Jamaa mmoja alikuwa mwoga sana, anaogopa sana adhabu. Kama kawaida ya jeshi. ilikuwa ni lazima utandike kitanda vizuri kwa style ya jeshi, kila kitu, shuka, blanketi, kitanda mess tin, kwa dressing. Haya yote unatakiwa ufanye kabla hujapurukushwa kwa wito wa 'FOLEN'! Basi huyu jamaa alikuwa anatandika kitanda chake vizuri usiku tukitoka disco, halafu alikuwa analala chini! Tulikuwa tunamcheka sana, lakini baadae tukawa tunamuonea huruma.
Njemba moja alikuwa akizurura kutwa na sururu. Akiulizwa, askari unakwenda wapi, anasema ametumwa kazi na afande fulani. Tulikuwa tunamuonea huruma maana alikuwa anazurura kutwa na sururu baada ya kulala porini kama sie wengine wajongomeaji.
Tulijifunza kutomaliza kazi mapema, maana ukiripoti umemaliza kazi uliyopewa, unabambikiziwa nyingine. Tulikuwa na midomo yenye fridge, maana kama jamaa yako alikuwa zamu jikoni, akikuchotea nyama au wali kwenye mess tin, unatakiwa umeze haraka, hata kama ni vya moto kiasi gani. Ulitakiwa uwe mwizi sana, hasa wa kofia, maana kama umeibiwa kofia na hukuvaa, unapewa adhabu. Mimi nilizoea kuwaibia maafande kofia zao, maana ilikuwa ni rahisi kwao kupata nyingine.
Katika kombania yetu tulikuwa na wahindi wawili. Siku moja kwenye disco, baada ya wiki kadhaa za kukaa jeshini, mhindi mmoja akawa anatufundisha wimbo wa kihindi. Tulijifunza, lakini yule mwingine akawa anacheka sana,. Sisi tukadhani kuwa maneno ya wimbo ule yanachekesha. Kesho yake ilibainika kuwa yule Mhindi aliyetufundisha ule wimbo ametoroka. Yule mhindi aliyebaki akatuambia alikuwa anacheka sana maana maneno ya wimbo ni: Kwaherini, mimi kesho natoroka!
Siku moja kombania yetu ilikuwa zamu. Platoon yetu ikapelekwa kwa kuku. Kama kawaida, ukishafika huko unakazana kubugia kwa wingi mayai mabichi kiasi utakachoweza. Baada ya kumaliza kazi, tukachukua mengine, tukajaza kwenye mifuko ya combat. Rafiki yetu mmoja akachukua mengine akayaweka kwenye jungle hat yake, halafu akaivaa. Tukawa tunaondoka kutoka kwa kuku, tukiwa na dhamira ya kwenda kwenye jongomeo letu msituni. Mara tukakutana na ma MP. Kitu kilichotuponza siku hiyo ni kutokuvaa vizuri. Hatukufunga kamba boot, mashati hayakufungwa vifungo nk. MP mmoja akasema, 'Askari, simama. Mbona mmevaa kama askari wa kukodiwa?' Akamuita yule jamaa aliyevaa jungle hat yenye mayai. 'We, kuja hapa, mbona umening'iniza kofia? Njoo hapa nikuonyeshe namna ya kuvaa'!! Akashika kofia, akaishusha kwa nguvu ili aizingushe zungushe kwa nguvu kichwani. Lo, si mayai yakavunjika! Yakaanza kumwagika usoni mwa jamaa. Basi tukazingirwa tusikimbie. Tukasachiwa likapatikana karai zima la mayai. Tukapigishwa fang fang usawa wa Quarter Guard, tayari kwa kufungwa na kuwa court marshalled.
Muda huo ulikuwa mchana na chakula cha ma MP kilikuwa kimeletwa. Basi ma MPwote, isipokuwa mmoja, wakaenda kula. Ikatokea kuwa kitabu cha kuandikisha mahabusu kimejaa, MP akaenda kuchukua kingine. Wakati huo tupo kwenye baraza la Quarter Guard, bado hatujawekwa ndani. Kuona upenyo huo, tukaamua tutoroke. Mmoja wetu akakumbuka kuwa tumesahau karai letu la mayai, akalirudia, tukatokomea nalo msituni. Mchana ule tulikula vizuri sana mayai ya kuchemsha .
Wakati wa usiku kwenye disco, tukaona kundi la ma Mp linakuja usawa wa kombania. Tukajua, leeo tumepatikana. Wakaongea na kamanda wa kombania, halafu muda si mfupi wakaondoka. Baada ya wao kuondoka,kamanda akasoma majina yetu na kutuita tutoke mbele. Akautuuliza, nyie mlikuwa kwa kuku leo? Tukamuambia ndio. Akasema safi sana, nyie askari wazuri sana, mmekamatwa, lakini mkaweza kutoroka, pamoja na mayai yenu. Huo ndio uaskari. Hatukupewa adhabu, disco likaendelea!