Mkutano wa uchumi na biashara kati ya Marekani na Afrika ulimalizika hivi karibuni. Wachambuzi wanasema kuwa serikali ya awamu mpya ya Marekani inayoongozwa na rais Joe Biden inatarajia kutumia fursa ya mkutano huo kudhoofisha ushawishi wa China barani Afrika. Hii ina maana kuwa Marekani inaeneza kwa vitendo “fikra za vita baridi” barani humo, yaani “kushindwa kwako ndio ushindi wangu”, na “vita vya kuigombea Afrika” ikiwa ni sehemu ya mashindano mapya ya siasa za kijiografia yaliyofanywa na Marekani dhidi ya China imeingia kwenye kipindi cha utekelezaji.
Afrika ni jukwaa kubwa la ushirikiano wa kimataifa, wala sio uwanja wa mashindano yanayofanywa na nchi zenye nguvu. Licha ya kushindana, China na Marekani zina maslahi mengi ya pamoja barani Afrika yakiwemo usalama, uchumi na afya ya umma.
Ushirikiano wa kiusalama
China na Marekani zina historia ndefu katika kusaidia Afrika kukabiliana kwa pamoja na matishio ya kiusalama. Mwaka 2008, China ilipeleka meli za kijeshi kuungana na Marekani na nchi nyingine kupambana na uharamia uliokithiri katika Ghuba ya Aden, na kuanza ushirikiano mkubwa wa kiusalama kwa mara ya kwanza kati yao, ambao umetatua kwa kiasi kikubwa tatizo hilo katika miaka mingi iliyofuata. Lakini vitendo vya uharamia vinaongezeka kutokana na janga la COVID-19, na China na Marekani zote zimeeleza wasiwasi wao juu ya hilo na kuchukua hatua mtawalia ili kujenga uwezo wa nchi zilizo katika eneo la Ghuba ya Guinea mashariki mwa Afrika katika kupambana na uharamia. Kwa kupitia njia hii, China na Marekani zinaweza kuchangia zaidi amani ya Afrika ili kuzinufaisha pande zote.
Mbali na tatizo la uharamia, China na Marekani pia zinaweza kuimarisha ushirikiano wao katika kulinda amani. China ni nchi iliyopeleka walinzi wa amani kwa wingi zaidi miongoni mwa nchi wajumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na pia ni nchi ya pili kwa kuchangia kiasi kikubwa zaidi cha pesa ili kuunga mkono operesheni za kulinda amani za Umoja huo ikiifuata Marekani, na wanajeshi wa China wanaonekana katika tume mbalimbali maalum za Umoja wa Mataifa barani Afrika zikiwemo za nchini Sudan Kusini na Mali. Kwa hivyo, chini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, operesheni za kulinda amani zinaweza kuwa jukwaa muhimu la China na Marekani kuimarisha ushirikiano wa kiusalama na kisiasa barani Afrika.
Ushirikiano wa kiuchumi
Katika miaka ya karibuni, uhusiano wa China na Afrika umeendelezwa kwa kasi, na China imedumisha kwa miaka mingi nafasi ya kuwa mwenzi mkubwa zaidi wa kibiashara wa Afrika. Ndio maana, Marekani imetoa hoja nyingi bila ya msingi kuishutumu China ikiwemo kuweka “mtego wa madeni” barani Afrika, na kuzilazimisha nchi za Afrika kuchagua kati ya Marekani na China. Lakini fikra hizi za vita baridi hazilingani na hali halisi ya biashara barani Afrika. Vilevile, uhusiano wa kiuchumi kati ya China, Marekani na Afrika hauna kiwango cha ushindani mkubwa kama baadhi ya wamarekani wanavyofikiria, badala yake kiwango cha kusaidiana ni cha juu.
Kwa mfano, takwimu za shughuli za kiuchumi za China na Marekani barani Afrika zimeonesha kuwa China inaangalia zaidi miundombinu ya kimsingi kama vile miradi ya ujenzi na uzalishaji viwandani, lakini Marekani inazingatia zaidi miundombinu “laini”, ikiwa ni pamoja na ushirikiano katika nguvukazi na mitaji ya kijamii. Ni wazi kuwa nchi za Afrika zinaweza kuchagua uwekezaji kutoka kila upande yaani wa China au Marekani ili kukidhi mahitaji tofauti. Vilevile, kuanzishwa kwa eneo la biashara huria la Afrika linaweza kuchangia ushirikiano wa kibiashara kati ya China, Marekani na Afrika.
Ushirikiano wa afya ya umma
Kwa hali ya sasa, pengine Afrika itakuwa kanda ya mwisho kupata chanjo za kutosha dhidi ya COVID-19. Takwimu zimeonesha kuwa barani Afrika, ni watu milioni 20 tu waliochanjwa kikamilifu, na kuchukua asilimia 1.5 ya watu wote. Dozi za chanjo zinazomilikiwa na Afrika ni asilimia 1.7 tu ya zile za dunia nzima, lakini Marekani inakosolewa kwa kuhodhi chanjo nyingi kupita kiasi na kulazimika kuzitupa baada ya muda wake kwisha. Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya hivi majuzi alipohojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza BBC alikosoa “sera ya utaifa wa chanjo” inayotekelezwa na baadhi ya nchi za magharibi bila kutaja jina la nchi, na kusisitiza kuwa Afrika inahitaji uwezo wa kuzalisha yenyewe chanjo zake.
Kwa mujibu wa uwezo wa China na Marekani kuzalisha chanjo ndani ya nchi, kunatekelezeka kwa kutoa chanjo za kutosha kwa bara la Afrika lenye watu bilioni 1.2. Mlolongo wa kwanza wa uzalishaji wa chanjo dhidi ya COVID-19 uliojengwa na kampuni ya China barani Afrika unazalisha dozi laki 3 hadi 6 kwa siku nchini Misri, huku kampuni ya Pfizer ya Marekani pia ikiwa imetangaza kuzindua mlolongo wa uzalishaji wa chanjo yake nchini Afrika Kusini, japo itakuwa ni kushughulikia kujaza rasilimali za chanjo na kusambaza tu, lakini hatua hii pia italeta matumaini kwa Afrika. Katika kukabiliana na virusi vinavyobadilika vya Corona yaani Delta, ushirikiano kati ya China na Marekani ni muhimu sana kwa sasa, sio tu katika kuhakikisha watu wa Afrika wanapata kinga mwili, bali pia unaoendana maslahi ya China na Marekani.
Bado tunakumbuka kuwa katika kipindi cha kuanzia mwaka 2013 hadi 2016, ugonjwa wa Ebola ulioibuka Afrika magharibi uliua maelfu ya watu. China na Marekani kila upande ulitoa msaada wenye thamani ya zaidi ya dola za kimarekani milioni 100 na kupeleka mamia ya watumishi wa afya kutoa matibabu. Tumeshuhudia watumishi wa afya wa China na Marekani wakifanya kazi katika maabara ya China, na pia kuona wafanyakazi wa Marekani wakipakua vitu vya msaada kwenye ndege za kijeshi za China.
Japo hivi sasa hali ya siasa ya kimataifa imekuwa tofauti sana na kipindi cha janga la Ebola, lakini ushirikiano huo umeweka bayana kuwa katika kukabiliana na janga la COVID-19, China na Marekani zinaweza kabisa kushirikiana katika sekta ya afya ya umma barani Afrika, na ushirikiano huo pia utathibitishwa kuwa ni kitendo cha haki kitakachowanufaisha watu wa Afrika.