Je tumbo lako huvurugika mara kwa mara ukiwa ofisini?

Je tumbo lako huvurugika mara kwa mara ukiwa ofisini?

Joined
Mar 9, 2013
Posts
5
Reaction score
1
Kwa mfanyakazi anayeshinda ofisini akiwa ameketi kwa saa 8 au zaidi, maumivu ya tumbo mara kwa mara na mabadiliko ya ghafla ya kwenda chooni si tu kwamba yanapunguza ufanisi wa kazi bali yanatengeneza mazingira magumu ya kisaikolojia.

Makala hii imeandaliwa maalum kabisa ili kuelimisha jamii ya wafanyakazi wa ofisini juu hali iitwayo; Irritable Bowel Syndrome”IBS” mara nyingi tumesikia wakisema mchafuko wa tumbo. Fikiria uko katikati ya kikao muhimu cha board, au unakaribia kuwasilisha ripoti muhimu mbele ya bosi wako. Ghafla unaanza kuhisi maumivu makali yanabana chini ya kitovu, au tumbo kujaa gesi, msukumo mkubwa unaokulazimu ukimbilie msalani haraka. Hali kama hii inaweza kuwa inawatokea mara kwa mara, na hujui ni nini chanzo chake.

Irritable Bowel Syndrome ni nini? Ni hali inayohusisha mkusanyiko wa dalili zifuatazo; ambazo ni maumivu makali ya kujirudia kwenye chembe ya tumbo, kuharisha (diarrhea), kukosa choo (constipation) au vyote kwa pamoja.

Tofauti na magonjwa mengine ya mfumo wa chakula, IBS haina dalili zozote zinazoonekana kama za uharibifu au vidonda kwenye utumbo wako. Wengi wamefanya vipimo na hakuna tatizo la moja kwa moja lililoonekana. Ukweli ni kuwa, hili ni tatizo linalohusisha zaidi mawasiliano kati ya ubongo na utumbo wako (brain – gut axis). Changamoto katika mfumo huu wa mawasiliano hupelekea ama misuli midogo midogo ya utumbo kukaza au kulegea sana katika hali isiyoya kawaida kabisa.

Kila mtu anaweza kuwa na dalili tofauti na mwingine kutokana na utofauti wa mwitikio wa miili yetu. Kwa mwingine anaweza kupatwa na hali hii na siku inapotokea inaambatana na dalili ya choo kuwa kigumu sana. Au kwa watu wengine inaweza kujitokeza na choo kinakuwa cha majimaji au laini sana, na akaharisha. Kwa kwa kundi lingine mtu anaweza kupatwa na dalili zote, yaani wakati mmoja anapata choo kigumu sana, au ikijitokeza wakati mwingine anaharisha sana.

Irritable Bowel Syndrome inaweza kumpata mtu yeyote, huku wanawake wakiwa kwenye hatari mara mbili zaidi ya wanaume, na mara nyingi hutokea kwa watu walio chini ya miaka 50. Sababu mbalimbali zinaweza kupelekea hali hii ambazo ni pamoja na; msongo wa mawazo na wasiwasi uliokithiri, kuketi muda mrefu na tabia bwete, lishe na historia ya maambukizi ya tumbo.

Athari za IBS kwa mfanyakazi hasa wa maofisini ni zaidi ya tumbo kuuma, mfanyakazi huchoka haraka na kupoteza umakini. Lakini pia, mtu huwa na wasiwasi, msongo, uchovu mwili uliokithiri (chronic fatigue syndrome) au maumivu ya misuli au viungo sehemu mbalimbali za mwili.

Kama umekuwa ukiteseka na hali hii, jambo la kwanza kabisa usipuuzie kabisa na acha kujitibia. Muune Daktari au Mtaalamu wa Afya kwa uchunguzi utakaopelekea ushauri wa mpango wa matibabu unaofaa kulingana na changamoto inayokupata.

Hatua ndogo ndogo ambazo zitakusaidia kukabiliana na hali yako ni; Kudhibiti msongo wa mawazo tenga angalau dakika 5 za kunyoonya viungo na kupumzisha akili. Kuwa mwangalifu sana na chakula unachokula, kila wakati chunguza ni vitu gani ukila vinakuletea changamoto wakati wa kazi na uepuke. Mwisho, kunywa maji ya kutosha, maji husaidia sana katika usagaji wa chakula.

Imeandaliwa na: Emmanuel Jacob, Afisa Mfiziotherapia & Mwenyekiti wa Tanzania Physiotherapy Initiative (TPI)
 
Back
Top Bottom