Hussein Massanza
JF-Expert Member
- Dec 26, 2012
- 1,016
- 2,195
Msanii wa muziki wa kizazi kipya, Marlaw amepotea kwenye ramani ya muziki wa Bongo Fleva, hasikiki tena, licha ya kutoa nyimbo mpya kila siku, lakini hapati tena kushikilia chati za redio kama ilivyo zamani na pengine hasikiki maeneo mengi kama ilivyoopata kutokea.
Tatizo liko wapi? Je, muda wake umeisha? Nyota yake imefifia? Yeye ni wa zamani kwa hiyo ni zamu ya wasanii wapya kutamba? Kwanini imekuwa ghafla?
Lipo jambo! Twende mdogo mdogo.
Ukimuuliza yeye mwenyewe, atakwambia kampeni za kisiasa alizozitumikia mwaka 2010 ndizo zilizomporomosha kimuziki, hivyo anajutia uamuzi wake wa kukubali kutumiwa na wanasiasa kwenye kampeni zao.
Kivipi? Ufafanuzi ambao ameutoa mara kwa mara, anadai kuwa amepoteza mashabiki wengi ambao hawakuwa wanachama wa chama alichokuwa akikipigia kampeni, hivyo walimbwaga!
Sawa, yeye ndiye anaona hivyo, je ukweli ni upi? Ngoja tuunganishe nukta.
Mwaka 2010, wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu nchini, vyama vya siasa vilitumia wasanii wa muziki wa kizazi kipya ili kujipatia wapigaji kura wengi kupitia kwa ushawishi ambao wasanii hao wanao katika jamii, wakiwemo wasanii wa muziki wa taarabu, dansi, mchiriku na Bongo fleva. Ulikuwa mwaka wa neema kweli kweli kwa wasanii!
Kwenye B'fleva, baadhi ya wasanii waliopiga kampeni kwa kutumia nyimbo zao majukwaani ni pamoja na Chege na Temba, Kidumu, Bushoke, Diamond, Mwasiti, Mataluma, Marlaw na kadhalika.
Hapa kilichofanyika, ni wasanii kubadili mashairi ya nyimbo zao ambazo zilikuwa na nguvu na kupendwa sana kwa wakati huo, kuwa ni mashairi ya kuhamasisha na kusifia utendaji wa Chama cha Mapinduzi, ili kichaguliwe tena kwa kura nyingi na kuweza kutwaa madaraka kwa miaka mingine 5. Lengo lilifanikiwa!
Ukiangalia hiyo list, asilimia kubwa ya wasanii walioshiriki bado wanatamba sokoni hadi leo. Tunawaona kwenye shows, tunasikia nyimbo zao mpya, tunaona mafanikio yao kwenye endorsements mbalimbali, kwa ufupi, bado wapo wapo!
So, kusema siasa za 2010 zimemshusha kisanii, si kweli, hiyo ni hoja dhaifu, lazima kuna tatizo mahali. Je, ni lipi? Na kwanini analificha? Au halijui?
Ngoja nifanye makisio..
1. MABADILIKO:
Muziki wa kizazi kipya umebadilika. Siku hizi mambo ya kutegemea bahati ili ung'are yameshapitwa na wakati. Mwendo uliopo ni sawa na ule msemo wa 'asiyefanya kazi na asile', yaani msanii asipojishughulisha kwa jitihada binafsi za kuusimamia muziki wake na ratiba zake za kimuziki, ni sawa na anajichimbia kaburi lake mwenyewe.
Kwa mfano, hali ya sasa inamuhitaji msanii kushiriki kwenye mitandao ya kijamii na kujimix na mashabiki, kuweka mabandiko na vionjo vya kazi zake mpya, kushea nini anafanya, yuko wapi, nini kinamuweka kimya na kadhalika.
Haya yote sijawahi kuona Marlaw akiyafanya, hivyo ameshindwa kwenda na kasi ya mabadiliko. Amebaki pale pale akikaza msuli studio na kusubiri 'zali' kama ilivokuwa 'enzi za mwalimu'.
No brother, get out of that comfort zone, tupo sayari nyingine siku hizi. wake up!
Hebu fikiria, mashabiki wako wanataka kujua vitu vyote hivyo kutoka kwa msanii wao, wewe huwapi, anatokea Timbulo anafanya hayo, kwanini asikuzidi kete? Kalagabaho!
Hii ni nukta ya kwanza. Tutoke hapo!
2. MAHUSIANO NA 'MEDIA'
Pengine kijana mstaarabu, Marlaw, hana mahusiano mazuri na Media, au hajui nguvu aliyonayo kama msanii. Nimesema Pengine, usininukuu vibaya.
Ukiwa msanii, hasa mwenye jina kubwa, kuna kitu kinaitwa 'spotlight', yaani wenyewe wanaita 'Nyota'. Nyota imng'ara kwa msanii, akatokea kupendwa na kufuatiliwa na kundi kubwa la watu katika jami, ni kitu ambacho kinawavutia sana wafanyabiashara, wanatamani kusafiria hiyo nyota kuweza kuteka soko lao pia kwa ajili ya bidhaa/huduma wanazotoa, ni njia rahisi ya wao kuuza zaidi.
Kwa maneno mengine, umaarufu na kupendwa ni Lulu. Sasa umewahi kuona wapi Lulu inamtafuta mchimbaji? Ikitokea bahati tu mtu unaweza kuokota Lulu njiani, lakini sio ukipita njia hiyo kila siku utakutana na Lulu, la hasha, hayo ni mawazo mgando.
Hata magazeti, vituo vya Tv na redio hupenda kuwatumia wasanii, lengo ni kuweza kunufaika na 'nyota' yao kibiashara, Hivyo hivyo kwa makampuni ya simu, mashirika makubwa, na kadhalika.
Kwa namna hii, thamani ya msanii hufanya atafutwe na agombaniwe kwenye interviews, matangazo, na dili mbalimbali kutoka kwa taasisi hizi. Ukichuja, ukapoteza mvuto, nao wanakuchekecha, huwafai tena. Iko hivyo duniani kote!
Sasa Marlaw, eneo hili sijui karata zake alizicheza vipi. Je, alivikwepa vyombo vya habari? Alizembea kutunza mvuto wake? Alitunisha mabega kama alivyowahi kufanya Ali Kiba? (najua kuna walioshtuka kumtaja Ali Kiba kwenye mfano, story yake ipo, sio mahali pake hapa). Jibu analo mwenyewe Marlaw.
Hiyo ni nukta ya Pili. Tutafakari na hii ya mwisho..
3. UBUNIFU:
Kuna jipya kwenye muziki wa Marlaw? Anatoa videos nzuri? Ana usimamizi unaoelewa soko linahitaji nini kwa sasa? Ushirikiano na wasanii wengine? Anaenda na wakati?.
Kama yote jibu ni HAPANA, basi ajikague upya, kisha atafakari kwa makini kama ni Kweli SIASA imempoteza kwenye ramani ya muziki!?
Nawasilisha..