu la Tanganyika, kutokana na haki na uraia wa watu binafsi (individuals), siyo haki na uraia kutokana na msingi wa makundi ya makabila au makundi ya watu wenye asili mbalimbali (Wazungu, Wahindi, Waarabu) na kadhalika.
Hakutakuwa na sehemu itakayotengwa kuwa ni ya Wazungu tu, ni ya Wahindi, Waarabu, Wasomali, Wahehe, Wanyamwezi, Waluguru, Wamakonde, Machotara, Wasukuma, Wayao, Wachaga, Wazaramo, Wamasai, Wandengereko, Wanyakyusa, Wadigo, Wangoni, Wanyasa, Wahaya, na kadhalika. Sehemu zote za Tanganyika zitakuwa ni za Watanganyika wote. Huo ndiyo moyo wa umoja wetu, si Tanzania tu, bali bara zima. Ndiyo maana Nkrumah aliwahi kusema kila nchi na mji katika bara la Afrika ni nyumbani kwake: "Every country and town in Africa is my home."
Nyerere aliwahi kusema: it is shame for Africans to be refugees in Africa - Waafrika kuwa wakimbizi nyumbani kwao Afrika. Kila nchi wanakokimbilia iwe ni nyumbani kwao.
Tumekuwa Watanganyika tangu tupate uhuru, na Watanzania baada ya kuungana na ndugu zetu wa visiwani Unguja na Pemba, na tumekuwa tunajisifu kuwa tuna umoja bila kujali kabila la mtu au rangi yake na asili yake. Tumekuwa na sifa hiyo, ya umoja na amani, karibu kuliko nchi zote katika bara letu.
Halafu sasa hata askari wetu wameanza kuuliza "wewe kabila gani?"
Tumerudi nyuma miaka mingi sana.
Enzi ya Nyerere, kulikuwa na ukabila hapa na pale, lakini ulikuwa hauvumiliwi.
Hatuna ukabila kama nchini Kenya, kwa mfano kati ya Wakikuyu na Wajaluo, au nchini Rwanda na Burundi ambako Wahutu na Watusi wamechinjana kwa miaka mingi sana. Lakini tusipojiangalia, tukiendelea kuvumilia ubaguzi wa aina yoyote mpaka watu wanajisifu na wanajiona ni bora kuliko Watanzania wengine kwa sababu wanatoka makabila fulani, na mikoa au ukanda fulani - "bila sisi, msingekuwa na wasomi nchi hii," "hamna akili nyie," "ukanda wetu una maendeleo ya pekee kuliko sehemu zote nchini kwa sababu tumewazidi akili, sisi ni vichwa" "watu wa kabila lenu, mbona mko nyuma sana?" - tutakuwa na matatizo sana kama taifa.
Kuna hata vyama vya siasa ambavyo vinasemekana ni vya makabila fulani, au vinaongozwa na watu wa kabila fulani au wa makabila fulani tu kwa sababu wanachama wa makabila mengine wanabaguliwa. Kuna wengine wanaosema watu kutoka makabila fulani hawastahili kuwa viongozi wa nchi yetu kwa sababu wana ubaguzi sana, wanawabagua watu wa makabila mengine.
Pia kuna ubaguzi kazini. Unavumiliwa hata kama kuna ushahidi watu wa makabila fulani wanapendeleana kupeana kazi.
Tusivumilie ubaguzi wa aina yoyote. Nani anakemea ubaguzi huo, na anamaanisha anachosema, kama Nyerere?
Bado tuna safari ndefu sana.
I weep for my country.