Jeshi la Polisi lijenge utamaduni wa kutolea mrejesho matukio yenye maslahi kwa umma wanayotelea taarifa za awali

DogoWaNjombe

JF-Expert Member
Joined
Feb 7, 2022
Posts
3,284
Reaction score
7,708
Kwa nyakati tofauti, Jeshi la Polisi limekuwa likijikuta kwenye mtihani wa kuaminika mbele ya umma kutokana na matukio yenye utata ambayo huacha maswali mengi bila majibu ya wazi. Mara nyingi, taarifa za awali hutolewa, lakini baada ya hapo umma hukosa mrejesho kuhusu hatua za uchunguzi au matokeo yake.

Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na taarifa za watu kupotea au kudaiwa kutekwa, huku baadhi yao wakidaiwa kuuawa au kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kutisha. Matukio hayo yameendelea kuibua hofu, mijadala na maswali mengi miongoni mwa wananchi.

Kwa mfano, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kiliwahi kueleza uwepo wa takribani watu 100 wanaodaiwa kupotea au kutojulikana walipo. Aidha, Ripoti ya Mwaka 2025 ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ilieleza uwepo wa mamia ya watu wanaodaiwa kupotea.

Si ripoti hizo pekee. Kwa mujibu wa Tume ya Kuchunguza Matukio ya Oktoba 29, iliyoongozwa na Jaji Mstaafu Othman Chande, zaidi ya watu 700 walitajwa kuwa wamepotea au hawajulikani walipo. Ripoti hiyo pia ilieleza kuwa matukio hayo yalikuwa miongoni mwa sababu zilizochangia matukio ya Oktoba 29 yaliyosababisha vifo na uharibifu wa mali.

Mbali na takwimu hizo, yapo matukio yaliyovuta hisia kubwa za umma kwa sababu ya mazingira yake na taarifa zilizokuwa zikitolewa, ambazo zingeweza kusaidia kuelekeza uchunguzi. Hata hivyo, licha ya kupewa uzito na wananchi, mengi ya matukio hayo yamebaki bila mrejesho wa kutosha.

Kwa kawaida, matukio yanaporipotiwa, Jeshi la Polisi hutoa taarifa za awali. Hali hiyo ilijitokeza katika matukio ya kudaiwa kutekwa kwa Humphrey Polepole, Mdude, Ali Kibao na hata tukio la hivi karibuni la Jumbe. Lakini baada ya taarifa hizo za mwanzo, ni nadra kwa umma kupata taarifa zinazoeleza hatua zilizofikiwa katika uchunguzi.

Kutokuwepo kwa mwendelezo wa taarifa kunaweza kutafsiriwa na sehemu ya umma kuwa matukio hayo hayapewi uzito unaostahili, ilhali yanagusa haki za msingi za binadamu, ikiwemo haki ya kuishi na haki ya usalama.

Ndiyo maana ni muhimu Jeshi la Polisi likaweka utamaduni wa kutoa mrejesho wa mara kwa mara kuhusu maendeleo ya uchunguzi. Mrejesho huo unaimarisha uwajibikaji wa taasisi na kujenga imani ya wananchi kwa vyombo vya dola. Kauli kwamba "uchunguzi unaendelea" ni muhimu, lakini haitoshi ikiwa haitafuatiwa na taarifa za maendeleo pale inapowezekana kisheria na kiuchunguzi.

Wananchi wanapofahamu kuwa hatua zinaendelea kuchukuliwa, hujenga taswira ya uwazi na uwajibikaji. Kinyume chake, ukimya huacha nafasi kwa uvumi, hofu na mashaka kutawala, jambo ambalo halisaidii taasisi wala jamii.

Kwa hiyo wito wangu, Jeshi la Polisi linapaswa kujenga utamaduni wa kutoa mrejesho hasa katika matukio yenye maslahi makubwa kwa umma na yanayoibua mijadala. Ikiwa wahusika wamekamatwa na kufikishwa mahakamani, umma unapaswa kufahamishwa. Vivyo hivyo, endapo uchunguzi umebaini ukweli tofauti na taarifa zilizokuwa zikisambaa, ni vyema taarifa hiyo ikawekwa wazi ili kuondoa taharuki na upotoshaji.

Lakini pia ni muhimu kutambua kuwa Jeshi la Polisi si chombo cha kutoa taarifa za muda mfupi zinazoweza kutafsiriwa kuwa ni kwa ajili ya kutuliza mjadala wa umma pekee. Ni taasisi iliyoanzishwa kwa mujibu wa sheria, yenye wajibu wa kutanguliza weledi, uwajibikaji na uwazi katika utekelezaji wa majukumu yake.

Kujenga utamaduni wa kutoa mrejesho wa matukio ambayo tayari yamepewa taarifa za awali hususani yenye maslahi ya umma na mguso kwa jamii kutasaidia kuongeza imani ya wananchi na kuimarisha uhusiano kati ya Jeshi la Polisi na jamii inayolihudumia, utamaduni huu unaweza kutekelezwa tokea ngazi za chini Wilayani hadi Kitaifa.
 
Hiyo itamaanisha kwamba wakiri makosa yao maana 90% ya matukio, they are the perpetrators.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…