Jasusi Honda ndani ya mpango wa Congo

Jasusi Honda ndani ya mpango wa Congo

RIWAYA : MPANGO WA CONGO.


SEHEMU YA 17


Akanyanyuka.

Wakati anafungua mlango ni wakati huo Kizibo alikuwa tayari alikuwa ameshavuka sebule na kuelekea kilipo chumba cha Simbi.

Sajini alitoka taratibu akiwa hana habari ya Kizibo kuwa huko aendako.

Na si Kizibo tu aliekuwa huko ila ndani ya Chumba kulikuwa na kidume mwingine aliekuwa amefaidi utamu wa Simbi usiku ule na ndie adui yao alikuwa amewalaza kichovu.

Kizibo alizidi kuukaribia mlango wa chumba cha Simbi.

Alipoufikia akasikilizia kwanza.
Akatazama kushoto na kulia hakuona mtu,akaingiza mkono mfukoni na kutaka kutoa funguo zake zisizoshindwa kitu.

Akasita!!

Alisita baada ya kusikia mabishano ya sauti mbili za kike na kiume.

Akavuta kumbukumbu ya sauti hiyo kama inaweza kufanania na sauti ya Sajini.

Haikuwa yenyewe!!

Akagwaya!

Haraka akaondoa dhamira yake ya ubakaji,akageuka ili aelekee chumbani kwa Sajini.
Hakugeuka hata hatua moja, akakutana na jicho kali la Sajini likimtizama, jicho lililokuwa limejaa husda na wivu.

Akagwaya!

Alibaki akiwa amezubaa asijue anataka kusema nini.

“Ulifuata nini huku komredi” alisema Sajini huku dhahiri akionekana kuwa na kovu la hasira na uchungu uliochanganyikana na wivu.

“hapana kiongozi ni…” hakumalizia kauli yake akakatishwa na Sajini.

“Hizo funguo je! Ulitaka kubaka mke wangu sio!!”

Kizibo midomo ikamuanguka na akashindwa ajitetee vipi.

Akakumbuka kuna sauti ya kiume chumbani kwa Simbi, akataka kumsanua Sajini Kebu.

“Kiongozi humu kuna…!” hakumalizia tena kauli yake akajikuta anachezea konde moja safi kutoka kwa Sajini ambae kipimo cha uvumilivu kilikuwa kimemwisha.

Konde alilopigwa Kizibo bila kutarajia likampeleka chini kama mzoga,akataka kunyanyuka akakutana tena na teke lililompelekea kujigonga kwenye mlango wa chumba cha Simbi na kumsambaratisha chini.

Kishindo kile ndicho kilichowasitua Simbi na Honda chumbani kwao.

Kizibo nae akashindwa kuvumilia akanyanyuka kama mbogo aliejeruhiwa na kumpelekea makonde mawili ya harakaharaka ambayo yote yalipanguliwa kisitadi na Sajini ambae nae akarudisha teke la mawashi lililopanguliwa na Kizibo kama mzaha.

Chumbani bado Honda alizidi kusikia vishindo vya watu wakipigana na kwa mdondoko tu,ilionesha wanaopigana ni wajuzi wa mambo.

Sasa kwanini wapigane na wapiganie ndani ya nyumba ya Simbi.

Akamgeukia Simba na kwa kumtazama tu tayari aliona kutetemeka kwa Simbi ni zaidi ya uoga ila ni uoga wa anachokijua.

Simbi nae akamtazama Honda na akakutana na macho yaliojaa viulizo.

Simbi akabaki kutikisa kichwa tu asijue ndio anakataa au anakubali au anasikitika.

“Najua unawajua,wasikilize tafadhali!!” alisema Honda huku tayari kichwani akijua cha kufanya kuepuka zogo.

Simbi hakuwa na namna kama ni maji sasa yalikuwa yanaelekea kuzidi unga.

Akaufuta mlango kinyonge kisha akaufungua.

Alichokishuhudia ni manundu usoni mwa wageni wake.

Hakusema kitu akabaki anawatazama wanaume wale waliotoshana nguvu.

Honda alikuwa anahitaji kuwajua waliokuwa wanatoana jasho huko nje ya chumba, hivyo akaanza kufuatilia kila hatua aliopiga Simbi na wakati alipokuwa akifuangua mlango wala hakujiuliza mara mbili kwa alichokiona.

Alimwona dhahiri shahiri Sajini Kebu na mwanaume mwingine ambae alikuwa amempa mgongo.

Hakutaka balaa usiku ule ikiwa hajui Sajini pale alipo ananguvu kiasi gani.

Hakujiuliza zaidi,macho yake yalielekea moja kwa moja lilipodirisha pana la vioo vya kisasa ambalo halikuwa na nondo ndani.

Akaliwahi na alipata nafasi nzuri ya kutimka baada ya Simbi kurudishia mlango nyuma yake.

