Wanajamvi, Kwanza napenda kumshukuru Mungu kwa nafasi hii aliyonipa ya uhai na afya tele kuweza kuleta swali hili kwenu.
Swali langu haliongelei kama inawezekana kila mtu akawa tajiri 'kiutendaji', la hasha. Bali je, logic inakubali kwa watu wote duniani kuwa matajiri bila kuacha masikini hata mmoja? au kwa wengine kuwa matajiri ni lazima kuwe na wahanga? (masikini)?
Nawasilisha.
Habari Mwanzilishi wa Mada. Nashukuru kwa aliyenitag katika mada hii kwani naamini anapenda kuona mchango wa watu mbalimbali na mimi nikiwemo katika kuelezea hii mada.
Kwa uelewa wangu na kwa jinsi nilivyosoma mada yako Naamini umezungumzia hasa utajiri wa Mali (Physical Things). Je ni kweli kwamba kila mwanadamu anaweza kuwa tajiri?
Kuna dhana mbalimbali watu wanazo juu ya utajiri lakini ninaweza kuelezea kwa kina kuhusiana na hilo.
Kwanza kabisa ni vyema kufahamu nini lengo la Maisha, Lengo la maisha ni kuwa na furaha. Kila mwanadamu anapenda kuwa na furaha. Kila kitendo tunachokifanya, shughuli tunayofanya na nia tunayoweka katika shughuli zetu ni kutafuta furaha. Unaweza ukawa hujaona kuwa furaha ndio mzizi lakini ni kweli, furaha ni mzizi mkuu na ni tegemei la mwisho kwa kila hatua. Unafanya kazi ili familia yako, marafiki, watu wako wa muhimu na wewe mwenyewe upate furaha na amani. Unaweza ukawa unasoma kwa lengo la maisha mazuri hapo baadaye, lakini bado maisha yayo mazuri ni kwa lengo la furaha hapo baadaye, unajituma na kuhakikisha unapata kipato ili kutimiza mahitaji yako, na mahitaji hayo ni chanzo au chemichemi ya furaha kwako. Hivyo kila hatua ya mwisho ni kuwa na furaha.
Je furaha inapatikanaje? Je furaha inapatikana tu kwa kuwa na mali, umaarufu, na vitu vingi? Je ukipewa kila kitu unachokitaka kama ni mke mzuri, mali za kununua utakacho, na umaarufu je utapata furaha? Je kila mwenye vyote ana furaha? Utagundua pia kwa upande mwingine hata mwenye kila mali, umaarufu, na utajiri hana furaha yote asilimia mia. Bado atajitahidi kulinda anaowapenda kama ni mke na watoto, bado atajitahidi kumaintain utajiri wake, bado atahitaji kujilisha na wanyang'anyi, bado anakufa, atazeeka na bado hawezi kudhibiti kufa na kuzeeka kwa anaowapenda. Pia bado akifa anaacha vyote hivyo alivyojitahidi kuvikusanya, je lengo la maisha ni nini hasa? Lengo la maisha ni kuitafuta furaha ya kweli, isiyoisha, isiyoibwa na wanyang'anyi na furaha ambayo haishikiliwi na vitu vya muda. Maisha ukiyachunguza yanatupa mafunzo kuwa vingi tunavyoviona ni vya muhimu havina umuhimu milele na pia kila mwanadamu anateseka (kutoridhika na hali).
Nature ya mwanadamu ni kutoridhika, utapenda kuwa ni hichi utakipata lakini bado utapenda kuwa na kingine utakipata lakini bado utapenda kuwa na kile, hakuna unachokipata kama mali na umaarufu na kuridhika daima. Pia mbali na kutoridhika nature ya akili ni kutamani. Akili ni kama samaki anayetapatapa, inatamani hiki na kile na kile na kile na kukujengea hamu. Hamu haikamiliki kwa nje bali inakamilika moyoni na sio akilini.
Hata kila mwanadamu akiwa na mali na kila kitu bado hatutaweza kuishi kwa amani. Bado tutahitaji mfano upendo, kujitambua, hekima, adabu na busara.
Mafanikio yanakuja pale unapokamilisha safari ya nafsi, Mfano mzuri ni speech ya Steve Jobs, alisema kila mwanadamu anapaswa kufahamu ni kwanini yupo leo hii ulimwenguni, na ukifahamu lengo la maisha yako na kulifuata utasaidia nafsi za wanadamu wengine ambazo zinahitaji kujitambua na utakuwa mwanga kwao wenye giza. Badala ya kufikiria nitakuwa na mali kiasi gani nifurahi fikiria nitafanya nini katika maisha yangu kuangaza wanadamu wengine. Leo tunafahamu kuna aliyeanzisha umeme, aliyegundua computer, aliyebuni kitu fulani, aliyetumia maisha yake kutoa huduma yake kwa wanadamu, na kadhalika wote hawa hawasahauliki. Kwa kutenda lengo lako la maisha, rehema na baraka hukujia na mafanikio yako huongezeka.
Hebu jiulize kwanini watu matajiri wa dunia bado wanajituma, wanajitahidi kuendeleza shughuli zao badala ya kukaa na kutumia mali zao tu? Kwa sababu lengo lao la maisha sio kujilimbikizia mali, wanafahamu kuwa furaha haiji kwa mali bali kwa kuridhika na hali na kuishi katika unachokipenda na ambacho ni lengo lako la maisha. Na kupitia wao wengine huona mwanga na kuamka.
Weka mali ambayo haina mwisho, ambayo hakuna mtu anayeweza kukuibia wala kukudhulumu. Kumbuka sisi ni sehemu ya Aliye Mkubwa, mali haiwezi kukununua wala hakuna dhamani inayoweza kulingana na wewe. Fahamu lengo lako la maisha na maisha yatajipanga kutimiza lengo lako. Tangu mamilioni ya miaka na miaka dunia imetumia muda kutokea kama ilivyo leo, kwanini wewe upo leo hii, ni bahati kubwa kuzaliwa mwanadamu, ni bahati kubwa kuwa Ufahamu unaoishi. Unautajiri mkubwa ndani kuliko utajiri wa nje.
Mali na umaarufu sio chanzo cha furaha na ndio maana haiwezekani duniani kila mtu akawa tajiri. Maisha yamefanya hivyo kutufunza kuwa kuna utajiri mkubwa zaidi ya mali.