Kizibo alitaka kujisafisha kwa kujitoa kwenye lawama za kutaka kumbaka Simbi; hivyo wakati ambao Sajini amezubaa akimtizama Simbi aliekuwa kwenye nguo za kulalia ndipo nae akatumia mwanya huo kuchoropoka na kuingia chumbani kwa Simbi.

Sajini Kebu akataka kumfuata ila Simbi akamwekea mkono kumzuia.

“Mnataka kupigania chumbani kwangu?” alihoji Simbi kwa sauti ya kitetemeshi ambacho Sajini hakujua kililetwa na nini.

“aah…” akababaika kujibu Sajini.

Mara akaja kwa kasi Kizibo.

“Wewe mwanamke ulikuwa unaongea na nani humu ndani?” aliuliza Kizibo baada ya kuingia ndani na kumkosa aliesikia sauti yake.

Simbi akagwaya na asijue cha kujibu.

“Acha dharau Kizibo,kwa hiyo umeamua kusingizia mengine.” Alihoji Sajini huku akipiga hatua kumfuata Kizibo.

Simbi aliingilia kati.

“umemkuta nani huko na ulimsikia nani huko!” aliuliza Simbi kwa ujasiri baada ya kugundua Kizibo hajamkuta Honda japo hakujua amejificha wapi. Hakutaka kulijua hilo wakati huo.

“Kuliku….” Akataka kusema kitu Kizibo ila Sajini akaingilia kati.

“Unasingizia mtu,mh mtu gani jamaa angu!”

Ikabaki kila Kizibo alipotaka kusema kusikia kwake sauti ya mwanaume pale ndani, hatia ya kunyatia vyumba vya watu ilimnyima kueleweka mbele ya Sajini ambae alikuwa amejenga chuki kwa Kizibo.

Malumbano yao yalikuja kukatishwa na sauti ya risasi huko nje na bila kungoja Kizibo na Sajini Kebu wakakimbilia vyumbani mwao kuchukua bastola walizokuwa wameziacha vyumbani walikokuwa kabla ya kitimtim hicho.

*****

Kojo alichoka kukaa ndani ya gari hivyo akashuka na kutembeatembea ili kunyoosha miguu iliokuwa imechoka kwa kukaa sana ndani ya gari huku kila mara akisonya kwa kuona muda unazidi kwenda huku waliokuwa ndani wakikawia kutoka.

Ni wakati akitaka tena kurudi ndani ya gari ndipo macho yake yakaona kivuli kikiwa juu ya ukuta na kisha kikachumpa na kuanguka chini.

Kwa msaada wa taa zilizokuwa zikiwaka kwenye nyumba za jirani; Kojo aliona mtu akinyanyuka na kujitikisa mikono yake.

Lakini kitu kimoja kilimsitua ni aina ya mtu aliemuona.

Kojo hajawahi kumsahau Honda,alimkariri kimo na mwendo lakini kilichomhakikishia kuwa aliemuona ni Honda ni mkoba uliokuwa ukining’inia mgongoni mwake.

Honda hajawahi kuuacha mkoba ule.

Kojo akajishauri kumfuata ila akajionya mana hakujua kule ndani ameacha balaa gani.


Akaanza kumvizia kwa kujikinga na gari kila alipohisi Honda anataka kugeuka.

Kitu ambacho Kojo hakujua ni kuwa Honda alikuwa ameliona lile gari tangu anaruka ukuta na kutua chini hivyo hata wakati anakawia kutokomea alikuwa anaipigia hesabu ya kuitumia ili awahi anakoenda.

Hivyo alishindwa kuamua lipi la kufanya,atumie miguu ama aibe lile gari.

Akaamua kulifuata.

Wakati Kojo akitaka kumalizia kujikinga na gari ndipo alipomuona Honda akigeuza na kulifuata gari lilipo.

Kojo akaingiwa na kiwewe,uwezo wa Honda aliujua japo hata yeye alijiamini ila alikubali amezidiwa mbinu na Honda hivyo akazidi kujionya ya kuwa akileta mbwembwe tu anakuwa tena chakula cha Honda. Hakutaka kuchekwa na Kizibo japo kwa alivyomjua Honda basi aliamini huko ndani kumeachwa balaa.

Kojo akainama kisha akakiweka vyema kivuli cha Honda na kuachia risasi ambayo ilimnyanyua juu na kumbwaga chini kama kiroba cha mirungi.

Kojo akatabasamu huku akitoka kule alipokuwa amejikinga kwenda kule alipoangukia Honda.

Alienda kumalizia kazi alioianzisha na alipanga kumshushia risasi zote zilizokuwa zimebaki kwenye bastola yake aina ya Revolver colt ya kipolisi.

Honda alinyemelewa na umauti….

****
 
Mwandishi anapenda tuwe tunakomenti. Sasa namuahidi kila baada ya dk5 nadondosha comment yaani nonstop niwachefue walio subscribe.
 
Kwahiyo demu ndo kamponza Honda


Sent from my iPhone using JamiiForums
 
Back
Top Bottom